Vyakula Bora kwa Wagonjwa wa Shinikizo la Juu la Damu (Presha)

Shinikizo la juu la damu ni hali ambayo inampata mtu pale presha ya mishipa yake ya damu inapokua kubwa kupitiliza.

 

Hali hii kama haitadhibitiwa inavyotakiwa inaweza kupelekea kupata matatizo mengine ya moyo kama vile kiharusi (stroke) na hata kusababisha kupoteza maisha.

 

 

Uelewa wa namna ya kula pindi unapogundulika una shinikizo la juu la damu ni muhimu sana hasa kwa sababu mabadiliko chanya katika ulaji ni sehemu kubwa ya matibabu ya hali hii.

 

Makala hii inagusa changamoto ambayo inapatikana katika maeneo mengi ya familia zetu kama watanzania na hata duniani. Shikizo la juu la damu sio kitu kigeni katika masikio yetu, na hasa katika familia zetu.

 

Hivyo basi huwa ninajaribu kuzungumza kwa ukaribu kidogo na wateja wangu nikifahamu kwa namna fulani jinsi wanavyojisikia hasa katika kufahamu ni vyakula gani wanapaswa kutumia, jinsi inavyopelekea uoga katika ulaji wa vyakula vingi.

 

Angalizo: Makala hii inalenga watu waliogundulika na shinikizo la juu la damu tu na hawana changamoto nyingine ya kiafya inayohusisha changamoto za kimetaboliki kama vile kisukari, changamoto za mfumo wa chakula na mengineyo yenye uhusiano na metaboliki.

 

Metaboliki ni nini hasa?

Hizi ni shughuli za kemikali katika seli za mwili zinazobadilisha chakula tunachokula kwenda kuwa nguvu ili kiweze kutumika katika shughuli mbalimbali ndani na nje ya mwili.

 

Kwa kusema hayo, tuingie moja kwa moja katika swala la namna unapaswa kula au vitu gani unapaswa kula kipndi unapokua na shinikizo la juu la damu.

 

Vyakula vya Moyo

Pindi unapogundulika na shinikizo la juu la damu unapaswa kuwa unatumia vyakula vyenye potasiamu nyingi na sodiamu kidogo kwani vyakula hivi ni vizuri sana kwa watu wenye changamoto ya shinikizo la juu la damu.

 

Mfano wa vyajula hivyo ni rojorojo ya ndizi. Rojorojo ya ndizi ina wingi wa potasiamu na magnesiamu na kwa kiasi kidogo sodiamu na hivyo basi ni chakula ambacho mtu mwenye shinikizo la damu anapaswa kutumia.

 

Potasiamu hii husaidia katika mfumo wa neva (nervous system) ambao ni mfumo wa mawasiliano mwilini na pia katika kazi za misuli ikiwemo misuli ya moyo katika kutanuka na kusinyaa katika vipindi vya kusukuma damu mwilini.

 

Hata hivyo potasiamu ni madini ambayo husaidia katika usambazaji wa viini-lishe vingine mwilini, yaani ndani ya seli kwa ajili ya matumizi ya mwili na pia utoaji wa taka/mabaki nje ya seli baada ya matumizi ya viini-lishe kumalizika.

Dondoo muhimu: Seli huwa na tabia ya kula kama vile sisi binaadamu tunavyokula mfano, kama mtu akiwa anakula samaki ndivyo hivyo seli zinakua zinatumia viinilishe na pindi mtu anayemla samaki yule akikutana na miiba huweka kando, hivyo ndivyo seli hizi huweka kando mabaki yatokayo katika viini lishe vilivyoletwa na potasiamu katika lango la seli hio kwa ajili ya kutolewa nje ya mwili kwa mfumo wa utoaji mabaki/taka mwilini.

Tuendelee…

Vyakula gani vingine vyenye kiinilishe cha potasiamu vinavyofaa kwa wagonjwa wa presha/shinikizo la juu la damu?

 

Vyakula hivi ni kama vile:

  • Viazi vitamu
  • Maharage meupe
  • Spinachi
  • Parachichi

 

Hivi ni baadhi tu ya vyakula ambavyo vina potasiamu kwa wingi na sodiamu kwa uchache ambavyo vinafaa kwa watu wenye shinikizo la juu la damu.

 

Jambo la kuzingatia ni kwamba katika uandaaji wa vyakula hivi haupaswi kutumia mafuta mengi na kuna viwango unaweza kutumia ili upate virutubisho mwilini.

 

Mfano:

  1. Ndizi iliyoiva moja inaweza kuwa na mpaka miligramu 420 za potasiamu.
  2. Kiazi (kitamu) kimoja kilichookwa chenye gramu 299 kinaweza kuwa na potasium miligramu 1600.
  3. Kikombe kimoja cha parachichi chenye gramu 150 kinaweza kukupatia kiasi cha potasiamu cha miligramu 1120.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa kiwango ambacho mtu mwenye shinikizo la juu la damu anapaswa atumie potasiamu kuwa ni kiasi cha miligramu 3,500 mpaka 5,000 kwa siku.

Kwa ushauri kamili utakaoendana na mahitaji yako binafsi ya mwili, wasiliana nami kupitia +255767226702 au fanya booking kwenye duka letu kwa kubonyeza ‘hapa’.

 

Uepuke nini?

Vyakula ambavyo vinapaswa kukwepwa pindi mtu anapogundulika na shinikizo la juu la damu ni vyakula vyenye chumvi nyingi.

 

Unaweza kujiuliza kwanini unaambiwa uepuke chumvi nyingi? Sababu ni moja!

Chumvi ina tabia ya kuvuta maji na hivyo ulaji wa vyakula vyenye chumvi nyingi au kuongeza chumvi nyingi hupelekea ongezeko la kiwango cha chumvi katika mzunguko wa damu na hivyo kupelekea kuvutwa kwa maji kutoka ndani ya seli kuja nje ya seli na kuongeza ujazo wa maji katika mzunguko wa damu na mwishoni msukumo wa damu kuongezeka kutokana na wingi wa maji haya katika mfumo wa mzunguko wa damu.

 

“Juisi ya Moyo”

Nimalizie kwa kukupa chakula kingine kilichofanyiwa utafiti na Chuo Kikuu cha Newcastle nchini Uingireza ambacho huitwa kiazi sukari (beetroot) au wengine huita kiazi damu au viazi vyekundu.

 

beetroot for hypertension patients

 

Kiazi sukari kilionekana kuwa na viinilishe vya naitreti ambavyo vimehusishwa na kutanua mishipa ya damu na kushusha mapigo ya moyo kwa watu wazima wenye ugonjwa wa shinikizo la juu la damu.

 

Utafiti huu pia ulionyesha kuwa nyanya ina viinilishe vinavyodhibiti angiotensini, na hivyo kushusha mapigo ya moyo.

 

Na figili, ambayo wengine huifahamu kama celery, imeonekana kuchochea figo na kutengeneza mkojo na kusafisha mwili.

 

Vitu hivi vitatu huweza kuchanganywa kwa pamoja na kutengeneza juisi ambayo mtu mwenye shinikizo la juu la damu anaweza kutumia kwa ajili ya kuimarisha afya ya moyo pamoja na kuupatia mwili viinilishe vinavyojenga afya.

 

Kama unahitaji kujua zaidi kuhusiana na vyakula mbalimbali pamoja na kupangiwa ratiba yako ya mlo tafadhali wasiliana nasi ili uweze kuongea na mimi kwa ushauri zaidi wa vyakula kama una changamoto ya shinikizo la juu la damu.

 

Asante!! Tukutane tena kwenye makala ijayo.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW