Njia 3 za Kiafya za Kuwa Mbunifu

Ubunifu ni kitu gani? Kuna haja ya kuwa mbunifu?  

Wanasayansi wanaelezea  ubunifu kama uwezo wa kuzalisha mawazo mapya yenye kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya kila siku. Kama wewe ni mdadisi wa mambo utakubaliana na mimi kwamba, kwa sehemu kubwa, maisha magumu uletwa na ukosefu wa ubunifu.

 

Maana yake, kushindwa kuzalisha na kufanyia kazi mawazo mapya ni kikwazo kikubwa katika mafanikio ya mtu yeyote. 

 

Unajua kwanini makampuni makubwa hutumia pesa kubwa sana kupata wafanyakazi wabunifu? Ni kwasababu ubunifu ndio chanzo kikubwa cha mapato kwa makampuni hayo. 

 

Mwanasayansi Albert Einsten katika ujumbe wake maarufu alisema, “Ubunifu ni kuona kila kitu ambacho kila mmoja ameona na kuwaza tofauti na vile ambavyo kila mmoja anakiwazia kitu hicho. 

 

Je, kuna njia za kiafya za kuongeza ubunifu wako? Jibu ni ndiyo!  

Ukweli ni kwamba kila mmoja amezaliwa mbunifu na ndio maana wakati ukiwa mtoto ulikuwa msumbufu sana kwa wazazi kwa sababau ya ile chemchemu ya udadisi iliyomo ndani yako.

 

 

Kwa bahati mbaya kadiri watu wanavyokua hupoteza ile hali na kujikuta wanakwenda na speed ya dunia. Sababu kubwa ni ubongo wako kujaa mambo mengi amabyo hufanya ubongo kukosa utulivu na focus. 

 

Kiafya, njia pekee ya kuleta ubunifu ndani yako ni kurudisha afya nzuri ya ubongo wako. Ubongo wako ukiwa na afya, lazima uwe mbunifu. 

 

Mambo yanayofanya ubongo wako ushindwe kutenegeneza mawazo mapya ni pamoja na  taarifa nyingi kutoka kwenye vyombo vya habari (hasahasa mitandao ya kijamii), kukosa utulivu, kukaa maeneo yenye kelele, kukosa muda wa kupumzika, n.k.  

 

Haya yote huchosha ubongo wako na hivyo uwezo wake wa udadisi hupungua sana. Hii ndio inakutofautisha na kipindi cha utoto wako ambapo haukuwa na mambo mengi kichwani hivyo kila siku ulikuwa na mawazo ya kutengeneza vitu vipya. 

 

Zifuatazo ni njia tatu za kiafya za kuufanya ubongo wako kuwa na uwezo mkubwa wa ubunifu: 

 

1. Mazoezi 

Tunaposema mazoezi watu wengi huguna na kubeza sana bila kujua sayansi ambayo iko nyuma ya faida za mazoezi kwenye ubongo wao.  Mimi ni shahidi wa hili kwa kiasi kikubwa. 

 

Mwaka 2020 nilianza mazoezi ya kukimbia kila subuhi; hii ilikuwa baada ya kusoma na kumaliza vitabu viwili, kimoja cha 5 Am Club kilichoandikwa na Robin Sharma na kingine ni Shoe Dog kilichoandikwa na Phill Knight (Muanzilishi wa kampuni ya Nike). Wote hawa walinihamasisha kuanza mazoezi, hasa kukimbia asubuhi. 

 

Kila nilipokuwa nakimbia asubuhi nilikuwa narudi na majibu ya changamoto mbalimbali zilizokuwa zinatutatiza mimi na mke wangu. Ilifika muda nikaanza kutegemea kukimbia ili kupata majibu ya changamoto zangu nyingi na majibu mengi yamenifikisha hapa nilipo. 

 

 

Sayansi yake hapa ni mkwamba kukimbia kunapunguza msongo wa mawazo, kunaleta mood nzuri na hali ya furaha. Stress inapokuwa chini na mood inapokuwa nzuri basi ubongo huwa na focus kubwa ya kuwaza nje ya box.  

 

Ndio maana wakati wa mazoezi unaweza kupata majibu na mawazo mapya ya changamoto yoyote inayokusumbua. Kwasasa mimi ni Daktari mfanyabiashara na nategemea zaidi mazoezi kupata ubunifu. 

 

Unataka kuwa mbunifu? Anza jogging, utaona mabadiliko makubwa katika uwezo wako wa kuzalisha mawazo mapya. Hii sio kila mtu anaweza kufanya na ndio maana wabunifu katika dunia hii ni wachache. 

 

Angalizo: Mazoezi yanayoweza kuweka ubongo vizuri ni mengi ikiwemo kunyanyua uzito, kutembea umbali fulani, kucheza mpira, kucheza mziki, kuruka kamba, n.k.  

 

Lakini isiwe katika kikundi cha watu. Lengo hapa ni kufanya mazoezi katika mazingira ya peke yako ili uweze kuwa na utulivu wa kutumia wakati huu kuwaza na kujenga mawazo kichwani.  

 

Ukifanya mzoezi katika kikundi cha watu hutapata faida hizi. Ndio maana kukimbia au kutembea peke yako huwa ni zoezi bora zaidi. 

 

2. Mazingira  

Ulishawahi kujiuliza kwanini watu wenye mafanikio hupenda kuishi sehemu zilizojitenga na zenye utulivu? Unadhani ni kwasababau wanapenda kujitenga na jamii? Sio kweli! Sababu kubwa ni kwamba wanatafuta mazingira yenye utulivu. 

 

Au unajua kwanini vyuo vikuu na shule maarufu zilijengwa maeneo ya mbali na miji? Angalia Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam (UDSM), Dodoma (UDOM), Sokoine, na Mzumbe kwanini havikujengwa katikakati ya miji?  

 

Sio kwamba walishindwa  kupata viwanja mjini, sababu ni kuweka mazingira ya utulivu kwa ajili ya wanafunzi  na waalimu wao. 

 

Mazingira ya utulivu yanaleta ubunifu sana; ubongo unapokuwa katika mazingira ya ukimya ndipo mawazo na ubunifu huja. 

 

 

Kuna tofauti kubwa sana ya umakini wa ubongo kati ya mtu anayekaa Manzese na mtu anayekaa Mbezi Beach. Ukikaa sehemu zenye makelele sana ubongo wako haupati utulivu wa kutosha na kila ukitaka kuwaza kuna changamoto itatokea.  

 

Mara mlevi kapita, majirani wanagombana, umeme umekatika, kelele za mwizi, joto kali, harufu mbaya ya choo, maji machafu, n.k.  

 

Vita ni nyingi sana kiasi kwamba huwezi kupata wasaa wa kuwa mbunifu. Ndio maana watu wakitaka kuwa wabunifu huenda mbali na makazi ya watu na kuweka kambi huko kwa muda. 

 

Billionea Bill Gates huwa ana utaratibu wake wa muda mrefu; kila anapotaka mawazo mapya au anapokutana na changamoto inayohitaji majibu mapya,  husafiri na kwenda mbali ya mji kwenye  nyumba yake ambayo anaiita thinking house. 

 

Huchukua vitabu vyake na kuweka kambi huko hata kwa wiki mbili na akirudi hurudi na majibu ya changamoto. 

 

Kwa miaka miwili nimekuwa nikifanya tabia hii ya Bill Gates, japo kwa udogo. Huwa  naendesha gari na kwenda mazingira ya nje ya mji kwenda kusali, kuwaza, na kutafuta majibu ya maswali yangu na kila mara lazima nije na wazo jipya. 

  

Inawezekana huwezi kuhama hapo ulipo kwa sasa lakini bado unaweza ukawa unatenga muda wa kwenda mahala penye ukimya na kupata walau masaa 4 ya utulivu ili kuwaza na kupata mawazo ya utofauti. 

 

3. Lala vizuri 

Kama wewe ni mimiliki wa simu janja (smartphone) bila shaka umegundua kwamba kuna muda simu yako inahitaji kupumzishwa ili system ifanye updates.

 

Kwa baadhi ya simu kama Apple na Huawei, huwa zinazima kwa kuingia kwenye restart mode na kuji’reset upya na baada ya apo simu inakuwa na speed ya kutosha kama mpya. 

 

Moja kati ya vitu vinavyoseti ubongo wako kuwa mpya na safi, kwa ajili ya kuwaza vizuri, ni kulala vizuri. Hapa bila shaka wewe ni shahidi.

 

 

Ukilala vizuri usiku walau masaa 6 na kuamka asubuhi huwa unajiskiaje?  Ukilala masaa machache au kuamka hovyo usiku, asubuhi ukiamka umechoka huwa unajiskiaje?  

 

Mtu asiyelala vizuri huwa ana mood mbaya, ni rahisi kuwa na hasira, ni rahisi kufanya makosa kadhaa hasa kwenye mambo yanayohitaji ubunifu mbukwa. 

 

Leo hii nikirudi katika ule umri wangu wa sekondari na chuo, nitajishauri kutosoma mpaka asubuhi. Nitajishauri kusoma kwa bidiii hasa kutumia muda wangu vizuri mchana na kulala muda wa kutosha usiku, labda ningeweza kufaulu zaidi ya nilivyofaulu kipindi kile. 

 

Sikujua kwa kipindi kile madhara yake kwenye ubongo lakini kwa sasa nimeshajua hasara yake. 

 

Ubunifu na mawazo mapya yanakuja kichwani pale ubongo wako unapokuwa kwenye free mode, ndio maana mtu anaweza kuwa amelala, akaamka, akaja na suluhisho.  

 

Ndiomaaana wanasayansi wengi kama Newton na Albert Einsten walikuwa wakipata mawazo mapya katika mazingira tulivu. 

 

Zoezi kama hili kwenye ubongo wa binadamu huja kwa kulala muda wa kutosha, walau kuanzia masaa 6 na kuendelea. 

 

Usipolala vizuri kuna uwezekano mkubwa ubunifu wako kuwa mdogo na hivyo kushindwa kuwaza project yako katika yale mapana yanayotakiwa. 

 

Unawezaje kulala vizuri?

Kwanza, weka muda maalumu wa kulala ambao kwa asilimia kubwa unaheshimu muda huo mfano saa tano usiku mpaka 11 alfajiri. Kuwa obsessed na muda huu kiasi kwamba ukifika tu lazima ukukute kitandani.  

 

Bahati nzuri ukishajenga mazoea haya, muda huu ukifika utaona unaanza kuchoka na kusinzia; basi huo ndio muda wako wa kulala. Watu waliofanikiwa hawana mchezo kabisa na muda wao wa kulala labda itokee dharula tu. 

 

Pili, unahitaji usingizi wenye ubora. Hapa hakikisha unaishi mazingira yasiyo na kelele ya miziki, baa na mpira. Sehemu za kuishi zipo nyingi, epuka nyumba za uswahilini.  

 

Pia jitahidi chumba chako kisiwe na mwanga sana na pia hakikisha umezima simu yako au kuiweke in silent mode ili kuepuka kuamshwa na notifications. 

 

Usile sana usiku na epuka kunywa maji mengi usiku, yawe kiasi ili usiamke usiku wa manane. Kuamka usiku wa manane inaharibu ile cycle ya mwili na kesho yake utaamka umechoka.  

 

Pia kabla ya kulala epuka matumizi ya vinywaji vyenye caffeine hasa Pepsi, Coca-Cola na kahawa. Matumizi ya sigara kabla ya kulala pia si nzuri. 

 

Ukiweka mazingira hayo utalala usingizi wenye ubora na itakuwa faida sana kwako. 

 

Mwisho

Kama mtu mpenda mafanikio, kiu yako kubwa iwe kwenye kuzalisha mawazo mapya. Kumbuka, pesa sio pesa bali ni mawazo. Mawazo na ubunifu ndio vyanzo vya mapato ya kifedha pamoja na mafanikio mengine. 

  

Kazi yako kama mtu unayetamani kufanikiwa iwe kuhakikisha afya yako ya akili iko timamu. Njia hizo tatu zitasafisha ubongo wako na kukufanya uzalishe mawazo kila mara. 

 

Endelea kusoma makala zangu na ukipata muda tembelea ofisi yetu ya vifaa tiba vya physiotherapy na rehabilitation inayopatikana Sinza Mori, jengo la Azaria (ofisi namba 14), opposite na Kitambaa Cheupe Sinza ili kuona namna tunavyoweza kuimarisha afya yako na ndugu zako kwa vifaa tiba vyetu vyenye ubora wa hali ya juu. 

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW