Je, Ni Lazima Kutumia Meno Bandia Ninapopoteza Meno?

Meno bandia – yaani dentures – ni zana unazoweza kutumia kama umepoteza (kung’oa) meno baadhi au yote katika kinywa chako.  Zana hizi hukusaidia kurejesha uwezo wako wa kutafuna au kung’ata, kuleta muonekano mzuri na kusaidia uso wako kutokusinyaa.

 

 

Zana hizi hutengenezwa kulingana na maumbile yako ya kinywa. Hivyo basi, huwezi kwenda duka la vifaa tiba au hospitalini ukanunua aina yoyote ya meno bandia na kuyavaa kwani hayatakutosha au yanaweza kusababisha maumivu. Meno bandia hutengenezwa kipekee kukutosha wewe tu.

 

Kwa matibabu hayo ni lazima kumtembelea daktari wa meno ambae hufanya uchunguzi wa kinywa na vipimo mbali mbali kukuandaa kwaajili ya kupata meno yako ya bandia kwaajili ya matumizi.

 

Ingawa mara nyingi unaweza ukahusisha meno ya bandia na uzee, ninaweza kukwambia kuwa si jambo la wazee peke yao. Watu wa umri tofauti wanaweza kuhitaji meno ya bandia aidha kutokana na majeraha, ajali au ukosekanaji wa meno kadhaa mdomoni kutokana na hali ya kuzaliwa ya mtu. Lakini kubwa zaidi ambalo linawapata watu wengi ni hali ya kung’oa meno kutokana na uozaji wa meno yao.

 

Wengine wengi, hata wewe labda, husema kuwa meno bandia hufanya meno kutokuonekana kuwa ya asilia na kuleta muonekano mbaya. Dhana hii ingekuwa kweli miaka 50 huko nyuma ila si kweli kwa sasa kwa sababu ya maendeleo ya hali ya juu katika vifaa tiba vya kinywa na meno.

 

Leo hii kuna zana zenye ubora zaidi ya hapo awali, hukufanya kuwa na muonekano mzuri na kuhisi kawaida tu kama meno yako ya asili.

 

 

Kama nilivyokwisha kusisitiza hapo awali kuwa meno haya ya bandia hutengenezwa kulingana na maumbile yako kinywani hivyo huundwa kwa kufatisha muonekano wa meno yako ya zamani.

 

Kwa mtu asiye na meno yote kinywani, mbali na vipimo ambavyo daktari atafanya ili kutambua ni aina gani ya meno au muundo wa meno upi utakufaa, ni vyema kuambatana na picha yako ya zamani ya kuonyesha meno yako yalivyokuwa mwanzo.

Hii ni aina mojawapo muhimu ya uchunguzi ambayo itamsaidia daktari wa kinywa na meno kuweza kufanya tathmini nzuri zaidi ya meno yako ya bandia.

 

Kama unavyojua kuwa hamna kitu kinachodumu milele, basi hata meno yako ya bandia utakayopewa na daktari wa kinywa na meno hayatadumu milele. Kulingana na aina gani ya meno bandia uliyonayo, muda wake wa kutumia hutofautiana kwa takribani miaka 5 mpaka 15.

 

Kwa kipindi chote hicho, mabadiliko makubwa hutokea kinywani hasa kwenye mfupa wa kwenye taya na kuchakaa na kupoteza ukali wa meno yako ya bandia.

 

Dalili za hali hii ni kama kuona meno hayo hayakutoshi tena, ukivaa yanavuka au yanakuletea muonekano mbaya. Hii itakulazimu kufanya marekebisho katika zana hiyo au wakati mwingine hupelekea kutengenezewa meno mengine ya bandia kulingana na mabadiliko yaliyokwishatokea kwa kipindi kilichopita.

 

Umuhimu wa meno ya bandia:

1. Kurejesha uwezo wako wa kutafuna

Unaweza kutumia meno haya ya bandia katika kutafuna chakula, kuongea, na hata kucheka. Unaweza ukawa unajiuliza kama meno haya yanaweza kung’ata mnofu wa nyama. Ndio yanaweza! Lakini nyama hiyo iwe laini na sio yenye kuhitaji nguvu nyingi. Huwezi kutumia meno haya kung’ata vitu vigumu kama miwa au kufungulia chupa ya soda.

 

2. Kuhifadhi muundo wa taya zako

Ukosefu wa meno kwenye taya husababisha mfupa wa taya kushuka na kulika kadri muda unavyozidi kwenda. Pia meno au jino la upande wa taya nyingine sambamba na lile lililotoka huwa na tabia ya kushuka zaidi (kama lipo taya ya juu) au kukua zaidi ya meno mengine kwenda juu (kama lipo taya ya chini).

 

Hali hii hupelekea kutokuwepo na uwiano sahihi wa meno mdomoni hivyo kusababisha majeraha katika joint ya meno na kufanya kusiwe kukutana vyema kwa meno mdomoni wakati wa kung’ata au kutafuna. Meno ya bandia husaidia kurekebisha haya yote.

 

3. Kuboresha namna yako ya kuongea

Kukosa meno mdomoni hasa kama huna meno yoyote kunaweza kusababisha shida ya kutamka maneno kadhaa na hivyo kukuletea shida katika kuwasiliana na wengine. Meno ya bandia hurejesha uwezo huo na kuongeza ujasiri wako wa mawasiliano kwenye jamii.

 

4. Huboresha muonekano wa uso na kuzuia uso kusinyaa

Meno yako ya asili hukusaidia kutabasamu lakini pia huchangia kwa kiasi kikubwa kushikilia misuli ya uso. Ikiwa umepoteza meno huwezi ukawa na muonekano mzuri wakati wa kutabasamu lakini pia uso wako husinyaa kwasababu nguzo za kushikia juu misuli huwa hazipo hivyo kukusababishia muonekano wa uzee.

 

5. Meno ya bandia husaidia kusapoti meno yaliyobaki mdomoni

Utumiaji wa meno ya bandia ya sehemu huwezesha meno yaliyobaki mdomoni kusogea katika nafasi za meno yasiyopo na hivyo kuhakikisha kuwa unang’ata vyema na kuzuia matatizo zaidi ya kinywa kama vile kuuma kwa joint za taya lako.

 

6. Hukuwezesha kujiamini na kuwa na ujasiri

Kinywa chako ni chanzo mojawapo kwa wewe kujiamini mbele za watu na jamii kwa ujumla. Kuwa na tabasamu zuri na uwezo wa kuwasiliana bila shida hukufanya kujiamini na kujiona mwenye mvuto zaidi. Hivyo meno ya bandia hukusaidia kuwa na kujiamini huku bila wasiwasi hata kama meno yako ya asili hayapo tena.

 

Aina za Meno Bandia:

Meno bandia Kamili (Complete dentures)

Meno haya hutumika ikiwa hauna meno yote mdomoni – yaani kibogoyo. Huweza kutumika kwa muda wa miaka 5 mpaka 10 bila kuhitaji marekebisho au kuhitaji meno mengine.

 

Meno bandia ya Sehemu (Partial denture)

Unaweza kutumia meno haya ikiwa huna baadhi ya meno mdomoni – aidha uliyapoteza kwa ajali, majeraha au katika kung’oa. Meno haya hukaa kwa miaka mpaka 15 bila kuhitaji marekebisho au kutengeneza aina nyingine.

 

Meno ya bandia ya Papo kwa Papo (Immediate denture)

Unapewa meno haya mara baada ya kung’oa jino au meno. Huandaliwa kwaajili yako kabla ya kung’oa jino au meno.

 

Meno ya bandia yaliyoshikiliwa na vyuma vya kupandikizwa (Implant-supported denture)

Meno haya hutengenezwa kukaa juu ya vifaa vya chuma ambavyo hupandikizwa ndani ya mfupa wa taya (dental implants) hivyo kusaidia kuongeza uimara wa meno hayo na kuimarisha utulivu wa meno mdomoni hata wakati wa kutumia.

Jinsi ya kutunza meno yako ya bandia

Hakikisha unayaondoa meno yako kinywani wakati wa kulala ili kupumzisha fizi zako. Yaweke meno hayo ndani ya glasi ya maji ili yawe katika hali ya unyevu unyevu wakati wote ili kuzuia uharibifu wa zana hiyo.

 

 

Unaweza kusafisha meno yako ya bandia na sabuni ya maji au maji safi peke yake pamoja na mswaki mlaini bila kutumia nguvu nyingi kuondoa uchafu wowote. Usitumie dawa ya meno katika kusafisha meno yako ya bandia.

 

Dawa ya meno huweza kusababisha zana yako kuwa na mikwaruzona kusababisha kuhifadhi uchafu wakati wa kutumia. Usitumie nguvu wala kitu kigumu kusugua meno yako ya bandia ili kuzuia mikwaruzo katika meno hayo.

 

 

Safisha na fizi zako kila baada ya kuvua kwa kupitisha kitambaa kisafi kilaini au mswaki mlaini kwenye fizi zako bila kutumia nguvu kubwa.

 

Iwapo meno yako yanakuumiza au yamekatika, mtembelee daktari wako wa kinywa na meno ili kurekebisha na kuyaboresha zaidi au kutengeneza meno mengine.

 

Kuna athari zozote za kuvaa meno bandia?

Kwakuwa zana hizi huwa ni kitu kipya kwenye mwili, ni kawaida wewe kuhisi utofauti mdomoni lakini pia kupata shida katika kuzoea kula au kuongea. Lakini mabadiliko haya ni ya muda mfupi na baadae utapata uzoefu zaidi katika kutumia meno yako ya bandia.

 

Wakati mwingine unaweza kupatwa na maumivu wakati wa kuvaa au kutumia meno ya bandia hivyo kukusababisha kutokuwa na utulivu. Ni vyema kuonana na daktari wako wa kinywa na meno na kumuelezea shida hii ili aweze kurekebisha.

 

Mmenyuko wa mzio (allergic reaction) huweza kutokea baada ya kuvaa meno yako ya bandia. Huenda ikawa ni hali ya muda mfupi kwani ni kitu kipya kinywani; kama ikiendelea ni vyema kuonana na daktari ili akubadilishie aina ya nyenzo aliyotumia kutengeneza meno yako ya bandia na kukuwekea itakayokubali mwili wako.

 

Mfupa wa taya zako pia unaweza kushuka na kulika kutokana na matumizi ya zana hii. Hivyo unatakiwa kumtembelea daktari wako wa meno ili kuhakikisha anafanya maboresho ya meno yako ili uweze kuendelea kuyatumia bila kuhisi kuwa yamelegea mdomoni.

 

Huweza kuhisi utengenezwaji wa mate mdomoni kuongezeka. Hii ni kawaida na ni hali ya muda mfupi na baadae hali hii huondoka na hurejea hali yako ya kawaida.

3 thoughts on “Je, Ni Lazima Kutumia Meno Bandia Ninapopoteza Meno?”

  1. Kennedy E. M DDS

    A very good way of presenting, congratulations.
    Do something for sensitivity, I’ve noted that many are complaining of teeth sensitivity, the etiology acquired from these complaining clients being consumption of sour or very sweet food stuff, teeth attrition, abrasions, erosion etc.

    1. Carolyn Mwasha, DDS

      Thank you for taking the time to go through the article and having offered such a great topic to consider. I will definitely consider it for my next articles

  2. Mimi nina shida meno yangu yana mianya na pia yameanza kulika pembeni karibu na taya. Solution ni nini….Kuna kipindi niliziba sehemu zinazolika lakini baadae Tena zile material zinabanduka. Mnapatikana wapi na hospitali yenu inaitwaje

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW