Kipindi cha mfungo kinaweza kudhaniwa kuwa ni kipindi cha mara kwa mara ambapo kuna dirisha dogo la kupiga msosi.
Hivyo watu wengi wanaofunga huwa na mategemeo ya kupungua uzito na matokeo ya matarajio haya hutofautiana kwa mtu na mtu.
Wengine hupungua uzito, wengine huongezeka na baadhi hubaki na uzito ule ule wa mara ya kwanza.
Watu wanaofunga, kwasababu mbalimbali, wakiwa na lengo la kupungua uzito wanakua na fikra ya kudhani kwamba kwa sababu sitakua nakula muda wa asubuhi na mchana kama kawaida basi kuna uwezekano nitapungua.
Hilo wazo linaweza kuwa na usahihi pale tu utakua unakula chakula kwa kiwango kidogo muda wa kufungulia, lakini kama utakua unafunga halafu unakula chakula kingi, sahau uwezekano wa kupunguza!
Kwanini?
Kufunga si suluhisho la kupunguza uzito kwasababu process ya kupungua hutegemea usawa wa kalori – hichi ni kipimo cha nguvu iliyoko katika chakula unachokula.
Ikiwa unakula kupita kiasi wakati wa dirisha la kula, utaongezeka uzito bila kujali kuwa unafunga kwa muda.
Hii ni kwa sababu utakua unaupa mwili kalori nyingi kuliko vile ambavyo mwili unahitaji na hasa pale ambapo baada ya kula utakua unapumzika na kulala baada ya masaa machache.
Mfano, kwa kawaida binaadamu huhitaji kalori 2,100 mpaka 2,300 kwa siku ambazo hizi hutokana na ulaji wa vyakula vyote kwa siku.
Kama chakula kitakua kingi na kalori nazo zitakua nyingi, na hii itapelekea ongezeko la uzito. Kama mtu atakua anakula kalori kidogo, basi hata uzito hautakua unaongezeka sana.
Vyakula vilivyokua na kalori nyingi na kusababisha unene ni vyakula vyenye asili ya wanga ambavyo ni nafaka kama vile mahindi, mchele pamoja na vyalula kama ndizi na vyakula vya wanga asili ya mizizi kama vile mihogo, magimbi , viazi vitamu na kadhalika.
Vyakula ambavyo vina kalori kidogo na havisababishi ongezeko la uzito mkubwa ni vyakula ambavyo viko kwenye kundi la mbogamboga na matunda mfano mboga za majani ya kijani, saladi yaani kachumbari, matango, maparachichi na kadhalika.
Jinsi ya kula katika kipindi cha mfungo ili kuwezesha kupunguza uzito
Kwanza kabisa, katika kipindi cha mfungo wa aina yoyote, ni muhimu kunywa maji ya kutosha katika mida ya kufungulia – sio chini ya glass 2; kama kuna wanaofunga na kuwa na ruhusa ya kunywa maji, basi wanaweza kutumia muda huo kunywa maji ya kutosha.
Lakini pia katika kipindi hichi cha mfungo inapaswa kuchagua kula vyakula visivyo na mafuta mengi na sukari nyingi kwa sababu vyakula hivi husababisha kalori nyingi kuhifadhiwa mwilini ambapo hizi hugeuka mafuta na kusababisha changamoto za kiafya.
Mfano wa vyakula vyenye mafuta mengi ni kama vyakula vyenye kukaangwa katika mafuta mengi kama vile nyama za kukaanga, viazi vya kukaanga au chips mayai.
Hivi huwa na mafuta mengi kutokana na mtindo wake wa upishi lakini pia kuzingatia kuweka mafuta kiasi wakati wa kuandaa vyakula kama vile mchuzi wa nyama, maharage au njegere kwa ajili ya kutumia wakati wa kula .
Mfano wa vyakula vya asili vyenye kiwango kidogo cha mafuta ni mihogo ya kuchemsha, magimbi ya kuchemsha pamoja na viazi vitamu vya kuchemsha.
Hata ndizi za kuchemsha, maharage yaliyopikwa na nazi kiasi au siagi ya karanga pia ni chakula sahihi kama unataka kupungua uzito wakati wa kufunga.
Umegundua namna ambavyo nimesisitiza vya kuchemsha?
Hii ni kwa sababu vyakula vya kuchemsha sio hatarishi kwa afya kama vyakula vya kukaanga na vyenye sukari nyingi – kama vile soda, biskuti, pipi, chocolate na kadhalika.
Suala hii huwa na maana hio hio kwa upande wa vyakula venye sukari, vipo ambavyo havina sukari nyingi ambapo hapa nashauri kutumia vyakula vyenye sukari asilia hasa matunda ya asili na hivyo kuepuka matumizi ya vyakula vilivyochakatwa viwandani na kuongezewa sukari kama vile maziwa ya yogati, soda, pamoja na juice za viwandani.
Je, wajua?
Muda wa kula na mzunguko wa chakula sio muhimu kama jumla ya ulaji wa kila siku wa mtu binafsi kwa ajili ya kupunguza uzito na hata ukuaji wa misuli.
Hii inamaanisha kwamba ratiba za kila siku za kula tulizoziweka hazileti mabadiliko katika mwili kwa sababu zile zinabaki kuwa ratiba tu lakini kiasi cha chakula kinacholiwa kwa ujumla kwa siku nzima ndicho kinachopelekea mabadiliko ya afya ya mwili.
Ndio maana kuna mtu anaweza kunywa chai, breakfast, saa 1 asubuhi, mwingine akanywa saa 4, mwingine akanywa saa 5 na kadhalika.
Hivyo hivyo hata kwa chakula cha mchana, kuna mtu anakula saa 6, mwingine saa 8 mchana na mwingine akapiga msosi wake hata saa 9 alasiri.
Hii hutuonyesha kwamba ile inabaki kuwa mida tu ya kula kutokana na utofauti wa ratiba za siku za kila mtu.
Na katika swala la mizunguko ya vyakula huwa tumetofautiana pia, kuna mtu anakula chakula cha wanga aina moja mchana, aina nyingine jioni.
Mfano, watu wengi wanaweza kuwa wamezoea kula ugali mchana na wali jioni.
Mwisho
Mara nyingi chakula kinacholiwa baada ya kufunga kinakua ni chakula chenye asili ya wanga kwa wingi, na kunakua na aina chache sana ya vyakula vya protini.
Hivyo basi pindi unapokua unaandaa chakula chako cha kufungulia, hakikisha unazingatia makundi yote ya chakula ili tupate mlo kamili hasa unaohusisha vyakula vyenye kirutubisho cha protini ambacho mfano wake ni mayai, kuku na samaki.
Lakini pia protini inayotokana na mimea inaweza kutumika kama vile maharage, njugu, njegere , kunde na kadhalika.
Muhimu: Usisahau kufanya mazoezi kipindi cha mfungo kwa ajili ya kuchangamsha mwili.

Providing nutrition education and counselling in Tanzanian local communities, currently in Mkuranga – Pwani region. My goal is to raise awareness on how to improve our health through nutrition – in all human life stages.
Makala nzuri sana dada Ester. Asante kwa madini!
Karibu sana sana.