Meno ya binadamu – mtu mzima – kwa kawaida huwa na rangi ya maziwa (cream) na sio nyeupe kabisa kama karatasi. Ubadilikaji wa rangi ya meno husababishwa na mambo mbalimbali kama vile kutosafisha kinywa vizuri, utumiaji wa vyakula na vinywaji kama vile kahawa, chai ya rangi, mbogamboga, matunda, pipi na kadhalika.
Matumizi ya tumbaku (kama vile uvutaji wa sigara), ajali iliyopelekea kupasuka kwa jino, magonjwa, uzee, na kuoza kwa jino pia huweza kupelekea meno kupoteza rangi yake ya maziwa na kuwa rangi ya utofauti, hasahasa ya njano.
Rangi hii ya njano huweza kusababisha tabasamu lako kukosa mvuto au kutokujiamini. Hivyo basi, ili kuboresha muonekano wa meno yako na tabasamu lako kuna njia kuu mbili ambazo unaweza kutumia ili kutimiza kusudi lako.
Yakwanza ni kupitia kusafishwa meno; ya pili ni kung’arishwa meno. Njia zote hizi hufanywa na mtaalamu wa afya ya kinywa na meno.
Je, ni nini huku kusafishwa au kung’arishwa kwa meno?
1. Kusafishwa meno (Teeth cleaning)
Kwa kawaida kila mtu hupiga mswaki (teeth brushing) asubuhi, na wengine hata jioni kabla ya kulala ili kuhakikisha usafi wa kinywa na meno. Wengi wetu hutumia maji, mswaki, pamoja na dawa ya meno katika usafi huu.
Lengo kubwa la usafi huu ni kuondoa plaki (plaque) na kuhakikisha meno yako yanaimarika zaidi kwa kupata madini ya florini kutoka kwenye dawa ya meno na kuepukika na harufu mbaya mdomoni.
Plaki ni utandu mlaini ambao hutengenezeka katika meno yako muda mchache baada ya kula au kunywa.
Ni muhimu kuuondoa huu utandu maana kadri unavyobaki kwenye meno yako hushikilia vyakula zaidi na kuwezesha mkusanyiko wa bakteria ambao husababisha uharibifu wa meno na harufu mbaya mdomoni.
Plaki huondolewa kwa urahisi kupitia kupiga mswaki bila hata kutumia nguvu nyingi. Hivyo, kupiga mswaki ni muhimu sana katika kuhakikisha meno, fizi na ulimi wako unaendelea kuimarika na kukingwa na magongwa. Vile vile, kuepuka harufu mbaya mdomoni na kuongeza kujiamini wakati wa kuongea na watu wengine.
Kusafisha meno ni mojawapo ya huduma ambazo hutolewa na mtaalamu wa kinywa na meno (dentist).
Sababu ya huduma hii ni kuhakikisha usafi wa kinywa kwa sehemu ambazo mtu binafsi huwezi kuzifika au kuona. Lakini pia, kuondoa mgandamano wa uchafu katika meno, ambao hauwezi kuuondoa kwa kupiga mswaki pekee, kama ilivyo kwa plaki.
Huu mgandamano mgumu wa uchafu katika meno huitwa ugaga (calculus).
Nini kinaweza kusababsha ugaga kwenye meno yako?
- Upigaji mswaki usio sahihi
- Utumiaji wa mswaki mmoja kwa muda mrefu
- Hali ya mate mdomoni
- Mpangilio wa meno mdomoni
Ugaga katika meno huonekana mara nyingi katika eneo la chini la jino karibu na fizi. Hali hii inaweza kupelekea meno yako kuwa na muonekano wa unjano zaidi.
Ugaga huu unaweza kusababisha mdomo wako kutoa harufu mbaya, kutokwa na damu kwenye fizi, na hata kulegea kwa meno yako mdomoni. Mbaya zaidi ugaga huu husababisha kutokupenya kisawasawa kwa dawa ya meno ndani ya meno na fizi zako, jambo ambalo si sawa kwani lengo kuu la dawa hiyo ni uimarishaji wa maeneo hayo ya kinywa chako.
Kama nilivyokwisha kukueleza kuwa ugaga hauondolewi kwa kupiga mswaki pekee, hivyo ni muhimu kumtembelea daktari wa kinywa na meno angalau mara mbili kwa mwaka ili kupata huduma ya kusafishwa meno.
Daktari wa kinywa na meno hutumia kifaa maalamu (ultrasonic scaler) kwa ajili ya kufanya usafi huu. Matokeo yake ni kuwa muonekano wa meno yako huwa mzuri zaidi, harufu mbaya mdomoni hukoma, fizi huacha kutoa damu, pia meno na fizi huimarika zaidi.
2. Kung’arishwa meno (Teeth whitening)
Kung’arisha meno ni njia ya kuongeza uweupe katika jino la binadamu. Njia hii hubadili rangi ya unjano katika meno yako na kuyapa muonekano wa kung’ara zaidi. Wakati mwingine hii njia huitwa bleaching.
Mara nyingi unaweza kufanya hivi katika meno yako ili kuondoa madoa katika meno na ubadilikaji wa rangi ya meno wa namna yeyote ile.
Mchakato huu hufanywa na mtaalamu wa kinywa na meno au na mtu binafsi lakini akiwa chini ya uangalizi wa daktari wa kinywa na meno (dentist-supervised at home bleaching)
Kuna aina mbili za ubadilikaji wa rangi ya meno ambapo ung’arishwaji hufanyika ili kuboresha rangi ya meno na kuyafanya kuwa meupe zaidi. Ubadilikaji wa rangi ya meno wa ndani na wa nje.
Ubadilikaji wa ndani wa rangi ya meno
Ni ule ambao rangi ya meno isiyoridhisha imo ndani kabisa ya sehemu za jino (enamel and dentine). Mara nyingi rangi hii hutengenezeka pale ambapo meno yako yanaundwa ndani ya mfupa wa kinywa chako kabla halijatokea kinywani.
Hii hali ya ubadilikaji wa rangi ya meno huweza kusababishwa na maumbile ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na familia yako.
Pia mazingira unapotokea yanaweza kupelekea kuwa na rangi ya tofauti ya meno mbali na ile rangi ya maziwa (cream). Mfano mzuri wa hili ni meno ya rangi ya kahawia (fluorosis) katika watu wengi wanaotokea Arusha kutokana na kiwango kikubwa cha madini ya florini katika maji wanayotumia.
Mbali na hayo, kama wewe ni mwanamke mjamzito, matumizi ya dawa ya tetracycline wakati wa ujauzito yanaweza kusababisha ubadilikaji wa rangi ya meno kwa mtoto wako.
Ubadilikaji wa nje wa rangi ya meno
Ni ule ambao rangi isiyoridhisha ya meno haipo ndani ya sehemu za jino (enamel and dentine), bali unatokana na hali za nje katika utumiaji wa kinywa wa kila siku katika kula na kunywa kama nilivyokwisha kukueleza pale mwanzoni – kunywa kahawa, chai, soda au uvutaji sigara.
Kung’arisha meno hufanywa kwa dhumuni TU la kuboresha muonekano wa meno na tabasamu kwa ujumla.
Mwisho
Ni muhimu kutambua kuwa kusafisha meno ni muhimu kwa uimara wa meno na fizi zako – na ni hulka njema mtu kujijengea. Lakini kung’arisha meno ni jambo mtu anaweza kufanya kwa kupenda, si jambo la lazima kwa kila mtu kulifanya angali kwamba unapendezwa na rangi halisi ya meno yako.

“For the love of words”
Asante sana daktari, elimu imefika.
Asante kwa elimu nzuri juu ya kutunza vinywa vyetu…
Je ni dawa gani nzuri kwa matumizi ya kusafisha meno na vinywa vyetu? Hasa ukizingatia madawa ni mengi sana katika maduka yetu ya ndani…
Utapata hii kwenye nakala ijayo
Hongera sana kwa kazi nzuri unayoifanya daktari.
Sisi kama Kinywa Salama Initiative tunapenda sana kufanya kazi pamoja na wataalam mbali mbali Ili kuifikia jamii kwa namna nzuri ya kufikisha elimu ya afya ya Kinywa na meno kwa jamii.
Thank you Mr. Yona. Karibu tuendelee kujifunza pamoja
Asante sana Daktari kwa kuendelea kuelimisha Jamii juu ya Afya ya kinywa na meno
Asante daktari. Karibu tuendelee kujifunza pamoja