Jinsi Mtazamo wa Dawa Unavyoweka Afya Yako Hatarini

Mtazamo ni kama miwani, ukivaa miwani meusi basi dunia na vitu vyake huonekana vyeusi, ukivaa miwani meupe hivyo hivyo mambo yataonekana meupe.” – Dr. Faustine Kamugisha (Priest and Faith Mentor)

 

Afya yako pia ni mtazamo wako. Mtazamo chanya huleta afya bora, kinyume chake ni afya mbovu. Wewe umevaa miwani ya rangi gani kwenye afya yako?

 

Mtazamo wa kumeza Dawa kwa kila ugonjwa ni changamoto kubwa sana inayoharibu Afya yako. Kila kinachotokea mwilini mwako hauwazi utatue vipi, unawaza umeze dawa gani?

 

Mtazamo wa dawa (medication mindset)

“Sasa Daktari hapa unashauri nimeze dawa gani?” Ni kauli ambayo nimeisikia mara nyingi sana katika kazi yangu. Nimeshuhudia watu wenye mtazamo wa kumeza dawa, wanapenda dawa mno. Watakupigia na kukueleza tatizo halafu mwishoni wanamalizia: nimeze dawa gani?

 

Mtazamo wao ni kwamba kila tatizo linalotokea mwilini lazima wameze dawa, hamna namna nyingine. Mtu wa namna hii ukimpa ushauri wa kufuata kwa ajili ya tatizo lake bila kumtajia dawa ya kumeza basi hataamini kama umemtibu. Atampigia daktari mwingine ilimradi aandikiwe dawa.

 

Akija hospitali haondoki mpaka aandikiwe walau Panadol, la sivyo ni ugomvi na hatakuona kama umemjibu. Ana uwezo wa kutoka kukuona wewe halafu akaingia mlango mwingine wa daktari, ilimradi tu aandikiwe dawa.

 

 

Kuna mgonjwa aliwahi kunishtaki kwa diwani kwamba nimekataa kumtibu. Alikuwa na tatizo la kutopata choo kwa siku tatu, basi nikamshauri njia ya kupata choo ni anunue kabeji – ale ya kutosha, anywe maji walau glasi nane kwa siku, ale maharage, na pia machungwa (kama akiyapata).

 

Nikamwambia akifanikisha hilo atapata choo ndani ya saa 24. Baada ya kumaliza kumuelezea akabaki ameniangalia anasubiri dawa, nikamwambia hiyo ndio dawa, akakasirika sana.

 

Mtu wa namna hii ndio utakuta ana furushi la dawa tofauti kama aina 7 na mbaya zaidi utagundua dawa kama za aina nne zote zinatibu kitu kilekile na ni za kundi moja, sema kampuni tofauti.

 

Mtazamo huu ndio unakufanya uzunguke kutoka kwa daktari mmoja kwenda mwingine na kuomba dawa tofauti tofauti kwa kudhani dawa uliyopewa kwingine haina msaada.

 

Hali hii inasababishwa na mtu kuwa na mtazamo wa dawa kuliko kitu kingine, anaamini kwamba kila dalili mwilini lazima aimezee dawa. Mbaya zaidi tabia hii humfanya mtu kutofata maelekezo mengine yasiyo ya dawa ya kutibu tatizo, hubakia tu kuangalia kama dawa haijafanya kazi siku tatu, basi ataenda kutafuta nyingine.

Watu wa namna hii ndio hufanya wamiliki wa maduka ya dawa wawe matajiri.

 

Sio kila dalili mwilini mwako inahitaji dawa…

Kuna dalili huja kwa sababu ya hali mbalimbali mwilini mwako. Mfano, mtu ukipata allergy, tiba pekee inaweza kuwa ni kuchunguza na kuondoa tatizo tu bila kuhitaji dawa. Inawezekana kuna sabuni au chakula au perfume mpya ambayo umetumia na ukiacha tu basi muwasho unaisha bila dawa.

Ndio maana huwa tunachukua maelezo kabla ya kuanza kutibu tatizo.

 

Mtazamo wa dawa unatokana na hali ya mtu kuwa na phobia na ugonjwa. Yaani kila unapopata changamoto kidogo unawaza labda usipomeza dawa utakufa na hivyo unakimbilia dawa. Bahati mbaya hata dawa unazomeza inawezekana sio za ugonjwa huo.

 

Mfano, inawezekana ukapata tumbo la kuhara kutokana na hofu au labda umetumia vyakula kama maziwa fresh ambayo yanaweza kukufanya kuharisha. Sasa utakuta mtu kashaanza kumeza fragyl kwa ajili tu ya kuharisha kumbe anatibu kitu ambacho hana.

 

Watu wanaoogopa kumeza dawa wakati mwingine wana faida nyingi kuliko watu wanaopenda kumeza dawa kwa kila kitu. Wasiopenda dawa mpaka wameze dawa lazima iwe wameshauriwa na daktari au mtaalamu fulani na sio tu kila tatizo dawa.

 

Figo Vs Dawa za Maumivu

Professor Janabi (Mtaalamu wa Magonjwa ya Ndani, Hospitali ya Jakaya Kikwete) alitaja sababu mbalimbali zinazosababisha Figo kuharibika, na mojawapo ya sababu hizo ni matumizi ya dawa za maumivu kwa muda mrefu.

 

Dawa hizi husababisha kukusanyika kwa chumvi na maji mengi mwilini na baadaye huweza kupelekea kuathiri figo na kuongeza presha mwilini.

 

Hatari iliyopo hapa ni kwamba, dawa za maumivu ni kati ya dawa zinazomezwa mara nyingi kupita kitu chochote kwa sababu ni rahisi kuzipata na ni rahisi mtu kuamua kuzimeza kila anaposikia maumivu.

 

Sio hilo tu, utafiti uliofanyika Katika Chuo kikuu cha Stanford Uingereza ulionyesha kwamba matumizi ya dawa za maumivu kwa muda mrefu au mara kwa mara huweza kufanya maumivu kuwa sugu.

 

Madhara mengine ni vidonda vya tumbo na kuathiri moyo. Bahati mbaya taarifa kama hizi huwa hazisemwi sana kwenye jamii na hivyo kupelekea madhara makubwa.

 

Sio kila maumivu lazima umeze dawa, maumivu mengine yanakuja na kuondoka au yana sababu ambayo ukiitibu basi yanaisha.

 

Mfano, maumivu ya kichwa yanaweza kusababishwa na uchovu, macho au kukosa maji ya kutosha mwilini. Lakini pia yanaweza kusababishwa na matumizi ya vyakula au vinywaji fulani au kupanda kwa presha.

 

Dawa yake hapo sio vidonge bali ni kupumzika, au kuchunguza sababu na kuikwepa lakini sio kuendekeza matumizi ya dawa za maumivu.

 

“Siri ya Siku Tatu”

Hivi unajua kwamba dawa ya maumivu haipaswi kutumika zaidi ya siku tatu mfululizo? Ndio, haipaswi kuzidi na kama maumivu yako hayaondoki baada ya siku tatu, ni lazima upate ushauri wa daktari ili aangalie nini hasa chanzo cha tatizo.

 

Mara nyingi maumivu sugu huja kwasababu ya kutibu dalili na sio chanzo. Mfano, kichwa kinachosababishwa na macho dawa yake bora ni miwani na sio Panadol.

 

 

Kuna baadhi ya maumivu yanaletwa na shida za kisaikolojia hivyo hata umeze dawa vipi, bila kuonana na mwanasaikolojia ni kazi bure, maumivu hayataweza kuondoka!

 

Kuna namna mbalimbali za kutibu maumivu ya muda mrefu; njia hizi zinahusisha mazoezi ya viungo (Physiotherapy), dawa ya kuchua (sio lazima umeze), huduma za massage, na huduma zingine kama mazoezi na matumizi ya kukanda au kutumia maji ya moto.

 

Sio lazima umeze dawa kila unaposikia maumivu bali unapaswa kumeza pale tu maumivu yanapokuwa hayavumiliki.

 

Unataka kumuua panya kwa bastola?

Matumizi ya Antibiotics mara kwa mara nalo ni tatizo kubwa. Hili ni janga kwa sababu watu wana uhuru wa kwenda kununua dawa pharmacy bila kuhitaji maelekezo ya daktari.

 

Matokeo yake ni kutumia Antibiotics hata kwa matatizo ya kawaida lakini kibaya zaidi ni kutumia dawa zenye nguvu kuliko tatizo ulilonalo.

 

Matatizo kama ya kikohozi yanahitaji dawa ya kawaida tu isiyo na nguvu sana lakini kwasababu wewe unaona dawa yenye gharama kubwa ndio inatibu vizuri basi unaamua kuua sisimizi kwa nyundo. Hii inachangiwa zaidi na mtazamo wako kwenye dawa.

 

Madhara ya kutumia antibiotics hasa zenye nguvu kwa maradhi ya kawaida na bila ushauri wa daktari ni kwamba unaweza kupata usugu wa maradhi na hivyo kwa baadaye unashindwa kutibiwa na dawa za aina nyingi.

 

Kuna magonjwa utakuta mtu anatibu kwa miezi miwili akidhani ni UTI ya kawaida kumbe ni maradhi ya zinaa. Hivyo anameza antibiotics, ikishindikana anachoma sindano za wiki nzima, ikishindikana anaenda kununua dawa za bei ghali lakini wapi, na baadaye atakuja kutibiwa na dawa za kawaida.

 

Sababu kubwa ni kwamba tunakimbilia dawa badala ya kuonana na wataalam kwanza, jambo ambalo sio busara. Sio kila maumivu yoyote ya mkojo yanatibiwa na Antibiotics, inawezekana ukawa na tezi dume lakini hujui!

 

Kuliko kutumia laki kwenye duka la dawa, kwanini usilipe Elfu 10 ukapima kwanza, halafu elfu 15 ukanunua dawa iliyoshauriwa na daktari na ukapona mazima badala ya kubadili dawa kama mashati?

 

Punguza “Ujuaji”

Matumizi ya dawa kiholela, mara nyingi, ni kwasababu ya ujuaji na kukalili. Kwakuwa mwaka jana uliumwa tumbo, ukatibiwa na fragyl na ukapona, basi mwaka huu tumbo likikuuma tena unadhani fragyl itafanya kazi kumbe zamu hii huna Amiba, una vidonda vya tumbo.

 

Matokeo yake ni kubugia vidonge na kuchosha mwili halafu baadaye ukija kupima unaanzishiwa dawa nyingine ya wiki mbili, matokeo yake ni kuupa mwili wako dawa nyingi sana zisizo za lazma!

 

Kosa hapo ni kukariri matibabu. Na hiyo ni kwasababu ya ujuaji mwingi. Lakini pia inawezekana ikawa ni ubahili, yaani unataka upige shortcut ili upate dawa. Ulishagundua kwamba shortcut kwenye matibabu ni long-turn baadaye?

 

Utaanzia duka la dawa utatumia elfu 15 halafu, kwasababu ulipewa dawa tu bila kupima, usipopona utaambiwa umuone kwanza daktari; utakuja kutumia elfu 20 huku na baadaye utanunua dawa nyingine na kujikuta umetumia zaidi ya ulivyotarajia.

 

Unapomeza dawa, ini na figo zako huingia kazini. Kazi ya maini ni kuchakata dawa unazomeza, kuondoa sumu ya dawa. Figo kazi yake ni kutoa nje dawa inayobaki mwilini. Kadiri unavyomeza dawa nyingi, na mara kwa mara, huweza kuathiri maini na figo zako. Baadhi ya dawa ni mbaya zaidi ya zingine.

 

Hivyo kwasababu ya sumu nyingi kwenye ini hupelekea mwili kuwa na sumu nyingi na baadhi ya madhara inaweza kumfanya mtu kuzeeka haraka na pia figo kufeli.

 

Ndio maana ni muhimu kunywa maji ya kutosha pindi unapomeza dozi ya dawa kwa ajili ya kusaidia utolewaji wake mwilini na kusafisha Figo zako.

 

Jinsi ya kuondokana na matumizi mabaya ya dawa

1. Fahamu kwamba sio kila ugonjwa unahitaji dawa

Baadhi ya Magonjwa yanahitaji ushauri tu wa daktari, Mfano :kuacha chakula fulani, kubadili vinywaji au mafuta fulani, au kufanya zoezi husika.

 

Hakikisha unauliza mtaalamu kwanza kabla hujaamua kwenda duka la dawa kununua dawa.

 

Kumbuka: Ukienda duka la dawa, wale watu hamna siku watakushauri usinunue dawa, watapata tu dawa ya kukupa.

 

Mwaka 2012 nilipopata tatizo la kukohoa, mwanzoni sikumwambia yeyote. Nilienda kununua dawa za kikohozi duka la dawa na kumeza kwa siku tano bila mafanikio. Nikabadili dawa nyingine kwa siku tano, wapi.

 

Nilimeza Antibiotics nikataka kuzimaliza madukani lakini haikusaidia chochote. Mpaka baada ya miezi 6 nilipomshirikisha mjomba wangu, ambaye ni Daktari, na hapo ndipo akanifungua macho. Kumbe nilikuwa na Allergy bhana halafu sikujua.

 

Baada ya hapo ilinichukua siku tano tu kupona. Dawa yake ilikuwa ni kuacha kula tangawizi tu!

Hapa ndio niliona umuhimu wa kuwa na daktari binafsi.

 

 2. Kuwa na daktari binafsi

Ukiambiwa uwe na daktari binafsi basi unahisi kama ni jambo la ajabu sana au kubwa. Ni sawa kwa sababu huduma kama hizi kwa Africa zimechelewa ila bara la ulaya na mabara mengine ni jambo la kawaida.

 

Ukiwa na daktari binafsi au wa familia unaepuka mambo mengi sana. Kwanza utapunguza kwenda hospitali kiholela mpaka ushauriwe na daktari. Kumbuka kuna baadhi ya shida ukimuelezea daktari anakuwa kashajua shida yako ni nini na hivyo wewe utaenda moja kwa moja kununua dawa aliyokushauri na sio hospitali.

 

Mimi ni daktari wa magonjwa ya binadamu, kwakweli sikumbuki wanangu wameenda hospitali mara ya mwisho lini. Sio kwasababu hawaugui ila mara nyingi shida ndogo ndogo nazimaliza mwenyewe bila kuhitaji wao kwenda kupima. Hii inaniokoa sana na gharama zisizo za lazima.

 

Ndugu zangu pia wanapoumwa huwa hawaarakishi kwenda hospitali bali wananipigia simu na kunielezea matatizo yao. Mara nyingi ushauri ninaowapatia unawasaidia mambo mengi kama kupata huduma ya afya moja kwa moja bila kuzunguka huku na kule.

 

Pia kuondokana na hatari ya kununua dawa hovyo au kwenda kupima vipimo kiholela kwa tatizo ambalo lingeisha kwa ushauri wa kawaida tu.

Mama yangu akiwa na sherehe na kuna dawa kameza, na kama unavyojua sherehe inapendeza ukinywa ka – bia, basi atanitafuta WhatsApp na kuniuliza, “nilimaliza dozi ya fragyl jana, naweza kunywa ka – bia?”

Basi nitamwambia hapana mpaka walau masaa 48 yapite. Huwa anaumia lakini baada ya hapo atanambia asante mwanangu, najivunia kuwa na daktari kwenye familia.

Isingekuwa rahisi kunipata angefanyaje? Angeenda hospitali kupanga mstari kwa ajili ya kuuliza jambo dogo kama hilo? Na je, kwa kukosa mtu wa kumuuliza, akiamua kunywa tu hivyo hivyo halafu akaishia kulazwa hospitali, atatumia gharama kiasi gani?

 

Hii ndio faida kubwa ya kuwa na daktari binafsi, unaongeza usalama wa afya yako kwa kiwango kikubwa.

 

Hivi Unajua kwamba asilimia 50 ya watu wanaoenda hospitali huwa ni kwa ajili ya maradhi ambayo wanahitaji ushauri tu na sio lazima waende hospitali?

 

Lakini watafanyaje? Maana hawana daktari binafsi wa kuwashauri au kumuona mgonjwa wao na kuwaambia wafanye nini.

 

Matokeo yake wanajikuta wanatumia gharama na muda mwingi kushinda hospitali siku nzima na kuonwa na daktari kwa muda usiozidi dakika tano tu!

 

Utaipatia wapi huduma ya “daktari binafsi”?

Baada ya kufatilia kwa ukaribu, mimi na timu yangu kupitia taasisi yetu ya Abite Nyumbani tumeamua kuja na huduma ya kuhakikisha wewe binafsi una daktari au daktari wa familia yako.

 

Kwanza huduma hii sio kwa ajili ya matajiri, ni huduma ya mtu yeyote anayethamini afya yake. Kwa watu ambao wana ndugu daktari kwenye familia watakuwa na uzoefu huu. Ni raha sana kuwa na daktari wa kumuuliza, kumshirikisha, kuomba ushauri na kupata msaada mbalimbali kama wa kuandikiwa dawa fulani au kushauriwa wakamuone daktari gani.

 

Kwa asilimia 50, ukishakuwa na daktari binafsi utajikuta unaepuka kwenda hospitali mara kwa mara na utatunza muda wa kutosha wa kufanya shughuli zako nyingine kwa kupata matibabu ya kawaida kutoka kwa daktari wako.

 

Huduma hii ya daktari inahusisha pia, kwa familia, kupatiwa elimu ya afya ya pamoja kila mwezi mara moja kwa ajili ya kuhakikisha mnakuwa na ujuzi na taarifa muhimu hasa afya ya uzazi na mitindo ya maisha (lifestyles).

 

Utafiti unaonyesha watu wenye madaktari binafsi, rafiki daktari, mke au mume daktari huudhuria hospitali mara chache na kwa matatizo yaliyo juu ya uwezo kuliko watu wasio na bahati hiyo.

 

Mfano mzuri ni wakati mimi na mke wangu tumepata mtoto wa kwanza, miezi ya mwanzoni alikuwa analia sana usiku. Kila mara mke wangu alikuwa akitaka kumpeleka hospitali, mimi nilikuwa nakataa kwa sababu nilikuwa najua tatizo la kuumwa kwake na tumbo ilikuwa ni chango (colic pain).

 

Tatizo hili ni la kawaida na linatibika kwa Mama kunyonyesha mtoto vizuri na kuhakikisha havuti hewa ya nje na sio kukimbilia hospitali. Nisingekuwa Daktari bila shaka tungepoteza hela nyingi kama walio wengi wakiwa na watoto wadogo.

 

Wakati mwingine unahitaji tu kujua tatizo hasa ni nini na linatatuliwa vipi ndipo presha inashuka, hata kama ukiona mtoto analia basi unajua daktari wangu kashanishauri, unatuliza boli.

Sio kila wanaoenda hospitali wana matatizo makubwa, wengine ni kukosa ushauri wa daktari tu; kuwashauri wapi waende na nini wafanye.

 

Sasa unaona umuhimu wa kuwa na daktari binafsi? Usiishe tu kutamani, kwa maisha ya sasa na ubize wa maisha, ni muhimu kuwa na daktari binafsi. Kwa karne hii, hili ni hitaji la lazma kama ilivyo mavazi na chakula.

 

Ingia “hapa” dukani kwetu ujiunge na kifurushi chetu cha mwezi na baada ya hapo Abite Nyumbani tutakupa daktari wako binafsi, awe wa ugonjwa wowote, lishe, saikolojia au hata daktari wa kumuona mgonjwa wako nyumbani mara kwa mara.

 

Mwisho

Matumizi ya dawa kiholela sio tu ni hatari sana kwa afya yako bali huchangia sana kwenye upotevu wa pesa. Inawezekana ni kwasababu unakosa mtu wa karibu wa kukushauri nini ufanye.

 

Kataa kumeza dawa hovyo. Pata ushauri wa daktari kabla. Mcheki daktari wako, muulize hili na lile, mtumie vipimo vya Presha yako, sukari yako; pata sehemu ya kujidai na kuishi kwa uhakika.

 

Kula chakula kama dawa, usije kula dawa kama chakula.” – Hajulikani.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW