Mwaka 2018 nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu niliyekuwa na matumaini makubwa na ndoto nyingi za kutimiza. Nilifurahia masomo yangu, marafiki walikuwa chanzo cha furaha yangu, na siku za usoni zilionekana kung’aa.
Ghafla nilipokaribia mwaka wa mwisho nilianza kuwa mtu wa mawazo na kufikiri sana kuhusu future yangu na nini nitafanya nikirudi mtaani. Nilianza kuhisi mabadiliko ya ajabu ndani yangu. Hali ya huzuni ilianza kunikumba polepole, kama giza linavyotanda usiku; na haikuondoka.
Nilipokuwa darasani, nilihisi uzito mkubwa kwenye kifua changu. Kila kitu kilionekana kuwa na giza na isiyo na maana wala sababu maalum. Siku moja, nikiwa nimeketi kwenye kiti changu darasani, nilihisi machozi yakianza kunilengalenga bila sababu yoyote. Nilihisi huzuni isiyo na kikomo, na akili yangu ilikuwa na uzito kama kwamba ilikuwa imefungwa na minyororo isiyoonekana.
Niliamua kujitenga na marafiki zangu, nikiamini kuwa wangeshuhudia udhaifu wangu. Siku baada ya siku, nilizidi kupoteza hamu ya kushiriki katika shughuli ambazo hapo awali zilinipa furaha.
Kucheza mpira, kutembea na marafiki, na hata kushiriki darasani kulionekana kuwa kazi ngumu na zisizo na maana. Watu walio karibu nami walianza kujiuliza ni nini kilichokuwa kinaendelea, lakini sikujua namna ya kuwaeleza hali yangu.
Usiku mmoja nilijikuta nikilala kitandani na macho yametanda gizani. Nilihisi kama mawimbi ya mawazo yasiyo na mwisho yalikuwa yanazunguka katika akili yangu. Nilijaribu kulala, lakini usingizi ulikuwa mbali nami.
Kila asubuhi nilipoamka nilihisi kama siku ilianza kwa kuchoka zaidi kuliko nilivyokuwa kabla ya kulala. Usingizi haukuwa na maana tena, ulikuwa ni sehemu nyingine ya mateso yangu ya kila siku.
Siku moja, nikiwa njiani kuelewa chuoni, nilianza kuhisi woga na wasiwasi uliopitiliza. Nilihisi kama uzito wa dunia ulikuwa mabegani mwangu, na mawazo ya kutoendelea kuishi yalinizidi.
Nilijua kwamba nilihitaji msaada, lakini sikujua wapi pa kuanzia. Nilikua naumwa Sonona.
Kuelewa Sonona
Sonona, au depression, ni hali ya kihisia ambayo inaweza kumpata mtu yeyote. Ni zaidi ya huzuni ya kawaida, ni hali inayozidisha huzuni na kuchukua nafasi ya furaha katika maisha ya mtu.
Kumpata mtu mwenye sonona si jambo rahisi kila wakati, kwani wengi huvaa sura ya tabasamu wakati ndani wanapigana na vita kubwa.
Mara nyingi, mtu mwenye sonona anaweza kuonekana kama amechoka, hana hamu ya kufanya chochote, au anajitenga na watu waliomzunguka. Anaweza kupoteza hamu ya kula au kula kupita kiasi.
Usingizi unaweza kuwa tatizo kubwa – ama analala sana au hapati usingizi kabisa. Unaweza kumuona mtu huyu akiwa na huzuni ya kudumu, kutokuwa na matumaini, au hata kuwa na mawazo ya kujidhuru au kujitoa uhai.
Wakati mwingine, mtu anaweza kuhisi maumivu yasiyoelezeka, kama maumivu ya kichwa au mgongo, ambayo hayaeleweki sababu zake za kimwili. Hisia ya kutojiweza na kujiona hana thamani inaweza kumzidi mtu huyu, na hata kazi ndogondogo ambazo hapo awali zilikuwa rahisi zinaweza kuonekana ngumu na zisizo na maana.
Nini husababisha Sonona?
- Mambo ya Genetics (kurithi): Kama kuna historia ya sonona katika familia, kuna uwezekano mkubwa wa mtu kuathirika pia.
- Mabadiliko ya Kibiokemia/kemikali za ubongo: Mabadiliko katika vichocheo vya ubongo vinaweza kuchangia hali hii.
- Matukio ya Maisha: Kupoteza mtu wa karibu, kuvunjika kwa uhusiano, au matatizo makubwa ya kifedha yanaweza kusababisha sonona.
- Mazingira: Hali ngumu za kimaisha kama vile umaskini, upweke, au msongo wa mawazo kazini pia zinaweza kuchangia.
- Magonjwa ya Kimwili: Magonjwa sugu kama vile ugonjwa wa moyo, saratani, au kisukari yanaweza kusababisha sonona kutokana na hali ya kudumu ya maumivu na usumbufu.
Aina za Sonona
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), sonona inaweza kujitokeza kwa aina mbalimbali, ikiwemo:
1. Major Depressive Disorder: Hii ni sonona kali inayoweza kudumu kwa muda mrefu na inaathiri uwezo wa mtu kufanya kazi za kila siku. Watu wanaopitia hali hii mara nyingi wanahisi huzuni kubwa, hawana hamu ya kufanya chochote, na wanaweza kuwa na mawazo ya kujidhuru au hata kujiua.
Mfano, unaweza kujikuta ukipoteza hamu ya kufanya kazi unayoipenda na kuacha kushiriki katika shughuli za kijamii. Kila asubuhi ukiamka unajikuta na hisia za kukata tamaa na kushindwa kabisa kuendelea na shughuli zako za kila siku.
2. Persistent Depressive Disorder (Dysthymia): Hii ni hali ya sonona ya kudumu ambayo inaweza kuwa na dalili zisizo kali lakini zinaendelea kwa miaka kadhaa.
Mfano, unaweza kuhisi au kujisikia huzuni na uchovu wa kudumu kwa miaka mingi. Ingawa unaweza kuendelea na kazi yako, furaha ya maisha inabaki kuwa changamoto. Hali hii inaweza kukufanya uonekane kama mtu asiye na msisimko na aliepoteza tumaini katika maisha.
3. Bipolar Disorder: Hii ni hali ambapo mtu hupitia vipindi vya sonona kali na vipindi vya furaha isiyo ya kawaida (mania). Wakati wa kipindi cha mania, mtu anaweza kuhisi furaha isiyo ya kawaida, kuwa na nishati nyingi, na kufanya maamuzi yasiyo na busara.
Mfano, unaweza kujikuta ukitumia pesa nyingi katika kipindi kifupi bila kujali athari zake, kisha kuingia katika kipindi cha huzuni kali ambapo hautaweza hata kutoka kitandani.
4. Seasonal Affective Disorder (SAD): Hii ni aina ya sonona inayotokea kwa vipindi maalum, mara nyingi wakati wa baridi ambapo kuna upungufu wa mwanga wa jua.
Mfano, unaweza kuhisi huzuni na uchovu kila wakati wa majira ya baridi. Unajikuta ukipoteza hamu ya kuamka asubuhi, kusoma, au hata kushirikiana na marafiki zako. Cha kushangaza kipindi cha majira kikianza, hali hii inatoweka na unaanza kurudi katika hali ya kawaida.
5. Postpartum Depression: Hii ni sonona inayotokea baada ya mwanamke kujifungua.
Mfano, mara baada ya kujifungua mtoto wa kwanza, baadhi ya wanawake wanaweza kuhisi huzuni kali na hofu kubwa kwa kudhani au kufikiria kwamba hawatoshi kama mama na mara nyingi wanaweza kuwa na mawazo ya kujidhuru.
Ingawa ni kawaida kwa wanawake wengi kuhisi “baby blues” baada ya kujifungua, hali ya mwanamke anayesumbuliwa na postpartum depression husumu na kuwa kali zaidi, ikihitaji matibabu na ushauri wa kitaalamu.
Kuelekea Matibabu
Kujua kwamba unahitaji msaada ni hatua kubwa ya kwanza. Nilipoamua kufungua moyo wangu kwa rafiki mmoja wa karibu, alinishauri niende kumuona mtaalamu wa afya ya akili.
Hii ilikuwa hatua ngumu zaidi kwangu, lakini muhimu zaidi. Nilijifunza kwamba sonona ina tiba, na hatua za kuelekea afya ya akili nzuri zinahitaji uvumilivu na msaada kutoka kwa wale wanaokupenda.
Nilipewa tiba ya kisaikolojia na dawa za kupunguza dalili za sonona. Kupitia tiba hii, nilijifunza mbinu za kukabiliana na huzuni na kujenga tena maisha yangu. Ingawa safari yangu haikuwa rahisi, niliweza kuona mwanga tena baada ya giza nene.
Mwisho
Sonona ni hali ya kisaikolojia inayoweza kuwa na athari kubwa kwa maisha ya mtu binafsi. Ni muhimu kutambua dalili mapema na kutafuta msaada wa kitaalamu ili kudhibiti hali hii na kuboresha maisha.
Kuelewa, kuelimisha, na kusaidia wale wanaopitia sonona ni jukumu letu sote katika kujenga jamii yenye afya bora ya akili. Kwa kuchukua hatua sahihi, tunaweza kusaidia kupunguza athari za sonona na kuboresha maisha ya wale wanaokumbwa na hali hii.

Tutor at abdurahman al Sumait Psychologist at Ampola tasakhtaa hospital.
Mm Nina Sonoma namba 5 Hadi Sasa haijaniachia na sababu moja wapo nilipatwa na pressure nikiwa mjamzito Hadi kujifungua hii Hali ni ngumu kuikubali inanipelekea sonona Dawa kumeza kila siku msongo was mawazo unaathir Manisha tangu furaha imepotea imebaki ndoto kuirudisha
Habari Fatma,
Pole sana kwa hali unayopitia. Ni vigumu sana kuelewa maumivu na changamoto unazokutana nazo, hasa kutokana na msongo wa mawazo na sonona. Ni jambo zito na linahitaji ujasiri mkubwa kulikubali na kulizungumzia.
Kwanza kabisa, nataka ujue kuwa hauko peke yako katika safari hii. Watu wengi hukabiliana na sonona na msongo wa mawazo, hasa baada ya kupitia vipindi vigumu kama ujauzito na kujifungua. Mabadiliko ya homoni, pamoja na shinikizo la maisha, vinaweza kuchangia hali hizi kuwa mbaya zaidi.
Kuhusu matumizi ya dawa, ni muhimu kufuata ushauri wa daktari wako. Dawa zinaweza kusaidia kudhibiti dalili za sonona na msongo wa mawazo, lakini ni muhimu pia kuzingatia mbinu nyingine za kujisaidia