Sumu Zinazoharibu Ubora wa Mbegu za Uzazi

Katika mtiririko wa makala zetu za masuala ya ugumba au kushindwa kushika mimba haraka, leo nitaongelea vitu vinavyoweza kupelekea mbegu za uzazi yaani mayai ya kike au kiume kupoteza ubora wake na kushindwa kutengeneza kijusi chenye afya.

Tunafahamu kuwa mbali na umri, mazingira na aina ya maisha tunayoishi yanathiri pakubwa ubora wa mayai – hasa kwa mwanamke kwa sababu yanatumia miezi mitatu mpaka minne kukomaa kabla ya kutoka kwenye mfuko wa mayai ili kukutana na mbegu ya kiume. 

Tofauti na mbegu za kiume ambazo zinatengenezwa kila siku katika mzunguko wa siku 60 mpaka siku 75.

Katika kipindi hiki, mwili wa mwanamke usipopata virutubishi vya kutosha, ukapata mifadhaiko kama vile msongo wa mawazo na kemikali kuingia mwilini inaweza kusababisha mayai kushindwa kukomaa ipasavyo na kupoteza ubora wa kutengeneza kijusi chenye afya. 

Miongoni mwa virutubishi ambavyo ni muhimu kupata mwilini wakati unajiandaa kupata ujauzito kwa njia ya kawaida au IVF ni madini chuma, madini joto, vitamini D, omega 3, zinc na virutubishi vingine kwa uchache wake kama vile vitamini A, E, B12, B6, C, selenium, calcium, iodine na magnesium

Aidha kuepuka au kupunguza visababishi vya msongo wa mawazo na stress nyingine mwilini kunasaidia mfumo wa homoni kufanya kazi vizuri na kukomaza mayai. 

Kubwa zaidi ni sumu ambazo zinapatikana katika maisha ya kila siku kuingia mwilini. Kundi baya zaidi ni kundi la sumu zinazovuruga mfumo wa homoni mwilini (hormone disruptors).

Hizi kemikali zinapelekea aidha kujishikiza katika maeneo ambayo homoni husika inatakiwa kufanya kazi na kusababisha mwili kureact kana kwamba homoni halisi imezalishwa au kujishikiza katika eneo la homoni na kusababisha homoni husika kushindwa kufanya kazi. 

Vile vile zinasababisha mwili kushindwa kutengeneza homoni au kutengeneza homoni nyingi zaidi ya kiwango kinachotakiwa. 

Pia kemikali hizi zinaweza kusababisha protini zinazoshikilia homoni mwilini kushindwa kufanya kazi au kuwepo kwa wingi kupitiliza. Kwa ufupi tu, ni kemikali ambazo zinaharibu kabisa mfumo wa homoni za mwili hasa homoni za oestrogen, androgen na thyroid ambazo ni muhimu sana katika mfumo wa uzazi. 

Sumu ni Zipi na Zinapatikana Wapi?

Sumu zinazovuruga homoni ziko nyingi lakini kwenye makala hii nitaongelea mahususi sumu zinazovuruga homoni za uzazi na baadhi ya athari zake kwenye maeneo mengine mwilini.

Bisphenol A (BPA)

Inawezekana umeshawahi kuona mabakuli ya plastiki au chupa za plastiki za watoto zimeandikwa BPA free; ni kwa sababu hii kemikali ni moja kati ya vivuruga homoni vikubwa sana! 

BPA inatumika kutengeneza plastiki, katarasi za risiti na hupakwa ndani ya makopo ya vyakula vinavyosindikwa (canned foods).

Tafiti zinaonyesha hata kiasi kidogo tu cha kemikali hii mwilini kinapunguza ubora wa mayai, kuchelewa kupata ujauzito kwa wenzi, ubora hafifu wa kijusi na hatimaye kutoka mimba. Wanawake waliogundulika na BPA walikua na historia ya kujirudia ya kutoka mimba zao. 

BPA zamani ilikua inajulikana kama homoni ya estrogen ya kutengeneza na ndo maana inaharibu mfumo wa homoni za uzazi na kupelekea changamoto za kupata ujauzito kwa wenza wengi. Na hata kwa watoto wadogo, BPA inakuwepo katika maziwa ya mama na inapita kwenye kondo la nyuma (placenta) kwenda kwa mtoto. 

Athari zake kwa kiumbe kitakachozaliwa ni pamoja na mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, kuathiri maumbile ya uzazi hasa kwa watoto wa kiume, kuathiri mayai ya mtoto wa kike aliye tumboni

Hata hivyo, BPA inahusishwa na maradhi mengine kama vile kisukari, shinikizo la damu na kansa. 

Jinsi ya kujikinga na kemikali hii

Kuzuia BPA katika maisha ya kila siku sio rahisi lakini inawezekana kupunguza ufikaji wa BPA ndani ya miili yetu hasa kama unataraji kuzaa au unanyonyesha, kama ifuatavyo:

  • Kutunza chakula kwenye mabakuli ya udongo au ceramic na sio plastiki, BPA inatoka kidogo kidogo kwenye plastiki kuingia kweye chakula chako hasa kikiwa cha moto.

  • Kupasha chakula kwenye microwave kwa kutumia vyombo vya udongo au ceramic. Hata kama bakuli la plastick limeandikwa microwave safe na BPA free, baadhi ya viwanda bado wanatumia BPA katika kiasi kidogo ambacho kinaweza kuleta madhara.

  • Kununua machupa ya mtoto au toys ziliozoandikwa BPA free ama kutumia toys za mbao, nguo na kupunguza toys za plastiki.

  • Kunawa mikono kabla ya kula hasa ukiwa umepokea risiti zile zinazotoka kwenye mashine; zinakua coated na BPA.

  • Kupunguza matumizi ya vyakula vilivyosindikwa na kutunzwa kwenye makopo ya chuma, yapo coated na BPA. 

Phthalates

Kemikali hii inatumika kutengeneza vyombo vya plastiki, vinyl za kusakafia na kupaka rangi ukutani, dawa za kuulia wadudu, vifungashio vya plastiki,  plastiki za PVC, na hasa inatumika kutengeneza vifaa vya urembo au vipodozi mfano manukato, losheni, rangi za kucha, na deodorant. 

Kwenye bidhaa nyingi utaikuta imefichwa katika majina marefu kama vile Diethyl phthalate, Di-n-butyl phthalate, Di(2-ethylhexyl) phthalate na kadhalika. 

Athari zake ni nini?

Athari za phthalates ni pamoja na kudumaza ukuaji, kuathiri figo na ini, na kuharibu mfumo wa homini za uzazi. 

Ikiwa imepita kwenye kondo la nyuma kipindi cha ujauzito mtoto anapata athari kama vile kuzaliwa na uzito mdogo, korodani kutoshuka kwenye pumbu na kubaki tumboni, uume kutokua vizuri, kufunguka urethra kwa chini (hypospadias) na kuwa na viungo vya kiume vilivyodumaa

MUHIMU: 

Hypospadias ni kasoro ya kuzaliwa ambapo mrija wa kutoa mkojo nje ya mwili unakua haupo kwenye ncha ya uume. Badala yake, hupatikana upande wa chini wa uume, wakati mwingine karibu na mapumbu, au chini zaidi shimoni.

Pia phthalates inahusishwa na kansa ya ini, kujaa sumu kwenye korodani, kutokomaza mayai kwa wanawake na hii hupelekea kushindwa kupata watoto au kupoteza mimba pale zinapotunga kwa sababu ya ubora hafifu wa mayai na kijusi.

Nitajikinga vipi na Phthalates?

Kuepuka phthalates moja kwa moja sio rahisi lakini kuna tunayoweza kufanya kupunguza exposure na athari zake kama vile;

  • Kutumia urembo wa asili kuanzia sabuni, shower gel, manukato, rangi za kucha kwa kutumia henna. 

  • Kupunguza matumizi ya vyombo vya plastiki na hasa PVC kama vile yoga mats zilizoandikwa PVC, na kutafuta mbadala wake.

Kemikali nyingine

Kemikali zinazoharibu mfumo wa homini ni nyingi na mbaya zaidi kwa aliyebahatika kushika ujauzito, zina uwezo wa kupenya kwenye kondo la nyuma la mama na kumfikia mtoto na kupelekea kuathiri kizazi kinachofata kushindwa kuendeleza kizazi kingine. 

Chache katika kemikali hizo ni pamoja na Atrazine (inapatikana kwenye dawa za kuulia wadudu mashambani hasa dawa za mahindi na miwa), Dioxins (inatumika kutengeneza dawa za kuulia wadudu na makaratasi ya risiti), Triclosan (kwenye bidhaa za usafi wa mwili na urembo kama vile shower gel na sabuni), na nyinginezo.

Nihitimishe kwa kusema… 

Wakati unaangalia sababu nyinine za vinasaba, hali ya mazingira na vitu unavyotumia kila siku vinachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mimba na watoto wenye afya. 

Kufahamu kemikali hizi na kujiepusha nazo ni muhimu sana hasa kwa wenza wenye changamoto ya kushika ujauzito. Haitoshi kujiepusha na sumu hizi pekee kusababisha kupata ujauzito, lakini kunaongeza nafasi hiyo. Kwani kufanikiwa kupata mtoto kunajumuisha mambo mengi sana. 

Katika makala ijayo nitaelezea virutubisho muhimu vya kutumia kabla na wakati wa ujauzito (na baada ya kujifungua). 

Subscribe kwenye blogu yetu ili uwe wa kwanza kuipata.   

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW