Mahitaji 3 Muhimu ya Afya na Mipaka Yake

Afya yako ina mahitaji mengi. Yapo mahitaji muhimu na lazima na yale muhimu lakini sio lazima sana.

 

Unaweza kuifananisha afya na nyumba. Inajengwa kwa vipimo maalum. Vifaa vya ujenzi wa afya havipaswi kuwa chini ya mahitaji au zaidi ya mahitaji.

 

 

“Ngoma ivumayo sana ndiyo hupasuka” ni methali ya kiswahili itumikayo kuonyesha kwamba kila kitu kina mipaka yake na kinapofanywa katika mipaka sahihi huwa na faida chanya, lakini kikizidi hupelekea kupata majibu kinyume chake.

 

Katika makala hii nitaainisha mambo matatu muhimu katika kujenga na kukuza afya yako, pamoja na mipaka yake.

 

1. “Tendo la ndoa”

Kufanya mapenzi/ngono ni muhimu katika mwili wa binadamu. Ni tendo linalotambulika kama haki ya mahusiano au ndoa. Bila kufanya mapenzi mahusiano huwa magumu.

 

Na kwa mtu binafsi kukaa muda mrefu bila kufanya mapenzi huweza kuleta madhara ya kiafya hasa kisaikolojia.

 

 

Tendo la ndoa lina manufaa mengi katika mwili wako na katika mahusiano kiujumla. Huweza kuyapa mahusiano msingi mzuri. Husaidia kutatua migogoro miongoni mwa wapendanao. Husaidia kumuweka mtu sawa kisaikolojia.

 

Kuna baadhi ya machapisho yameonyesha kufanya ngono (tendo la ndoa) walau mara tatu kwa wiki huweza kuongeza muda wa kuishi.

 

Kwa upande mwingine ngono ikifanywa zaidi ya kawaida inaweza kugeuka adui wa mwili na afya yako. Kwa hali ya kawaida ngono huambatana na mwili kupoteza nguvu – kwa wote wanawake na wanaume – baada ya mshindo (kumwaga shahawa).

 

Mshindo mmoja huweza kuufanya mwili kupoteza kalori (energy) kiasi cha 100 mpaka 150. Hivyo ukienda mishindo mitatu huweza kufanya mwili kupoteza kalori 300 mpaka 450 kwa siku. Ukifanya walau mara tatu kwa wiki mwili utapoteza kalori 1000 mpaka 1200. Sio kiasi kibaya mwili kukipoteza.

 

Ukizidisha nini hutokea?

Kufanya ngono mara nyingi huweza kupelekea changamoto mbalimbali kwa afya yako. Upotevu wa nguvu nyingi huufanya mwili wako kuwa mchovu mara kwa mara na hivyo kuwa hauna nguvu hasa za miguu.

 

Kwa sababu ya mishindo mingi, husababisha ubongo wako kuwa mchovu na kutofikiri vizuri. Uwezo mdogo wa kufikiri huweza kupelekea mtu kufanya maamuzi ya kichovu na Kupoteza focus.

 

Kuna utafiti uliwahi kuhusisha ‘Kufanya mapenzi mara kwa mara’ na ‘umaskini’. Mtu anayewaza Ngono muda mwingi kila siku huwa muoga wa kufanya maamuzi magumu. Huweza pia kupata msongo wa mawazo hasa pale anapokosa mtu wa kulala naye.

 

Ngono ni kitu kizuri lakini inapaswa kufanya kwa wastani la sivyo inaweza kuathiri afya yako  ya mwili na akili kwa kiwango kikubwa sana.

 

Je wajua? Binadamu anaweza kukaa muda mrefu bila kufanya ngono na hakuna madhara yoyote makubwa ya kiafya yaliyoonekanaa kutokea.

 

Pakua kitabu changu cha Faida za Kutofanya Mapenzi kwa Muda Mrefu kutoka dukani kwetu ili ujpatie elimu ya kutosha kuhusu ya faida ya kutofanya Mapenzi kwa muda mrefu.

 

2. Chakula

Mwili unahitaji chakula ili kuweza  kuwa na Afya njema. Vyakula vikuu kama wanga, protini, na mafuta ni muhimu sana na vikikosekana hupelekea utapiamlo. Hivyo ni muhimu kupambana kuupatia mwili mlo kamili.

 

Pamoja na mwili kuhitaji chakula, kuna aja pia ya kujua mwili wako unahitaji kiasi gani kulingana na matumizi ya mwili wako.

 

Kutokujua hilo ndio hupelekea mwili kuwa na akiba nyingi ya chakula na hivyo kupelekea kuongezeka uzito na adha zingine za kiafya.

 

 

Kiasi sahihi cha chakula kitaupa mwili nguvu na afya nzuri. Kiasi zaidi au chini ya kawaida kitakufanya kuongezeka unene au kuleta utapiamlo na kupelekea kudhoofika kiafya.

 

Unahitaji kula kiasi gani?

Kwa siku mtu wa kawaida huitaji kalori kuanzia 1500 mpaka 2000 kutegemeana na mahitaji au matumizi binafsi. Tatizo hapa linakuja kwamba “utajuaje kwa kiasi ulichokula ni kalori ngapi?”

