Fahamu athari 4 za kung’oa meno yaliyoharibika

Kuna msemo maarufu kwenye jamii zetu usemao “dawa ya jino ni kung’oa!”. Hii dhana ambayo imeshikiliwa na watu wengi, inawezekana hata wewe pia umewahi kuiskia ikizingumzwa mahali.

 

Umekuwa sio msemo tu, watu wengi huutendea kazi. “Daktari, naomba ulitoe tu jino hili, linaniuma sana”, ni sentesi ambayo nakutana nayo mara kwa mara katika eneo langu la kazi.

 

Sikatai kuna meno huwa hayakwepeki kung’olewa kutokana na hali mbaya ya ubovu inayokuwa nayo, ila pia nakataa kuwa dawa ya kila jino ni kung’oa.

 

Ni vyema kumshirikisha daktari wako wa kinywa na meno ili kuangalia kama kuna uwezekeno wa kuokoa jino hilo.

 

Ziuatazo ni athari zitokanazo na kung’oa meno kutoka kwenye kinywa chako. Hizi athari huonekana ndani ya muda mfupi baada ya kung’oa jino.

 

Ni vyema kufahamu mambo haya ili isikushangaze baadae ukiona dalili za athari hizi, na ikusaidie kufahamu umuhimu wa kuhifadhi meno yako ili kuziepuka.

 

1. Kupungua kwa mfupa wa taya yako

Unapong’oa jino, mfupa wa taya yako unaouzunguka na kushikilia jino unaweza kusagika na kuisha; upotevu huu wa kiwango cha mfupa huwa ni wa polepole. Hii inaweza kusababisha kupungua kwa uwiano na kiasi cha mfupa kwenye taya – kwa muda.

 

2. Kusonga au kusogea kwa meno yanayopakana na lile ulilong’oa

Pengo lililoachwa na jino lililong’olewa linaweza kusababisha meno yanayopakana nalo kusonga (drift) au kuinama (tilt) na kuingia kwenye nafasi hiyo.

 

 

Hii hupelekea kuathirika kwa muundo wa kung’ata na afya ya jumla ya meno.

 

3. Mpangilio mbovu wa meno yanayobaki

Mpangilio mbaya wa meno hutokana na kusonga kwa meno kinywani mwako baada ya kung’oa yale yanayopakana nayo.

 

Hii huweza kuonekana pale ambapo meno ya juu na mwenzake wa chini hayakutani pamoja wakati wa kung’ata au kutafuna.

 

Hali hii ikiwepo kwa muda mrefu huweza kupelekea shida wakati wa kutafuna, kuongea na hata kupelekea matatizo katika jointi ya taya lako (TMJ Disorders).

 

Mabadiliko katika kung’ata na makutano ya meno yako (bite alignment and occlusion) hupelekea stress kujengeka katika joint ya taya zako.

 

Nitajuaje kama nina changamoto ya taya?

Dalili za kukujulisha hali hii ni kupata maumivu ya taya ya upande ambapo meno yameng’olewa, unasikia sauti ukiwa unafunga au kufungua mdomo.

 

 

Wengine husema wanasikia sauti zinatokea sikioni na hii ni kwasababu joint ya taya ipo karibu na sikio lako.

 

Dalili nyingine ni kichwa kinaweza kukuuma sana na hali ikiwa mbaya zaidi, mtu kushindwa kufungua au kufunga mdomo.

 

4. Kupungua kwa uzuri wa muonekano

Hasa pale mtu anapong’oa meno yanayoonekana. Mapengo pia huathiri kujiamini kwa mtu, kuogopa ukiwa mbele za watu au hata kupelekea msongo wa mawazo.

 

Muhimu…

Sio wote hupoteza meno yao kwa kung’oa, wengine huyapoteza hata katika ajali. Ni vyema kufanya utaratibu wa kuwekewa ya bandia au implants za meno ili kurejesha uhalisia wako na kujiamini zaidi.

 

Kama umeng’oa sana meno yako ya nyuma, hii huathiri katika kazi muhimu ya kutafuna. Inakuwa vigumu sana mtu kung’ata nyama na kufurahia vyakula mbalimbali kiujumla. Hivyo humpelekea mtu kuwa na mipaka ya vyakula anavyoweza kula.

 

Ni vyema, kama inakulazimu kung’oa meno yako, uzungumze kwa mapana na daktari wako wa kinywa na meno juu ya athari zitakazotokea baada ya muda mrefu kupita ili upate ushauri sawa, iwapo kuna matibabu utaweza pata ya ziada kuzuia athari hizi kutokea.

1 thought on “Fahamu athari 4 za kung’oa meno yaliyoharibika”

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW