Nikiungua Moto Nichukue Hatua Gani za Mapema?

Jamii ina utaratibu wake wa kufanya pale mtu anapoungua. Wewe unajua upi?

Kwenye utamaduni wangu nimekuwa nikiona mtu akiungua anamwagiwa mkojo kwenye sehemu aliyoungua na imekuwa ikiaminika kwamba inasaidia.  

Wengine huwa wanawahi kuweka asali sehemu iliyoungua wakiamini ni msaada mkubwa.  Wengine mafuta ya taa, petroli na kadhalika. Ninyi kwenu huwa  mnafanyaje

Kuungua ni tukio la taharuki sana hasa wakiungua wazee na watoto. Mtu anapoungua mambo mengi huja kichwani; Ameungua kwa ukubwa gani? Atapona au atalemaa? Maswali huwa ni mengi. 

Hatua zinazochukuliwa mapema, mtu anapoungua, huwa na mchango kwenye matokeo ya kuungua kwake pamoja na tiba kwa ujumla. 

Unajua ni nini unapaswa kufanya unapoungua? Basi niruhusu nikupitishe katika mtiririko wa mambo matatu muhimu ya kufanya kabla ya kwenda hospitali kutafuta matibabu.

Kwanza

Unashauriwa kumwagia maji ya bomba au yaliyo kwenye ndoo (sio ya baridi sana au barafu) kwenye sehemu iliyoungua mfano mkono au mguu.

Ikiwezekana hata kutumbukiza sehemu iliyoungua kwenye ndoo au beseni la maji. Mwagilia maji hayo kwa dakika 20. 

Kufanya hivi husaidia kwanza kupoza sehemu iliyoungua na hivyo kuzuia joto la chanzo kuendelea kuunguza sehemu ya ndani ya ngozi.

Fahamu kwamba unapomwagikiwa au kugusa kitu cha moto, kuungua hakuishii  tu nje ya  ngozi, lile joto huwa linaendelea kuunguza sehemu za ndani za ngozi ndio maana moja ya malalamiko ya mtu aliyeungua ni kuendelea kusikia maumivu ya kuunguza sehemu ya ndani ya pale alipoungua.

Kwa maana bado lile joto linaendelea kuunguza na sehemu ile isipopozwa, basi itakuja kutengeneza kidonda kikubwa baadaye maana sehemu za ndani zitaendelea kuungua.

Ndio maaana mtu anapoungua mwanzoni unaweza kuona sehemu ndogo lakini baada ya masaa kadhaa uta shangaa kidonda kinachimbika sana na kuwa kikubwa kwenda ndani.

Pili

Baada ya kuungua, mtu huanza kupata malengelenge kwenye sehemu iliyoungua. Haishauriwi kuyatumbua mpaka mgonjwa afike hospitali na daktari aangalie na kujiridhisha hali ya mgonjwa. 

Pengine anaweza kuacha mpaka yapasuke yenyewe kwa manufaa ya mgonjwa. Hii pia hupunguza hatari ya kidonda kuwa wazi mapema hasa nje ya mazingira ya hospitali na pia hupunguza maambukizi ya bakteria ya mapema.

Tatu

Baada ya mgonjwa kuungua na kumwagia maji sehemu aliyoungua, basi unapaswa kuufunika mwili wake kuepusha upotevu wa joto la mwili hasa kwa wale walioungua sehemu kubwa, zaidi ya asilimia 10% ya mwili.

 

Pia kufunika eneo lilioungua na kitambaa safi huwa na msaada katika kupunguza maumivu yatokanayo na upepo kwenye sehemu iliyoungua.  

Epuka matumizi ya bandage au kitu kinachobana kidonda moja kwa moja. 

Epuka kuweka vitu kama mafuta ya kujipaka, mafuta ya uto, dawa ya meno, majivu, n.k. 

Vitu hivi havishauriwi kiafya, vinaweza kupelekea kuongeza uwezekano wa maambukizi kwenye sehemu iliyoungua.

Muhimu: Mgonjwa aliyeungua kwa zaidi ya asilimia 10 ya mwili  anapaswa kuwahishwa hospitali walau ndani ya masaa 8 ya kwanza toka alipoungua.

Muda huu huwa ndio hatari zaidi na ndipo vifo vingi hutokea kwa wagonjwa walioungua sana. Hakikisha unamuwahisha mgonjwa ndani ya muda huu! 

Pia mgonjwa aliyeungua kichwa, uso, vidole, viungio vya mikono na miguu (joints) na sehemu za siri ni lazima apelekwe hospitali hata kama ni sehemu ndogo kwa maana sehemu hizi huwa ni muhimu sana na zina hatari ya kulemaa na kuleta ulemavu wa kudumu.

Matumizi ya Asali yanasaidia kwa mtu aliyeungua?

Ndio! Asali huwa na faida kwenye kidonda baada ya kuungua. Husaidia seli za mwili kurudi haraka na kidonda kupona, na pia asali husaidia kuzuia na kuua bakteria wanaokuja  kwenye kidonda.

Cha kuelewa tu ni kwamba haitasaidia mwanzoni kabla ya kidonda kuwepo hivyo achana nayo kwa mwanzoni, inaanza kutumika pale tu baada ya kufika hospitali ambapo tayari kuna kidonda. 

Matumizi ya mkojo je?

Hakuna utafiti ulioonyesha umuhimu wa kumwaga mkojo kwenye sehemu iliyoungua.Tumia maji ya kutiririka kama nilvyoeleza hapo juu.

Mwisho unapaswa kujua kwamba kinga ni bora kuliko tiba, hivyo jitahidi kujiepusha na kulinda familia yako kutopata ajali ya moto.

Weka uangalizi mzuri wa mtoto kutocheza karibu na vyanzo vya moto, kama ni mfanyakazi wa viwandani hakikisha unavaa vitendea kazi muhimu kuepusha ajali za kuungua kwa mvuke, vyuma vya moto na kemikali. 

Endelea kusoma makala za Abite Afya kuzidi kuelimika zaidi. Kwa uhitaji wa ushauri wa daktari, unaweza kupiga “hapa”. 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

en_USEN