Umekosa Hamu ya Kula na Hujui Nini Ufanye?

Hali ya kutokutamani kula ni hali inayoweza kumkuta mtu yeyote; haitegemei tu kama mtu anaumwa. 

 

Binadamu wote, pamoja na wanyama, hutegemea chakula ili kuweza kuishi wakiwa wenye nguvu za kufanya kazi na afya bora lakini wakati mwingine tunakumbwa na hali za kukosa hamu ya kula.

Leo tuangalie nini hasa huweza kusababisha hali hii.

 

Sababu za kukosa hamu ya kula

1. Hali ya kuwa na ugonjwa

Hali hii inaweza kutokea pale ambapo mwili unakua umeshambuliwa na maradhi na hivyo hamu ya kula hupungua au huisha kabisa. 

 

Hapa ndipo watu wengi hulazimishwa kula vyakula mbalimbali kama vile uji, maziwa, juice, supu na kadhalika. Hichi ni kipindi ambacho unahitaji kula vyakula vyenye virutubishi vingi yaani nutrient dense foods.

 

Hii inaenda moja kwa moja katika uandaaji wa mlo kwa ajili ya wagonjwa ambapo mlo hupaswa kuwa kiasi kidogo chenye virutubishi vya kutosha.

 

2. Kukosa hamu ya kula kutokana na ulaji mbovu kabla ya hali hii kukupata

 Baadhi ya watu wamekua na ulaji mbovu kwa maana ya ulaji wa vyakula ambavyo havichangii katika kuimarisha afya ya utumbo; wengi wao hupendelea vyakula vyenye mafuta mengi na wanga kwa wingi ambavyo si rahisi kumeng’enywa na tumbo na huwa na mabaki mengi.

 

Nitakupa mfano ambao nilimpa mteja wangu:

 Sakafu ya nyumbani au ukuta unapokua unamwagikiwa na mafuta ya kupikia bila kusafishwa, mwisho wa siku ukuta au sakafu ile huwa na muonekano mbaya na baada ya muda inakuwa ngumu kusafisha sakafu au ukuta ule.

 

Hali hii hutokea hata katika matumbo yetu ambapo kukiwa na mafuta mengi muonekano wa utumbo unakua si mzuri; na kunakua na uchafu katika tumbo.

 

Jinsi gani unaweza kusafisha tumbo lako?

Vipo vyakula ambavyo vinaweza kufanya kazi za kufagia au kudeki matumbo yetu ili kuweza kuweka hali ya usafi katika matumbo yetu na tayari kwa ajili ya kupokea vyakula vingine. 

 

Vyakula hivi huwa na asili ya nyuzi nyuzi ili kuweza kupita kama fagio katika maeneo ya tumbo lako; na kama lifanyavyo fagio, ndivyo hivyo hivyo vyakula hivi vinaweza kuondoa taka katika matumbo yetu na kuyatoa nje.

 

Mfano wa vyakula hivi ni matunda (mfano mananasi), mboga za majani kama vile matembele, spinachi na mchicha, pamoja na mboga mboga zingine kama vile kabichi.

 

Mwisho

Kuna swali la muhimu ambalo watu wengi hupenda kuuliza kuhusiana na matunda: Je! Ni kipi bora kati ya kula matunda na kunywa juice?  

 

Jibu ni kwamba japo vyote vina virutubishi lakini ulaji wa tunda huongeza nyuzi nyuzi ambazo ndio fagio la maeneo ya tumbo. Hii ndio sababu ambayo inakupasa wewe kutumia tunda na sio juice peke yake.

 

Jambo la kuzingatia

Tujitahidi vyakula ambavyo tunakula viwe vinajumuisha matunda pamoja na mbogamboga; pia visiwe na mafuta mengi  na viwe vya moto wakati wa kula. 

 

Vyote hivi husaidia katika kuleta hali ya kuwa na afya katika matumbo yetu na kuepukana na hali za kutokua na hamu ya kula, kwani unapopatwa na hali hii inaweza kupelekea kukosa hitaji la virutubishi vya siku.

Na kama hali hii itakua endelevu hupelekea upungufu wa virutubishi na hata utapiamlo.

1 thought on “Umekosa Hamu ya Kula na Hujui Nini Ufanye?”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW