Sehemu 1: Mifupa Yako Ina Mengi ya Kujifunza! Je Wajua?

Leo ningependa kukutanisha na facts 12 kuhusu mifupa yako ambazo – labda – ulikua huzijui. JE, WAJUA?

 

Je wajua?

Mtoto huzaliwa akiwa na idadi ya mifupa 275 katika mwili wake. Akikua baadhi ya mifupa huungana kutengeneza mifupa mirefu. Akiwa mtu mzima, mifupa hubaki 206 tu.

 

Je wajua?

Mifupa hiyo 206 ndiyo huungana kutengeneza frame ya mwili (skeleton) ambayo unaweza kuifananisha na frame ya ghorofa kabla haijawekwa cement na mchanga.

 

Frame hii ndiyo hutoa umbo na uimara wa mwili na kusimama. Ndiyo hukufanya utembee. Ndiyo hulinda viungo vyako vya ndani kama moyo, mapafu, inni, figo, uti wa mgongo, ubongo na kadhalika.

 

Je wajua?

Mifupa pia ina kazi nyingine za muhimu katika mwili wako ambazo ni kutengeneza seli hai za damu na kutunza baadhi ya madini ambayo yakihitajika na mwili – mfano calcium – basi mifupa huyatoa.

 

Je wajua?

Ugumu wa mifupa yako ni sawa na ugumu wa mwamba (rock). Ni imara sana lakini pia ni myepesi na huchangia asilimia 20 tu ya uzito wako. Ugumu huu husababishwa na uwepo wa madini ya aina mbili: Calcium na phosphorus.

 

Madini haya yameoakiwa katika mifupa kwa mgandamizo mkubwa hivyo kufanya mifupa kuwa migumu na sio rahisi kuvunjika.

 

Je wajua?

Mifupa yako ni seli zanazoishi, huwa na mgao wa damu na mishipa ya ufahamu, na ndio maana huendelea kukua na kuongezeka ukubwa kadiri umri unavyoongezeka.

 

Na huimarika zaidi kulingana na matumizi. Mfano mifupa ya mtu anayefanya mazoezi huwa na seli nyingi na hukomaa zaidi ya mtu aisyefanya mazoezi.

 

 

Pia mfupa wako unaweza kutumika kukuongezea maji ya dripu au damu ikiwa mishipa yako ya damu haionekani. Hii process huitwa “Intraosseous infusion”.

 

Je wajua?

Ndani ya mifupa huwa kuna ukuta (layer) wa sponji wenye matobo matobo (pores) ambayo hutoa nafasi kubwa ndani ya mifupa na ndiyo hufanya mifupa kuwa na uwepesi (lightweight).

 

Je wajua?

Mfupa unapovunjika na kupona, mahala palipopona hutengeneza uimara mkubwa kiasi kwamba huwa pagumu zaidi ya sehemu nyingine za mifupa. Ndio maana sio rahisi kuvunjika mahala pale pale mara ya pili hasa kwa vijana wanaokua.

 

Ikitokea mvunjiko mara kwa mara mahali palipovunjika kabla, basi mtu huyu anaweza kuwa na ugonjwa wa mifupa milaini (brittle bones) uitwao Osteogenesis imperfecta. Ugonjwa huu hutokana na tatizo la vinasaba ambavyo mifupa yako haiimariki ipasavyo.

 

Tatizo hili huanza, mara nyingi, kuonekana utotoni. Na huweza kuwa la wastani au kubwa zaidi. Watoto hawa huweza kuvunjika hata mara tatu kwa mwaka na kukaa hospitali mara nyingi.

 

Kama mwanao anavunjika kirahisi basi anaweza kuwa na tatizo hili. Lakini pia tatizo hili huwa linaweza kuonekana hata kwa watu wazima.

 

Mfupa uhitaji nguvu kubwa kuvunjika. Mfano mfupa wa paja uhitaji nguvu kiasi cha Newton 4000 kuvunjika, kwahiyo ukikuta mtu kavunjika kwa kusukumwa kidogo tu, basi jua ana tatizo la mifupa.

 

Afanye nini sasa?

  • Kwanza anahitaji kuonana na daktari bingwa wa mifupa
  • Pili atahitajika kujiweka mbali na vitu vizito pamoja na mazoezi yanayotumia nguvu kubwa.
  • Tatu anapaswa kujilinda na mivunjiko maana mvunjiko mmoja kwake huchukua muda mrefu sana kupona.

 

Je wajua?

Kadiri unavyokuwa kiumri mifupa yako huweza kuogezeka ugumu mpaka miaka 30. Baada ya hapo ubora (density) huanza kupungua, hivyo kukaribisha urahisi wa kuvunjika.

Ndio maana wachezaji wanapofika miaka 30 huanza kuonekana wamezeeka. Ni kwa sababu wana uwezekano mkubwa wa kupata majeraha ya mifupa kuanzia hapa.

Je wajua?

Wanawake wanapofika kipindi cha hedhi kukoma (menopause) huanza kupata upungufu wa homoni za oestrogen; homoni hizi ni muhimu sana kwa mwanamke katika kila kiungo.

 

Katika mifupa, homoni hizi ndizo huusaidia mfupa kufanya muunganiko na ufanyaji kazi wa seli za mifupa (osteocytes, osteoblasts na osteoclast) ambazo ndizo huusika na ubora wa mfupa.

 

Sasa oestrogen ikiwa ndogo ubora huu hupungua. Upungufu wa homoni hii husababisha tatizo linaitwa osteoporosis ambapo mfupa huwa unachuja na kuwa dhaifu na hivyo huongeza uwezekano wa kuvunjika kirahisi au kuwa na maumivu ya mifupa ya muda mrefu.

 

Ndani ya mada ijayo tutaangalia namna ya kuongeza ubora wa mifupa katika kipindi cha menopause.

 

Je wajua?

Kwakuwa seli za damu huzalishwa katika uboo wa mifupa (bone marrow), athari zozote za sehemu hii inaweza kupelekea mwili kupata seli zenye uwezo mdogo au kupunguza utoaji wa seli nyekundu au nyeupe na kupelekea kansa ya damu.

 

Je wajua?

Mfupa wako huunganishwa na mfupa mwingine katika joint na tishu zinazoitwa ligament. Tishu hizi huwa ni rahisi kuziona hasa kwenye nyama ya ngombe au mbuzi katika joint.

 

Tishu hizi pia huweza kuumia na kuchanika hasa kwenye ajali au michezo pale joint inapogeuka vibaya. Ligament ikiumia (ligament tear) inaweza kuchukua mpaka wiki sita kupona, na maumivu yake huwa kama mvunjiko.

 

Mtu pia hushindwa kutembelea au kutumia kiungo hicho kwa muda huo. Hali hii hutokea sana kwa wanamichezo.

 

Je wajua?

Mfupa unapovunjika huchukua wiki 6 mpaka 8 kupona. Aidha kuna mambo mbalimbali yanayoweza kufanya upone au usipone haraka. Mfano lishe nzuri yenye vitamin C, D na K huweza kuiharakisha mifupa yako kupona mapema zaidi.

 

Uvutaji wa sigara, utapiamlo, magonjwa kama kisukari huchelewesha kupona kwa mifupa yako.

 

Kuna msemo kuwa kufanya mapenzi wakati una mvunjiko huchelewesha kupona. Ulishawahi kuambiwa hivyo na wataalamu wa afya?

 

Ukweli ni kwamba hilo bado halijathibitishwa ila amini lisemwalo lipo. Kuna mambo hayajathibitishwa kisayansi ila kutokana na uzoefu unaoonekana wazi.

 

Mwisho

Kuna elimu nyingi kuhusu mifupa. Kumbuka ni katika kupata elimu ya kitu ndipo unaweza kujua namna ya kukilinda.

 

Je, unajua namna ya kufanya ili kuimarisha na kulinda mifupa yako? Je, unafahamu namna ya kupunguza matatizo ya mifupa uzeeni hasa kwa wanawake? Je, unajua nini cha kufanya ukiumia mfupa au joint?

 

Basi endelea kufuatilia sehemu ya pili ya makala hii. Kwa maoni yeyote, usisahau kuniandikia hapo chini kwenye comments.

 

Asante.

2 thoughts on “Sehemu 1: Mifupa Yako Ina Mengi ya Kujifunza! Je Wajua?”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW