Malaria: Visababishi, Dalili, Jinsi ya Kujikinga na Matibabu

Ni wazi umeshawahi kuusikia ugonjwa wa Malaria kabla ya kusoma makala hii. Na si aghalabu kuwa umeshawahi kuumwa malaria, au ndugu yako, au mtoto wako, au mtu unayemfahamu ameshawahi kusumbuliwa na ugonjwa huu wa malaria.

 

Je, unajua malaria inasababishwa na nini? Je, unajua kimelea cha malaria kiingia mwilini kinafanya nini au kinasababisha vipi hali ambayo mgonjwa anajisikia? Je, ni dawa ipi inatumika kutibu ugonjwa wa malaria? Basi soma makala hii kufahamu zaidi.

 

Malaria inasababishwa na vimelea vinavyoitwa plasmodium, ambavyo vipo vya aina nyingi ila vinavyosababisha malaria kwa binadamu vipo vya aina tano: Plasmodium falciparum, Plasmodium vivax, Plasmodium ovale, Plasmodium knowlesi na Plasmodium malariae.

 

Katika aina zote hizi, Plasmodium falciparum na vivax ndio wanaoongoza kwa ugonjwa na vifo vya malaria.

 

Kwa upande wa nchi yetu ya Tanzania, maambukizi ya ugonjwa wa malaria yameendelea kupungua. Takwimu kutoka utafiti wa demographia na viashiria vya malaria wa mwaka 2022 umeonyesha kiwango cha maambukizi ya malaria ni asilimia 8, ambapo mkoa wa Tabora unaongoza kwa asilimia 23.

Katika maambukizi yote, vimelea vya Plasmodian falciparum vinaongoza kwa maambukizi ya malaria.

 

Ramani ya Tanzania inayoonyesha maambukizi ya malaria kwa watoto kati ya miezi sita hadi miaka mitano mwaka 2022.  

 

Ramani ya Tanzania inayoonyesha maambukizi ya malaria kwa watoto kati ya miezi sita hadi miaka mitano mwaka 2022.

 

Je, Dalili Za Malaria ni Zipi?

Dalili zote za malaria zinatokana na namna gani ugonjwa huu unavyoingia mwilini na kusababisha mabadiliko katika mifumo mbali mbali. Sasa, huyu kimilea P.falciparum ana sifa kubwa ya uwezo wa kuingia seli nyekundu za damu na kujishikiza ambayo ndio inapelekea dalili mbalimbali katika mifumo yote ya mwili.

 

Miongoni mwa dalili za malaria ni pamoja na homa, kichwa kuuma, kuharisha, kutapika, kuchoka, viungo kuuma, kukosa hamu ya kula, kuvimba kwa bandama (mara nyingi hutokea kwa watoto wadogo). Hizi ni dalili kwa mtu ambaye hana malaria kali.

 

Aidha vimelea vya malaria vikisababisha malaria kali dalili zake kwa mgonjwa ni pamoja na mwili kukosa nguvu kabisa, ngozi kuwa ya njano, kuchanganyikiwa, kupata degedege, kupumua kwa shida, kutapika kila kitu anachokula, kushindwa kula (au kunywa) na kushindwa kunyonya kwa watoto wachanga.

 

Aina zote za malaria, bila kujali ni kali au sio kali, inahitajika kutibiwa kwa haraka kuepusha kuharibika kwa mifumo ya mwili.

 

Unajikinga Vipi na Malaria?

Namna ya kwanza ya kujikinga ni kuhakikisha hung’atwi na mbu anayesambaza vimelea vya malaria. Na ikitokea mbu amekung’ata na umepata malaria, basi ni kufanya matibabu haraka ili kuzuia hatari ya kuharibika kwa mifumo ya mwili kama vile figo, kupungiwa sana damu na malaria ya ubongo.

 

Njia za kujikinga kung’atwa na mbu ni kama vile kulala kwenye chandarua chenye dawa kila siku. Kwa mama mjamzito na watoto, vyandarua vinatolewa kliniki bila malipo yoyote  lakini pia kuna kampeni nyingine za ugawaji vyandarua ikiwemo kampeni ya ugawaji wa vyandarua kwenye kaya (ambayo inafanyika kwenye baadhi ya mikoa); ugawaji vyandarua mashuleni (kwa wanafunzi wa shule za msingi).

 

Pia, kuvaa nguo ndefu na zenye mikono mirefu wakati wa jioni na asubuhi. Japokuwa mbu anayesambaza malaria anang’ata sana kuanzia usiku bado wapo ambao wanaanza kung’ata mapema hata ya saa 12 jioni.

 

Hivyo ni muhimu kuvaa nguo zinazoficha sehemu kubwa ya viungo vya mwili kama vile mikono na miguu ili kuepuka kung’atwa na mbu na kupata malaria. Pia kupaka mafuta yanayofukuza mbu.

 

Vile vile, kuhakikisha mazingira ya nyumbani ni safi na hamna mazalia ya mbu kama vile maji yaliyotuama.

 

Matibabu ya Malaria

Unapoona dalili za malaria wahi kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kipimo na matibabu. Dawa za malaria zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya Tanzania kote.

 

Ni muhimu na lazima kabla ya kunywa dawa za malaria, ugonjwa uthibitishwe kwa kipimo cha haraka au kwa kuangalia uwepo wa vimelea kwenye damu kwa kutumia hadubini.

 

Tutambue hakuna matibabu ya aina moja kwa kila mtu kila mara, kwani matibabu ya malaria yanategemea aina ya malaria – kama ni ya kawaida au kali.

 

Matibabu pia huzingatia umri na uzito wa mtu, ndio maana Dawa Mseto ya malaria kwa  mtoto au mwenye uzito mdogo anapewa vidonge vichache kulinganisha na mtu mzima au mwenye uzito mkubwa.

 

Matibabu ya malaria hapa nchini kwetu mara nyingi yanafanyika kwa kutumia Dawa za Mseto za Artemisinin na ndio zenye uwezo mkubwa wa kutibu kimelea cha P.falciparum. Mfano wa dawa hizi za Mseto ni Artemisinin + Lumefantrine (ALU) – dawa ambayo inatolewa katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya bila malipo.

 

Kwa wagonjwa wenye malaria kali, wanatibiwa kwa sindano ya Artesunate kulingana na uzito wao. Baada ya kumaliza sindano na kuweza kula na kumeza, mgonjwa anatakiwa kuendelea na dawa mseto ya vidonge  kwa siku tatu kulingana na maelekezo ya mtoa huduma.

 

Kanusho: Makala hii haijalenga kuwa mbadala wa ushauri wa daktari au kutumika kama njia ya matibabu. Lengo kuu ni kuchochea uelewa na ufahamu kwa jamii yako na yangu kwamba kutokomeza malaria kunaanza na sisi!

 

Malaria Inazuilika, Malaria Inatibika. Ziro Malaria Inaanza na Mimi.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW