Mkojo Unakataa Kutoka? Tezi Inaweza Kuwa Sababu!

Tezi dume ni nini?

Kila mwanaume huzaliwa na tezi. Tezi hii ni kiungo katika mfumo wa mkojo ambacho hufanya kazi ya kutoa majimaji (semens) ambayo husaidia shahawa za kiume kuogelea wakati wa  kutoka nje kupitia kwenye njia ya mkojo. 

Pia maji hayo husaidia kuandaa njia ya mkojo kuondoa ule utindikali na hivyo kusaidia shahawa kupita salama bila kuathiriwa.  

Tezi huongezeka ukubwa taratibu kadiri mtu anavyoongezeka umri.  

Kuongezeka huku huambatana na kutanuka kutoka nje kwenda ndani ambapo ikitanuka sana kwa baadhi ya wanaume huanza kuleta mgandamizo kwenye njia ya mkojo (urethra) na hivyo mwanaume huanza kupata changamoto za kukojoa na kadhalika. 

Utafiti unaonesha kwamba mwanaume akifikisha miaka 50 na kuendelea anakuwa na asilimia 20% mpaka 25% za kupata tezi dume na kuanzia miaka 70 na kuendelea uwezekano wa kupata tezi dume hufika mpaka asilimia 80 – 90%. 

Umegundua nini hapa? 

Kama wanaume wote wangeruhusiwa kukua na kufikisha miaka 80, basi asilimia 90% wangekutwa na tezi kubwa! Japo kitaalamu sio wote watakuwa na dalili za tezi dume.

Tezi dume inasababishwa na nini hasa? 

Tafiti nyingi zimeonesha kwamba tezi dume inasababishwa zaidi na vichocheo vya homoni za kiume – hasa testosterone katika kipindi cha kuanzia miaka 50 na kuendelea.  

Lakini kuna mambo kadhaa ambayo yanakuweka kwenye uwezekano mkubwa wa kupata tezi dume kama ifuatavyo: 

  • Umri: Kadiri umri wako unavyoongezeka ndipo unakaribia kupata tezi dume, na kwa asilimia kubwa kuanzia miaka 50 na kuendelea ndio hali hii huanza kushamiri.  Kwa uzoefu wangu sijawahi kukutana na mtu chini ya maika 50 mwenye tezi dume. 

  • Vinasaba vya kifamilia: Kama babu au baba yako alikuwa na tezi dume, basi na wewe uko kwenye nafasi kubwa ya kupata tezi dume. Babu yangu alikuwa na tezi dume kwahiyo na mimi najiandaa kisaikolojia, kuna vitu nafanya nitakushirikisha mwishoni.

  • Uzito mkubwa: Utafiti umeonesha kwamba watu wenye uzito mkubwa wako kwenye hatari ya kupata tezi dume. Ukiwa na uzito mkubwa unakuwa na mafuta mengi ambayo huchangia balance mbaya ya vichocheo (testosterone hormones) lakini pia huchochea kuvimba kwa seli mbalimbali za mwili na tezi ikiwemo. 

  • Kutofanya mazoezi: Utafiti unaonesha watu ambao hawafanyi mazoezi mara kwa mara wanakuwa na hatari ya kupata tezi dume kwa asilimia 25%.   

  • Magonjwa ya kisukari na moyo nayo yameonesha kuongeza uwezekano wa kupata tezi dume.  

Pamoja na kuwepo Kwa visababishi kama hivyo hapo juu, bado utafiti unaendelea katika harakati za kubainisha sababu nyingine za tezi dume.  

  

Nitajuaje nina dalili za tezi dume?

Dalili nyingi za tezi dume hujionesha mapema katika mabadiliko ya mfumo wa mkojo ambazo huja kwa sababu ya tezi kukua na kuweka mkandamizo kwenye njia ya mkojo. 

Dalili hizi ni kama kupata ugumu kukojoa ambapo humlazimisha mtu kusukuma mkojo kwa nguvu ili kuweza kutoa mkojo na wakati mwingine mkojo hugoma kabisa kutoka na baadaye hutoka kwa muda wake usio maalum (urine incontinence).  

Pia wakati wa kukojoa mkojo hautoki Kwa nguvu kama kawaida bali huja kimakundi na mara nyingi mtu huishia kukojolea suruali hasa ule mkojo wa mwishoni kumalizia.  

Dalili zingine ni kama kupata mambukizi ya UTI mara kwa mara na kila muda kuhisi kama mkojo hauishi kwenye kibofu.  

Dalili hizi huwa ni za mwanzoni na huendelea kuongezeka nguvu kadiri muda unapoenda na mwisho wake huweza kusababisha hata mkojo kutotoka tena.  

Wakati mwingine unaweza kuwa na dalili kama hizo hapo juu lakini kila ukipima unakuta tezi yako iko size ya kawaida sio?

Hii huweza kusababishwa na wewe kuwa na maambukizi ya bakteria ya tezi. Tatizo hili huambatana na maumivu yanayokuwa katikati ya mfuko wa korodani na mkundu.  Hali hii inatibika kwa dawa za antibiotic baada ya kufanya kipimo cha kuotesha mkojo. 

Matibabu ya tezi dume ni yapi?

Tezi dume inatibiwa kulingana na hatua iliyofikia na namna ambavyo dalili zake zinaathiri ubora wa maisha ya mtu. 

1. Matibabu ya kwanza yanahusu matumizi ya dawa ambazo husaidia kupunguza ukubwa wa tezi na kusaidia mkojo kupita

Wagonjwa ambao bado tezi yao haijawa kubwa sana au ambao ndio kwanza wanapata dalili hizi na kipimo kimeonesha kwamba tezi yao imekuwa kubwa basi huanza na vidonge. 

Vidonge hivi pia vinakuwa na msaada sana hasa kwa wale ambao wana hali nyingine za kiafya ambazo haziwaruhusu kufanyiwa upasuaji kwa wakati huo. 

2. Ikitokea hadi matumizi ya vidonge hayana msaada basi njia ya mwisho ya matibabau ni upasuaji wa tezi dume.

Njia ya upasuaji hufanywa kwa kuondoa sehemu ya tezi ambayo inakandamiza njia ya mkojo huku sehemu ya nje ya tezi ikiachwa. Upasuaji huu huondoa kabisa changamoto hii ya kushindwa kukojoa vizuri.

Angalizo

Upasuaji wa tezi dume huweza kuambatana na changamoto kadhaa kama kuumiza kibofu cha mkojo, na pengine kupoteza uwezo wa kusimamisha uume, kutokwa na damu nyingi na kadhalika.

Madhara haya yapo, japo sio kwa kiwango kikubwa. Kwa maana hiyo unapopanga kufanyiwa upasuaji huu, hakikisha unafanyiwa katika hospitali yenye wataalamu wenye uzoefu na huduma hii.

Epuka kutafuta unafuu wa gharama na kuishia kufanyia mtaani upasuaji kama huu. 

Je! Tezi dume inazuilikaje?

Katika kuangalia visababishi vya tezi dume, kuna baadhi ya visababishi ambavyo ni ngumu kuvibadilisha mfano umri na vinasaba vya kijenetiki, lakini bado kuna njia kadhaa za kupunguza uwezekano wa kupata tezi dume.

Moja ni kuhaikiksha unakuwa na uzito wa kawaida. Uzito mkubwa umeonesha kuleta hatari ya watu wengi kupata tezi dume.

Pili, hakikisha unajikinga na magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo. Magonjwa haya yameonesha kuwa chanzo kikubwa cha tezi dume kwa walio wengi.

Tatu, jitahidi kuwa mtu wa mazoezi mara kwa mara. Tafiti zimeonesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara, hasa ya kukimbia na viungo, huweza kupunguza hatari ya kupata tezi dume kwa asilimia 25% na pia imeonekana kupunguza uwezekano wa upasuaji wa tezi dume kwa asilimia 25%.

Pia tafiti zimeonesha kujihusisha katika mazoezi ya kutembea walau saa 1 mpaka 3 kwa siku imeweza kupunguza athari ya kupata vimelea vya kansa ya tezi kwa asilimia 86%.

Angalizo

Pamoja na kufanya hivi vyote, bado watu wamekuwa wakipata tezi dume jambo ambalo bado linazidi kuhamasisha utafiti zaidi ili kujua vichochezi vingine. Hata hivo mitindo ya maisha kama kujihusisha kwenye mazoezi na kuwa na uzito wa kawaida kisayansi vimeonesha kupunguza tezi dume. 

Muhimu zaidi ni nini?

Ni vizuri kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa tezi (screening) ambao hufanywa mahospitalini. Uchunguzi huu huusisha vipimo vya homoni na kuangalia ukubwa wa tezi kwa kutumia kidole. 

Ufanyaji wa uchunguzi wa mara kwa mara huweza kuondoa uwezekano wa kupata madhara ya tezi kuwa kubwa na kansa ya tezi, pamoja na kupata huduma mapema iwezekanavyo. 

Matibabu yakianza mapema basi uwezekano wa kupona na kuepuka changamoto nyingine ni mkubwa. 

Kumbuka: Kuwa na tezi dume sio kihatarishi cha kupata kansa ya tezi (prostate cancer). Mambo haya mawili huwa na visababishi tofauti na hutokea katika maeneo tofauti ya tezi na havihusiani kabisa. 

Endelea kusoma makala zetu kuendelea kujifunza mambo mengi zaidi. Una mgonjwa mwenye changamoto ya maumivu ya muda mrefu kama mgongo, magoti na changamoto za uzee kama kushindwa kusimama, kushindwa kuchuchumaa chooni?

Tupigie simu kwenye namba +255 767 226 702 kwa ushauri na matibabu kwa kutumia vifaa tiba. 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

en_USEN