Mara ya kwanza kusikia presha ya mimba ulikuwa wapi au ulikuwa na hali gani?
Binafsi niliifahamu presha ya mimba wakati niko katika mafunzo ya udaktari. Kabla ya hapo nilikuwa sina taarifa yoyote (mweupe kabisa) ndio maana nahisi nawewe waweza kuwa hauna ufahamu wa elimu hii.
Zamani nilidhani presha ya mimba ni ile hofu anayokuwa nayo mama wakati wa mimba na kabla ya kujifungua, kumbe wapi! Isije ikawa na wewe unawaza hivyo.
Ujauzito ni hali ambayo huja na mabadiliko mengi kwa mwili wa mama. Kupanda kwa presha wakati wa mimba ni mojawapo ya matokeo ya ujauzito ukiachana na maswala mengine kama uchovu, kifafa cha mimba, kupungukiwa damu, kuvimba miguu, moyo kutanuka na kadhalika.
Mimba inapotungwa huleta mabadiliko katika mwili wa mwanamke ambayo husababishwa na homoni za mimba. Maziwa hukua, maji huongezeka mwilini, uzito huongezeka, rangi ya ngozi huweza kubadilika, hamu ya vyakula fulani hupotea au huongezeka na baadhi hupelekea presha ya damu kupanda.
Presha ya mimba ni nini hasa?
Hili ni shinikizo la kupanda la damu linalotokea kwa mama mjamzito mara nyingi kuanzia wiki ya 20 ya mimba na kuendelea mpaka muda wa kujifungua.
Presha ikitokea kabla ya muda huu, chini ya wiki ishirini, basi mara nyingi huenda mama alikuwa nayo kabla ya ujauzito.
Inasababishwa na nini?
Mimba inapokuwa inatungwa huweza kujikuta inajishikiza vibaya kwenye ukuta wa uzazi na hivyo kufanya damu isiende vizuri kupitia mishipa kati ya mama na mtoto. Hali hii huitwa faulty implantation kwa kizungu.
Sasa kutokana na hali hii, utoaji wa homoni zinazopelekea presha ya damu huweza kuogezeka.
Hali hii ndio hufaya presha ya mama mjamzito kupanda na kupelekea presha ya mimba (pregnancy induced hypertension).
Pamoja na sababu hiyo, kuna vichocheo vinavyoweza kupelekea mfuko wa uzazi kujipandikiza vibaya mfano mimba katika umri mdogo, uwepo wa vinasaba vya hali hii katika familia, kubadili baba (mimba ya baba mwingine), mama kuwa tayari ana tatizo la presha, uvutaji wa sigara, na kadhalika.
Kifafa cha Mimba
Wakati mwingine presha ya mimba inaweza kwenda mbali zaidi na kuleta madhara katika figo na ubongo hivyo kupelekea madhara makubwa yajulikanayo kama presha ya hatari ya mimba (Pre – eclampsia) au kupelekea kifafa cha mimba (eclampsia).
Dalili za hatari ya hali hii zinaweza kuanza na presha kupanda (hii huwa haionekani mapema), miguu kuvimba, kichwa kuuma, maumivu ya tumbo, kiasi kidogo cha mkojo na kadhalika. Dalili hizi ni moja ya vitangulizi (Pre-eclampsia) kabla ya mama kupata kifafa cha mimba.
Hali hii inaweza kumpata mama mjamzito hasa wale ambao hawaudhurii kliniki ipasavyo kutokana na uelewa mdogo au kutojali. Kwa wajawazito wanaohudhuria kliniki vizuri, hali hii hutambulika kwa wakati na kutibika vizuri tu.
Presha ya mimba na kifafa cha mimba ni miongoni ya changamoto za mimba ambazo dunia imefanikiwa kupambana nazo kwa mafanikio ya hali ya juu na kilichobaki ni kuongeza uelewa wa afya kwa wagonjwa.
Una mpango wa kubeba mimba?
Katika utafiti wangu wa miaka zaidi ya mitatu kuhusu mama wajawazito nimeshuhudia mambo kadhaa kama ifuatavyo:
- Presha za mimba huleta madhara makubwa zaidi kwa wajawazito wasiohudhuria kliniki ipasavyo – aidha kwa kutojali, kutojua au kuhisi kama ni wazoefu sana wa mimba.
- Presha ya mimba huweza kusababisha mtoto kufa tumboni au wote, mama na mtoto, kufa endapo haijadhibitiwa kwa wakati.
- Uvutaji wa sigara ni moja ya vitu vinavyoweza kuzidisha uwezekano wa presha ya mimba kupanda na kuwa hatari kwa mama na mtoto.
- Kifafa cha mimba kinachotokea nyumbani kama presha haikudhibitiwa mapema hupelekea mtoto tumboni kufa (huwa mtoto anaathiriwa sana na kifafa cha mama).
- Kubeba mimba katika umri mdogo huchangia sana mama kupata presha ya mimba, hivyo jiepushe na mimba za udogoni. Walau shika mimba kwanzia miaka 20.
- Wakati mwingine huwezi kuzuia presha yako isipande, cha muhimu ni kuwa karibu na watoa huduma wa afya ili wakusaidie.
Kwa kumalizia, tambua kwamba dalili za presha huwa sio dalili wazi sana, mara nyingi sio rahisi kutambua presha yako iko juu mpaka uwe muhudhuriaji mzuri wa kliniki.
Kuwa mjanja, usiwe mzembe, presha ya mimba ni hatari kwa afya yako na ya mwanao. Hakikisha unakuwa karibu na msaada wa afya.
AbiteAfya tuna maktaba ya vitabu vya afya kwa ajili yako, ingia dukani kwetu at shop.abiteafya.com kuona kipi kinakugusa.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Very informative dr Ansbert. Thanks for the info..
Thank you so much, you’re welcome miss Adele