Kiharusi: Nini Hutokea Baada ya Kukipata? 

Bila shaka huwa una tabia ya kujifunza namna ya kuepuka magonjwa mbalimbali kama malaria, UKIMWI, kaswende, kansa, n.k. Lakini ulishawahi kujifunza namna ya kujikinga na kiharusi (stroke)?  

Kama bado basi nakusihi uanze sasa kujua namna gani ya kujikinga na changamoto ya kiharusi kwasababau sio ugonjwa mzuri na una matokeo hasi sana ikiwa utaupata. 

 

Ugonjwa wa kiharusi unaweza kuwa wa muda mfupi, ambapo mtu hurejea hali yake ya mwanzo mapema; unaweza pia kuwa wa muda mrefu hasa kwa wale wanaopata kiharusi kutokana na baadhi ya mishipa ya damu kwenye ubongo kupasuka. 

 

 

Asilimia 80% ya ugonjwa wa stroke husababishwa na mitindo ya maisha (lifestyle) itokanayo na ulaji mbovu, uvutaji wa sigara, matumizi ya dawa za kulevya na kadhalika. 

 

Mitindo hii ya maisha inaweza kupelekea changamoto mbalimbali kama presha kuwa juu, mafuta kuwa mengi kwenye damu, uzito mkubwa, damu kuganda, na mengineyo. 

 

Hapo utagundua kwamba una asilimia 80% ya kujikinga na kiharusi kwa kuondoa visababishi hivyo hapo juu, na asilimia 80% kupata kiharusi kama ukiendekeza mitindi hiyo ya maisha. 

 

Ukishapata kiharusi, nini hutokea? 

1. Sonona/msongo wa mawazo (Depression) 

Pigia picha una miaka 45 na una nguvu zako; unajifanyia kila kitu, unakula unachotaka, unakwenda unakotaka, unakutana na unayemtaka na mara ghafla huwezi kufanya vitu hivi mpaka usaidiwe na mtu, utajisikiaje? 

 

 

Ukishapata kiharusi kwa asilimia kubwa utategemea zaidi wana familia ndio wawe msaada wako kuhakikisha wanakutimizia matakwa yako. Kuna muda utatamani kula hiki au kile lakini mpaka mtu mwingine aamue kukuletea lasivyo hutopata. 

 

Hali hii huleta majuto na uchungu sana pale unapoona huwezi kitu na ndipo kuchanganyikiwa huanza. Utaanza kuwaza kila mara, kukosa usingizi na baada ya muda utaanza kukata tamaa na mwisho wake ni sonona. 

 

Unapopata kiharusi hakuna anayeweza kukadiria utapona lini, inaweza kuwa miezi au miaka mingi.  

Kutokana na kuumwa muda mrefu, ndugu na familia huanza kuchoka kukuhudumia na kuanza kukunyanyapaa (sio kwa wote). Hii huleta msongo wa mawazo zaidi. 

 

Hali ya kushindwa kujihudumia kama zamani sio nzuri na huaribu saikolojia yako kama mgonjwa.  

 

Ni rahisi sana mwenza wako kuacha kukujali hasa pale unapokuwa huwezi tena kumtimizia matakwa yake ya kimwili, kifedha na malezi kwa ujumla. Marafiki nao huanza kupungua na pengine kuacha kuja au kukupigia simu na, mbaya zaidi, kukusahau kabisa. Yote haya hupelekea msongo wa mawazo. 

 

Utagunduaje mgonjwa wa stroke ana msongo wa mawazo?

Huanza kukasirika kila mara, kufoka katika vitu vya kawaida, kuwa na huzuni, kukataa kuongea inapobidi, kulalamika kila kitu na kukosa usingizi usiku.  

 

Kwa bahati mbaya hii humuweka katika hali ngumu zaidi kutokana na watu wake wa karibu kuanza kukwazika kwa kuona kama hana shukrani kwa wanayomfanyia na hivyo wanaanza kutumia hiyo kama sababau ya kukaa naye mbali. 

 

Nini cha kufanya?

Wewe kama mtu wake wa karibu unapoanza kuona dalili kama hizi ni vizuri kujaribu mambo kadhaa ili kumsaidia na kuepuka kuharibu mawasiliano yenu. 

 

Kwanza, mtafutie mtaalamu wa saikolojia 

Mara nyingi kwa wewe binafsi sio rahisi kuwa na msaada kwasababu hili ni tatizo la kisaikolojia linalohitaji kufanyiwa kazi na wataalamu. Hii itasaidia kuirudisha saikolojia yake vizuri na kufanya mazingira ya kumuhudumia kuwa salama. 

 

Pili, wewe kama msaidizi wake lazima uwe na uelewa mkubwa.  

Kumbuka mtu huyu kabla ya kupata changamoto hiyo alikuwa na furaha na hakuwa msumbufu kiasi hiko. Usumbufu umeanza baada ya tatizo hili la kiharusi hivyo usiwe mtu wa kukasirika haraka au kuona kama unatukanwa.  

Ni vizuri kuwa na subira na kumuhudumia kwa upole na ukimya bila kuanzisha mabishano ya mara kwa mara. 

 

Uelewa mkubwa na kuchukulia mambo kwa kawaida itasaidia sana katika kumuhudumia. 

 

2. Kulemaa viungo (deformity) 

Viungo vya binadamu vimeumbwa kutembea/kutumika na sio kukaa sehemu moja. Baada ya kupata kiharusi mgonjwa hujikuta hawezi kutumia upande uliopata changamoto na hivyo upande huo hautumiki kama zamani. Hapa ndipo hatari ya kuzidi kulemaa viungo huanza. 

 

Moja ya kanuni ya sayansi ya mazoezi tiba ni kwamba “Any slight movement is key for strength to resume” ikimaanisha hata mwendo mdogo tu wa kiungo ni muhimu kwa ajili ya kiungo kuanza kupata nguvu yake kama zamani. 

 

 

Iko hivi:

Ukifanya mazoezi yoyote, hata kama ni madogo vipi, kwenye kiungo cha mwili kilichopooza husaidia ubongo kutafsiri kwamba sehemu hii inahitaji kufanya kazi hivyo husaidia kutengeneza mishipa mipya ya fahamu, kusaidia kuleta taarifa katika kiungo hicho.

Hii ndio jinsi mazoezi tiba yanavosaidia kurejesha nguvu sehemu iliyopooza. Bahati mbaya baadhi ya wagonjwa wa kiharusi huachwa nyumbani bila kufanya mazoezi yoyote na baada ya muda mikono, vidole na joint za miguu huwa ngumu na kukaza na kupelekea ulemavu wa kudumu.  

 

Hii mara nyingi inatokana na ukosefu wa elimu ya afya na faida ya mazoezi tiba kwa wagonjwa wa kiharusi. 

 

Mgonjwa wa kiharusi asipoendelea kutumia viungo vyake vilivyopooza  mwisho wa siku vitapata ulemavu wa kudumu. Hii itamchelewesha kupata nafuu, baada ya kupona hali yake anaanza kupambana tena na matatizo mengine ya ulemavu mfano mguu, vidole, mikono kutonyooka, viungo kuwa vidogo kutokana na kusinyaa kwa misuli.  

 

Akianza mazoezi mapema anaweza kupunguza athari hizi. 

 

Nini cha kufanya kuepuka hili?

Kwanza, mgonjwa anapaswa kuanza mazoezi mapema iwezekananvyo!

Pamoja na kuwepo na mazoezi maalum ya viungo (physiotherapy), bado mgonjwa anaweza kufanyiwa baadhi ya mazoezi akiwa nyumbani.  

 

Kinachotakiwa ni msaidizi wake kujifunza namna ya kufanya yale mazoezi ya msingi; yale mazoezi maalum yatafanywa na wataalamu. 

 

Mdogo wangu alipozaliwa mwaka 2003 alikuwa na changamoto ya mishipa ya fahamu ya mkono wa kushoto baada ya kuvutwa bega wakati anazaliwa. Baada ya hapo Baba yangu  alishauriwa kumpeleka mtoto kwa wataalamu kwa ajili ya mazoezi tiba.  

Kutokana na huduma hiyo kuwa mbali, wazazi waliweza kumpeleka kwa vipindi maalum na sio wakati wote.  

 

Siwezi kusahau namna ambavo Baba yangu alikuwa na juhudi ya kumfanyia mazoezi mwenyewe nyumbani. Alichofanya ni kuuliza yale mazoezi ya msingi yanafanywaje na baaada ya hapo aliufanya wajibu wake na ratiba yake kuchua na kumfanyia mazoezi mdogo wangu kila siku. 

 

Baada ya muda mrefu mkono wake uliweza kupata nafuu na haukulemaa zaidi. Sasa mdogo wangu amekua na anatumia mkono wake kama kawaida. 

Sawa huna uwezo wa kumpelekea mgonjwa wako mazoezini kila siku lakini hata mazoezi ya kunyoosha mikono na miguu kuepuka ulemavu yanakushinda? Usifikie huko!

Pili, mtafutie mtaalamu wa mazoezi tiba amabaye atasaidia walau mara moja kwa wiki au wiki mbili kama uchumi sio mzuri. Hii itasaidia kuharakisha uponaji wake. 

 

Kutokana na gharama za kumsafirisha mgonjwa kila mara kwenda kwenye mazoezi kuwa kubwa, unaweza kupunguza ukali kwa kuwa na mtaalamu wa mazoezi anayemtembelea na kumfanyisha mazoezi nyumbani.  

 

Huduma hii inatolewa na Abite Nyumbani, kama unahitaji wapigie hapa. 

 

Mwisho

Kama nilivyosema hapo mwanzo, baada ya kupata kiharusi changamoto nyingi hutokea na kwa asilimia kubwa huwa ni mbaya. Habari njema ni kwamba tunaweza kujiepusha kwa asilimia 80% kwa kurekebisha mfumo wa maisha (lifestyle).  

 

Kiharusi sio kwa wazee tu bali hata kwa kijana anayevuta sigara, kutumia madawa ya kulevya, mwenye uzito mkubwa, na kadhalika. 

 

Tafiti mbalimbali zimeonyesha madawa ya kulevya, mfano cocaine, kuwa chanzo cha kiharusi hasa kwa vijana chini ya miaka 35. 

 

Wakati unavuta sigara, kula hovyo na kunenepa hovyo, kuishi unavyotaka, na kukataa kufatilia presha yako, kumbuka kuna adui anaitwa kiharusi. Ameharibu ndoto za wengi na kurudisha familia nyuma kichumi na kimahusiano, jali afya yako!

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW