Mambo 5 Yanayoharibu Afya ya Mfumo wa Chakula na Kupelekea Utumbo Kuvuja

Magonjwa mengi huanzia katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Dosari katika mfumo huu hupelekea shida kubwa katika sehemu nyingine za mwili.

 

Tafiti zinaonyesha kuwa upo muunganiko wa moja kwa moja wa ubongo na mfumo wa chakula, moyo, na hata ngozi pia.

Utimamu wa afya yako unaendana na uimara wa afya katika mfumo wako wa chakula.

 

Good vibes na kinga imara huanzia katika mfumo wa chakula

Zaidi ya asilimia 90 ya kemikali iitwayo serotonini hupatikana katika mfumo wa chakula, siyo ubongo. Serotonini ni kemikali inayosaidia kukupa good vibes na kukusaidia kurejesha hali yako ya furaha kipindi ukiwa una sonona au mfadhaiko.

 

Zaidi ya asilimia 70 ya kinga ya mwili hupatikana katika mfumo wako wa vyakula.

 

 

Mfumo wa chakula pia ni maskani kwa zaidi ya bakteria trilioni 100. Mkusanyiko huu hujulikana kama gut microbiota. Bakteria huwa na faida kubwa ndani ya mwili ikiwemo kuzalisha baadhi ya virutubisho, kusaidia umeng’enyaji wa chakula, na mfumo wa kinga mwilini.

 

Uwiano kati ya bakteria wazuri (microbiota) na bakteria wabaya ukicheza hupelekea matatizo katika mfumo wa chakula na hata nje ya mfumo wa chakula. Kinga yako ya mwili na hali ya furaha hutegemea sana uimara wa kuta za mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

 

Fahamu machache kuhusu ‘utumbo unaovuja’ (Leaky gut)

Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula umeundwa kwa muunganiko wa viungo kuanzia mdomoni mpaka sehemu ya kutolea haja kubwa. Pia umeunganishwa na viungo vingine vya muhimu kama ini, kongosho na mfuko wa nyongo. Matokeo ya mwisho ya mmeng’enyo wa chakula kwa kiasi kikubwa hufyonzwa katika kuta za utumbo mwembamba.

 

Kuta za mfumo wa chakula (hususani tumbo na utumbo mwembamba) huwa ni imara sana, zimetengenezwa kwa namna ambayo huzuia kuvuja kwa kitu chochote kinachotoka ndani ya mfumo wa chakula  ikiwemo bakteria wabaya, sumu, na mabaki ya chakula ambayo hayajameng’enywa vizuri.

 

Kunapotekea dosari ndani ya mfumo wa chakula na kupelekea kuta za utumbo mwembamba kutoboka, hii hali huitwa intenstinal permeability au leaky gut.

 

Leaky gut hupelekea kuvuja na kuingia kwenye damu kwa bakteria wabaya na sumu na kupelekea magonjwa mbalimbali katika mwili yakiwemo magonjwa yanayotokana na kinga za mwili kushambulia sehemu mbalimbali za mwili yaani autoimmune diseases.

 

Pia husababisha ugonjwa wa tumbo ujulikanao kama Inflammatory Bowel Syndrome. Tatizo la leaky gut (utumbo kuvuja) hupelekea vimeng’enywa kama amino acids, vitamini, na fatty acids kushindwa kusharabiwa mwilini.

 

Nitajuaje kama nina utumbo uliovuja?

Watu wengi ambao husumbuka na tatizo hili hupata mvurugiko katika mfumo wa chakula na sehemu zingine za mwili. Mkusanyiko wa dalili za utumbo uliovuja ni kama zifuatazo;

  • Shida katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kama tumbo kujaa gesi
  • Matatizo ya ngozi kama psoriaris na chunusi za muda mrefu
  • Mwili kuchoka mara kwa mara na maumivu ya viungo
  • Kupata allergy kwa baadhi ya aina za vyakula
  • Kushindwa kuongezeka au kupungua uzito

 

Mambo yanayopelekea utumbo kuvuja:

1. Pombe

Pombe huharibu kuta za mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kwa kupunguza ufyonzwaji wa chakula. Hupelekea intestinal permeability au leaky gut, yaani kuharibika kwa kuta za utumbo mwembamba hali inayopelekea kupenya kiurahisi kwa sumu, bakteria, na vipande vya vyakula ambavyo havijameng’enywa vizuri.

Hukuza bakteria wabaya tumboni, na kuua bakteria wazuri.

 

2. Gluten

Gluten ni aina ya protini inayopatikana katika nafaka nyingi, kwa kiasi kikubwa inapatikana katika ngano. Aina hii ya protini haiwezi kuchakatwa na mwili. Ni watu wachache sana wanye uwezo wa kuhimili gluten katika miili yao.

 

Wengi wetu tuna kile kijulikanacho kama gluten insensitivy, yaani miili yetu ina mwitikio hasi juu ya gluten, na kupelekea kutoboka na kuharibika kwa kuta za tumbo na utumbo mwembamba.

 

Hali hii husababisha dalili – katika mfumo wa chakula – kama tumbo kujaa gesi, kiungulia, na kuharisha.

 

Fahamu: Zaidi ya asilimia 80 ya watu wenye gluten insensitiity hupata dalili zilizo nje ya mfumo wa chakula kama mwili kuchoka kupita kiasi, maumivu ya viungo, matatizo ya ngozi, na utapia mlo. Muunganiko wa dalili hizi husababishwa na leaky gut.

 

3. Sukari aina ya fructose

Kila mtu anapenda sukari. Sukari ya mezani imeundwa kwa glucose na fructose katika uwiano wa 50% na 50%. Fructose pia hupatikana kwa wingi katika matunda matamu na juisi zake, vinywaji baradi vya viwandani kama soda, na katika fructose syrup.

 

Tofauti na glucose ambayo hutumiwa kama chanzo cha nishati na seli zote za mwili, fructose huchakatwa katika ini pekee na hubadilishwa kuwa mafuta. Fructose ni moja kati ya kihatarishi kikubwa kabisa cha afya ya mfumo wako wa chakula.

 

 

Sukari aina ya fructose sio kwamba tu inaharibu kuta za mfumo utumbo mwembamba na kupelekea intestinal permeability, pia hukuza uwezekano wa kupata shambulio la mwilini yaani inflammation hali ambayo pia huharibu kuta za tumbo.

 

4. Matumizi holela ya Antibiotics

Zaidi ya 30% ya watu hutumia dawa za kuua bakteria, antibiotics, kwa namna isiyofaa hivyo kupelekea kuharibu uwiano wa bakteria wazuri wa kazi – wa kwenye mfumo wa chakula – yaani gut microbiota na bakteria wabaya.

 

Kiasi cha bakteria wazuri hupungua, kile cha bakteria wabaya huongezeka. Kucheza kwa uwiano huu huathiri utaratibu na muundo wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

 

Tafiti pia zinaonyesha matumizi yaliyokithiri ya viua wadudu vingine nje ya ngozi kama vitakasa mkono (sanitizers), sabuni za kuogea na shampoo huathiri pia uwiano wa gut microbiota.

 

5. Msongo wa mawazo

Kiasi fulani cha msongo unachoweza kukistahimili ni kizuri kwa afya. Lakini kuishi katika hali ya stress kwa muda mrefu hupelekea intersinal permeability.

Utafiti uliofanyika mwaka 2015 ulionesha kuwa hata stress kubwa tunayoipata kutokana na hofu ya kuzungumza mbele ya watu wengi hupelekea hali ya intersinal permeability. Hata sonona na hofu hupelekea hali hiyohiyo.

Kuwa na msongo wa mawazo wa muda mrefu halafu ukawa unakula mlo wenye kiasi kingi cha wanga na sukari ni kuhatarisha kabisa afya yako.

 

Muhimu

  • Hali yako ya afya kwa ujumla haiwezi kuzidi utulivu ulio ndani ya mfumo wako wa chakula.
  • Humo ndani ndipo ambapo kuna zaidi ya 70% ya kinga ya mwili wako na 90% ya kemikali ya serotonini inayokupa vibe.
  • Kama unasumbuliwa na mvurugiko wa mfumo wa chakula na dalili nyingine za nje ya mfumo kama chunusi, maumivu ya viungo na kuchoka mara kwa mara kuna uwezekano ukawa na tatizo katika kuta za mfumo wa mmeng’enyo wa chakula
  • Unaweza kuwa na matatizo 100 na kidogo katika afya, lakini kuimarisha mfumo wa mmeng’enyo wa chakuka kutaondoa matatizo 99.
  • Kuanza ni rahisi; punguza matumizi ya ngano na sukari, mudu msongo wa mawazo, tumia antibiotics pale inaposhauriwa na daktari, na achana na matumizi ya pombe.
  • Ngano iliyosindikwa (fermented) huwa ina kiasi kidogo sana cha gluten. Hivyo uandaaji wa mkate kwa namna ya kizamani hufaa kwa watu wenye gluten insensivity.

 

Ndugu msomaji, asante kwa kuendelea kufuatilia makala zetu. Usisite kutoa maoni au kuuliza swali kwa changamoto yoyote utakayokutana nayo.

 

Usisahau pia kutembelea duka letu ujipatie copy ya kitabu changu cha mwongozo wa kudhibiti kisukari na vitabu vingine vya kuvutia vya afya.

1 thought on “Mambo 5 Yanayoharibu Afya ya Mfumo wa Chakula na Kupelekea Utumbo Kuvuja”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW