Chronic Headache: Maumivu Sugu ya Kichwa Yanayopoteza Ladha ya Maisha

“Kichwa changu kikianza kuniuma huwa natamani kufa…nipumzike na hii taabu!”

Ulishawahi kusikia kauli kama hiyo?  Embu jaribu kufikiria mpaka mtu anafikia kusema hivyo, anapitia mateso kiasi gani?

 

 

Maumivu ya kichwa ya muda mrefu (chronic headache) ni moja ya janga kubwa unaloweza kukutana nalo katika maisha yako; pia ni moja kati ya matatizo yanayowaleta watu wengi hospitali mara kwa mara.

Shirika la Afya Duniani WHO limeelezea chronic headache kama maumivu ya muda mrefu ya kichwa ambayo hutokea walau zaidi ya mara 15 (15 episodes) kwa mwezi kwa zaidi ya miezi mitatu na kuendelea.

Una maumivu sugu ya kichwa? Hauko peke yako! Utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2021, ulibaini kwamba tatizo hili linaathiri asilimia 40 ya watu duniani, sawa na watu Billion 3.1!

 

Baadhi ya madhara ya maumivu sugu ya kichwa ni kama kupoteza ladha ya maisha, kupata msongo wa mawazo, kuwaza kujiua, hali ngumu ya kiuchumi kwa familia na kuathiri utendaji wa kazi.

 

Utajuaje maumivu yako ya kichwa ni sugu?

  • Kuumwa na kichwa mara kwa mara, muda wowote na bila sababu yoyote: Maumivu ya kawaida ya kichwa huwa na sababu mfano, ukiwa na UTI, Malaria, mafua, au uchovu kichwa kitauma na ukitibu hayo mambo kichwa hupona.

 

Ila maumivu sugu huja bila Dalili au sababu nyingine yoyote kati ya hizo hapo juu, na huja mara kwa mara na muda wowote.

 

  • Maumivu ya kichwa endelevu zaidi ya miezi mitatu, kila mwezi zaidi ya mara 15, pamoja na kumeza dawa za maumivu.

 

  • Kama unapata maumivu ya kichwa ambayo ni sawa na anayopata ndugu yako wa karibu – kama Mama, Baba, Mjomba au Shangazi – inawezekana ni maumivu Sugu ambayo yako katika vinasaba vya familia.

 

Kwanini maumivu ya kichwa yanakuwa sugu?

“Kushindwa kujua kisababishi”

Hii ni moja ya sababu kubwa kwanini unaweza kuumwa na kichwa muda mrefu na kikageuka kuwa sugu.

 

Mara nyingi tunapoumwa na kichwa huwa tunakimbilia kumeza dawa za maumivu tu na kukituliza kwa muda bila kujua nini hasa sababu ya kichwa hiki.

 

Baadhi ya maumivu ya kichwa yanatibiwa pale tu unapojua kisababishi chake. Kichwa ambacho kinakuja mara kwa mara, muda wowote, maana yake kuna sababu nyuma yake. Hivyo usipotafuta sababu hiyo basi unaweza kuumwa kwa muda mrefu sana.

 

Mfano, kichwa kinachosababishwa na ‘presha kupanda’ kitapona pale tu utakaposhusha presha yako na sio kwa Panadol.

 

Kichwa kinachosababishwa na uvimbe kichwani kitapona pale tu uvimbe utakapotibiwa au kuondolewa, na sio kwa kumeza Panado!

 

Kichwa kinachosababishwa na macho kitaendelea kukutembelea mpaka utakapotibu macho yako.

 

Lakini kuna baadhi ya maumivu sugu ya kichwa, chanzo chake bado hakijulikani mpaka sasa hivyo kuwa miongoni mwa maumivu sugu kama tutakavyoona mbeleni.

 

Kuna aina ngapi za maumivu sugu ya kichwa?

Maumivu sugu ya kichwa yako katika makundi mawili ambayo ni primary chronic headaches na secondary chronic headaches.

 

1. Primary chronic headaches

Maumivu ya kichwa ya kundi hili huwa visababishi vyake havijulikani. Chanzo chake husemekana kutokana na mvurugiko wa kemikali za kinurologia na huwa ni ngumu kutibika.

 

Sifa yake mara nyingi huja na kukaa muda fulani halafu hutoweka na kuja tena baada ya muda fulani. Aina hizi za maumivu ya kichwa huwa zipo nyingi ila nitakutajia tatu tu ambazo ndizo huwaathiri watu wengi duniani.

 

I: Migraine

Hii ni mojawapo ya aina ya maumivu ya kichwa ambayo ni kawaida sana kwa watu wengi. Bahati mbaya huchukua muda mrefu kwa watu kujua kwamba wana migraine kutokana na kutotambua dalili zake mapema na hivyo kuendelea kupata taabu ya kichwa kwa muda mrefu.

 

 

Utajuaje maumivu yako ya kichwa ni Migraine?

  • Kichwa kupiga upande mmoja au pande zote mbili. Aina ya maumivu yake ni ya kupiga kama nyundo (Pounding pain), huweza kuwa ya wastani au makali sana.
  • Zaidi migraine huambatana na kichefuchefu, kutapika au kukwepa mwanga (Photophobia).
  • Kabla ya Migraine kuanza, unaweza kuanza kujiskia kizunguzungu, kuona maluweluwe (nyota), kichefuchefu na baadaye kichwa huanza kuuma.

 

Kama unapatwa na kichwa cha namna hii basi inawezekana una migraine. Migraine inaweza kukaa walau mpaka masaa 72 baada ya kuanza.

 

Migraine huweza kutibuliwa (Triggers) na mambo mbali mbali mfano pombe, sigara, stress, kuangalia TV muda mrefu, matumizi ya caffeine na kadhalika.

 

II: Tension headache

Aina hii ya maumivu ya kichwa huweza kuja na maumivu ya kati au makali sana.

Huathiri pande zote za kichwa. Pia maumivu yake ni ya kukandamiza (pressing or squizing), sio kuponda kama migraines.

 

 

Aina hii ya kichwa inaweza kutibuliwa na mambo mbali mbali kama msongo wa mawazo, hofu, kutolala usiku, uchovu wa kazi na matumizi ya vilevi.

Kama kichwa chako ni cha aina hii, basi wewe una tension headache.

 

III: Cluster headache

Maumivu ya kichwa ya namna hii huwa yanashambulia upande mmoja wa kichwa, huathiri mpaka upande wa jicho moja na mara nyingi yanaweza kusikika nyuma ya jicho.

 

 

Huambatana na kuvimba kwa upande husika pamoja na kuwa mwekundu, kutoa machozi, makamasi puani n.k. Maumivu haya mara nyingi huja ghafla bila taarifa yoyote, japo wakati mwingine huweza kuambatana na kichefuchefu au kutapika.

 

Huwa na tabia ya kuja katika kipindi fulani cha msimu. Huweza kuchukua walau dakika 15 na kuacha halafu hurudi tena. Huwa na muendelezo wa mara kwa mara na yanaweza kukaa wiki mpaka miezi.

 

Kichwa cha namna hii huweza kuamshwa na vitu kama pombe na sigara. Watu wanaopatwa na aina hii ya kichwa mara nyingi huwa ni wavutaji sigara.

 

Maumivu ya kichwa ya aina hizo tatu ndio hutokea mara kwa mara na ndio chanzo cha maumivu sugu ya kichwa.

 

Kwakuwa chanzo cha maumivu ya kichwa hapo juu huwa hakijulikani basi hufanya hali hizo kuwa hazitibiki zaidi ya kutumia dawa za kutuliza maumivu. Hivyo ukiwa na aina hizi za maumivu ya kichwa, utahitaji kuwa na msaada endelevu wa daktari kwa ajili ya ushauri na muongozo.

 

Unaweza kujiunga na huduma yetu ya daktari kiganjani kwa ajili ya huduma endelevu.

 

2. Secondary headaches

Aina hizi za maumivu ya kichwa hutokea kwa sababu maalumu katika mwili wako. Na ndio maana usipogundua chanzo, basi aina hii ya maumivu ya kichwa huweza kukaa muda mrefu na kuwa kikwazo kwenye harakatI zako za kila siku. Baadhi ya mifano yake ni kama:

 

  • Hypertension headache: Hiki ni kichwa ambacho huja kwa sababu ya presha kuwa juu. Ukimeza dawa zako na presha ikashuka, basi kichwa hiki hupona.

 

Inaweza kuwa dalili pekee ya Presha. Aina hii ya kichwa huathiri watu wengi kuanzia umri wa miaka 35 na kuendelea. Matibabu yake ni kuhakikisha Presha yako iko katika hali ya kawaida.

 

  • Eye strain headache: Aina hii ya kichwa huwapata watu wenye shida ya macho. Na kwakuwa mtu anaweza asijue, anaweza kuumwa kichwa mara kwa mara kwa muda mrefu mpaka tu pale atakapopima macho yake na kupatiwa dawa au miwani.

 

  • Tumor headache: Aina hii ya kichwa huweza kusababishwa na uvimbe kichwani. Inaweza kuwa dalili ya kwanza ya uvimbe kichwani.

 

 

  • Post trauma headache: Baada ya kupata ajali ya kichwa, muathirika anaweza kuanza kupata maumivu ya muda mrefu ya kichwa.

 

  • Stress headache: Aina hii ya maumivu ya kichwa huwapata watu wanaoishi au kufanya kazi katika mazingira yanayoleta mzunguko wa mawazo wa mara kwa mara. Na wakibaki katika mazingira haya, basi maumivu yao ya kichwa huendelea na kuwa sugu.

 

Maana ya secondary headaches ni kwamba maumivu ya kichwa yana sababu. Hivyo namna pekee ya kutibu maumivu haya ni kuondoa au kutibu visababishi na sio maumivu tu. Kutotambua visababishi ndio sababu hufanya aina hii ya maumivu kuwa sugu.

 

Unatakiwa kufanyaje?

Vita yako ya kwanza katika hili iwe ni kupambana kufahamu wewe una aina gani ya maumivu ya kichwa.

 

Hii inaweza kuhusisha kuongea na Daktari pamoja na kufanya vipimo mbalimbali vya kugundua chanzo cha maumivu yako ya kichwa.

 

Kwa kukusikiliza tu na kuchukua maelezo ya kutosha, Daktari anaweza kugundua aina ya maumivu ya kichwa uliyonayo na kukushauri matibabu au vipimo vya kufanya.

 

Katika hali Isiyo ya kawaida, kumekuwa na kuchanganya matibabu ya maumivu ya kichwa.

Mfano: Mtu mwenye migrane kutibiwa kama tension headache au mtu mwenye hypertension headache kutibiwa kama stress headache.

 

Epuka matumizi ya muda mrefu ya dawa za maumivu bila kufahamu chanzo cha maumivu yako. Matumizi ya dawa za maumivu kiholela, kwa muda mrefu, huweza kupelekea maumivu kuzidi na kutosikia dawa tena.

 

Jenga tabia ya kuwa na daktari wako wa kukushauri kuhusu afya yako binafsi na ya familia yako. Abite Nyumbani tuna huduma ya Daktari Kiganjani ambayo itakusaidia kuwa na daktari binafsi atakayekushauri mambo mbalimbali kuhusu shida uliyonayo, dawa ya kumeza, vipimo vya kufanya pamoja na wapi uende kupata tiba ya uhakika.

 

Jiunge na huduma yetu kupata ushauri fasaha wa afya yako na familia yako. Kumbuka ushauri wa mapema utakupunguzia changamoto ya kumeza dawa au kwenda hospitali bila sababu.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW