Fahamu kiwango sahihi cha kunywa maji kwa siku

Maji ni kinywaji muhimu sana katika mwili; maji hufanya kazi kubwa sana ya kusaidia maswala mbalimbali katika mwili mfano mmeng’enyo wa chakula.

 

Kuna msemo mmoja wa kiingereza ninaopenda kuutumia ambao husema “Eat your water” (kwa kiswahili unaweza kusemwa “kula maji yako”) badala ya “drink your water” japo kwasababu maji ni mfumo wa kimiminika hivyo lugha inayotumika ni kunywewa.

 

 

Kupitia makala hii utaelewa ni muda gani unakua unakula maji yako .

 

Ukisikia kauli isemayo “eat your water” maana yake ni hamasa ya kutumia vyakula ili kupata maji. Vyakula hivi huwa katika kundi la mbogamboga na vingi huwa ni matunda.

 

Mfano wa vyakula vinavyoliwa ili kupata maji ni matikiti-maji, maembe, machungwa, mananasi, matango, nyanya, karoti, zabibu, na bila kusahau apples.

 

Je, ni kiasi gani cha maji unachopaswa kunywa kwa siku?

Kiashiria cha kwanza cha kwamba unapaswa kuwa unakunywa maji ni hali ya kusikia kiu. Kiu inatokana na upungufu wa maji mwilini lakini kama utajenga tabia ya kunywa maji kiu itakua inakuja yenyewe.

 

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kua kiu huwa inapungua kutokana na umri, watu wafikapo umri wa uzee huwa na hali ya kupungukiwa kwa kiu tofauti na utotoni na katika ujana.

 

Katika jamii zetu imezoeleka kwamba maji yanatakiwa kunywewa kwa wingi na mara nyingi watu husema unapswa kunywa maji lita 2, 3 mpaka 5 kwa siku.

 

Lakini kitengo cha lishe, Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani, kinasema kwamba wastani wa unywaji wa maji kwa mwanaume asiye na tatizo la kiafya ni vikombe 13; kwa upande wa mwanamke ni vikombe 9 ambapo kikombe kimoja kinakua na ounce nane ambazo ni sawa na mills 236.

 

Maana yake mwanaume anapaswa kunywa lita 3 za maji na kwa mwanamke ni lita 2 za maji kwa siku.

 

 

Jambo la kuzingatia

Mtu mwenye matatizo ya kiafya anapaswa kuwa na umakini katika unywaji wa maji hasa kama kuna tatizo la figo na kuna ukusanywaji wa maji mwilini ambapo kitaalamu tunaita fluid retention.

 

Unywaji wa maji kwa watu wa aina hii hutegemeana na kiasi cha maji kinachotoka mwilini kwa njia ya mkojo (urine output).

 

Ni muhimu kuwasiliana na wataalamu mbalimbali wa Afya ikiwemo maafisa lishe pindi ambapo una tatizo hili ili upate ushauri wa namna ya kula vyakula vyako na kunywa vimiminika mbalimbali vinavyoongeza kiwango cha maji mwilini.

 

Hii itakusaidia kuzuia madhara yatokanayo na kiwango kikubwa cha maji yaliyojikusanya mwilini ambapo mara nyingi huonekana kwa dalili ya mwili kuvimba katika maeneo mbalimbali ya mwili, au mwili mzima, hali inayojulikana kitaalamu kama oedema.

 

Mahitaji/faida za maji mwilini

Mahitaji au faida za maji mwilini hutegemea hali ya mwili, kwa mfano:

  1. Hali ya kuwa na homa hupandisha joto la mwili hasa pale unapokua unaumwa na kupoteza maji hivyo mwili huitaji maji kwa ajili ya kushusha joto.

 

  1. Umeng’enywaji wa chakula pia hutegemea maji kwa kiasi kikubwa kwani maji hurahisisha hali ya kuvunjwa vunjwa kwa chakula.

 

  1. Rangi ya mkojo pia ni mojawapo ya kiashiria kinachokuonyesha kiasi cha maji mwilini. Watu wengi huamini kwamba kwa sababu mkojo ni wa njano basi itakua ni magonjwa ya mfumo wa mkojo; kunaweza kuwa na usahihi katika hili lakini si kwa kila wakati. Rangi ya mkojo inapokua imekolea huashiria kuna upungufu wa maji katika mwili hivyo unapaswa kuongeza unywaji wa maji ili kuondoa rangi hii.

 

“Unywaji wa maji kupitiliza”

Katika hali ya kawaida ya kiafya, bila changamoto za kiafya, mwili wa binadamu huweza kutoa nje maji yaliyozidi kwa njia ya mkojo pale mtu anapokua amekunywa maji kwa usahihi ambayo ni kidogo kidogo na si kwa mara moja.

 

Makala iliyoandikwa na Chuo cha Harvard nchini Marekani imeongelea hasara inayoweza kutokea pindi mtu amekunywa maji yote yanayopaswa kunywewa kwa mara moja, ambapo imesema inaweza kusababisha hali ya upungufu wa madini chumvi mwilini, kwa jina la kitaalamu hyponatremia.

Hali hii ni kutokana na kulazimishwa kwa figo kufanya kazi kubwa sana kwa muda mfupi.

 

Hyponatremia huweza kuonekana kwa watu ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri na pia kwa wanamichezo ambao hunywa maji mengi sana. Madini chumvi haya pamoja na maji hupotea kwa njia ya jasho.

 

Hitimisho

Maji ni kinywaji kizuri sana cha burudani ambacho mtu anaweza kunywa na kisifanye aongezeke mwili kwani hakina sukari wala kalori kama vinywaji vingine vyenye sukari.

 

Kama umezoea kunywa vinywaji vyenye sukari unaweza kuona maji kama sio yenye ladha ya kuvutia hivyo nashauri kuongeza malimao katika maji au machungwa katika maji yako.

 

Wengine hupendelea strawberries au matunda ya kiwi ili waweze kupata ladha tofauti yenye ushawishi wa kunywa maji hayo.

 

Lakini pia unaweza kutafuta chupa yenye rangi ya kuvutia itakayoweza kukushawishi kunywa maji na sio kutumia vyombo vya kawaida.

 

Asante kwa kutenga muda wako kusoma makala hii. Ukitaka kuwasiliana nami, fanya booking yako mapema kupitia hii “link“.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW