Mambo 10 ya Kuzingatia Wakati Unafanya “Dieting” ili Kupungua Uzito

Nimeamua kuandika makala hii kwa sababu watu wengi huwa wanatamani kujua vitu vya kufanya ili waweze kupungua uzito hasa katika eneo la tumbo au kitambi.

 

Uzito uliozidi umekua ukihusishwa moja kwa moja na hatari ya mtu kupata magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mifupa, kisukari na kadhalika.

 

 

Hivyo ni muhimu kufanya mabadiliko ya kitabia ambayo yatapelekea kupungua kwa uzito.

Nianze kwa kusema Dieting haimaanishi kujinyima kula kila siku lakini unaweza kufanya mabadiliko madogo madogo ya kitabia ambayo yatapelekea kupata matokeo ya kupungua uzito.

 

Mambo haya ni kama ifuatavyo:

1. Ulaji wa nyama isiyo na mafuta (lean meat)

Nyama hii inakua na kiwango kikubwa cha protini kuliko mafuta, katika ulaji wa nyama hii ni muhimu kuchagua nyama ambayo haijawa processed kutoka viwandani kwa sababu nyama hizi zilizochakatwa zinakua zimeongezwa chumvi na zina mafuta yanayoganda ambayo yana hatari ya kuganda katika mishipa ya damu.

 

Mifano ya nyama hizi zinazopaswa kuliwa ni nyama ya kuku, nyama ya samaki, na nyama ya bata mzinga – kwasababu amefanana na kuku kwa maana ya virutubishi vilivyopo.

 

Muhimu: Kwa wanaofanya mazoezi, ulaji wa lean meat husaidia kupata protini ya kujenga misuli baada ya kukata mafuta kwa kufanya mazoezi.

 

2. Kunywa maji zaidi

Unywaji wa maji husaidia kukwepa hali ya utupu katika tumbo na kufanya ujisikie umeshiba. Unapokua umekunywa maji, hasa kabla ya kula, unakua umepunguza hali ya kula chakula kingi kwa sababu unakua na hali ya kushiba.

 

3. Zingatia unachokula

Hii inamaanisha kwamba katika ulaji wako wa kila siku inabidi uzingatie lengo la kupungua uzito na hivyo basi utafakari unachokula kwa upande wa faida zake na hasara zake.

 

Hii itakusaidia kukwepa vyakula vinavyopelekea kuongezeka uzito kwa haraka kama vile vyakula vyenye mafuta mengi na sukari kwa wingi.

 

4. Kula taratibu na kwa utulivu

Hii itasaidia katika kupunguza uzito kwani utakua unaweka umakini katika kiwango cha chakula unachokula na hautakua unakula sana kwa sababu utaipa akili yako muda wa kutambua kuwa umeshiba na hauhitaji kula tena.

 

Lengo la kufanya hivi ni kwamba ukiwa unakula haraka haraka hasa kwasababu unanjaa unaweza kuwa unakula chakula kingi tofauti na ukiwa unakula taratibu.

 

5. Kula vyakula vyenye nyuzinyuzi kwa wingi

Vyakula vya nyuzi nyuzi ni mifano ya vyakula vilivyopo katika kundi la wanga lakini havichakatwi katika utumbo mdogo kama vile sukari.

 

Ukihusisha vyakula hivi katika milo yako itakupa hali ya kujisikia kushiba ambayo itapelekea kupungua uzito.

 

6. Epuka kutumia vinywaji vyenye calorie nyingi kama vile soda, juice, bia pamoja na cocktails kwa sababu vinaongeza uzito kwa kasi vinapokua vinaliwa na vyakula vingine.

 

 

Mbadala wa vinywaji hivi unaweza kuwa maji kwa sababu maji ni kinywaji kisichokua na calories.

 

7. Kula mlo wa asubuhi yaani breakfast

Kifungua kinywa ni mlo muhimu wa siku na hupaswi kuacha kula asubuhi kwani ni mlo ambao utakusaidia kupata nguvu ya kufanya kazi za siku.

 

Watu wengi wamekua na tabia ya kuacha kula chakula cha asubuhi wakiamini wanaweza kupungua uzito wakati milo mingine wanakua wanakula zaidi kwa sababu ya kusikia njaa kwa muda mrefu, au wengine huwa wanakula snacks znye sukari nyingi kama vile keki na biscuits na kadhalika.

 

8. Weka kumbukumbu ya vitu unavyokula – hasa kwa kuandika.

Hii itakusaidia kuona vitu unavyoweza kupunguza hasa vile vinavyoongeza uzito. Unaweza kuwa na food journal ambayo inaweza kuwa katika daftari au simu.

 

Kama utakua na tabia ya kula chakula cha aina moja kwa mfululizo au kwa sana, hapa utaweza kubaini hilo kwa sababu utakua umeweka kumbukumbu.

 

9. Zingatia kiwango cha chakula kinachotakiwa hasa kwa kutumia sahani ya mlo kamili inayofaa, ambayo itakufanya uwe unakula portion size sahihi kwa kila mlo.

 

Kusoma zaidi kuhusu “sahani inayofaa”, nenda hapa.

 

10. Mfungo wa vipindi

Kufunga kwa masaa 6 mpaka 8 kwa siku husaidia kuleta urahisi katika usawa wa mfumo wa umeng’enywaji wa vyakula. Kusoma zaidi kuhusu aina mbalimbali za mifungo, gusa hapa.

 

Kumbuka…

Dieting sio kujinyima kula kwani ukijinyima kula unaweza kupelekea magonjwa mbalimbali kama vile vidonda vya tumbo. Lakini pia, katika kufanya dieting unapaswa kushirikisha wataalamu wa maswala ya lishe ili uweze kufanyiwa mpangilio wa mlo utakaoendana na mahitaji ya mwili wako.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW