“Prebiotics na Probiotics” – Mapacha Wanaolinda Mfumo Wako wa Chakula

Chukulia kwamba mfumo wako wa chakula ni shamba, ambapo viumbe – kwa maana ya microrganisms kama bakteria – hufanya kazi kwa pamoja ili kuleta ustawi wa mazao. Prebiotics ni kama mbolea katika ‘shamba’. Wakati probiotics ni kama mbegu au uoto wenye manufaa katika shamba lako. Tukishaelewa huu mfanano turudi katika bailojia ya mfumo wa chakula.

 

Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ni maskani kwa zaidi ya bakteria trilioni 10. Mkusanyiko huu hujulikana kama gut microbiota. Bakteria huwa wana faida kubwa ndani ya mwili ikiwemo kuzalisha baadhi ya virutubisho, kusaidia umeng’enyaji wa chakula, na kusaidia mfumo wa kinga ndani ya mwili.

 

Uwiano kati ya bakteria wazuri na bakteria wabaya – ambao hujulikana kama normal flora – ukicheza  hupelekea matatizo katika mfumo wa chakula  na hata nje ya mfumo wa chakula.

 

Prebiotics ni nini hasa?

Prebiotics ni nyuzinyuzi, yaani fibers, za mimea ambazo hustawisha bakteria wazuri ndani ya mfumo wa chakula (tumbo, utumbo mdogo na utumbo mkubwa). Bakteria ndani ya tumbo hujipatia mahitaji yao ya chakula kutoka kwenye prebiotics.

 

Nyuzinyuzi hizi zitokanazo na mimea huwa hazimeng’enyenywi katika mfumo wa chakula. Ni kama mbolea katika mkitadha wa shamba.

Chukulia kwamba prebiotics ni chakula ambacho bakteria wazuri ndani ya tumbo hula. Unapokula vyakula ambavyo havina nyuzinyuzi, jua kwamba rafiki zako hawa wanashinda njaa!

Zingatia: Inashauriwa kujipatia kiasi cha gramu 150 za fibers kwa siku. Kutokana na mabadaliko katika mfumo wetu wa chakula, wengi watu tunapata chini ya gramu 15. Tunakula vyakula vilivyowisha kukobolewa na kuondoshewa sehemu ya nyuzinyuzi. Mfano ugali wa sembe na vyakula vingine vya ngano.

 

Nitapata wapi Prebiotics kwa wingi?

Vyakula vingi vitokanavyo na mimea ambavyo havijachakatwa vina prebiotics kwa wingi. Mfano wa vyakula hivyo ni;

  • Nafaka na vyakula vya mbegu mfano maharage, karange, na kunde
  • Mboga za majani kama spinanchi, kabichi, broccoli, mulenda
  • Viungo kama vitunguu maji na vitunguu swaumu
  • Matunda kama parachichi, mapera, berries
  • Ndizi mbichi (kijani)

 

 

Hongera! Sasa unafahamu ni wapi unaweza kupata vyakula vyenye nyuzinyuzi ambavyo vinatajwa kuhusika katika kukufanya ujisikie vizuri na mwenye furaha, kuwa na kinga imara, na hata kuishi maisha marefu.

 

Je, Wajua?

Watu waliopo kwenye ndoa hudhaniwa kuwa wanafanana kwa muonekano. Kuna sababu ya kisayansi ya kuelezea hili. Watu waliokaa pamoja kwa muda mrefu huwa na bakteria wanaokaribia kufanana ndani ya mfumo wa chakula. Bakteria ndio huhusika na hisia za huzuni, furaha au chuki na mwitikio wa hisia hizi kwenye uso.

 

Probiotics ni nini?

Tofauti na prebiotics, probiotics ni bakteria wazuri ama wenye afya ambao tunawapata katika vyakula vilivyochachushwa (fermented foods). Probiotics ni bakteria hai ambao wanafanana na bakteria wazuri walio ndani ya mwili. Kumbuka ule mfano wetu wa shamba; probiotics ni kama mbegu nzuri au mimea yenye manufaa shambani mwako.

 

Faida za Probiotics Mwilini

Probiotics huongeza uwiano wa bakteria wazuri mwilini dhidi ya wale wabaya. Zifuatazo ni baadhi tu ya faida za probiotics ndani ya mwili wako:

 

1. Huimarisha kinga ya mwili

Kama tulivyoona hapo awali sehemu kubwa ya kinga ya mwili ipo katika mfumo wa chakula hususani utumbo mkubwa, ambao huchangizwa na uwiano wa bakteria wabaya na wale wazuri. Probiotics huimarisha kinga na kusaidia mwili kukabiliana na maambukizi yaletwayo na bakteria na baadhi ya virusi.

 

2. Huzuia magonjwa na pia hutumika katika matibabu

Probiotics hutumika kutibu na kuzuia magonjwa ya mfumo wa chakula kama Inflammatory Bowel Disease (IBD), Irritable Bowel Syndrome (IBS) na allergy ya vyakula. Magonjwa haya kwa kiasi kikubwa husababishwa na kinga ya mwili kuushambulia mfumo wa chakula kutokana na sababu mblimbali ikiwemo gluten iliyo kwenye ngano.

 

Kwa wadada: Tofauti na magonjwa ya zinaa; sababu nyingine ya kutokwa na ute mchafu na wenye harufu mbaya ukeni ni kuwa na idadi kubwa ya bakteria wabaya kuliko wazuri ukeni. Probiotics hurejesha uwiano huu sawa.

 

3. Huimarisha Afya ya mfumo wa chakula

Vyakula vilivyoandaliwa ili kuhifadhi probiotics husaidia kuponesha mfumo wa chakula unaovuja. Hivyo huongeza uwezo wa kuta za utumbo mwembaba kufyonza virutubisho vya vyakula. Lakini pia hupunguza tumbo kuvuruga.

 

Vyakula gani vyenye hizi Probiotics?

Probiotics sio dhana mbya kabisa, kila jamii imekuwa ina aina ya vyakula vinavyoandaliwa kwa namna inayohifadhi probiotics. Watanzania tuna togwa, Wajerumani wana sauerkraut, na Wakorea wana kimchi.

 

Vyakula na vinywaji vingi vilivyoandalia kwa kuchachishwa yaani fermentation huwa na kiasi kingi cha bakteria hai. Vyakula na vinywaji hivyo ni kama maziwa mgando, togwa, yogati, sauerkraut, kombucha, brem, na kefrir. Pia kuna vidonge vyenye probiotic supplements.

 

 

Katika mazingira ya kawaida ya kitanzania ni rahisi kuandaa vyakula na vinywaji kama togwa, maziwa ya mgando na sauerkraut. Unaweza kuandaa uji wa mtama, na ukauacha kwa muda wa saa 72 au zaidi ili uchache. Utakuwa umepata probiotics wa kutosha.

 

Sauerkraut haina maajabu yoyote. Hii ni kabeji iliyoandaliwa kwa kukatwa vipande vidogovidogo kisha kuhifadhiwa kwenye chupa ya kioo ambayo haipitishi hewa na kuwekwa mbali na mwanga wa jua. Unaweza kwenda YouTube kuangalia video za namna ya kuandaa sauerkraut.

 

Zingatia yafuatayo

Probiotics haziwezi kuondosha madhara ya vitu unavyotumia kila siku vinavyoharibu afya ya mfumo wako wa chakula pamoja na kuvuruga uwiano wa bakteria wazuri dhidi ya wale wabaya.

 

Mazoea kama ulaji wa sukari kupindukia, allergy ya gluten iliyo kwenye ngano, msongo wa mawazo uliokithiri, matumzi holela ya dawa za kuua bakteria pamoja na unywaji wa pombe yatafanya usione faida za probiotics moja kwa moja. Achana na vitu hivi, utafurahia probiotics.

 

Asante kwa kuendelea kusoma makala zetu na kuwa mmoja wa wafuasi pendwa wa blogu yetu. Usisahau kutoa maoni, kuuliza swali, na kuwashirikisha wengine makala zetu.

2 thoughts on ““Prebiotics na Probiotics” – Mapacha Wanaolinda Mfumo Wako wa Chakula”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW