Nitagunduaje Dalili za Mapema za Malaria?

Sio kila homa ni malaria bhana” ni kampeni maarufu sana ambayo Wizara ya Afya imekuwa ikiitumia mara kwa mara kuwakumbusha wananchi kuacha kununua dawa na kujitibu kiholela na pia kwenda mapema kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupima ili kuthibitisha uwepo wa vimelea kabla ya kutumia dawa ili kuepuka changamoto kubwa zinawoweza kujitokeza kwani malaria ni ugonjwa ambao ukichelewa kutibiwa madhara yake ni makubwa.

 

Mwaka 2021, nikiwa nimelala baada ya uchovu wa kazi, nilishtushwa na makelele ya Dada wa kazi aliyekuwa akiita, “Baba, Baba, Atu amelegea kazidiwa hawezi hata kukaa, na ana homa kali!

 

Sijui nilitokaje chumbani lakini nilijikuta sebuleni na mtoto aliyekuwa kalegea sana na homa kali. Nilifanya kumbeba haraka na kumpeleka Kituo cha Afya ambako baada ya vipimo aligundulika ana malaria.

 

Shida sio hiyo, shida ni kwamba nilishamuona mtoto siku kama mbili zilizopita alikuwa anakohoa na mafua, na homa ya wastani lakini sikutilia maanani. Niliona ni mafua tu mpaka alipokuja kuzidiwa.

 

Angeweza kupatwa na tatizo kubwa zaidi kama nisingekuwepo kwa wakati huo; pia kama Kituo cha Afya kingekuwa mbali na sina usafiri.

 

Hapo nikajifunza, “sio kila mafua, kikohozi na homa ni vya kuchukulia kawaida”. Ni muhimu kupima mapema na kuhakikisha hamna vimelea vya malaria. Tokea hapo mwanangu akichemka huwa nakuwa makini kumfatilia kwa ukaribu; kama kuna dalili sizielewi, najisalimisha hospitali mapema sana!

 

Dalili za mwanzo za malaria huwa ni ngumu kutofautisha na dalili za magonjwa mengine kama mafua, kikohozi, kuhara, na typhoid ila uonapo dalili zifuatazo ni muhimu kuwahi hospitali kufanyiwa vipimo:

 

1. Homa

Homa sio dalili ya malaria pekee. Inaweza kuletwa na magonjwa mengine ikiwemo malaria. Mgonjwa wa malaria huwa na homa za vipindi (huja katika mzunguko fulani) ambazo huchanganya zaidi asubuhi, jioni na usiku na kuambatana na baridi na kutetemeka. Mgonjwa atapendelea kukaa juani au kuvaa sweta huku akitetemeka.

 

2. Kichwa kuuma

Kichwa kuuma sio dalili ya malaria tu, bali hata changamoto zingine kama UTI lakini kikiambatana na homa na kutapika, nenda hospitali kufanya vipimo.

 

3. Kichefuchefu na kutapika

Hii nayo ni dalili ambayo sio ya malaria peke yake ila mgonjwa akiwa na homa ambayo inaambatana na kukosa hamu ya kula, kichefuchefu na kutapika inaweza kuwa malaria.

 

Mgonjwa wa malaria baada ya muda anaweza kuanza kutapika kila kitu anachokula. Ukiona dalili hizi wahi Kituo cha huduma za afya mara moja

 

4. Viungo na misuli kuuma

Dalili hii sio tu kwa malaria, inaweza kusababishwa pia na magonjwa kama Korona na Dengue, lakini ikiambatana na dalili hizo hapo juu basi nenda Kituo cha huduma za afya ili upime.

 

Dalili zingine ni kama tumbo kuuma, kuharisha, kukohoa, mafua na mwili kuchoka sana. Hizi ni dalili za mapema za malaria na kwa bahati mbaya hufanana na magonjwa mengine.

 

Mfano, mtu anaweza kuwa na mafua na kikohozi na homa we ukadhani ni mafua tu kumbe kuna malaria. Utaanza kutibu kikohozi lakini baadaye mgonjwa anazidiwa.

Kosa hapa ni kwamba dalili zilikuwepo ila hukumpima mgonjwa kwanza kabla ya kununua dawa. Makosa kama haya yamesababisha vifo vingi hasa kwa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Kwa watoto na wajawazito dalili zinaweza kuwa tofauti kidogo. Mfano, kwa mtoto anaweza kuwa analia tu na kukataa kunyonya na kuchemka bila kutapika au kukohoa. Hivyo ukiona mtoto analia sana na hataki kula na anachemka ni bora kuwahi haraka kituo cha huduma za afya ili achunguzwe na daktari.

 

Angalizo

Dalili za malaria hutofautiana kwa mtu na mtu; pia sio kila mwenye dalili zote hapo juu ana malaria, wengine wanaweza kuwa na mchafuko wa tumbo, au maambukizi ya virusi, typhoid, mafua, maambukizi ya tonsils na kadhalika.

 

Hivyo uonapo au kuhisi dalili hizi usinunue dawa za malaria na kumeza kiholela, ni lazima uthibitishe kwa vipimo ili kutibu kwa uhakika na uweze kupona.

 

Mwisho

Wizara ya Afya katika kuadhimisha kilele cha siku ya malaria Duniani tarehe 25 Aprili inakukumbusha kwamba ni muhimu kuwahi kituo cha huduma za Afya  kama utaona dalili zinazofanana na za malaria kama zilivyotajwa hapo juu.

 

Malaria isipotibiwa mapema huweza kuathiri ubongo, figo, maini, na bandama na kupelekea madhara kama kuishiwa damu, degedege, kupoteza fahamu na hata kifo.

 

Usichukulie powa, bora kuwahi Kituo cha huduma za Afya uonekane una kiherehere kuliko kuchelewa ukaonekana mzembe, utajilaumu maisha yako yote.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW