Uric Acid ni kemikali ambayo ikiongezeka kwa wingi mwilini hupelekea utengenezwaji wa chembe ngumu, watu wengine huita mawe, ambayo hujikusanya na kusababisha gout au arthritis kwa upande wa miguu na mifupa.
Lakini pia, katika mfumo wa mkojo uric acid hii hupelekea kutengenezwa kwa chembe ngumu ambazo hujulikana kwa lugha iliyozoeleka kama mawe katika figo.
Nini kinasababisha ongezeko la Uric Acid mwilini?
Ongezeko la uric acid mwilini hutokea baada ya ulaji wa vyakula vinavyosababisha mkusanyiko wa uric acid mwilini kwa wingi.
Mfano wa vyakula hivi ni nyama nyekundu, nyama zitokanazo na viungo vya ndani kama vile maini na figo, pamoja na samakigamba kama vile kaa na kamba.
Lakini pia uric acid huweza kuongezeka pale ambapo mtu anakunywa vinywaji vilivyoongezwa sukari aina ya fructose kama vile soda na juisi za boksi, pamoja na unywaji wa pombe hasa bia.
Ongezeko la uric acid katika mwili huweza kupelekea matatizo kama vile gout katika miguu, matatizo ya figo kama vile ‘mawe katika figo’ na matatizo mengine ya kiafya.
Ufanye nini ili kuepukana na ongezeko la uric acid mwilini mwako?
Mambo ya kufanyika ili kupambana na ongezeko la uric acid katika mwili
Makala mbalimbali zilizoandikwa na madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani zimeorodhesha mapendekezo mbalimbali ambayo hata sisi maafisa lishe tunapendekeza kufanyika ili kuweza kupunguza kiwango cha uric acid mwilini:
1. Utumiaji wa vyakula vyenye asili ya mimea (plant-based diet/vegetarian diet) ambayo imeonekana katika tafiti kupunguza hatari ya kupata gout.
Vyakula hivi vinapaswa kuwa katika kundi la nafaka zisizokobolewa. Mfano, ugali wa mtama, ugali wa dona, mchele usiokobolewa na kadhalika.
2. Utumiaji wa vyakula vya protini, vyenye kazi ya kujenga mwili, vinavyotoka katika kundi la mikundekunde.
Vyakula hivi vitatumika kama mubadala wa samakigamba kama vile kamba na kaa. Pia kuepuka matumizi ya nyama ni muhimu kwa sababu ina uwezo wa kuongeza uric acid katika mwili wako.
Mfano wa vyakula vya jamii ya mikunde kunde ni choroko, maharage, njegere, kunde, njugu na kadhalika.
3. Kuepuka unywaji wa pombe kwa sababu pombe ikiingia katika mwili huvunjwa vunjwa na mwisho wa siku hupelekea kupatikana kwa purine ambayo huwa uric acid mwilini.
Tafiti zinaonyesha kwamba unywaji wa pombe huongeza hatari ya kupata gout katika muda wa masaa 24 baada ya kunywa pombe hali ambayo ni tofauti kwa mtu ambaye sio mnywaji wa pombe.
4. Kuepuka unywaji wa vimiminika vilivyoongezwa sukari kama vile juisi za viwandani pamoja na soda.
Soda hizi huwa na sukari aina ya fructose ambayo imehusishwa na ongezeko la uric acid katika mwili na kuonyesha kupelekea magonjwa kama vile gout.
5. Unywaji wa maji kwa wingi – kama lita mbili kwa siku.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kiasi kingi cha maji mwilini husaidia kupunguza hali ya utengenezwaji wa mawe katika mwili.
Hii ni kwasababu mawe haya yana mfano wa chumvichumvi na ili chumvi chumvi itengenezwe maji yanapaswa kuondoka kwani katika uwepo wa maji ni ngumu kwa chumvi chumvi zile kutengenezwa.
Vivyo hivyo katika miili yetu, maji mengi huzuia ukusanyikaji wa mawe katika viungo mbalimbali vya mwili kama figo.
6. Ulaji wa vyakula vyenye vitamin C
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kwamba utumiaji wa vitamin C kwa kiwango cha milligramu 500 kwa siku husaidia kupunguza kiwango cha uric acid mwilini na kuongeza utolewaji wa taka mwili kwa njia ya mkojo.
Vitamin C hii hupatikana katika mbogamboga na matunda mbalimbali kama vile maembe, machungwa, matunda aina ya kiwi pamoja na pilipili-hoho.
7. Swala la mwisho ambalo ningependa kukazia ni kufanya mazoezi lakini pia kutafuta ushauri wa wataalamu wa lishe pamoja na wataalamu wengine wa Afya ili kuweza kupata msaada pale unapogundulika na matatizo ya ongezeko la uric acid mwilini.
Lakini pia hakikisha unazingatia swala la kuwa na uzito sahihi wa mwili kwasababu tafiti zinaonyesha watu wenye uzito mkubwa huwa katika hatari ya ongezeko la uric acid ambayo inapelekea ugonjwa wa gout tofauti na watu wenye uzito mdogo.
Kwa maswali yoyote kuhusu makala hii, usisite kuniandikia kwenye comment section. Unaweza pia kutembelea duka letu at shop.abiteafya.com kwa vitabu na huduma mbalimbali za afya.

Providing nutrition education and counselling in Tanzanian local communities, currently in Mkuranga – Pwani region. My goal is to raise awareness on how to improve our health through nutrition – in all human life stages.