Mimba ina mambo mengi sana. Unapobeba mimba kutakuwa na mabadiliko mengi sana kwasababu ya homoni za mimba. Mara kuvimba miguu, kuhema haraka, kuchoka, kutapika, kukojoa mara kwa mara n.k. Mambo ni mengi, muda mwingi.
Kama wewe ni mama na una watoto inawezekana hujawahi kupata kifafa cha mimba maana huwa ni nadra sana kutokea. Kati ya wajawazito 20 basi mmoja anaweza kupata kifafa cha mimba.
Lakini kuna uwezekano umesikia au umeona kwa rafiki zako au hata wajawazito wenzako wakati uko labour.
Ulishawahi kujua kifafa cha mimba ni nini na kinatokea kwa sababu gani?
Mwaka 2023 wakati nipo zangu zamu ya mchana, wodi ya wanawake, nikitazama wagonjwa wangu kama kawaida; kulikuwa na dada mjamzito alikuwa kwenye uchungu na alikuwa akizunguka zunguka kama kawaida ya wajawazito wakiwa kwenye uchungu.
Basi wakati tukiendelea kuona wagonjwa tukasikia sauti ya mtu kudondoka kama kapiga kichwa chini na ikasikika sauti ya watu wakiomba msaada.
Kutoka nje, tukakuta yule dada anagalagala kama mtu mwenye kifafa, mapovu mdomoni; hali hii ilichukua dakika moja wakati tukifanya liwezekanalo kumsaidia kutibu tatizo.
Ilikuwa taharuki sana, kwetu na ndugu wa mgonjwa.
Baada ya hapo ndugu walinifata na kunambia wanataka wamuite mchungaji inawezekana kuna mtu amemtumia mapepo binti yao kwani hajawahi kuanguka kifafa toka azaliwe. Sasa imekuwaje anaanguka kifafa?
Niliwaelewa na nikajaribu kuwapa elimu na kuwaondoa wasiwasi. Basi nikaita jopo la madaktari kwa pamoja tukamsaidia na ndani ya masaa manne alifanyiwa operation akapata mtoto wake.
Bila shaka umewahi kushuhudia hali kama hii au umesikia kwenye radio au kuona kwenye movie au kusoma sehemu lakini hujaelewa.
Sasa kifafa cha mimba ni nini?
Kifafa cha mimba (eclampsia) ni degedege inayotokea wakati wa ujauzito walau kwanzia wiki ya 20 ya mimba na kuendelea.
Kifafa hiki huwa sawa na kifafa cha kawaida ila utofauti ni kwamba, hiki kinaletwa na uwepo wa mimba. Mara nyingi kifafa hiki hutanguliwa na presha ya mimba.
Husababishwa na nini?
Kifafa cha mimba (eclampsia) mara nyingi hutanguliwa na presha ya mimba (Pre-eclampsia). Presha hii huanza mapema baada ya wiki ya 20 ya mimba; isipotibiwa vizuri husababisha mishipa ya damu kusinyaa na kutopeleka damu vizuri kwenye ubongo na kupelekea kupata kifafa (convulsions).
Presha hii husababishwa na mfuko wa mtoto (placenta) unapopata hitilafu kwenye kujishikiza kwenye mji wa mimba (uterus), kwa kiingereza tunasema faulty placentation, na kusababisha utoaji wa homoni ambazo ndizo huja kufanya presha ipande.
Hivyo mama mjamzito anapokuwa na presha ya juu ni lazima apate uangalizi wa daktari na manesi na hili hufanyika kama mama anahudhuria kliniki ipasavyo.
Visababishi vingine ni kuwa na vinasaba vya tatizo la kifafa cha mimba mfano, kama mama au dada zako walishapata hali hiyo kwenye mimba zao basi nawewe unaweza kuwa kwenye hatari ya kupata.
Kama ulishawahi kupata kifafa cha mimba kwenye mimba zilizopita basi unaweza kupata tena. Mabadiliko ya mzazi (baba mwingine), mfano mimba uliyonayo kama ni ya baba tofauti na wa mimba zilizotangulia inaweza kukuweka kwenye hatari ya kupata presha ya mimba na kupelekea kifafa.
Pia mimba za utotoni chini ya miaka 20 au uzeeni kuanzia miaka 40 huweza kuongeza uwezekano wa kupata kifafa cha mimba.
“Kifafa cha Mimba ni Adui Asiyetabirika”
Ni miaka 13, tangu 2011 mpaka sasa, Shirika la Afya (WHO) duniani kwa kushirikiana na nchi wanachama ikiwemo Tanzania limekuwa likija na miongozo kuhusiana na namna ya kuzuia kifafa cha mimba ikiwemo kuja na kufanya mabadiriko ya dawa za matibabu za ugonjwa huu.
Miongozo hii imefanikiwa kupunguza vifo vya mama na mtoto, kwa asilimia kubwa, vilivyokuwa vinasabishwa na presha ya mimba pamoja na kifafa cha mimba.
Pamoja na dalili za presha ya mimba kujulikana na kudhibitiwa mapema, bado kuna baadhi ya mama wajawazito waliopata kifafa cha mimba pamoja na presha zao kuwa za kawaida. Kwa maana hiyo mtu mwenye presha ndogo ya mimba (mild preeclampsia) anaweza kupata kifafa cha mimba kinyume na matarajio hivyo kufanya tatizo hili kuwa tishio.
Sio hiyo tu bali baadhi ya wagonjwa wamepata vifafa baada hata ya kujifungua. Ni kweli kwamba kifafa cha mimba huweza kutokea hata saa 24 baada ya kujifungua lakini kuna utafiti ulionyesha ndani ya siku 42 baada ya kujifungua mama anaweza kupata kifafa.
Kutokana na hali hii ni muhimu hospitali kuwa katika maandalizi muda wowote kupambana na hali hii endapo ikijitokeza. Pia mgonjwa kuwa makini kurudi hospitali anapoendelea kupata presha ya juu au dalili kama nilizozitaja hapo juu.
Repoti za mbalimbali za afya zinaonyesha tatizo la kifafa cha mimba huathiri wajawazito kwa asilimia 3% mpaka 8% na huweza kusababisha vifo kwa asilimia 5% mpaka 20% hivyo hii inaweka msisitizo mkubwa kwenye kupambana na hali hii kwa nguvu zote kuanzia kwa mama mjamzito mpaka watumishi wa afya na wizara kwa ujumla.
Nini unaweza kufanya kupunguza uwezekano wa kupata kifafa?
Kifafa cha mimba ni hatari zaidi ukiwa nje ya hospitali na inaweza kupelekea uwezekano mkubwa wa kuleta madhara kwa mama na mtoto.
Mama mjamzito ni vizuri kuwa makini anapokuwa na mimba. Kuna dalili ambazo ukiziona basi zinaweza kuhashiria hali ya hatari na hivyo ni muhimu kutafuta msaada wa kiafya mapema.
Kama tulivyosema, kabla ya kifafa basi hutanguliwa na presha yako kupanda. Presha ya mimba (Pre-eclampsia) huweza kuja na miguu kuvimba, kichwa kuuma, maumivu ya tumbo hasa upande wa juu kulia (sio chini ya kitovu), kuzunguzungu, kifua na kaadhalika.
Uonapo dalili kama hizi basi nenda hospitali mapema kwa ajili ya kufanyiwa vipimo maalum kuhakikisha hauna presha ya mimba. Kuchkulia powa dalili hizi kumesababisha wajawazito wengi kupata vifafa nyumbani.
Pia dalili hizi huweza kugundulika ukiwa unahudhuria kliniki mara kwa mara. Kliniki ya miezi mitatu ya mwanzoni ni muhimu sana kwa ajili ya vipimo vya awali. Pia kliniki ya kuanzia wiki ya 20 mpaka 24 ni lazima sana ili kuhakikisha hauna dalili za mapema za presha ya mimba.
6 kati ya 10 ya wajawazito wanaopata kifafa cha mimba huwa na rekodi mbaya ya mahudhurio kliniki. Utakuta wamehudhuria mara chache sana na utakuta presha yao iko juu na hawajawahi kumeza dawa.
Kama ukigundulika una presha ya mimba basi hakikisha unameza dawa kama maelezo yalivyo na hudhuria clinic mara kwa mara inavyotakiwa kuhakikisha presha yako iko vizuri.
Kama una moja ya visababishi nilivovitaja kule juu, basi unapaswa kuwa makini zaidi unapokuwa na mimba.
Baadhi ya mila potofu kuhusu kifafa cha mimba
1. Mjamzito hupata kifafa cha mimba kama amebeba Mimba ya baba mwingine?
Jibu: Sio lazima, inaweza kusababishwa na mambo mengine. Kuchelewa kupata mtoto mwingine pia inaweza kuwa sababu, mimba ya kwanza (Prime gravida) inaweza kuwa sababu.
Pia kama ulishawahi kupata kifafa kwenye mimba za nyuma inaweza kuwa sababu. Kiufupi mtoto kuwa wa baba mwingine ni moja ya sababu lakini sio peke yake, zipo nyingi. Usigombane na mkeo kisa kapata kifafa, sababu ni nyingi.
2. Kifafa cha mimba ni mapepo ya kutupiwa na wasiopenda ubebe mimba?
Hapana, ni ugonjwa unaosababishwa na mimba kama nilivyoielezea hapo juu.
Una mpango wa kubeba mimba? Usiogope, kifafa cha mimba hutokea kwa nadra sana! Zingatia ushauri wa daktari hasa unapokuwa na presha ya mimba.
Hudhuria kliniki ipasavyo na kuwa karibu na huduma za afya. Uonapo dalili yoyote ya hatari wahi hospitali.
Kwa kumalizia…
Kupitia ukurasa wetu wa Instagram, tunatoa ushauri wa afya bure, tutafute kama una changamoto ya kiafya au uzazi.
Kama wewe ni mjamzito, unafahamu vyakula muhimu vya kutumia wakati wa mimba na baada ya kujifungua? Soma makala za Afisa Lishe wetu, Esther Mndeme, kupitia link hii.
Mwisho tembelea duka letu kwa ajili ya kujipatia huduma ya vitabu vya afya.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.