Vyakula Vinavyoongeza Maziwa ya Mama Baada ya Kujifungua

Je, umeshajifungua na maziwa hayotoki mengi? Leo nitakuelekeza namna ya kufanya ili ikusaidie wewe mama unayenyonyesha kupata maziwa ya kutosha kwa ajili ya mtoto wako na pia ni namna gani unapaswa kumnyonyesha mtoto wako ili aongezeke uzito.

 

Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na UNICEF wanapendekeza kuwa mama anapojifungua anapaswa kumnyonyesha mtoto ndani ya lisaa limoja baada ya kujifungua na kwa kipindi cha miezi sita bila kumpa kitu chochote.

 

 

Nimeandika makala hii baada ya kukutana na mtoto wa mwezi mmoja ambaye hakua na muonekano wa mtoto wa mwezi mmoja! Alikua bado anaonekana kama amezaliwa siku mbili zilizopita.

 

Nikamuuliza huyo mama “mtoto wako ana uzito wa ngapi?” Akanijibu “kilo tatu”. Nilisikitika sana kwasababu mtoto yule hakuwa na maendeleo mazuri.

 

Alitakiwa aongezeke japo kilo moja baada ya mwezi ule wa mtoto kuzaliwa. Hii ni kwa sababu baada ya miezi mitatu, mtoto anapaswa kuwa na mara mbili ya uzito aliozaliwa nao.

 

Mtoto huyu alizaliwa na kilo tatu na bado akarudi mwezi unaofuata akiwa hajaongezeka uzito. Nilimshauri Mama huyu namna ya kula na jinsi ya kumnyonyesha mtoto wake ili aweze kuongezeka uzito.

 

Tuanze na wewe mama mpya…

Kwanza nikupe hongera kwa kujaliwa kupata mtoto au watoto wazuri.

Kipindi mama anapojifungua anapaswa kula vyakula vyenye virutubishi vingi zaidi ya kipindi kile ambacho mama huyu anakua mjamzito kwani kipindi hichi mwili huwa na shughuli ya kurudi katika hali ya kawaida. Kwa maana ya viungo vya uzazi kutakiwa kupona

 

Pia katika kipindi hichi mwili hutakiwa kutengeneza maziwa kwa ajili ya mtoto kwasababu kipindi cha ujauzito mtoto hupata chakula kupitia kondo la uzazi na mara baada ya kujifungua mtoto hutegemea kupata chakula kutoka katika titi la mama.

 

Tuangalie vyakula mbalimbali ambavyo mama aliyejifungua anapaswa kula pale tu anapojifungua ili kusaidia katika kuongeza maziwa.

1. Vyakula vilaini au vyenye asili ya kimiminika ambavyo vimamengenywa kwa urahisi na kufyonza virutubishi mwilini kiurahisi. Mfano wake ni uji au mtori (unaweza kuwa wa ndizi au wa viazi)

 

2. Vyakula vyenye asili ya protini kama vile nyama, samaki, kuku, dagaa, na vyakula vya protini kundi la pili ambalo huwa linatoka katika jamii ya mikunde kunde kama vile maharage, njegere, na choroko ambazo zinasaidia sana katika kuongeza kiasi cha protini na virutubisho vingine muhimu katika maziwa ya mama.

 

Vyakula hivi ndio sehemu pekee ambayo itakusaidia kupata maziwa yenye virutubisho vya kutosha kwa ajili ya ukuaji wa mtoto/watoto wako.

 

3. Mbegu za uwatu (fenugreek)

Machapisho mbalimbali ya kisayansi yameonyesha ushahidi kuwa mbegu za uwatu husaidia katika kuongeza kiwango cha maziwa. Mbegu hizi hupatikana masokoni kwa wauzaji kwa viungo vya chakula, na huuzwa kwa bei nafuu sana.

 

Unaweza kusaga mbegu hizi na ukawa unaweka unga wake kwenye maziwa, au chai na kunywa kama unavyounga sukari.

 

Njia nyingine ni kuchemsha kiasi kidogo cha mbegu hizi za uwatu na kunywa maji yake. Ongezeko hili la maziwa litasaidia pia kuongezeka kwa uzito kwa watoto na kupunguza hali za utapiamlo kwa watoto chini ya miezi sita.

 

Muhimu: Kunyonyesha mtoto wako katika vipindi maalum ambapo ni kila baada ya masaa mawili husaidia kupeleka ushawishi mzuri kataika ubongo wako kwa ajili ya kutengeneza maziwa ya mtoto kwasababu usipomnyonyesha mtoto wako kila baada ya masaa mawili, ubongo utakua haupati taarifa za uhitaji wa utengenezwaji wa maziwa hayo kwa ajili ya mtoto.

 

Kumbuka, kipindi hichi cha kunyonyesha unapaswa kula milo mitano mpaka sita kwa siku na sio kula milo mitatu tu kwasababu mwili huhitaji virutubisho kwa ajili ya shughuli za kila siku na utengenezwaji wa maziwa yaliyo na ubora kwa ajili ya mtoto.

 

Sayansi ya Kunyonyesha

Kuna elimu nyingi sana katika jamii zetu zinazohusu unyonyeshaji wa watoto walio chini ya miezi sita.

Katika pitapita zangu sehemu ninayofanyia kazi, nilikutana na mwanamke mmoja akimkazania mama anayenyonyesha na kumwambia amkamulie mtoto ziwa maana hapo mtoto anakua hanyonyi vya kutosha .

 

Nilisimama na kumuangalia mtoto nikagundua kuwa mtoto yule alikua ananyonya vizuri tu. Nikawapa elimu watu wale juu ya unyonyeshaji na wakaelewa.”

 

Nimeanza kwa kusema hivyo ili kukufahamisha wewe msomaji kwamba mtoto mchanga huwa anazaliwa na kitu ambacho kitaalamu kinaitwa reflexes, na mojawapo ya hizi reflexes ni kunyonya.

 

Hakuna mtoto anafundishwa jinsi ya kunyonya kwasababu anazaliwa akiwa anajua namna ya kunyonya; kama mtoto atakua hanyonyi basi inaonekana kuwa ni changamoto fulani na anakua anaangaliwa kwa ukaribu .

 

Hivyo mtoto hakamuliwi ziwa, anapaswa kuwekwa katika mkao wa kunyonyesha kwa kupakatwa na kunyonyeshwa kwa muda wa dakika 15 mpaka 20. Na ziwa moja moja .

 

Ziwa la kwanza linapoishiwa ziwa na kuonyesha kulegea ndipo mtoto anapopaswa kuhamishiwa ziwa la pili. Baada ya kumyonyeshwa mtoto anapaswa kuwekwa begani na atakapocheua ndipo hulazwa katika kitanda – kwa style ya ubavu au kwa tumbo.

 

Hii ni kwasababu watoto wakilazwa chali, mara baada ya kunyonyeshwa, huwa kwenye hatari ya kupaliwa kwani hawana uwezo wa kumeza mate kama watu wazima.

 

Vitu muhimu vya kuzingatia

1. Mtoto anapaswa kunyonyeshwa kila baada ya masaa mawili ambapo ni mara 8 mpaka 12 kwa siku (masaa 24). Na katika ziwa anapaswa kukaa dakika 15 mpaka 20.

2. Mtoto hapaswi kupewa chochote zaidi ya maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya maisha kwasababu maziwa ya mama yanakua na virutubishi vinavyomsaidia mtoto kukua.

 

Maziwa yana seli za kinga mwilini dhidi ya magonjwa mbalimbali, na pia yanakua na maji kwa ajili ya kukata kiu.

 

Mwisho

Mama ndio anashika usukani katika swala hili la unyonyeshaji kwasababu mama ndiye anahusika katika utengenezaji wa maziwa ya kutosha (na  yaliyo bora). Na hii itawezekana kama wewe, mama unayenyonyesha, unakula vizuri.

1 thought on “Vyakula Vinavyoongeza Maziwa ya Mama Baada ya Kujifungua”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW