Fahamu Usichokijua Kuhusu Kansa ya Mdomo

Kansa ya kinywani ni aina ya ugonjwa wa kansa unaoweza kutokea katika sehemu yoyote ya mdomoni, ikiwa ni pamoja na kwenye lips, ulimi, ufizi, paa ya mdomo (palate), sakafu ya mdomoni (floor of the mouth) au sehemu ya ndani ya mashavu.

 

Kama magonjwa mengine ya kansa, kansa ya mdomo inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa haitagunduliwa na kutibiwa mapema.

 

Aina za Kansa ya Mdomo

Kuna aina mbalimbali za kansa ya mdomo, zinazoweza kujumuisha ifuatavyo:

1. Kansa ya Midomo (Lip Cancer): Inaweza kuathiri sehemu za nje za midomo.

 

Kansa ya Midomo (Lips Cancer)

 

2. Kansa ya Ulimi (Tongue Cancer): Inaweza kutokea kwenye sehemu ya juu au ya chini ya ulimi.

 

Kansa ya Ulimi (Tongue Cancer)

 

3. Kansa ya Ufizi (Gum Cancer): Inaweza kutokea kwenye sehemu ya gumu au tishu laini za kinywa.

 

4. Kansa ya paa ya mdomo (Palate Cancer): Inaweza kutokea kwenye sehemu ya ndani ya mashavu.

 

Kansa ya Paa ya Mdomo (palate cancer)

 

5. Kansa ya Tishu za Mdomo (Oral Mucosa Cancer): Inaweza kutokea kwenye utando laini wa ndani wa mdomo.

 

Kansa ya Tishu za Mdomo (Oral Mucosa Cancer)

 

6. Kansa ya sakafu ya mdomoni (Floor of the mouth cancer): Hii hutokea meaneo ya chini mdomoni mwako, baada ya ulimi.

 

Ishara na Dalili za Kansa ya Mdomo

Kuna dalili kadhaa za uwezekano wa kansa ya mdomo ambazo zinaweza kujitokeza, kama vile:

  • Kuvimba au uvimbe ambao hauishi au/na wenye kutoa damu
  • Maumivu ya kudumu au kutokwa na damu kwenye mdomo
  • Vidonda ambavyo haviponi vizuri au kwa muda mrefu (zaidi ya wiki mbili; hata baada ya kutumia dawa)

 

  • Maumivu ya koo au ugumu wa kumeza
  • Kupoteza uzito bila sababu za msingi

 

Hatua za Kuchukua Unapogundua Dalili za Kansa ya Mdomo

Ikiwa una dalili au ishara zozote za uwezekano wa kansa ya mdomo, ni muhimu kuchukua hatua za haraka zifuatazo:

1. Tembelea Daktari: Pata uchunguzi wa mara kwa mara na daktari wa meno au daktari wa upasuaji wa kinywa ili kufanyiwa uchunguzi wa kina.

 

2. Vipimo vya Kitaalam: Daktari anaweza kuamua kufanya vipimo kama biopsy (uchunguzi wa kipande cha tishu) ili kuthibitisha au kukanusha uwepo wa kansa.

 

3. Matibabu: Matibabu ya kansa ya mdomo yanaweza kujumuisha upasuaji, tiba ya mionzi (radiotherapy), na tiba ya kemikali (chemotherapy) kulingana na ukubwa na eneo la ugonjwa.

 

4. Usimamizi wa Baada ya Matibabu: Baada ya matibabu, mgonjwa anaweza kuhitaji huduma maalum ya kinywa ili kuhakikisha uponyaji mzuri na kudumisha afya ya mdomo, hasa lishe ya mgonjwa.

 

Vichochezi vya Hatari vya Kansa ya Mdomo

Kuna vichochezi kadhaa vya hatari vinavyoweza kuongeza uwezekano wa mtu kupata kansa ya mdomo, na kila moja ina njia yake ya kuchangia kwenye maendeleo ya ugonjwa huo. Hizi ni kama vile:

 

Matumizi ya Tumbaku

Matumizi ya tumbaku ni moja ya sababu kuu ya hatari ya kansa ya mdomo. Tumbaku ina kemikali nyingi zenye sumu ambazo zinaweza kusababisha madhara kwenye seli za mdomo na kusababisha mabadiliko ya kibiolojia ambayo yanaweza kusababisha kansa.

 

Miongoni mwa kemikali hizi ni nitrosamines ambazo zinaweza kusababisha DNA kuharibika na kuunda seli za kansa.

 

Vipengele vya tumbaku pia vinaweza kusababisha uchochezi wa muda mrefu kwenye tishu za mdomo ambayo inaweza kuchangia kwenye mabadiliko ya seli za kawaida kuwa za kansa.

 

Matumizi Mabaya ya Pombe

Matumizi mabaya ya pombe pia ni sababu ya hatari ya kuongeza uwezekano wa kansa ya mdomo. Pombe inaweza kusababisha uchochezi (irritation) na kuharibu seli za mdomo, ikisababisha mazingira yanayoweza kukuza ukuaji wa seli za kansa.

 

Aidha, pombe inaweza kusababisha kuharibika kwa DNA na kuathiri mfumo wa kinga ya mwili, ambayo inaweza kuathiri uwezo wa mwili kupambana na ukuaji wa seli za kansa.

 

Maambukizi ya HPV

Virusi vya Human Papillomavirus (HPV), hasa aina ya HPV-16, vimehusishwa na baadhi ya kesi za kansa ya mdomo. Kirusi hichi husambazwa kwa njia ya ngono na mwenzi aliye na kirusi hicho, ngono ya mdomo au ya kupitia sehemu za haja kubwa (anal sex).

 

 

HPV inaweza kuingia kwenye seli za mdomo na kusababisha mabadiliko ya kijenetiki ambayo yanaweza kusababisha ukuaji wa seli za kansa.

 

HPV inaweza kusababisha upungufu wa kazi ya protini za kuzuia kansa na kusababisha kuzaliana kwa seli zisizo za kawaida, ambayo inaweza kuongoza kwa maendeleo ya kansa.

 

Lishe Duni

Lishe duni yenye ukosefu wa matunda na mboga inaweza kuongeza hatari ya kansa ya mdomo kwa sababu ya upungufu wa chembechembe za kuzuia mabadiliko ya seli za kawaida, antioxidants na virutubisho vingine muhimu ambavyo vinaweza kusaidia katika kuzuia uharibifu wa seli na kudumisha afya ya seli za mdomo.

 

Lishe duni inaweza pia kuathiri mfumo wa kinga ya mwili na kufanya mwili uwe dhaifu katika kupambana na mabadiliko ya seli za kansa.

 

Mionzi kwenye Mdomo au Shingo

Mionzi ya muda mrefu kwenye mdomo au shingo, kama ile inayotumika katika matibabu ya kansa ya kichwa na shingo, inaweza kusababisha uharibifu wa DNA na kusababisha mabadiliko ya seli za mdomo ambayo yanaweza kusababisha kansa.

 

Mionzi inaweza kuchangia kwenye mchakato wa kuzaliana kwa seli za kansa na kusababisha ukuaji wa seli za kansa zisizo za kawaida.

 

Kila moja ya vichochezi hivi vya hatari ina njia yake ya kuchangia kwenye maendeleo ya kansa ya mdomo kupitia mabadiliko ya kibaolojia ambayo inaweza kusababisha ukuaji wa seli za kansa.

 

Matumaini na Huduma ya Kudumu

Matibabu ya kansa ya mdomo yanaweza kuwa na matokeo mazuri hasa ikiwa ugonjwa unagunduliwa na kutibiwa mapema.

 

Ni muhimu kwa wagonjwa kufuata maelekezo ya matibabu na kuhudhuria mikutano ya kliniki ili kuhakikisha tathmini ya mara kwa mara ya maendeleo yao na kusaidia katika usimamizi wa muda mrefu wa afya ya kinywa.

 

Kwa kuhitimisha, uelewa wa kansa ya mdomo ni muhimu katika kuchukua hatua za kuzuia, kama vile kuacha uvutaji wa sigara, kupunguza matumizi ya pombe, na kudumisha lishe bora.

 

Kwa kugundua mapema na kutibu kansa ya mdomo, inawezekana kuongeza nafasi za kupona na kuishi maisha marefu yenye afya.

 

Unaweza kupata ushauri wa kina wa afya yako ya mdomo kwa kupiga simu hapa na kuweka booking yako mapema.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW