Nilipokea simu kutoka kwa rafiki yangu akiwa na sauti yenye maswali mengi. Simu hii ilienda hivi:
“Ninaomba ushauri wako, naomba usimjulishe mtu kuhusu hili maana ni kitu cha aibu hata kwangu binafsi. Nimegundua kuwa huwa natoa harufu sana mdomoni kwangu. Sijajua hali hii inatokea kwasababu gani ila sipendezwi nayo kabisa angali huwa napiga mswaki vizuri kila siku kwa dawa ya meno na maji safi. Nifanyeje? Naomba unisaidie”
Aliongea kwa msisitizo mkubwa sana.
Si yeye tu aliyewahi kujiuliza haya. Wewe, mimi au hata watu wako wa karibu walishawahi zungumzia jambo la harufu mbaya kinywani. Sawa! Najua hata uamkapo inawezekana kabisa huwa unakuwa na harufu mbaya kinywani lakini mimi siongelei hiyo, kuna ile hali mtu anakuwa nayo hata kama amekwishafanya usafi wa kinywa chake vizuri.
Kupitia makala hii utaweza kujua kwa kina sababu za harufu mbaya ya kinywa, athari zake kwa watu binafsi na jamii, ishara za uwepo wake, na jinsi ya kuzuia na kudhibiti hali hii.
Sababu za harufu mbaya ya kinywa
Harufu mbaya ya kinywa (halitosis) ni tatizo linalowaathiri watu katika ngazi binafsi na pia linaweza kuwa na athari kubwa kwa jamii kwa ujumla wake. Sababu za harufu mbaya ya kinywa ni nyingi, zikianzia kutoka kwenye usafi duni wa mdomo hadi matatizo ya kiafya ya msingi.
Usafi duni wa mdomo
Uoshaji na kusafisha kwa kiasi kisichotosha kunaweza kusababisha bakteria kukusanyika mdomoni na kupelekea utoaji wa harufu mbaya. Pia kutojali kusafisha ulimi husababisha uwepo wa bakteria wengi, hali ambayo inaweza kuchangia harufu mbaya ya kinywa.
Magonjwa ya meno
Uvimbe kinywani, magonjwa ya fizi, na matatizo mengine ya meno yanaweza kuhifadhi bakteria na kutoa harufu mbaya. Vile vile kinywa kikavu hupelekea harufu mbaya mdomoni. Hii hali mara nyingi – inayosababishwa na dawa au hali za kiafya – inapunguza uzalishaji wa mate na kutengeneza mazingira yanayofaa kwa bakteria wanaosababisha harufu mbaya.
Tabia za lishe
Vyakula fulani kama vitunguu swaumu, kitunguu maji, na viungo vingine vina mchanganyiko kadha wa kadha ambao huchangia harufu mbaya. Kufunga mlo au lishe yenye wanga kidogo kunaweza kusababisha kuvunjika kwa mafuta mwilini na hivyo kuzalisha ketoni zenye harufu mbaya.
Matumizi ya tumbaku na pombe
Kuvuta sigara na kutumia tumbaku kunachangia harufu mbaya ya kinywa na kuongeza hatari ya ugonjwa wa fizi.
Matumizi ya pombe yanaweza kusababisha ukavu wa kinywa kwa kupunguza uzalishaji wa mate na kuchochea ukuaji wa bakteria.
Hali (magonjwa) za kiafya
Maambukizo ya njia ya hewa, kisukari, magonjwa ya ini na figo, na reflux ya asidi yanaweza kusababisha harufu mbaya ya kinywa na hivyo kuwa mojawapo ya kiashiria cha magonjwa hayo. Hali za kudumu kama vile sinusitis na majimaji kuvuja puani pia zinachangia harufu mbaya ya kinywa.
Ishara za harufu mbaya ya kinywa
- Ladha mbaya (na isiyofurahisha) ya kudumu: Ukiwa na harufu mbaya kinywani ni kawaida sana kujikuta na ladha isiyofurahisha muda wote mdomoni.
- Ulimi uliofunikwa na uchafu wenye rangi: Ulimi wenye rangi nyeupe au njano ni ishara ya ukuaji wa bakteria.
- Kuwa na kinywa kikavu: Kutokuwa na mate, inayosababisha kinywa kavu, ni ishara ya harufu mbaya ya kinywa.
Athari kwa watu binafsi
Ukiwa na harufu mbaya ya kinywa unaweza kuwa na upweke katika jamii unapotokea. Upweke huu hubebana na aibu na kuonekana kama mtu asiyejitunza vyema. Hofu ya kuhukumiwa inaweza kukusababishia kuepuka kuwasiliana na watu kwa uhuru kwenye jamii yako hivyo ikaathiri mahusiano na ustawi wako kiakili.
Pia harufu mbaya ya kinywa inaweza kuathiri mahusiano yako kazini au mahojiano ya kikazi, na maendeleo yako kazini. Wenzako wanaweza kukuchukulia kama mtu usiye na ufanisi au usiyezingatia usafi binafsi.
Jinsi ya kuzuia na kuthibiti hali hii
1. Usafi sahihi wa kinywa
Hakikisha unasafisha meno kwa dawa ya meno na kutumia nyuzi za meno kuondoa uchafu katikati ya jino na jino hudhibiti ukuaji wa bakteria wasababishao harufu mbaya kinywani. Pia, usafi thabiti wa ulimi, husaidia kudhibiti hali hii. Ulimi usafishwe na kuhakikisha kuwa hakuna utandu mweupe au wa njano kwenye sakafu yake.
2. Kunywa maji mengi
Hii husaidia kudumisha uzalishaji wa mate na kuondoa mkusanyiko wa bakteria ambao wengesababisha harufu mbaya mdomoni.
3. Pata lishe bora
Hakikisha unapata lishe yenye matunda, mbogamboga pamoja na wanga kiasi. Hii inaweza kuchangia afya njema ya kinywa chako.
4. Acha matumizi ya tumbaku na punguza unywaji wa pombe
Kuacha matumizi ya tumbaku na kupunguza matumizi ya pombe kunaweza kuboresha afya ya kinywa hasa katika kuzuia harufu mbaya kinywani.
Mwisho
Tembelea kliniki za meno kwaajili ya uchunguzi na elimu mbalimbali za namna gani ya kuboresha afya yako ya kinywa ili kuzuia harufu mbaya mdomoni, kwani tunasema mganga hajigangi, hivyo inawezekana kuna jambo halijakaa sawa hivyo ni vyema kuchunguzwa na kupewa ushauri wa nini cha kuanya ili kuboresha hali ya maisha yako kiujumla.
Kwa kumalizia….
Je wajua? Si lazima uwe na harufu mbaya kila uamkapo asubuhi! Fanya usafi wa kinywa chako kabla ya kulala usiku. Kinywa kisafi hakihifadhi bakteria wa kuzalisha harufu mbaya hivyo utaamka asubuhi na kuweza kuongea bila wasiwasi kwani harufu mbaya mdomoni huwa haipo kama ukifanya usafi kabla ya kulala.

“For the love of words”