Hii ni kauli ambayo utaisikia sana miongoni mwa watu wengi. Uvivu wa kunywa maji ni jambo la kawaida kwa walio wengi.
Hali hii imekua mazoea kwa watu wengi, hasahasa maeneo ya mjini, na wengi wao wameshajitengenezea visingizio vyao kama sababu. Lakini kuna sababu za muhimu ambazo zinaweza zikamfanya mtu asinywe kiwango sahihi cha maji.
Mfano, ladha mbaya ya maji (kwa wale wasioweza kununua maji safi na salama – maeneo ya vijijini), kushindwa kuvuta maji nyumbani kwasababu ya kutofikiwa na DAWASCO, mawazo potofu kwamba ukinywa maji mengi unaweza kufanya damu yako kuwa nyepesi na kadhalika.
Maji ni sehemu muhimu sana mwilini mwako. Ndiyo hutengeneza asilimia 60 ya uzito wa mwanadamu. Uhitaji wa maji kwa masaa 24 ni kiasi cha lita 2.5 mpaka 3. Hiki ndio kiasi ambacho mwili hukiitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli zake za kawaida.
Kama unafanya shughuli za ziada kama mazoezi, lazima utahitaji maji mengi zaidi. Sasa jiulize, wewe kwa siku unakunywa maji kiasi gani?
Hasara za kutokunywa kiasi sahihi cha maji
Hakuna sababu yoyote inayoweza kusemwa ya kutetea kutokunywa maji, kwa sababu maji ndiyo malighafi ya kutengeneza kila kitu ndani ya mwili wako.
Upungufu wa maji uliopitiliza mwilini unaweza kukuletea matatizo ya kiafya kama:
- Figo zako kupunguza uwezo wa kufanya kazi.
- Moyo wako kuugua na kutanuka.
- Choo chako kuwa kigumu.
- Homoni zako kutokua na usawa unaohitajika kwa usahihi.
- Ngozi yako kunywea na kunyauka.
- Kutopata usingizi usiku.
- Mwili kushindwa kuondoa taka mwilini, na kadhalika.
Inawezekana haunywi maji lakini unakunywa sana vinwaji kama juice. Tatizo hapa ni kwamba, juice inaweza kuwa na maji lakini bado hayatoshi kukidhi mahitaji ya mwili.
Utafiti unaonesha sababu kubwa ya watu kutokunywa maji ni kutokua na hamu ya maji na kutoyapenda, sio kwamba wanasahau bahati mbaya. Mfano mzuri hapa ni Mama yangu. Yeye ni nadra sana kumuona akinywa maji, anasema hayapendi.
Wanawake walio wengi hawanywi maji ya kutosha, hivyo ngozi zao hunyauka na kupoteza uasili wake, ndio maana hupendelea kutumia vipodozi zaidi kutengeneza muonekano fake.
Wanaume wengi hunywa maji, na hivyo ngozi zao huwa asilia na kupunguza uhitaji wa vipodozi.
Jinsi ya kufanya zoezi la kunywa maji kuwa rahisi na jepesi
Hatua zifuatazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa:
1. Yafanye maji yako yawe na ladha
Moja ya njia kubwa ya kufanya hili ni kuyaboresha maji yako kwa kuongeza ndimu au limao. Ladha ya ndimu/limao hufanya maji kuwa matamu. Hukufanya kila mara utamani kumimina maji na kunywa.
Hapa unakuwa umeua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza unaongeza maji ya kutosha mwilini, pia limao ina kazi ya kupunguza hamu ya kula hivyo kuhusika katika kupunguza ulaji mwingi na kupelekea kupunguza kilo zako.
2. Tengeneza juice ya limao, weka kwenye chupa, itie kwenye fridge
Fuata ratiba kama hii ninayoifuata mimi. Asubuhi baada ya chai, mimina glasi moja ya maji halafu weka juice kiasi ya limao, changanya, kunywa maji.
Mchana baada ya chakula, kunywa tena glasi moja au mbili kulingana na uhitaji wako. Limao itafanya unywe hata glasi tatu kwasababu ya ukakasi wake. Fanya hivo tena jioni ukishatoka kazini au kabla na baada ya mazoezi.
Kale kamazoea ka limao katakusukuma kunywa maji mengi sana na baada ya muda utaanza kunywa maji mwenyewe bila kufikiria.
Nitatumia nini kama nina shida ya vidonda vya tumbo?
Kwa wale wenye madonda ya tumbo wanaweza kutonufaika na njia hii, au wakatakiwa kuweka limao kiasi kidogo zaidi. Ikishindikana basi unaweza kutumia juice kidogo ya matunda kumiminia au chungwa kwa ajili ya kuleta ladha.
Fanya hivyo na tatizo la kunywa maji halitakuwa lako tena na utakuwa miongoni mwa watu wanaojali afya zao.
Dalili zipi zitaonesha unakunywa maji ya kutosha?
- Kukojoa mara kwa mara – walau mara tatu mpaka nne kwa siku
- Mkojo wako kuwa mweupe na mwingi. (Kumbuka: Mkojo wa njano kali sio dalili ya UTI, ni dalili kwamba haunywi maji ya kutosha)
- Mwili wako kuwa na nguvu ya ziada.
- Choo yako kuwa laini.
- Ngozi yako huwa na rangi ya asili na inayongaa.
Dalili za mtu asiyekunywa maji ya kutosha
- Kukojoa mara chache, mkojo wa njano iliyokolea.
- Kupata choo kigumu.
- Kuumwa kichwa mara kwa mara.
- Mwili kuwa mchovu bila sababu.
- Kukosa usingizi wa kutosha usiku.
- Maradhi ya UTI ya mara kwa mara.
Kumbuka, mwili wako ili uweze kufanya kazi kwa ufasaha unahitaji maji ya ziada.
Ulishawahi kuona matunda yakisagwa kwenye Brenda bila maji? Jinsi Brenda inavyohangaika? Ndivyo mwili wako unavopata taabu usipokunywa maji ya kutosha!
Utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham Uingereza unasema, kwa tabia ya kunywa maji tu, unaweza kuondoa matatizo lukuki katika mwili bila hata ya kutumia dawa. Kiufupi maji ni dawa unayopaswa kunywa kila siku ya Mungu.
Ifanye kawaida kunywa maji kama sehemu ya chakula, sio tu kwa sababu una kiu. Kila ukipiga msosi, maji yasikose!
Wewe ni mnywaji pombe?
Acha nikuibie siri: Kabla hujapiga safari ya kwenda baa, piga glass ya maji. Hii husaidia kupunguza uhitaji wa pombe hasa pale tumbo linapokuwa na maji, hivo utajikuta unakunywa bia chache tu na unaridhika. Asubuhi pia ukiwa na hangover, weka limao kwa maji, piga glass. Utanishukuru!
Kama una maoni ya ziada au unataka kueleweshwa zaidi, usisite kutuandikia kwenye comments au kututafuta kupitia mawasiliano yetu.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Awesome