 

Ugumu wa kuijua hili hupelekea kula chakula zaidi ya kinachotakiwa na mwili hivyo kusababisha changamoto zingine.

 

Kwa kawaida milo mitatu kwa siku itakupa kalori zaidi ya 2000, achilia mbali vyakula au vinywaji vingine vya katikati (snaks)  kama soda, juisi, chocolate, supu ya pweza, karanga, au biskuti ambavyo hufanya kalori kufika mpaka 3000 kwa siku.

 

Hivyo kwa hali ya kawaida ni lazima kutengeneza usawa kati ya unachoingiza na unachotoa. Unaweza kutumia njia mbili zifuatazo:

Kwanza, mazoezi: Utaratibu wa mazoezi ya mara kwa mara kama kutembea, kukimbia au mazoezi ya kubeba ‘vyuma’ huweza kuleta usawa wa kalori za mwili wako.

 

Unaweza ukala milo mitatu lakini ukafanya mazoezi ya kutosha ya kuchoma kalori za ziada ulizoweka mwilini mwako. Njia hii ni rahisi lakini ngumu kwa walio wengi kwa sababu wengi wao huanza mazoezi wakiwa wameshafika hatua mbaya ya vitambi na uzito mkubwa hivyo huhitaji kazi ya ziada kuweza kukata Mafuta. Ni jambo gumu ila inawezekana ukiamua.

 

Sifa kubwa ya mazoezi ni kwamba matokeo yake huja taratibu na watu wengi hukata tamaa kwa sababu wanataka majibu ya haraka.

 

Pili, kufunga kula (fasting): Njia hii sio tu huusaidia mwili kutumia kilichopo kwanza bali huuweka mwili sawa katika nyanja mbalimbali.

 

Kufunga walau masaa 16 bila chakula – bali maji tu – huupa mwili nafasi ya kuchoma kalori zilizo ndani kwa kutumia akiba iliyopo kabla ya kutumia vya kutoka nje. Hii husaidia kupunguza uzito na mwili kutumia mafuta yako kama chanzo cha nguvu mwilini.

 

Hali hii husaidia kupoteza kalori nyingi mwilini na kuleta usawa katika mifumo mingine ya mwili kama utoaji wa acid na homoni mbalimbali zinazosababisha unene.

 

Je wajua?

Kufunga kula chakula sio tu hupunguza uzito bali kuna faida nyingine zilizojificha. Mfano nguvu ya ketone itokanayo na mwili kutumia mafuta huwa ni nguvu kipenzi cha ubongo. Ubongo kwa kutumia nguvu hii huweza kuwa na nguvu ya kuona kwa ufasaha na kuwa na utulivu wa hali ya juu. Mtu anayefuga ubongo wake huwa umeamka, sio wa kizembe.

 

3. Mazoezi

Mazoezi ni muhimu sana katika mwili wako. Huupa mwili ukakamavu, huongeza kujiamini, huleta utimamu wa Ubongo, hukuza misuli ya mwili na kadhalika.

 

 

Ila faida hizi zote zinakuwa na msingi kama mazoezi yanafanywa katika kiwango thabiti. Kitaalamu mazoezi ya walau dakika 30 kwa siku yanatosha kuuweka mwili sawa. Hivyo dakika 150 kwa wiki zinatosha kuuweka mwili katika hali ya usawa.

 

Katika kufanya mazoezi kuna malengo tofauti ya aina mbili. Moja ni kuongeza ukakamavu. Hii huusisha mazoezi ya aerobic kama kukimbia, kuruka kamba, kuogelea, kuendesha baiskeli, kutembea na kadhalika.

 

Lengo lingine la mazoezi ni kujenga misuli. Haya ni mazoezi ya kubeba uzito mkubwa (weight lifting). Aina hii huitaji muda wa wastani wa lisaa 1 mpaka 2 kwa siku, hivyo masaa 10 kwa wiki sawa na dakika 600.

 

Pamoja na kufanya mazoezi ya aina zote hapo juu kuna kikomo chake. Ni muhimu kupata walau siku mbili kwa wiki kupumzisha mwili na kuruhusu misuli kujijenga na ku’adjust.

 

Kufanya mazoezi makali wiki nzima bila kupumzika huweza kuleta matatizo mbalimbali kama misuli kusinyaa badala ya kukua, maumivu ya joint ya muda mrefu, uchovu wa mara kwa mara wa mwili, na kupata mchaniko wa ligament za joint (huweza kutokea kama ukibeba uzito mkubwa kabla mwili wako haujazoea).

 

Kumbuka: Katika mazoezi, mwili unaweza kuzoea kukua katika ukubwa wa ajabu. Kinachotakiwa ni kujua namna ya kufanya mazoezi kwa hatua sahihi kama kuongeza uzito kwa hatua, kuongeza spidi kwa wakati, kubeba uzito sahihi pamoja na kupumzisha misuli kwa muda sahihi.

 

Kwa kumalizia…

Ngono, chakula na mazoezi ni mambo muhimu katika afya lakini tatizo kubwa ni kwamba yana uwezo wa kuleta uteja (addiction). Tatizo hili ndilo hupelekea matumizi ya ziada ya starehe hizi na kupelekea madhara kiafya.

1 thought on “Mahitaji 3 Muhimu ya Afya na Mipaka Yake”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW