Nilipokuwa mdogo nilikuwa nashangaa kwanini tusipoweka chandaru baba anatugombeza sana! Mzee alihakikisha anapita chumbani kila usiku na kama chndarua hakijawekwa vizuri alikuwa anakirekebisha na kuhakikisha tuko ndani ya vyandarua.
Na kweli kwa wakati huo sikumbuki lini nimelazwa hospitali kwasababu ya malaria.
Mwaka 2012 nilipojiunga na Chuo Kikuu, nilikutana na utaratibu tofauti: rafiki zangu hawakupenda kutumia vyandarua kabisa kwa visingizio wakivitumia wanajisikia joto, mara hawapati hewa vizuri hivyo ulikuwa ni mwendo wa kutumia feni tu chumbani.
Cha kushangaza safari za hospitali na kulazwa zilikuwa ni nyingi sana, walau kila wiki mmoja wetu alikuwa anameza dozi ya malaria na kukosa masomo mara kwa mara.
Miezi sita baada ya kujiunga na Chuo, niliumwa malaria mara tano na kulazwa mara moja. Nilikosa wastani wa siku 30 darasani, na athari yake ilikuwa kubwa kimasomo, kiuchumi na kiafya.
Hapo nikagundua kwanini baba alikuwa mkali kwenye mambo ya chandarua. Matumizi ya chandarua yana faida kubwa zaidi ya unavofikiria.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya malaria duniani, April 25, Wizara ya Afya kupitia mpango wa taifa wa kudhibiti malaria (NMMCP) inahakikisha unazijua faida za kutumia chandarua chenye dawa.
1. Kukukinga na malaria
Kama wewe ni mkubwa kama mimi bila shaka unafahamu mateso ya malaria. Ukipata malaria mara moja inakuchukua karibu wiki mbili kukaa sawa na kurejesha nguvu zako kama mwanzo. Hapo hujaongelea muda na gharama ulizotumia.
Mbu waenezao malaria mara nyingi wanakuuma usiku muda ambao unakuwa umelala. Matumizi ya vyandarua vyenye dawa yanafanya mbu wasikupate na hivyo kukukinga dhidi ya kuumwa malaria; faida yake ni kubwa sana kiafya na kiuchumi. Binafsi toka nianze kutumia chandarua chenye dawa, sikumbuki nimeumwa lini tena malaria.
2. Chandarua kitakupa kulala kwa utulivu na usingizi wa starehe
Ili uwe na Afya nzuri ya unapaswa kulala kwa utulivu bila bugudha. Matumizi ya chandarua yanakupa faida hii. Fikiria umelala usiku mara unasikia mbu wanaunguruma masikioni, unaamka saa nane unaanza kufukuza. Unalala tena kidogo mara mbu hao unaamka tena unafukuza.
Unajikuta kati ya masaa nane ya kulala wewe umelala manne, sasa kesho yake utakuwa sawa kweli? Jali afya yako kwa kutumia chandarua.
3. Kuokoa upotevu wa pesa
Kwani neti ni shilingi ngapi? Kataa kutumia elfu 7 kununua chandarua, halafu utumie pesa nyingi kutibu malaria, hasa kwa watoto. Kwako wewe utapoteza hela nyingi pale utakapoumwa muda mrefu na kupoteza kibarua chako.
Ukisisitiza matumizi ya chandarua chenye dawa utaokoa upotevu wa pesa na muda, na uchumi wako utaimarika.
Je, wajua?
- Vyandarua vinavyotolewa sasa tayari vina dawa ya kuua mbu, hivyo hauna haja ya kuweka dawa nyingine. Dawa hii hudumu muda wote mpaka pale chandarua chako kitakapoharibika au kufikia tamati ya matumizi yake.
- Unapaswa kukitunza na kufua chandarua chako pale kitakapochafuka ili kuhakikisha kinadumu na unalala kwenye chandarua kisafi.
- Chandarua chenye dawa kinapaswa kuanikwa kivulini ili kulinda ubora na nguvu ya dawa ya kuuwa mbu.
- Sio kweli kwamba dawa iliyo katika chandarua inapunguza nguvu ya kiume. Huu ni uzushi na kisayansi dawa hii haina madhara yoyote kwa binadamu.
- Vyandarua vyenye Dawa hutolewa bila malipo kupitia kampeni za ugawaji vyandarua kwenye kaya, kupitia kliniki kwa wajawazito na watoto na kupitia shule za msingi. Mama mjamzito anapoanza kliniki anapimwa malaria na kupewa chandarua chenye dawa; pia watoto wanapopatiwa chanjo ya miezi 9 ya surua/rubella nao hupewa chandarua chenye dawa. Ni wajibu wako kutumia nafasi hizo kujipatia chandarua kwa ajili ya kuwalinda uwapendao.
- Matumizi ya chandarua chenye dawa pekee hayatoshi kujikinga na malaria. Njia za nyongeza kama kuvaa nguo zilizofunika mwili, kuchoma na kupaka dawa za kufukuza mbu na kusafisha mazingira vitakuokoa sana na malaria.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.