Bila shaka swali kama hili sio geni kwako au inawezekana na wewe ni muhanga wa changamoto hii. Unapambana nayo vipi? Au unaishi nayo tu kama kawaida?
Binafsi kama daktari nimekutana na wagonjwa wa namna hii mara kwa mara na nimekuwa nakijitahidi kutoa elimu ili kuhakikisha kila ninayekutana nae anapata msaada.
Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wanahisi UTI yao haiponi na inajirudia mara kwa mara basi usiache kusoma makala hii mpaka mwisho. Itakusaidia kupata njia sahihi ya kupita; njia namba tano itakushangaza.
Neno UTI ni kifupisho cha neno la kiingereza lijulikanalo kama Urinary Tract Infection, yaani maambukizi ya njia ya mkojo. Maambukizi haya, mara nyingi, husababishwa na bakteria mbalimbali ambao wanaweza kutoka katika mazingira tofauti tofauti.
Ikitokea wadudu wa bakteria wakaingia na kutawala eneo la njia ya mkojo basi mtu hupata dalili za maambukizi hayo ambazo zinahusisha kukojoa mara kwa mara, maumivu wakati au baada ya kukojoa, mkojo kuwasha au kuunguza wakati wa kukojoa, uchovu wa mwili, kichwa kuuma mara kwa mara na kadhalika.
Ugonjwa wa UTI hutibiwa na kupona ndani ya siku tano mpaka saba kama kama mtu amepata dawa na dozi sahihi.
Sasa inakuwaje umepimwa ukakutwa na UTI na ukapewa dawa lakini bado dalili ziko pale pale au kila ukirudi kupima haiishi? Zipo sababu kama tano na nitazielezea hapa;
1. Changamoto kwenye dawa
Katika swala la dawa, kuna mambo makubwa mawili tofauti. Kwanza, kuna watu hawapendi kumeza dawa hivyo wanapopewa dozi ya siku tano, wao hukwepa na kwenda pharmacy kununua dawa ya siku chache.
Mfano mtu atanunua Azuma ya siku tatu na kumeza, na kuhisi atapona. Bahati mbaya huishia kumeza dozi chache na hapo maambukizi hujikusanya tena na baada ya wiki mbili mtu huyu hurudi hospitali na kulalamika hajapona.
Pili, inawezekana umepewa dawa lakini haina nguvu ya kutibu maambukizi uliyonayo, lakini wewe umeinunua kutokana na mambo ya kiuchumi au kukariri dawa na matokeo yake haikusaidii.
Mfano, Amoxicillin ni dawa ya bei rahisi lakini haitibu UTI kwa ufasaha. Cha kushangaza watu wengi wakisikia dalili za mkojo kuuma au kuwasha, au kuwa mzito huwa wanaenda moja kwa moja pharmacy na kununua Amoxicillin au Fragyl na kumeza na matokeo yake hawaponi UTI na huumwa tena ndani ya muda mfupi.
Hakikisha dawa unayomeza imeandikwa na daktari baada ya vipimo fasaha au amekushaurisha hivyo baada ya kusikia dalili zako, na hakikisha unamaliza dozi yako ya dawa.
Kama dawa ulizopewa ni nyingi, unaweza kushauriana na daktari akakupa machaguo mengine kama sindano, ila sio kuchukua maamuzi mkononi.
Katika ripoti ya mwaka 2020 iliyotolewa na Shirika la Afya duniani (WHO), moja ya changamoto kubwa ambayo inafanya ugonjwa huu uendelee kuwa tishio imeonekana kuwa usugu wa dawa za antibiotics zinazotibu ugonjwa huu.
Hivyo inawezekana pia ukawa na usugu wa dawa, ndio maana ni muhimu kufanya vipimo kwa ufasaha.
2. Kutibu kitu ambacho sio
Sio kila kitu kinachowasha kwenye sehemu za siri ni UTI. Pengine ni maambukizi ya fangasi au kaswende ila wewe hukufanya vipimo, ulikimbilia kumeza dawa kutoka pharmacy.
Kutokana na kutokuwa na elimu sahihi ya UTI, asilimia kubwa ya watu hulalamika UTI yao haiishi kumbe wakimaanisha maambukizi mengine ambayo pengine hayajatibiwa kwa ufasaha.
Changamoto kama fangasi wa uke, bakteria vaginosis, pelvic inflammatory diseases (PID) kwa wanawake au kaswende huja pamoja na utoaji uchafu sehemu za siri na huitaji aina maalumu ya matibabu ambayo huwa hujayapata kutokana na kutoenda hospitali au kwenda kwenye vituo vya afya vyenye hadhi ndogo ambapo shida yako halisi haijamulikwa vizuri.
Hali hii husababisha kuambiwa wana UTI na kutibiwa kwa dawa za kawaida kumbe wana magonjwa ya zinaa na kadhalika.
Kabla hujajibatiza kwamba una UTI sugu isiyopona hakikisha umefanyiwa vipimo stahiki vya mkojo na kuthibitisha hilo.
Kuna aina ya bakteria huwa wanahitaji kuotesha mkojo kujua ni bakteria gani na vyote hivyo hufanywa katika hospitali kubwa, epuka kujitibu kwa uelewa wako.
Mfano, leo umefanya mapenzi bila kinga halafu kesho mkojo unauma na kuna uchafu unatoka; hii sio UTI, ni ugonjwa wa zinaa. Matibabu yake pia sio ya kawaida, yana dawa zake maalaumu.
Sasa kwasababu ya kukosa uelewa, mtu ataenda pharmacy kuulizia dawa yoyote ya UTI, mfano Amoxiclav, ataanza kujitibu kwa siku tano na mwisho wa siku atajikuta hali ishakua mbaya hivyo atahitaji tiba ya muda mrefu kwa kumeza vidonge vingi ambavyo wengi huwa hawavimalizi.
Matokeo yake? Ugonjwa ambao ungetibiwa ndani ya siku moja unageuka kuwa hadithi ya muda mrefu.
Ndio utamkuta anasema mimi nina UTI sugu kumbe ni ugonjwa wa zinaa uliochukuliwa na kutibiwa kama UTI.
3. Umetibiwa na mwenza wako?
Moja kati ya falsafa muhimu ya kutibiwa na kupona maambukizi ya njia ya mkojo, ambayo hata Wizara ya Afya huisisitiza, ni kuhakikisha mwenza wako naye amepima na kutibiwa kama ana maambukizi.
Hii haimaanishi kwamba UTI ni ugonjwa wa zinaa, bali kutokana na ninyi kuchangia vitu vingi kama bafu, taulo, na dodoki, ni rahisi bakteria kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine na kusababisha wewe kupata UTI.
Hivyo hakikisha kama unaishi na mwenza wako ukitibiwa UTI naye apime na kumeza dawa na kufanya hivi imekuwa na msaada sana kwenye kukaa muda mrefu bila kupata tena maambukizi ya UTI.
Bahati mbaya wenza, hasa wanaume, huwa ni wabishi kutoa ushirikiano na hivyo hufanya changamoto hii kuendelea kwa muda mrefu. Lakini kwakuwa umesoma hii makala, bila shaka utaanza kutilia uzito ushauri huu.
4. Unajisafishaje?
Katika jamii nyingi za kitanzania imezoeleka kwamba kutumia vyoo vya public (kuchangia vyoo vya watu wengi) ndio sababu kubwa ya kupata maambukizi ya UTI na huu umekuwa wimbo wa taifa hasa kwa wanawake wengi.
Lakini nikuulize swali, mbona kuna watu wanakaa nyumbani, hawafanyi kazi maofisini, wanatumia choo chao cha ndani (hawachangii na mtu) na bado wanapata UTI?
Tatizo kubwa sio tu kuchangia vyoo, tatizo kubwa ni namna ya kujisafisha.
Wizara ya Afya pamoja na Shirika la Afya duniani wamekuwa mstari wa mbele kuelekeza hasa kwenye miongozo namna ya kujisafisha hasa baada ya kujisaidia haja kubwa.
Mwaka 2020 Shirika la Afya duniani lilitoa report yake iliyoonyesha kwamba zaidi asilimia 50 ya maambukizi ya UTI huwapata wanawake na hii inaweza kuonekana hata katika nchi yetu.
Chanzo kikubwa, kuachana na sababu zingine, ni makosa wakati wa kujisafisha hasa baada ya haja kubwa. Kama ulikuwa hujui , wadudu (bakteria) jamii ya E.coli ambao ndio husababisha sana UTI huwa wanapatikana katika haja kubwa na hivyo baada ya haja kubwa, usipojisafisha vizuri, una hatari kubwa ya kuwapata wadudu hawa na baadaye UTI.
Najisafishaje vizuri?
Njia bora ya kujisafisha ili kupunguza maambukizi ya UTI ni kujisafisha kuanzia sehemu ya haja kubwa kurudi nyuma, yaani kuanzia kwenye puru (mkundu) kuelekea nyuma kwenye mgongo na kurudia zoezi hilo mpaka pawe pasafi.
Kwa maana hiyo ukiwa umechuchumaa au umekaa chooni, kwenye kujitawaza mkono wako utokee nyuma na sio katikati ya mapaja. Mkono ukitokea nyuma inakuwa rahisi kujisafisha kwa kuvutia/kuelekea nyuma, uelekeo wa uti wa mgongo.
Epuka kujisafisha kwa kuelekea mbele, hapa ndipo makosa yanafanyika. Njia hii ya kujisafisha ni kwa wote wanaume na wanawake. Epuka kugusa uke au uume baada ya kugusa haja kubwa.
Changamoto huja pale ukiwa unatumia maji kujitawaza, maana yake kama kinyesi ni kingi utahitaji kutumia maji mengi na inawezekana kiasi kadhaa cha maji kikatiririka kuja kwenye uke.
Kukabiliana na hili, nchi zilizoendelea wao husisitiza kutumia zaidi toilet paper kuliko maji. Ukitumia toilet paper sio rahisi kinyesi kuingia kwenye sehemu ya mbele na unajisafisha mara nyingi uwezavyo mpaka pawe pasafi.
Inawezekana hii ikawa sababau kwanini nchi nyingi zilizoendelea au wanaotumia hii njia ya toilet paper wakawa na maambukizi kidogo sana ya UTI? Binafsi bado naendelea kutafakari na kufanya uchunguzi zaidi.
Ulishawahi Kuwasikia Wadamara?
Jamii ya Wadamara nchini Namibia wantumia vyoo vya kukaa, iwe mjini au kijijini. Cha kushangaza hawanaga UTI.
Kama daktari sikumbuki ni mara ngapi nilitibu UTI katika mkoa ule. Kiufupi huu ugonjwa kwao wanaupata sana wazee, wajawazito na wagonjwa wa muda mrefu.
Utofauti wao na sisi ni kwamba wanatumia toilet paper kujitawaza na sio maji. Bado naendelea kufanya uchunguzi zaidi kujua kilichopo kwenye utofauti wa matumizi ya maji na toilet paper.
Kwakuwa maisha ni kujaribu, kama unapata UTI mara nyingi, unaweza kujaribu kutumia toilet paper lakini kwa kufuata utaratibu sahihi wa kujitawaza kama nilivyo fafanua hapo juu halafu uone itakavyokuwa.
Kwa kutumia toilet paper unasafisha mpaka uone hamna kitu kwenye ile karatasi nyepesi, hapo unajua uko msafi.
Sikuhizi kuna vyoo vya kisasa vinavyotumia maji ya presha ya kujitawaza. Una hakika ile presha haifanyi maji kutiririka mpaka ukeni? Pia kwa wanaume, una uhakika yale maji hayaendi kugusa uume wako? Nadhani ni swala la kufatilia zaidi.
Kwa ufanisi zaidi unaweza kuwa na toilet paper chooni. Ukimaliza kijisaidia unapangusa kwanza na toilet paper, pakiwa pasafi unapitisha maji kiasi kwa ajili ya kuwa msafi zaidi kwa kufuata utaratibu uleule wa kuanzia pale kurudi nyuma na baadaye pitisha tena toilet paper kwa ajili ya kuleta ukavu katika sehemu ile.
Kwa maelezo au kujifunza zaidi unaweza kutembelea YouTube kujionea kwa vitendo.
Mwanaume pia anapaswa kusafisha uume wake baada ya kukojoa?
Ndio! Baada ya kukojoa, ni vizuri kukausha uume wako kwa toilet paper pale ambapo mkojo hutokea, au kusafisha kwa maji kuanzia mbele kurudi nyuma walau mara moja.
Pia hakikisha baada ya kukojoa, unatikisa uume wako vizuri kuhakikisha hakuna mkojo unaobaki kwenye njia ya mkojo. Kubaki kwa mkojo huu huweza kutengeneza mazingira ya bakteria wa UTI.
Kwa ujumla, usipokuwa na usafi wako binafsi unaozuia maambukizi ya bakteria kwenye nyeti zako basi wewe UTI itakuwa rafiki wako.
5. Unakunywa maji ya kutosha?
Kama wewe sio msafi sana kimazingira lakini unakunywa maji mara kwa mara na kukojoa mara kwa mara, nina habari njema kwako: Una asilimia kubwa ya kutopata maambukizi ya UTI!
Binafsi toka nilipoanza tabia ya kunywa maji asubuhi, mchana na jioni, mambo ya UTI kwangu imekuwa historia kabisa.
Ukinywa maji mengi mara kwa mara, mkojo unakuwa mwingi na ukikojoa walau mara nne kwa siku unakuwa unasafisha njia ya mkojo mara kwa mara na hivyo hutoi nafasi kwa mkojo kubaki katika njia na kuwa chanzo cha wadudu wa UTI kuzaliana na kusababisha maambukizi.
Maji hapa hayawi kama tiba ya UTI bali ni kinga dhidi ya mazingira ya kupata UTI na ukizoea mtindo huu basi UTI itakaa mbali na wewe.
Nikuibie siri
Wakati nasomea udaktari, kuna mambo mawili niliyaelewa sana darasani na nikabahatika kuyafanyia majaribio, na kweli yamekuwa nguzo sana katika maisha yangu ya kila siku.
Mojawapo ni kunywa maji ya kutosha kabla ya kufanya tendo la ndoa. Logic yake ni kwamba, mara tu unapomaliza tendo utakuta mkojo umekubana na kwakuwa umekunywa maji mengi mkojo huwa mwingi.
Sasa ukienda kukojoa pale tu baada ya tendo, unakuwa unasafisha vizuri njia yako ya mkojo kiasi kwamba kama kulikuwa na wadudu ambao umewakomba wakati wa tendo basi hatari yako ya kupata UTI huwa inapungua.
Ni moja ya njia ya kupunguza UTI hasa kwa wale wanaoishi na wenza wao.
Angalizo:
Maji sio tiba ya UTI hasa ukiwa umeshapata maambukizi ila yanaweza kuharakisha kupona kwa kusaidia kuondoa wadudu nje ya kibofu na njia ya mkojo.
Maji ni kinga ya UTI kwa maana ya kwamba ukiwa unakunywa maji ya kutosha na unakojoa mara kwa mara kwa siku, UTI haitakuzoea kabisa na utaisahau.
Mwisho
Kama hatua zote hapo juu hazina shida kwako na bado unaona UTI haiponi, inawezekana ukawa na changamoto nyingine ambazo zinahitaji utafiti zaidi.
Mfano, kama ni mwanaume unaweza kuhitaji uchunguzi wa tezi dume, figo, kibofu na njia ya mkojo kwa ujumla na vipimo vingine muhimu kama sukari na kinga ya mwili.
Kwa mwanamke, unaweza kuhitaji kufanya ultrasound kujua hali ya mirija yako, mlango wa uzazi na kizazi chako kwa ujumla.
UTI haipaswi kuwa sugu na mara nyingi hasa vijijini ukiskia UTI sugu inawezekana ikawa ni magonjwa ya zinaa ambayo hayajawahi kutibiwa au yanatibiwa kama UTI.
Ni vizuri kwenda kwenye hospitali kubwa ili ufanyiwe vipimo kuliko kumeza madawa mengi, tena ya kienyeji.
Kumbuka namna pekee ya kujilinda na kulinda afya yako sio tu kuwa na bima ya afya, bali kuwa na elimu ya kuepuka magonjwa.
Endelea kusoma makala nyingine za Abite Afya kupitia hapa.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
