Njia Pekee 4 Zitakozokusaidia Kufikia Malengo Yako ya Afya ya 2024

Kila mwisho na mwanzo wa mwaka, mamilioni ya watu huweka malengo au maazimio ya mwaka mpya.

 

Lakini cha ajabu, katika kila watu 100 waliojiwekea malengo au maazimio ya mwaka mpya, watu 23 huachana nayo mara tu baada ya wiki ya kwanza ya mwezi Januari, huku wengine 43 huachana nayo katikati ya mwezi wa pili.

 

Setting goals for 2024

Aina za malengo ya kiafya

Malengo au maazimio ya mwaka mpya, yaani New Year’s Resolutions, yanaweza kuwa malengo rahisi au magumu kutegemea na unavyoyachukulia.

 

Malengo rahisi ni kama kutandika kitanda kila siku asubuhi, kuanzisha utaratibu wa kuandika hisia na mawazo yako, na kupata mlo wako wa mwisho kabla ya saa mbili usiku.

 

Malengo pia yanaweza kuwa kama ile changamoto ya kupunguza uzito, ambayo karibia asilimia 45 ya watu duniani wanajaribu kupunguza kilo.

 

Mengine ni kubadili mfumo wa chakula na unywaji, ikiwa ni pamoja na kuachana na kula vyakula visivyo na tija mwilini (junk foods). Zaidi ya hapo, unaweza kuwa na malengo ya kuboresha muonekano wa mwili kwa mazoezi.

 

Ili kurahisha utekelezaji wa malengo ya mwaka mpya, unaweza yagawa katika makundi kuu mawili.

 

Kundi la kwanza ni malengo yanayohusisha kujenga tabia mpya au kuendeleza iliyokuwepo. Malengo haya ni kama kuanza kufanya mazoezi, kulala mapema, kunywa maji ya kutosha kila siku, na kuwa na wakati bora na familia yako.

 

Kundi la pili ni yale malengo yanayohusisha kuachana na tabia au mazoea ambayo huhitaji kuendelea nayo katika mwaka mwingine. Haya huhusisha kuacha kunywa pombe na vinywaji vingine vinavyoharibu afya yako, kupunguza muda unaoutumia mtandanoni au kuaangalia TV, au kuacha kuvuta sigara.

 

Kwanini watu huishia njiani?

Ni watu 9 tu kati ya wale 100 ambao hutimiza malengo yao ya mwaka. Huenda wewe na mimi, ni kati ya hao watu 91 ambao hatutoboi hadi mwisho wa mwaka. Hii hutonakana na sababu zifuatazo;

1. Kutokuwa tayari

Kuweka malengo wakati ambao hauko tayari kubadilika. Ingawa wataalam wa tabia ya binadamu wanapendekeza wakati mzuri wa kuanzisha tabia mpya ni wakati ambapo kuna badililo la mwaka au mwezi au hata sehemu ya kuishi au kazi, watu wengi huwa hawako tayari kubadilika kwa wakati huu.

 

Ikiwa una nia ya kubadilika, mabadiliko ya majira na mahali yanaweza kukurahisishia kazi yako.

 

2. Kukosa ustahimilivu

Sababu ya pili ni kushindwa kustahimili vikwazo. Lengo au azimio lolote hata liwe dogo kiasi gani, huwa lina vikwazo ndani yake. Linaweza kuwa rahisi tu kama kupiga mswaki mara baada ya kula chakula cha usiku.

 

Kushindwa kuvibainisha vikwazo na kupanga namna ya kuvishinda ni uhakika kwamba hautatoboa.

3. Kushindwa kuwajibika

Unahitaji kuwajibika ili kujenga tabia mpya. Katika hili, unahitaji mdau wa kukusimamia. Huyu mdau anaweza kuwa application ya kwenye simu itakayokukumbusha kunywa maji kila baada ya dakika arobaini au reminders za muda wa kufanya mazoezi.

 

Tafiti zinaonyesha kuwa endapo ukiweka malengo yako bila ya mdau katika uwajibikaji, yaani accountability partner, basi unajiandaa kufeli mapema sana.

 

4. Malengo yasiyopimika

Sababu nyingine ni kutokuweka malengo ambayo hayakupi changamoto lakini pia hayapimilki. Mfano, unahitaji kupunguza uzito kutoka kilo 110 mpaka 80 ndani ya mwaka 2024.

 

Hii inawezekana. Ni changamoto kubwa kiukweli lakini usipoenda mbali zaidi na kuiweka katika malengo ya wiki na mwezi, uwezekano wa kutokutoboa au kuongezeka kilo mpaka 123 katika huu mwaka ni mkubwa.

 

Namna ya kutimiza malengo yako ya kiafya mwaka 2024

Socrates, mwanafalsafa wa Kigriki, anasema “Siri ya mabadiliko haipo katika kupambana na mazoea ya zamani, bali katika kujenga tabia mpya.”

 

Kumbuka; lengo kuu la kuweka maazimio ni kujenga taswira mpya ya maisha yako. Lengo sio kupunguza uzito tu, bali ni kujenga afya njema.

 

Kanuni kuu 4 za kujenga tabia mpya

Kuna kanuni kuu nne katika ujenzi wa tabia mpya, nazo ni kuifanya tabia ionekane mara kwa mara, kuifanya iwe ya kuvutia, kuirahisisha kuifanya, na kuifanya iwe ya kuridhisha.

 

Kama unawaza kuanza kufanya mazoezi, kwa mfano, ili kulifikia lengo hili ambalo linahusisha ujenzi wa tabia mpya; unaweza kuweka ishara za kukukumbusha mara kwa mara, inaweza kuwa ni picha, au application katika simu yako.

 

Fanya mazoezi yanayokuvutia, katika hili unaweza kuhusisha kuvutiwa na muonekano wako mpya baada ya siku 365.

 

Kuhusu kuifanya tabia hii iwe rahisi, unahitajika kupanga muda ambao ni rafiki kwako, na kuchagua aina ya mazoezi kutokana na mahali ulipo. Inaweza kuwa gym, au mazoezi ya kukimbia, mazoezi ya nguvu kwa muda mfupi (HIITS), ama mazoezi ya nyumbani kwa ajili ya kujenga misuli (calisthenics).

 

Muda unaweza kuwa ni asubuhi, au jioni baada ya kazi. Ili kurahisha tabia, unaweza kuwa unatembea na nguo za mazoezi kwenye begi, au kuziweka sehemu rahisi kuzifikia.

 

Hakuna kitu kinavutia kama kuwa na muonekano mzuri. Ni status symbol, hakuna mtu anayeweza kukupatia hilo. Umeonesha nidhamu kuupata. Hii ndio dhana ya kuridhisha katika ujenzi wa tabia.

 

Pia, unaweza kujipa bonus kila baada ya mazoezi, ikiwa ni pamoja na kujinunulia vitu ambavyo umekuwa ukivitamani.

 

Unavunjaje mazoea mabaya?

Huenda mwaka huu umedhamiria kuacha kula vyakula visivyo na tija mwilini yaani junkies. Inaweza kuwa ni kuacha kula vyakula au vinywaji vyenye sukari, chipsi, soda, pipi, na cookies nyingine. Unaanzaje kuvunja haya mazoea ya kila siku?

 

Katika hili tunahitaji kwenda kinyume na zile kanuni nne za mara ya kwanza. Yaani ifanye hii tabia isiwe inaonekana mara kwa mara, isikuvutie, ngumu kuifanya, na isiyoridhisha. Kumbuka vitu vyote vitamu na junkies zinaonekana mara kwa mara, matangazo yake yametengenezwa kumvutia mlaji, hupatikana kwa urahisi, na ukivitumia unahisi kupata burudiko mwilini.

 

Hutashinda vita hii ikiwa umejaza friji yako na vyakula na vinywaji vyenye sukari. Ni muhimu kuvifanya hivi vitu viwe vigumu kuvifikia na wakati mwingine hata kuviona. Hivi ndivyo unaifunza nia yako ambayo ni dhaifu na hujaribiwa kwa kuona.

 

Huhitaji kuwa snacks mezani kwako. Manunuzi yako ya kila mwisho wa wiki inabidi yajazwe na vyakula vingine kama mayai, samaki, mboga za majani, nafaka na matunda.

 

Wakati mwingine ukijaribiwa kutumia vyakula hivi, tumia tunda au kunywa maji.

 

Kila mara unapochagua vyakula vizuri dhidi ya junkies, fikiria hii ni kama kura ya ndio kwa maisha yenye afya na tija. Hii hisia inaridhisha na kukupa nguvu ya kuendelea kupiga kura nyingi za ndio.

 

Umuhimu wa wadau katika malengo yako

Unakumbuka kuwa sababu moja wapo ya asilimia 23 ya watu kuachana na malengo yao ndani wiki ya kwanza ni kukosa uwajibikaji? Unahitaji kuwajibika kwako mwenyewe. Ili kuongeza kiwango cha uwajibikaji, utahitaji accountability partner. Hawa ni wadau katika uwajibikaji wako.

 

 

Inaweza kuwa ni familia yako, mwenzi wako, rafiki zako wa karibu, au wafanyakazi wenzako.

 

Pia anaweza kuwa ni mtaalam wa maendeleo binafsi, yaani personal development coach. Ukweli ni kwamba unahitaji mtu kama huyu maishani mwako.

 

Unaweza pia kujiunga na makundi katika jamii yako, au hata mtandaoni, yenye lengo kama lako. Mfano vikundi vya watu wanaofanya mazoezi ama wanaopambana kupunguza uzito.

 

Mwambie mdau wako huu mwaka sinywi pombe. Hii itakufanya uone ulazima wa kutimiza ahadi, lakini pia kukupa mtu wa kukuhoji na kukusimamia. Kama huwa mnakunywa wote kila Ijumaa kujipongeza baada ya wiki ngumu kazini, rafiki yako atakutoa kwenye hiyo mipango.

 

Accountability partner sio lazima awe mtu. Inaweza kuwa ni application ya kwenye simu kama Supporti na Accountable2You.

 

Usisahau kufuatilia mwenendo wa malengo yako

Unahitaji kuwa na lengo moja kubwa, na kisha kutengeneza hatua za kila siku za kufikia lengo lako. Mfumo wa kufuatilia unaweza kuwa rahisi kama kuwa na daftari au kalenda ambapo utakuwa unazungushia tarehe ambayo umefikia lengo lako.

 

Kuona mnyororo wa tarehe ukiwa kamili, kunatia hamasa ya kusonga mbele.

 

Kuna applications pia za kwenye simu kama Zero na BodyFast kwa watu wanaofanya mfungo tiba kwa sababu mbalimbali, na HabitBull kwa watu wanaojenga tabia mpya.

 

“Ni ndefu sana, sijasoma yote…”

Usijali, kiufupi nilikua nazungumzia na kuwekea msisitizo kwamba:

  • Sio rahisi kufikia maazimio au malengo ya mwaka mpya. 91% ya watu huwa hawatoboi.
  • Ili kuwa moja ya kati ya wale 9%, unahitajika kujenga tabia zitakazobadili unavyojiona.
  • Kuna kanuni nne za ujenzi wa tabia mpya; kuifanya tabia mpya inaonekana mara kwa mara, kuifanya iwe ya kuvutia, kuirahisisha, na kuifanya iwe ya kuridhisha.
  • Usiwe pekee yako, unawahitaji sana wadau. Wasitue.
  • Furahia ushindi mdogo njiani. Fuatilia maendeleo yako. Na usione shida kujispoil.

 

Una malengo ya kujenga na kuimarisha afya yako katika mwaka mpya wa 2024? Usisite kuwasiliana nasi moja kwa moja kupitia kurasa hii.

 

Tunakutakia heri na fanaka wewe na familia yako katika mwaka mpya 2024.

2 thoughts on “Njia Pekee 4 Zitakozokusaidia Kufikia Malengo Yako ya Afya ya 2024”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW