Neno utapiamlo sio geni masikioni mwako. Bila shaka umelisikia sana sehemu mbalimbali ikiwemo kusoma mahali hasa kwenye Biolojia shule ya msingi au kuwaona watoto wenye utapiamlo.
Utapiamlo ni hali ya mwili kukosa uwiano wa virutubisho muhimu kwa maana ya kuwa navyo vingi au pungufu. Jamii huitazama hali hii ya kiafya kwa upande mmoja wa upungufu au ukosefu wa virutubisho muhimu mwilini na kusahau kwamba hata kuwa na virutubisho vingi mwilini huleta utapiamlo.
Utapiamlo sio tu ukosefu wa lishe bali ni ukosefu wa mlo kamili kwa maana ya kukosa uwiano mzuri wa wanga, protini, mafuta (fats), vitamini na maji.
Mwaka 2022, Shirika la Afya duniani (WHO) liliripoti utafiti wa dunia nzima wa utapiamlo ambapo watoto milioni 149 walikuwa wafupi ukilinganisha na umri wao (stunted growth), million 45 walikuwa wamekonda (wasted) na million 37 walikuwa na uzito uliopitiliza na vitambi.
Zipi ni dalili haswa za utapiamlo?
Kwanza utapiamlo kama tulivyosema unaweza kujionyesha kwa dalili mbalimbali kama kushindwa kurefuka kwa watoto, kwa maana katika ukuaji lazima kuwe na uwiano wa umri na urefu, kama umri unapanda lakini urefu haufatani basi inaweza kuwa dalili ya utapiamlo hasa kwa watoto.
Pili ni kutoongezeka uzito kwa watoto, ambapo mtoto hukua kiumri lakini mwili haukui.
Ukipima uzito wake unakuta hauendani na umri wake katika viwango vya Shirika la Afya duniani. Hali hii hasa kwa watoto huweza kuwa dalili ya utapiamlo.
Tatu ni mwili kukosa nuru, kukauka, kushindwa kuona vizuri, vidonda vya mdomo mara kwa mara, kupungukiwa damu, kuwa na tumbo kubwa (kiribatumbo), kuvimba miguu, nywele kunyonyoka na mwili kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara.
Kutokana na utapiamlo kushusha kinga ya mwili, basi inaweza kupelekea urahisi wa kupata Magonjwa ya kuambukiza kama kifua kikuu (Tuberculosis), Pneumonia, nk.
Nne ni uzito uliopitiliza na kitambi. Hali hii ya utapiamlo ipo mara nyingi kwa watu wazima japo utafiti umeonyesha hali hii kuongezeka kwa watoto pia.
Kinyume na mtazamo wa jamii wa kuona kitambi kama dalili ya utajiri na maisha mazuri, kitambi ni dalili kwamba virutubisho vyako vimepitiliza na hivyo hamna uwiano katika mwili.
Kama ukosefu wa virutubisho unavyopelekea kushusha kinga ya mwili, kitambi hukuweka katika hatari ya magonjwa yasiyoambukizwa kama kisukari, presha na kiarusi (stroke).
Sasa utapiamlo una athari gani katika ukuaji wa watoto?
Mnamo July mwaka 2022 ilitolewa ripoti ya utafiti uliofanywa kwa watu 55 waliozaliwa kuanzia kati ya mwaka 1967 mpaka 1972. Utafiti huu uliojulikana kama Barbadian cohort ulilenga kustadi hali ya ubongo wa watu hawa katika umri wao wa miaka 45 mpaka 55.
Watu hawa ni wale waliopata utapiamlo wakiwa na umri chini ya mwaka mmoja. Walipata utapiamlo wakiwa chini ya mwaka mmoja, baadaye walihudumiwa na serikali kwa kupata Lishe bora mpaka miaka 12. Lengo ilikuwa ni kujua hali zao za ubongo kwa sasa.
Ripoti hii pia ililinganisha watu wa umri huo huo ambao hawakupata utapiamlo katika umri mdogo. Matokeo yake yalikuwa kama ifuatavyo.
Watu hawa 55 waliofanyiwa stadi walikuwa na mambo yafuatayo:
- Baadhi yao walikuwa jela kwa makosa ya kinidhamu
- Baadhi walikutwa katika hali ya msongo wa mawazo
- Baadhi yao walikutwa na tatizo la Attention Deficits Disorder (hali ya mtu kushindwa kuwa na focus ya jambo fulani)
- Kushindwa kutawala hisia (poor emotional intelligence)
- Baadhi yao walikuwa wamejaribu kujiua
- Wengine walikuwa na mahusiano mabaya na ndugu pamoja na wapenzi wao
- Matatizo ya hasira iliyopitiliza
- Lakini pia baadhi yao walikuwa na IQ ndogo, uchizi na mafanikio madogo kiuchumi,
- Uteja kama ulevi, utumiaji madawa na kadhalika.
Riport hii iligundua kwamba, utapiamlo chini ya mwaka mmoja hupelekea ubongo na baadhi ya mishipa ya fahamu kushindwa kukua vizuri.
Waligundua kwamba hali hii ya utapiamlo husababisha matatizo ya muda mrefu ya ubongo ambayo mtu anaweza kukua nayo mpaka uzeeni.
Kipindi cha chini ya miaka mitano ni muhimu sana katika ukuaji wa ubongo wa mtoto. Hapa ndipo ile mishipa ya fahamu na tishu za ubongo huongezeka na kukomaa. Utapiamlo hufanya hatua hizi kudumaa kutokana na ukosefu wa virutubisho muhimu kama protini, mafuta na madini kama Zinc, Phosphate na Vitamin B.
Hali hizi huanza kujionesha kwanzia nyumbani. Watoto hawa huwa wagumu kuelewa hata mambo ya kawaida.
Mfano ugumu wa kutekeleza maagizo ya wazazi kwa sababu ya kumbukumbu ndogo. Hii hupelekea ugomvi wa mara kwa mara wa mzazi na mtoto.
Watoto hawa pia huwa na tabia ya ugomvi na hasira kali hasa kwa watoto wenzao.
Watoto hawa huwa na tatizo la kusoma na kuelewa shuleni kutokana na kuwa na IQ ndogo pamoja na kumbukumbu ya chini kabisa.
Wazazi na walimu wa watoto hawa, kwa kutokujua tatizo lao, huwa wakali na kuwalazimisha kuelewa. Hivyo hufanya watoto hawa kuchukia shule.
Pia kwa sababu ya utapiamlo watoto hawa huwa katika hatari ya kupata magonjwa ya akili pamoja na kifafa katika umri wa mapema.
Watoto wengi wanaoonekana kufeli kimaisha mapema hasa wale kutoka familia duni kiuchumi mara nyingi tatizo lao kubwa ni utapiamlo. Kwa watoto walio katika familia nzuri utapiamlo unaweza usiwe shida, bali sababu zingine kama malezi mabovu kuhusika.
Kwanini utapiamlo katika umri mdogo?
- Mama kukosa maziwa.
- Ukosefu wa elimu kwa wazazi
- Magonjwa ya watoto kama vile mtindio wa ubongo, kuzaliwa njiti au matatizo ya kimaumbile.
- Kutowajibika kwa wazazi na ndugu wa karibu.
- Umaskini wa wazazi
- Maradhi au majanga kama vita.
Tufanye nini kupambana na tatizo la utapiamlo?
Kwanza unapaswa kujua kwamba mtoto wako ni mtaji. Ukiwa na mtoto mwenye akili nzuri na uwezo wa kungamua mambo, basi uwezekano wa kupata faida Katika maisha yako ni mkubwa.
Faida ya mtoto sio tu kupata kazi na kukupa hela, hapana! Faida ya mtoto huanza wakati akiwa mdogo unapoanza kumtuma, niletee hiki, niletee kile, pika hiki, pika kile, nenda huku nenda kule.
Sasa utajiskiaje mtoto wako akipata utapiamlo na akawa mzito hata kumuagiza huwezi? Hakuna hasara kubwa kama hii.
Basi katika mambo makubwa unayopaswa kuyapambania kama mzazi ni kuhakikisha mwanao hapati utapiamlo.
Shirika la chakula duniani limeendelea kupambana kuhakikisha linaondoa tatizo hili la utapiamlo, lakini bado haitoshi.
Hizi ndio njia nne kuu za kupambana na utapiamlo kwa watoto:
1. Elimu ya afya kwa wazazi
Elimu ya afya ni muhimu kwa wazazi hasa wanapokuwa wanajiandaa kupata mtoto. Elimu hii huusisha umuhimu wa kumnyonyesha mtoto mara tu baada ya kuzaliwa. Hii huambatana na kujua namna ya kumuweka mtoto kwenye ziwa.
Wazazi wengi hasa wa mara ya kwanza hawajui namna ya kunyonyesha mfano, mtoto anapokuwa ananyonya chuchu yote inabidi iwe mdomoni, kusiwe na ukelele wa kufyonza.
Chuchu inapokuwa nusu nje ndani hufanya mtoto kunyonya hewa hivyo hashibi vizuri.
Pia wazazi wanahimizwa kumuweka mtoto kwenye ziwa hata kama maziwa ni machache. Hii huusaidia kuendelea kuhamasisha mwili kutoa maziwa kwa kuamsha zile homoni za kutoa maziwa.
Ulaji wa virutubisho kama unga wa mbegu za maboga, kahawa na pili pili manga huweza kusaidia kutoa maziwa.
SIO kila mama akijifungua huwa anatoa maziwa hapo hapo, baadhi yao hushindwa kutokana na kujifungua kwa “kisu” (operation), au msongo wa mawazo au sababu za homoni hivyo ni muhimu kuwatia moyo, kuwasisitiza kunywa maji ya kutosha na kutumia muda mwingi kupumzika.
Kuna dawa za asili pia za kuongeza maziwa ya mama. Dawa hizi zimekuwa msaada sana kwa wamama wasio na maziwa.
Mfano, mke wangu alipojifungua mtoto wa kwanza, mbegu za maboga zilitusaidia sana. Mtoto wa pili vile vile, tulitumia dawa ya asili kutokwa kwa Shangazi yangu. Maziwa yalianza kuja mengi sana.
Kuna haja ya kutembelea uasili wetu pia maana wazee wa zamani hawakuwa na tatizo kama hili la kukosa maziwa.
Kizazi hiki cha dini nyingi kimekumbwa na changamoto ya kuamini maombi zaidi na kuona tiba asili kama uchawi.
Kipindi cha korona tulishuhudia namna watu walivoamini katika malimao, majani ya kujifukizia na kadhalika; kama unakula limao kwanini ukatae kutumia dawa ya asili ya mimea?
Mimi ni Daktari lakini sijawahi kudharau dawa za asili yangu. Siku ukijua kwamba hata Panadol inatokana na mimea ndio utajua kwamba ‘unajifungia’ sana kudharau dawa za asili.
Pia lishe ya mtoto inapaswa kuwa na wanga, protini, vitamin, mafuta n.k. Sio unampa mtoto uji wa mahindi tu kila siku! Atapata utapiamlo. Ni lazima kuchanganya vyakula Ili kupata virutubisho muhimu.
Asilimia 50 ya wazazi wanawapa watoto lishe bila kujua wanatoa nini na nini, wao wanaanda chakula tu. Bahati yao watoto hawapati utapiamlo, ila ni muhimu kujua mtoto anahitaji nini na nini, kama utakavyoona kwenye mada zingine za lishe ya watoto.
Utafiti uliofanywa na Journal of Food and Agriculture nchini Lesotho mwaka 2012 ulilenga kufahamu elimu ya Lishe kwa wazazi wenye watoto kuanzia miezi 0 mpaka 24. Utafiti huu ulihusisha wamama na wababa wasomi, na wasio wasomi.
Ripoti ya tafiti hii ilionyesha kwamba asilimia 81 ya wazazi wasomi walikuwa na elimu nzuri ya Lishe kwa watoto wakati asilimia 61 ya wazazi wasiosoma walikuwa na elimu kidogo ya Lishe.
Hali hii inatoa wito kwa Wizara ya Afya kuongeza mkazo kwenye elimu ya Lishe kwa wazazi ili kuepuka kupata watoto mazuzu.
2. Tuimize uwajibikaji
Mimba huchukua miezi 9, sio jambo la dharula! Tuhimizane kujiandaa hasa kifedha. Jua tu kwamba lolote laweza kutokea wakati wa kujifungua na jua kwamba mama anaweza kukosa maziwa.
Ni vyema kujiandaa kiuchumi kuepuka changamoto za lishe. Baada ya miezi sita maziwa ya mama hayatatosha maana mtoto anaanza kukua kwa haraka sana hivyo wazazi waweze kumpatia uji wa lishe, vyakula mbalimbali na kadhalika.
Tupambane watoto wetu wasidumae maana ni taifa la leo na kesho. Mama usimtegemee sana baba kwenye lishe ya mtoto, hata kama baba hatoi pesa ya kutosha, jinyime wewe mtoto apate lishe bora.
Kwani mtoto anakula chakula kiasi gani? Inashangaza sana mama analaumu baba hatumi hela ya mtoto wakati huohuo mama ananunua smartphone, jeans, wigi za bei nzuri tu halafu hanunui unga wa lishe kisa baba wa mtoto hatumi matunzo.
Huu ni uzembe wa hali ya juu sana! Mtoto ni wenu nyote hivyo mama kwanza pambana, baba atafata baadaye. Kwani mtoto akidumaa itamuathiri baba peke yake?
Katika ulimwengu huu wa kidijitali, kupata watoto imekuwa rahisi hivyo wababa wengi sio wawajibikaji.
Mwanamke mjinga atasubiri baba atume hela. Mwanamke mwenye busara ataweka akiba wakati wa mimba ili imsaidie baada ya kujifungua.
Mwanamke kukataa kunyonyesha kisa maziwa yataanguka ni dhana mbaya sana ambayo imechangia kwenye utapiamlo wa watoto. Unajiuliza huyu kabeba mimba miezi 9 halafu baadaye anaona msala kunyonyesha?
Nikwambie tu maziwa kuanguka ni genetics, haviusiani na kunyonyesha, nimewaona wamama wenye watoto watano na wana maziwa yaliyosimama.
3. Pata msaada wa afya mapema
Moja ya visababishi vya utapiamlo kwa watoto ni kuchelewa kuwapatia huduma ya afya. Mama anapaswa kujua dalili za hatari za mtoto anayeumwa.
Mfano, mtoto anayeharisha na kutapika kila kitu maana yake anapoteza virutubisho vingi na ukikaa nae nyumbani muda mrefu, baada ya wiki mbili, atapata utapiamlo.
Mtoto akiharisha au kutapika zaidi ya mara 4, basi muwahishe hospitali akatibiwe. Vile vile magonjwa yanayohusisha homa, kukooa n.k, ni vizuri kuonana na daktari.
Wakati mwingine watoto hupata kifua kikuu na hivyo kukooa muda mrefu na kupoteza uzito. Asilimia kubwa ya watoto wenye kifua kikuu huwa na utapiamlo. Hivyo kuwahi huduma ya afya ni muhimu sana.
4. Kupambana na umaskini
Umaskini ndio unatufanya tukimbie majukumu yetu. Unatufanya tukatae watoto, unatufanya tushindwe kuwapa watoto wetu lishe bora. Umaskini ni adui yako namba moja kwa kila sekta.
Umaskini ndio unafanya mke wako akukimbie. Umaskini unafanya wanao wakudharau kwasababu wanaona huna mchango wowote.
Kati ya vitu vya kuvichukia hapa duniani ni umaskini, sio bosi wako wala baba mwenye nyumba! Chukia umaskini na pigana kujikwamua mtu wangu.
Umaskini ndio utafanya wanao wapate utapiamlo na waishie kuwa mazombi. Kila unapolala na kuamka sera yako iwe moja, kupambana na umaskini kwa kufanya kazi kwa bidii, kuachana na tabia zinazopoteza pesa kama kubeti, kamali, ulevi uliopitiliza, na umalaya.
Focus kwenye kupata kipato na kutunza akiba. Kwa kufanya hivi, neno utapiamlo utakua unalisikia kwenye redio tu.
Bonus: Kuna utapiamlo unasababishwa na ulaji uliopitiliza kwa watoto. Watoto hawa huwa na BMI kubwa na vitambi. Aina hii ya utapiamlo nayo ipo japo haiimbwi sana. Ni muhimu kupata usawa sahihi wa chakula kwa watoto ili kuhakikisha wanakua vyema.
Mwisho
Kama mzazi jua kwamba kuitwa Mama au Baba haiishi hapo, kuna uwajibikaji wake. Furaha ya mzazi ni kumuona mwanae anakua vizuri, mwenye furaha na afya nzuri ya akili.
Hebu jiulize kama wazazi wetu wasingetupigania leo hii tungekuwa na akili timamu? Labda tungeshakufa zamani.
Sitasahau siku nilipomwona Mama yangu akianguka mieleka miwili akiwa anakimbia hospitali kumuwaisha mdogo wangu alipokuwa anaumwa, nilikuwa nakimbia nyuma yake. Naweza kupima upendo wake kwa mwanaye kwa kukumbuka hii siku.
Wazazi tuwajibike kwa watoto wetu, tupambane walau mikono iende kinywani. Hii ni pamoja na kupambana kiuchumi walau kuweza kuweka chochote mezani, kuwapatia familia mlo kamili. Watoto wakiwa na afya nzuri hata wewe unakuwa salama.
Ni gharama kubwa ya muda na kifedha kumuuguza mtoto mwenye utapiamlo, unaweza kukaa hospitali zaidi ya mwezi na mbaya zaidi mtoto akishapata utapiamlo wa level ya juu “severe malnutrition”, afya yake ya ubongo huwa hairudi tena kuwa nzuri kama nilivyoeleza mwanzoni.
Endelea kujifunza elimu ya afya kupitia blogu yetu. Pata vitabu kadhaa vya afya ambavyo vimeandikwa na wataalam wetu.
Kitabu changu cha “Njia tano za kisaikolojia za kulinda afya yako” kipo tayari dukani kwetu. Kisome kiwe nguzo yako katika safari ya afya.
Huduma ya daktari kiganjani ni moja ya huduma unazoweza kupata pia kwenye duka yetu.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.