Nilipokuwa sekondari kuna Padri mmoja nilikuwa nikimuona kila siku ana bandeji ya hospitali mguuni, alikuwa anachechemea na hakuwahi kuvaa viatu vya kufunika, bali viatu vya wazi.
Nlipodadisi kwa undani nikaambiwa ana kidonda cha sukari, ndio maana hakiponi haraka. Sikuelewa maana yake kwa wakati huo mpaka nilipokua na kupata elimu ya kutosha kuhusu vidonda vya kisukari.
Nilipokuwa Daktari, nikapata uelewa halisi kuhusu kisukari na vidonda kuchelewa kupona. Kwanini mtu mwenye kisukari akipata kidonda ni habari tofauti kabisa?
Kidonda cha sukari ni nini?
Hiki ni kidonda ambacho hutokea kwa mtu mwenye ugonjwa wa kisukari. Kidonda cha sukari ni maarufu kwa sababu ya tabia ya kuchelewa kupona kinapotokea kwa mtu mwenye kisukari wakati, kidonda cha aina hiyo hiyo, akipata mtu asiye na kisukari hupona kawaida na mapema.
Jina lingine maarufu huwa ni Diabetic Foot au diabetic wound kulingana na ukweli kwamba asilimia 90 ya vidonda vya kisukari hutokea mguuni.
Vidonda vya kisukari hutokeaje?
Vidonda vya sukari (Diabetic wounds) hutokea kwa namna 3 kama ifuatavyo:
- Ajali ya kuchomwa au kukatwa na kitu: Hii ni hali ya kawaida tu ya kupata kidonda kutokana na mazingira mbalimbali na hivyo kupelekea kidonda katika sehemu ya mwili. Kama kidonda hiki atakipata mgonjwa wa sukari, hapo ndio huitwa kidonda cha sukari maana uponaji na mabadiriko yake hayatokuwa ya kawaida.
- Kuchubuka kwa sehemu ya mwili: Mchubuko huu hutokea mara nyingi miguuni na huanza ukiwa mdogo na baadaye huongezeka, kuchimbika na kusababisha kidonda kikubwa. Inaweza kusababishwa na uvaaji wa viatu vinavyobana na hivyo kuchubua au kuunguza sehemu ya mwili, ukizingatia sehemu hiyo tayari haipati damu ya kutosha kwa sababu ya madhara ya kisukari.
- Upasuaji: Baada ya upasuaji, kidonda kinaweza kuchkua muda mrefu kidogo kupona kwa mtu mwenye kisukari.
Kisukari kinasababishaje kidonda kutopona haraka?
Ukiangalia hizo njia tatu za kupata kidonda ni za kawaida kabisa kwa mtu yeyote lakini kwa mtu mwenye kisukari, stori hubadilika! Sababu ni nini?
Mnamo Mwezi April mwaka 2009, mtandao wa American Diabetes Association ulitoa chapisho lenye utafiti wa vidonda sukari. Utafiti huu ulionyesha kwamba kila mgonjwa wa kisukari ana asilimia 25 ya kupata kidonda cha sukari.
Kati ya hao, asilimia 85 ya vidonda vya sukari huendelea kukua na baadaye kupelekea kukatwa kiungo (Amputation).
Habari njema ni kwamba hatari ya kukatwa kiungo inaweza kupunguzwa kwa asilimia 40 endapo kutakuwa na uangalizi wa karibu wa vidonda hivi ikihusisha kuhakikisha sukari iko katika viwango vya kawaida na kufata masharti ya sukari ipasavyo.
Kidonda cha kisukari sifa yake ni kuchelewa kupona, kuendelea kuongezeka ukubwa, urahisi wa kupata maambukizi ya bakteria na uwezekano wa kupelekea kiungo kukatwa, mfano mguu.
Nini hufanya kidonda hiki kitokee na kiwe kigumu kupona?
1. Uharibifu wa mishipa ya fahamu (Neuropathy)
Kutokana na mkusanyiko wa sukari nyingi katika damu, kemikali mbaya ambazo huathiri mishipa ya fahamu hasa ya sehemu za mwili za pembezoni (Peripheral) hutengenezwa na hivyo kupelekea sehemu hiyo kutokuwa na ufahamu wa kutosha.
Unapoguswa au kuungua, mwili huwa na namna ya kutambua haraka na kukuondoa kwenye hatari haraka aidha kwa kuondoa kiungo hicho sehemu ya hatari – na hivyo kusaidia kuepuka ajali – au maumivu. Hii ni moja ya body defence.
Bahati mbaya, kwa mtu mwenye kisukari, njia hii ya kujihami huwa iko chini kwa sababu ya kuharibika kwa mishipa ya fahamu na hivyo ni rahisi kwake kuumia au kupata mchubuko na asitambue kabisa mpaka kidonda kitakapokuwa kikubwa na kuanza kuuma. Hii ni sababu kwanini ni rahisi kupata mchubuko bila kujua.
Kwakuwa mishipa ya fahamu ni muhimu hasa kwenye kutanuka na kusinyaa kwa misuli na mishipa ya damu basi kidonda hiki kikitokea uponaji wake unaweza kuwa mgumu kwa sababu mishipa ya damu ya eneo hilo huwa imesinyaa na haipeleki damu na virutubisho vya kutosha kusaidia kupona haraka. Mishipa ya damu inategemea sana mishipa ya fahamu kufanya kazi vizuri.
2. Ugonjwa wa mishipa ya damu (Vascular disease)
Mkusanyiko wa sukari nyingi mwilini hupelekea kutengeneza kemikali haribifu ambazo huaribu sehemu ya ndani ya mishipa ya damu (Endothelium). Sehemu hii ni muhimu sana kwa ajili ya kutanuka na kusinyaa kwa mishipa ya damu.
Ikiharibiwa huathiri uwezo wa mwili kusafirisha oxygen, virutubisho na seli muhimu kwenda kwenye sehemu za pembezoni za mwili na hivyo hupelekea kidonda kushindwa kupona kwa wakati.
Sababu hii ndio hufanya mtu mwenye kisukari akishapata kidonda kisipone au kuchelewa kupona. Kidonda ili kipone haraka huwa kinategemea mishipa ya damu iweze kuleta seli za mwili, virutubisho na oxygen; vitu hivyo vikiwepo basi kidonda hupona haraka.
Kwa mgonjwa wa kisukari, mishipa yake hasa ya pembezoni huwa myembamba na hutanuka na kusinyaa kwa shida na hivyo kufanya kidonda badala ya kuchukua wiki, huchukua miezi kadhaa kupona.
Pia ni rahisi kidonda hiki kupata maambukizi ya bakteria kwa sababu damu haifiki vizuri kwenye sehemu ya kidonda na mara nyingi hii ndio hupelekea mgonjwa kukatwa kiungo cha mwili ili kuepuka kidonda kusababisha madhara katika sehemu nyingine za mwili.
Vidonda vya kisukari mara nyingi huathiri miguu ukilinganisha na sehemu nyingine kwa sababu ni rahisi kupata mchubuko wa miguu kuliko sehemu zingine.
Angalizo: Kupata kidonda halafu kikachelewa kupona bila sababu inaweza kuwa dalili ya kwamba una kisukari. Usichukulie poa, nenda kapime sukari yako!
Vidonda vya sukari vinaepukika?
Kuna baadhi ya kanuni ambazo ukizifuata unaweza kuwa na uwezekano wa kuepuka kupata vidonda vya sukari, au hata ukipata vikapona haraka kama mtu wa kawaida.
Fuata kanuni zifuatazo:
1. Hakikisha sukari yako iko kawaida
Sawa una kisukari lakini haizuii sukari yako kuwa ya kawaida kama unameza dawa zako vizuri. Kumeza dawa vizuri inaendana na kupata mchanganyiko sahihi wa dawa na kuzimeza kila siku kwa wakati.
Sukari ikiwa ya kawaida, kinga na uwezo wa mwili huongezeka. Kumbuka sukari nyingi huua seli za mwili na kuathiri mishipa ya damu inayosafirisha damu kufika kwenye sehemu za pembezoni mwa mwili (Peripheral).
Sukari yako ikiwa kawaida walau zaidi ya miezi mitatu basi mwili wako hurudi kuwa kama wa mtu wa kawaida.
Hivyo ukipata kidonda ni rahisi mwili kupambana na maambukizi ya bacteria na kupona haraka.
Kumbuka sukari kukaa sawa sio swala la dawa tu, bali hata lishe yako. Pata kitabu cha “How to Reverse Type 2 Diabetes” kutoka dukani kwetu uongeze uwezo wako wa kuweka sukari sawa na kujiweka katika nafasi nzuri ya kupona vidonda kirahisi.
2. Epuka uvutaji wa sigara
Mtandao wa Center for Disease Control (CDC) nchini Marekani uliainisha kwamba mgonjwa wa kisukari anayevuta sigara ana asilimia 40 zaidi ya kupata vidonda vya sukari na asilimia 80 ya kukatwa mguu au kiungo.
Sigara ina kemikali ya Nicotine ambayo huaribu mishipa ya damu na kuifanya isinyae. Hivyo ukaiongeza na madhara ya sukari katika mishipa ya damu ambayo hufanya vile vile unakuwa na double effect.
Katika uzoefu wangu wa kazi, kati ya wagonjwa 10 wanoishia kwenye kukatwa mguu au kiungo kwa sababu ya Diabetic wound, 7 kati yao wanavuta sigara!
Tayari mwili wako una dosari, hivyo kuendelea kuvuta sigara ni sawa na kumsukuma mlevi kwenye mteremko, ACHA!
Unataka kujua athari za sigara na namna ya kuacha? Pata kitabu cha “Sigara – Jasusi Anayetabasamu” dukani, upate hamasa ya kuacha.
3. Jenga tabia ya kukagua miguu yako
Kama nilivyosema, kwa sababu ya kupoteza fahamu ya viungo, mfano miguu, unaweza kupata mchubuko na usijue.
Hivyo mgonjwa wa kisukari unashauriwa kila siku, kabla hujalala, kukagua miguu yako na kuhakikisha iko sawa haina mchubuko.
Epuka kuwa na miguu mikavu sana, jitahidi kuipaka mafuta iwe laini kuepuka kupasuka au kulika.
Unapofanya kazi jaribu kuvaa viatu vya kufunika kuepuka kuangukiwa na vitu au kugonnga mkuu wako kwenye ncha kali na kupata kidonda.
Viatu vyako visiwe vya kubana sana, viwe size yako kuepuka kuungua au michubuko. Pia kumbuka kukata kucha zako kuepuka kujichoma katikati ya vidole.
4. Mazoezi ya kutembea walau kila siku kwa dakika 30
Yatasaidia kuongeza mzunguko wako wa damu na kuongeza afya ya seli za mwili na hivyo kupunguza uwezekano wa kupata vidonda.
5. Mwisho, kuhudhuria kliniki walau kila mwisho wa mwezi itakuongezea uwezekano wa kuwa na sukari iliyo imara.
Kumbuka: Elimu ya lishe ya sukari na namna ya kuweka sukari yako sawa ni muhimu sana ndio maana nakushauri usome kitabu hiki cha “How to Reverse Diabetes Type 2” kutoka dukani kwetu. Kitakupa mwongozo wa jinsi ya kuifanya sukari yako kuwa kama sio mgonjwa.
Elimu mbaya ya kisukari ni kudhani kwamba kumeza dawa tu ndio suluhisho. Lakini watu waliofanikiwa kuweka sukari yao vizuri wanajua namna ya kuchanganya dawa na mtindo mzuri wa maisha kukaa sawa.
Vidonda vya sukari ni moja kati ya janga la kukwepa sana kwa mgonjwa wa kisukari. Lakini nani anaweza kukwepa ajali kwa asilimia 100?
Ndio maana ujanja ni kuhakikisha sukari yako iko katika viwango salama kiasi kwamba ukipata kidonda kinapona upesi.
Abite Nyumbani tunakuletea huduma ya lishe na daktari kiganjani. Hamna kuhangaika tena kula bila mpangilio kwa sababu utapata mpangilio wa lishe utakaoendana na mahitaji yako. Kupitia vifurushi vyetu vya lishe utapata mpangilio mzuri wa sahani ya kisukari (Diabetic plate).
Vile vile huduma ya Daktari kiganjani itakuwezesha kuwa na daktari wako binafsi kupata ushauri mbalimbali mwezi mzima bila kulazimika kutumia gharama nyingi bila sababu kwa jambo la kawaida.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.