Kutana na Facts 14 Ulizokua Hujui Kuhusu Presha ya Kupanda na Kushuka

Je wajua?

Presha ya kupanda huweza kutokea katika umri wowote ule; inategemea kisababishi ni nini. Kwahiyo ni vizuri kujua kiasi cha presha yako walau kila baada ya miezi sita.

 

Je wajua?

Ugonjwa wa presha unaweza kurithiwa kutoka katika ukoo au familia. Hivyo kama mmoja wa ndugu zako – aidha babu, shangazi, mjomba, baba, dada au mama – ana ugonjwa wa pressure inawezekana na wewe umebeba vinasaba vya ugonjwa huo.

 

 

Hivyo anza mapema kujenga utaratibu mzuri wa maisha kama kutovuta sigara, kufanya mazoezi mara kwa mara, kunywa maji ya kutosha na kuweka uzito wako katika hali ya usawa.

 

Tafiti zimeonyesha ukianza mambo hayo mapema unaweza kuondoa uwezekano wa kupata ugonjwa wa presha.

 

Je wajua?

Ugonjwa wa presha hauna dalili za wazi sana, mara nyingi dalili zake hufanana na hali zingine za uchovu na kujiskia hauko sawa au kichwa kuuma kwa mbali. Ndiyo maana presha hujulikana kwa neno maarufu “Silent killer”.

 

Jenga tabia ya kuangalia presha yako hasa unapokuwa katika umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea. Njia rahisi ya kufanya hivi ni kununua kipimio chako na kuwa nacho nyumbani.

 

Je wajua?

Kunywa maji ya kutosha husaidia presha yako kuwa katika hali ya sawa. Kisayansi mwili unapokuwa na maji machache (dehydration) huweza kuwa na chumvi nyingi aina ya sodium. Sodium katika kiasi kikubwa huweza kulazimisha figo kutoa homoni ambazo hufanya presha kupanda.

 

Kunywa walau glasi 5 mpaka 8 kwa siku kutasaidia mwili wako kuwa na maji ya kutosha.

 

Hata hili litakushinda?

 

Je wajua?

Matumizi ya chumvi nyingi hasa ya kuongeza (chumvi mbichi) ni adui mkubwa wa presha ya kupanda. Au uko kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu kama nilivyosema kwenye fact ya nne hapo juu.

 

Mkusanyiko wa chumvi mwilini ndio chanzo hasa cha presha kupanda kwa walio wengi. Hakikisha chumvi unayotumia ni ya kiasi – iliyopikiwa kwenye chakula – sio ya kuongeza mezani. Ukikuta chakula hakina chumvi, kula hivyo hivyo. Acha maswala ya kuomba chumvi ya kuongeza.

 

Je wajua?

Kahawa huwa na tabia ya kupandisha presha hivyo matumizi ya kahawa kila siku sio mazuri kama una presha ya kupanda. Huenda ndio maana unajitahidi kumeza dawa kwa usahihi lakini presha haishuki. Sababu inaweza kuwa hii.

 

 

Jenga mazoea ya kunywa chai, acha wengine wanywe kahawa, wewe angalia afya yako.

Je wajua?

Sigara ni kisababishi kikubwa cha presha kuwa juu. Kama wewe uko kwenye hatari ya kupata presha au una presha tayari, kuendelea kuvuta sigara ni kosa kubwa litakalokuhumu baadae. Sigara ina kemikali ya nicotine ambayo husababisha uteja wa kahawa lakini pia husababisha mwili kupandisha presha na kuongeza hatari ya shambulio la moyo.

 

Ukweli mchungu, kama wewe una presha ya kupanda, sigara itabidi uzikimbie tu.

 

Je wajua?

Kufanya mazoezi walau dakika 30 kwa siku tano kila wiki husaidia kushusha presha yako na kuifanya iwe kawaida kwa masaa 24 mpaka 48.

 

Kwa maana hiyo ukiwa na utaratibu wa kawaida wa kutokwa jasho kwa dakika 30, unafanya presha yako na mapigo ya moyo kuwa ya kawaida, hivyo kuondoa madhara ya muda mrefu ya presha kwenye moyo, mishipa ya damu na figo.

 

 

Utafiti unaonyesha mazoezi ya nusu saa hushusha presha kwa kiwango cha 2-3 mmhg kwa muda huo.

 

Je wajua?

Unywaji wa pombe usiozidi bia tatu kwa mwanaume na mbili kwa mwanamke – kwa siku – huwa na faida katika mwili na inaweza kusaidia  kupunguza kiasi cha cholesterol mwilini hivyo kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo.

 

Utumiaji wa pombe zaidi ya hapo huwa na hatari ya kupandisha presha yako juu. Ulevi na presha haviendani kabisa. Pombe ikishakuwa nyingi inakuwa na effect kinyume kabisa.

 

Kunywa kwa misimu, usiwe mlevi wa kila siku na jenga tabia ya kuridhika na pombe kiasi tu.

 

Je wajua?

Presha ya kushuka nayo inaweza kuwa changamoto sana kwa watu mbalimbali. Una presha ya kushuka na madaktari wamethibitisha hilo?

 

Matumizi ya kahawa na kuongeza chumvi kiasi kwenye chakula yanaweza kusaidia kupandisha presha yako katika kiwango cha kawaida.

 

Kama una presha ya kushuka, siku zote tembea na maji ya kunywa in case ukisikia kizunguzungu. Pia usisahau kununua mashine ya kuangalia presha yako.

 

Je wajua?

SIO kila mwenye presha ya systolic chini ya 100 ana presha ya kushuka, wengine ndio presha zao za kawaida hizo. Hivyo hakikisha kuna dalili zingine kama kizunguzungu, moyo kwenda mbio au mapigo ya moyo kuwa chini ya 50bpm.

 

Je wajua?

Kutumia dawa za presha sio kigezo cha kufanya presha yako iwe kawaida. Wangapi wanameza dawa na bado presha zao hazikai sawa?

 

Cha muhimu ni nidhamu ya vyakula na  mazingira. Kama unameza dawa lakini visababishi vyote tulivyotaja hapo juu wewe hutaki kuacha au kupunguza, sahau kuhusu presha yako kushuka! Utaambulia kuongezewa madawa na kuuchosha mwili zaidi.

Kama unameza dawa halafu kila siku wewe ni migogoro ya kifamilia na kijamii, sahau kuhusu presha yako kushuka mpaka ufanye utatuzi wa mambo yako. Hakuna kitu kinachopeleka presha juu kama stress.

 

Je wajua?

Presha isiyoshuka muda mrefu inaweza kuleta uharibifu mwilini hasa katika vile viungo muhimu. Mfano huweza kupanua moyo, kupasua mishipa ya damu na kuleta stroke, kuuwa Figo taratibu, kuleta upofu na kadhalika.

 

Wakati unagoma kupima na kutibiwa presha yako usisahau hili.

 

Je wajua?

Stress hufanya presha kupanda sana. Unapaswa kujitahidi kwa hali na mali kukwepa mazingira yatakayokupa msongo wa mawazo. Huwezi kukwepa matatizo lakini unapaswa ujue jinsi ya kuyapokea na kuyatatua.

 

Katika makala yangu ya njia tano za kisaikologia za kulinda afya, utayakuta majibu yake, lakini kubwa zaidi ni kujifunza kuwa mtu wa kuwaza suluhisho la tatizo kuliko kuwaza tatizo lenyewe.

 

Endelea kujifunza afya kupitia blog yako pendwa. Tuna mada nyingi zinazokuhusu. Pia usisahau kununua vitabu vyetu vifupi kupata maarifa zaidi.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW