Habari yako? Leo tutajifunza jambo jipya, lenye ukakasi kidogo, kuhusu afya yako ya kinywa: Athari za ngono ya mdomo kwenye kinywa.
Ingawa mada hii, mara nyingi, huepukwa kujadiliwa kwa uwazi katika mazungumzo ya umma au hata kikawaida kati ya marafiki na hata wapenzi, ni muhimu kuijadili kwa ukweli na heshima.
Kuelewa hatari zinazoweza kutokea na hatua za kujikinga ni muhimu kwa kudumisha afya na ustawi kwa ujumla.
Maana
Ngono ya mdomo inahusisha kusisimua viungo vya uzazi kwa kutumia mdomo, midomo, au ulimi.
Ingawa ni tabia ya kawaida kati ya wapenzi, ni muhimu kutambua kwamba inaweza kuwa na athari chanya na hasi kwa afya ya kinywa chako ikiwa afya ya mpenzi wako haiko sawa.
Hebu tuangalie vipengele mbalimbali na athari zake.
Maambukizi yanayohusiana na ngono ya mdomo
1. Magonjwa ya zinaa (STIs)
Mojawapo ya wasiwasi mkubwa ni maambukizi ya Human Papillomavirus yaani HPV. Baadhi ya aina za HPV zinahusishwa na saratani za koo (oropharyngeal carcinoma) zinazoathiri nyuma ya koo, msingi wa ulimi, na tonsili zako.
Virusi hivi hupatikani katika sehemu za siri (aidha mwanamke au mwanaume) na husambazwa kwa njia ya ngono.
Virusi huhama kutoka sehemu za siri za muathirika wakati wa ngono ya mdomo na kumuingia mwenza wake.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kiwango cha saratani za koo zinazohusiana na HPV kimekuwa kikiongezeka kila mwaka. Hivyo kuna hatari ya mtu kupata saratani hii kwa kufanya ngono kupitia mdomo.
Si kila mtu anayefanya hivi hupata saratani, lakini ni vyema kutambua kuwa ni jambo ambalo lipo.
Matumizi ya mdomo kufanya ngono pia yanaweza kusababisha maambukizi ya Herpes Simplex Virus (HSV-1) – ambayo kawaida husababisha vidonda vya mdomo; na HSV-2 – ambayo kawaida husababisha vidonda vya sehemu za siri.
HSV-1 huambukizwa kupitia kinywa na HSV-2 kupitia ngono. Pata picha sasa huo mchanganyiko utakao tokea hapo wa virusi!
Kitendo hichi, kwenye sehemu za siri, hubadilisha biolojia ya sehemu ya siri ya mwanamke kwa kiasi kikubwa na kupelekea maambukizi kirahisi ya vijidudu wengine.
Kama ni wewe unayetenda ngono ya mdomo inawezekana unabeba HSV-2 kutoka kwenye sehemu za siri za mwenza wako au unapeleka HSV-1 kwa mwenza wako.
Virusi vya HSV-2 husababisha vidonda na majipu yenye maumivu kwenye kinywa.
Kupitia ngono ya mdomo unaweza kupata pia maambukizi ya bakteria wa ugonjwa wa kisonono au klamidia (gonorrhea and chlamydia) kutoka kwenye sehemu za siri za mwenza wako ambae ana maambukizi hayo, aidha mwanamke au mwanaume.
Bakteria hawa hutoka sehemu za siri za mwenza wako na kuingia kinywani mwako kupitia ngono ya mdomo. Inaweza kuathiri koo na kusababisha dalili kama vile koo kuuma, uwekundu, na uvimbe.
Mara nyingi maambukizi haya hayana dalili, hivyo ni rahisi kupuuzia maambukizi na hivyo kujikuta unaishi na ugonjwa huu kwa muda mrefu.
Pia maambukizi ya kaswende yaani syphilis yanaweza kukupata kupitia ngono ya mdomo, pale ambapo mwenza wako anakusisimua kupitia mdomo au ulimi wake.
Dalili za maambukizi haya kinywani huonekana kama vidonda au vidonda kwenye kinywa chako na koo. Ikiwa haitatibiwa, maambukizi ya kaswende yanaweza kusababisha matatizo makubwa kiafya.
2. Homa ya ini au kitaalamu tunaiita Hepatitis
Virusi vya Hepatitis B na C ni virusi ambavyo husambazwa mara nyingi kupitia ngono, pale ambapo kunakuwa na kujaamiana na mabadilishano ya maji maji katika sehemu za siri haina ya wapenzi.
Virusi hivi vinaweza kuambukizwa kupitia ngono ya mdomo pia, hasa ikiwa kuna mikato au vidonda kwenye mdomo au fizi zinavuja damu.
Utajuaje umepata maambukizi ya ngono ya domo?
Dalili mbalimbali za maambukizi ya ngono ya mdomo huwa ni tofauti na hutofautiana kati ya mtu na mtu. Kuwa na ufahamu wa dalili za maambukizi haya ni muhimu. Dalili hizi ni kama vile:
- Koo kuuma kwa muda mrefu au maumivu wakati wa kumeza.
- Kuonekana kwa vidonda visivyo vya kawaida, majipu, au malengelenge kwenye mdomo.
- Uwekundu na uvimbe kwenye koo au mdomo.
- Harufu mbaya ya pumzi au ladha isiyo ya kawaida inayodumu.
- Kuvimba kwa tezi za shingoni; huuma wakati wa kumeza au ukizishika.
Hatua za kujikinga
1. Mawasiliano na ridhaa
Ni vyema kuwa na mawasiliano mazuri ya ukweli, uwazi na yenye uaminifu kati yako na mpenzi wako kuhusu afya zenu za ngono; na historia zenu ni muhimu sana. Ridhaa na makubaliano ya pamoja ni msingi wa mazoea salama ya ngono.
2. Matumizi ya kinga
Kutumia kondomu wakati wa ngono ya mdomo kunaweza kupunguza sana hatari ya kuambukizwa magonjwa. Vizuizi hivi hufanya kazi kama safu ya kinga, kuzuia mawasiliano ya moja kwa moja na majimaji ya mwili.
3. Kupata chanjo
- Chanjo ya HPV ina ufanisi mkubwa katika kuzuia maambukizi kutoka kwa aina za HPV zinazohusiana na saratani za koo. Inapendekezwa kwa wanaume na wanawake, ikiwezekana kabla hawajaanza kufanya ngono.
- Chanjo ya Hepatitis B ni sehemu ya ratiba za kawaida za chanjo, lakini watu walio katika hatari kubwa wanapaswa kuhakikisha wamepata chanjo hii.
4. Desturi ya ukaguzi wa afya
Ukaguzi wa kawaida wa kinywa na afya ya mwili unaweza kusaidia katika kugundua mapema na kutibu maambukizi yoyote yanayoweza kutokea.
Madaktari wa meno mara nyingi wanaweza kuona dalili za maambukizi ambayo yanaweza kupuuzwa.
5. Kuhakikisha usafi wa mdomo
Kudumisha usafi mzuri wa mdomo ni muhimu. Kupiga mswaki mara mbili kwa siku, kutumia uzi wa meno (dental floss), na dawa ya kusafisha meno kunaweza kupunguza hatari ya maambukizi.
6. Kama humwamini mpenzi wako basi kuepuka ngono ya mdomo wakati una mikato, vidonda, au fizi zinavuja damu ni hatua nzuri ya kujikinga na athari zinazoweza kutokana na mazoea haya.
7. Kuwa na uhusiano wa kudumu
Wakati wanandoa wanapokuwa waaminifu kwa wenzi wao, hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa inapungua sana. Uaminifu na kujitoa kwa mpenzi mmoja kunasaidia katika kudumisha afya njema.
Baadhi ya dhana potofu
Dhana Potofu: Ngono ya mdomo ni salama kabisa na haiwezi kusababisha maambukizi ya zinaa.
Ukweli: Ingawa ngono ya mdomo inachukuliwa kuwa na hatari ndogo ikilinganishwa na aina nyingine za ngono, bado inaweza kusababisha maambukizi ya aina mbalimbali za magonjwa ya zinaa.
Dhana Potofu: Watu walio kwenye mahusiano mengi ya kimapenzi ndo ambao wako katika hatari.
Ukweli: Magonjwa ya zinaa yanaweza kumuathiri mtu yeyote anayefanya ngono, bila kujali idadi ya wapenzi walio nao. Mazoea salama ni muhimu kwa kila mtu.
Lakini kupitia kazi za watu kama madaktari au manesi, wao wanaweza kupata maambukizi kupitia utoaji wa huduma kwa wagonjwa mbalimbali wanaokutana nao hospitalini.
Aidha maambukizi haya yanaweza kutokea kupitia kujichoma na sindano iliyomchoma mgonjwa mwenye maambukizi.
Hata wale wanaojidunga madawa ya kulevya kupitia sindano wanazoshirikiana, wapo katika hatari ya kujisambazia maambukizi pia.
Ni muhimu kuendeleza mazingira ambapo watu wanajisikia huru kujadili afya ya ngono. Elimu na ufahamu vinaweza kuwawezesha watu kufanya maamuzi sahihi. Kuelewa athari za ngono ya mdomo kwa afya ya mdomo ni muhimu kwa kudumisha ustawi wa jumla.
Hivyo basi, kwakuwa wewe umesoma makala hii na umepata ufahamu huu, tufanye kazi pamoja kukuza uelewa na afya katika nyanja zote za maisha yetu hata afya zetu ya kinywa.

“For the love of words”
asante sana daktari kwa elimu ya kina na ya wazi. Ukweli umefafanua vema mambo ya msingi sana. Endelea kutuelimisha