Jinsi Ugonjwa wa Kisukari Unavyoweza Kuathiri Afya Yako ya Kinywa

“Kisukari” au ugonjwa wa kisukari (diabetes) ni ugonjwa uliosheheni sana katika jamii zetu. Kisukari ni hali ya kiafya inayotokea wakati kiwango cha sukari (glucose) kwenye damu kinapokuwa juu sana.

 

Kuna aina tofauti za kisukari, ikiwa ni pamoja na kisukari cha aina ya 1, kisukari cha aina ya 2, na kisukari cha ujauzito (gestational diabetes). Hali hii inatokea wakati mwili hauwezi kutumia vizuri au kuzalisha insulini, homoni inayosaidia mwili kutumia sukari.

 

Kisukari kinaweza kuwa na athari kubwa katika mifumo yote ya mwili wako kama vile mfumo wa moyo, figo, macho, na hata kusababisha matatizo ya kuganda kwa damu. Mbali na hayo, kisukari pia kina uhusiano wa karibu na masuala ya afya ya mdomo. Uhusiano wa kina kati ya kisukari na afya ya mdomo umekuwa swala lenye umuhimu unaoongezeka katika tiba ya afya ya kinywa na meno.

 

Mara nyingi tumekuwa tukikimbilia kuongelea mifumo mingine ya mwili na kusahau ni kwa jinsi gani mfumo wa kinywa unavyoathirika na ugonjwa huu. Soma zaidi kujua athari za kisukari katika kinywa chako na hatua za kufuata upatapo matatizo hayo.

 

Athari ya ugonjwa wa kisukari kwenye kinywa ni kama zifuatazo:

1. Magonjwa ya fizi

Moja ya dalili zinazojulikana zaidi kwenye uhusiano wa kisukari na afya ya mdomo ni hatari iliyoinuka kwa namna ya magonjwa ya fizi. Kisukari kinavuruga uwezo wa mwili kupambana na maambukizi, hivyo kuongeza hatari ya magonjwa ya fizi.

 

Kisukari kisipotibitiwa kisawasawa kinaweza kusababisha kiwango cha juu cha sukari mwilini, hii hutoa mazingira yanayofaa kwa ukuaji wa bakteria na kusababisha uchochezi kwenye fizi. Uchochezi huu wa muda mrefu unaweza kusababisha periodontitis, aina kali ya ugonjwa wa fizi inayoweza kusababisha upotezaji wa jino ikiwa haitatibiwa.

 

2. Ukavu wa mdomo (Xerostomia)

Kisukari pia kinaweza kuchangia ukavu wa mdomo, hali inayojitokeza kwa sababu ya uzalishaji mdogo wa mate. Mate yana jukumu muhimu katika kudumisha afya ya mdomo kwa kufyonza asidi, kusafisha chembe za chakula, na kuzuia ukuaji wa bakteria.

 

Kwa watu wenye kisukari, uzalishaji hafifu wa mate unaweza kuongeza hatari ya meno kuoza, magonjwa ya fizi, na maambukizo ya mdomo.

 

3. Kuchelewa kupona kwa majeraha

Kisukari kinaweza kuzuia uwezo wa mwili kupona, na hii inaathiri pia uponyaji wa majeraha na madhara ya mdomo. Matibabu ya kawaida ya meno kama vile kutoa jino au matibabu ya fizi yanaweza kuchukua muda mrefu kupona kwa watu wenye kisukari.

 

Kisukari kisichodhibitiwa kinaweza kuongeza tatizo hili, na hivyo kuwapa wataalamu wa meno changamoto katika kusimamia huduma nzuri baada ya matibabu.

 

4. Burning Mouth Syndrome

Baadhi ya wagonjwa wa kisukari wanaweza kuwa na hali inayojulikana kama “burning mouth syndrome” inayojitokeza kwa hisia kali ya kuungua au kutoa tindi kwenye mdomo. Ingawa chanzo kamili hakieleweki, inaaminika kuwa uharibifu wa mishipa ya fahamu inayohusiana na kisukari (neuropathy) unaweza kuchangia kwa kiasi fulani kwenye hali hii.

 

Kwahiyo…

Kama unapatwa na magonjwa ya fizi au ukavu wa mdomo ni vyema kuonana mapema na daktari wa meno ili upatiwe matibabu. Lakini pia kuna mate ya kutengenezwa (artificial saliva) ambayo unaweza kununua katika duka la dawa ili kuboresha hali ya unyevunyevu kinywani.

 

Ni muhimu kwa watu wenye kisukari kuchukua hatua za kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu kwa kufuata lishe bora, kufanya mazoezi, na kuchukua dawa au insulini kama ilivyoelekezwa na wataalamu wa afya.

 

Kwa kuwa na udhibiti mzuri wa kisukari, unaweza kupunguza hatari ya matatizo ya afya ya kinywa na meno yanayohusiana na ugonjwa huu.

3 thoughts on “Jinsi Ugonjwa wa Kisukari Unavyoweza Kuathiri Afya Yako ya Kinywa”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW