Madhara ya Kutomwambia Ukweli Daktari Wako

Mara nyingi tunapoenda hospitali hatusemi ukweli aslimia 100. Huenda unaogopa kumwambia daktari wako juu ya dalili zote ulizopitia, au muda ulioumwa, au kama umeshatumia mitishamba au dawa yoyote nyumbani kabla ya kwenda kumuona daktari. 

Je, unajua madhara ya kutosema ukweli?

Kunapoteza Muda Wako!

Nimeshuhudia wagonjwa wengi wakipoteza muda hospitalini kwa kitu kidogo tu ambacho hawakusema ukweli mwanzoni. 

Kwa mfano, kama una historia ya ugonjwa wa muda mrefu, kama vile presha au kisukari, na hutumii dawa zako vizuri ni muhimu kusema kabla hata ya kwenda kuandikiwa vipimo bila kuficha. 

Kama daktari nakuuliza, “Una ugonjwa wowote wa muda mrefu amabao unatumia dawa?” ukajibu “hapana”. 

Bila shaka kuna vipimo kama vya figo na ini au kuchunguzwa macho sitakuandikia kwa wakati huo kulingana na dalili ulizokuja nazo. Lakini ikiwa vipimo nilivyoandika vikaonyesha tofauti na nilichofikiria, lazima nitaandika vipimo vingine urejee maabara tena. 

Yamkini, ungelisema mapema vipimo vyote vingeandikwa kwa wakati mmoja na ukaenda maabara kwa mara moja. Unalazimika kupoteza masaa mengine kusubiria foleni ya maabara na kupata majibu kwa sababu tu kuna kitu ulificha mwanzo.

Kupotezea Pesa!

Kwa mfano mdogo tu, hujasema ukweli juu ya dalili zako zote au muda ambao umeumwa. Tuchukulie kikohozi; umemwambia daktari una siku mbili-tatu unaumwa na hujapungua sana  uzito kwa sababu yoyote ile. 

Daktari hawezi kufikiria kifua kikuu, atakuandikia vipimo vya damu tu kumbe kifua kikuu kinahitaji kupima X-ray na makohozi, ambayo ikiwa una pesa kidogo angeweza kusitisha kipimo cha damu na kupima hivi viwili muhimu kwanza. 

Itakulazimu kwenda kutafuta pesa nyingine ikiwa vipimo vya damu vimerudi hakuna tatizo na inabidi ufanyiwe uchunguzi zaidi.  

Kupoteza pesa hakuishii kwenye vipimo tu, ugonjwa usipogundulika kwa wakati huo kisa ulificha baadhi ya dalili, baada ya muda ugonjwa utakua mkubwa na kukutaka utumie pesa nyingi zaidi, gharama ya muda na kurejea hospitali mara kwa mara na pengiNe kununua dawa zenye uwezo mkubwa zaidi kuliko ambazo ungetumia mapema. 

Haya yote yanahitaji fedha na ungeweza kulinda fedha yako kwa kusema ukweli.

Kugharimu Zaidi Afya Yako!

Mfano kuna baadhi yetu tunaenda hospitali, tunapatiwa matibabu na hatukalimishi matumizi ya dawa. Tukiona hakuna nafuu tunahamia hospitali nyingine na kuficha kile tulichofanyiwa katika hospitali ya awali na hatusemi kama hatukumaliza dozi ya dawa. 

Je, unajua vidonda vya tumbo vinaweza kusababisaha mfuko wa chakula kutoboka na kupelekea ufanyiwe operation?

Unajua bakteria wengi wasipotibiwa vizuri na dawa kikamilifu wanasababisha kansa baadaye? 

Sasa basi, unapomficha daktari kuhusu mambo kama matumizi ya dawa na dalili zako unasababisha ashindwe kukushauri na kukutibu kikamilifu. Baada ya muda inakuhitaji kufanyiwa upasuaji ambao huchukua muda zaidi kupona na unaweza kupata kidonda ambacho kikasumbua zaidi. 

Au ifikapo ukapata kansa kwa bahati mbaya, sio sawa na kama ungesema ukweli kuhusu afya yako kabla. 

Kupoteza maisha!

Ndio, kutosema ukweli kwa daktari wako kunaweza kupelekea upotezaji wa uhai wako. Kwa mfano, matumizi ya mitishamba kwa mama mjamzito. 

Kuna baadhi ya makabila wanaamini kumpa mama mitishamba atajifungua haraka, mama huyu anaenda hospitali na maumivu makali ya tumbo na akiulizwa kama ametumia dawa yoyote nyumbani anakana. 

Yawezekana mitishamba alizokunywa zikamfanya apate uchungu mkali sana na kusababisha mfuko/mji wa mimba kupasuka (uterine rupture). Hali hii inapelekea kifo cha mtoto na mama ikiwa msaada wa haraka haujapatikana kama vile kufanyiwa upasuaji. 

Ili hali, mama angesema ukweli mapema kuwa ametumia hizo mitishamba ni rahisi kwa nesi au daktari kufanya maamuzi ya haraka na kukuangalia kwa karibu zaidi.

Mwisho

Nikuache kwa msemo wa waswahili unaosema “Mficha maradhi, kifo humuumbua!”. 

Kutosema ukweli kunagharimu! Sema ukweli kulinda pesa yako, muda wako, afya yako na uhai wako. 

Kwenye comments section, naomba uniandikie mambo gani yanaweza kukufanya ushindwe kusema ukweli unapokuwa katika chumba cha daktari. Asante!

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW