Vidonda vya mdomoni, maarufu kama apthous ulcers au canker sores, ni tatizo la kawaida la afya ya mdomo kwani huwakumba watu wengi; inawezekana hata wewe ulishawahi ugua vidonda hivi.
Vidonda vya mdomoni ni vidonda vidogo vinavyotokea kwenye utando laini wa kinywa kama vile ndani ya mashavu, ulimi, au sehemu ya nyuma ya koo.
Mara nyingi vidonda hivi huwa na umbo la mviringo au la ovo na huwa na rangi nyekundu au nyeupe yenye mzingo mwekundu kwenye tishu laini ya mdomo.
Hivi vidonda hupelekea maumivu makali kinywani mwako wakati wa kula au hata wakati wa kuzungumza.
Watu wenye umri wowote wanaweza kuwa na vidonda vya mdomoni, lakini mara nyingi huathiri zaidi watu wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 40. Na tafiti mbali mbali zimeonyesha vidonda hivi kuwapata hasa vijana.
Sababu gani husababisha vidonda hivi?
Kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha vidonda mdomoni mwako. Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na:
- Majeraha au kuumia kwa tishu ya mdomo, kama vile kukwaruzwa au kugongwa kwa tishu na meno.
- Mfumo dhaifu wa kinga yako mwilini.
- Msongo wa mawazo au mabadiliko yako ya homoni.
- Utumiaji wa vyakula vyenye asidi nyingi (kama machungwa, malimao, maziwa ya kiwandani, na kadhalka) au viungo vya chakula vinavyoweza kusababisha mzio (allergy).
- Uvutaji wa sigara.
- Viwango vya chini vya vitamini au madini mwilini mwako, kama vile vitamini B12, asidi ya folic, au chuma ya mwili (iron deficiency).
Je, vidonda hivi huisha baada ya muda gani?
Kwa kawaida, vidonda vya mdomoni hukaa kwa muda wa wiki moja hadi mbili kabla ya kupona kabisa. Hata hivyo, kuna baadhi ya hali ambazo zinaweza kufanya vidonda hivi kudumu kwa muda mrefu au kujirudia mara kwa mara.
Kama nilivyokwisha kukujulisha juu ya vitu vinavyokuweka hatarini kupata vidonda hivi, hivyo basi ikiwa una vigezo hivyo na havijaondolewa, vidonda hivi huweza kukaa kwa muda zaidi ya wiki mbili au vikarejea tena baada ya kupona.
Ikiwa ni kawaida kutokea kwa vidonda hivi katika familia yako, itabidi kila vikirejea uvitibie kwasababu hauwezi kubadili genetics ya mwili wako.
Lakini kama ni swala la utumiaji wa tumbaku, lishe duni, msongo wa mawazo na kadhalika basi ni vyema kusitisha hali hizo ili kuepukana na vidonda hivi.
Vidonda hivi hutibika?
Matibabu ya vidonda vya mdomoni mara nyingi hulenga kupunguza maumivu na kusaidia uponyaji kwasababu havinaga dawa maalum bali huisha vyenyewe bila kuhitaji matibabu.
Hivyo basi, moja wapo ya dawa ambazo huwa na vigezo vikuu vinne vya kukuwezesha kupunguza maumivu lakini pia kupunguza au kusaidia uponyaji ni pamoja na kutumia tube iitwayo quadragel.
Dawa hii ina uwezo wa kupunguza maumivu na kuuwa bakteria hivyo ni njia nzuri ya kupunguza maumivu na kuzuia maambukizi.
Dawa hii huwa katika tube na unaitumia kwa kuipaka moja kwa moja mdomoni kwenye maeneo yote yenye vidonda.
Tambua: Kutumia mswaki laini na kunywa maji mengi yanaweza kusaidia kuharakisha uponyaji.
Msaada wa Kitaalamu
Mbali na matibabu binafsi, ni muhimu kushauriana na daktari au mtaalamu wa meno ikiwa vidonda vya mdomoni vinarudiwa mara kwa mara au vinadumu kwa muda mrefu.
Daktari anaweza kufanya uchunguzi wa kina na kupendekeza matibabu yanayofaa kulingana na hali yako binafsi.
Vidonda vya mdomoni ni tatizo la kawaida la afya ya mdomo ambalo linaweza kuleta usumbufu mkubwa. Hata hivyo, kwa matibabu sahihi na msaada wa kitaalamu, unaweza kupata nafuu na kurejea kwenye afya bora ya kinywa chako.

“For the love of words”
Hii mada imetatua tatizo langu la muda mrefu. Mara nyingi huwa napata tatizo hili nikiwa nakula chakula kitamu najiuma.
Good