Trigeminal Neuralgia: Maumivu Makali Zaidi ya Usoni

Ugonjwa wa trigeminal neuralgia ni moja kati ya tatizo la mshipa wa fahamu wa usoni unaojulikana kama “trigeminal nerve”.

 

Mishipa ya trigeminal ni seti mojawapo muhimu ya mishipa ya fuvu katika kichwa. Mishipa hii huusika na kutoa hisia usoni.

 

Mshipa mmoja wa trigeminal hukimbilia upande wa kulia wa kichwa, na mwingine unakimbilia kushoto.

 

 

Ugonjwa huu katika mishipa ya trigeminal husababisha maumivu makali sana kwenye uso. Maumivu kwa kawaida huhusisha uso wa chini na taya, ingawa wakati mwingine huathiri eneo karibu na pua na juu ya jicho.

 

Maumivu haya hupatikana katika eneo mojawapo katika upande mmoja wa uso au upande wote (kulia au kushoto), na siyo uso mzima.

 

Trigeminal neuralgia mara nyingi hutokea kwa watu wenye umri wa miaka zaidi ya 50, ingawa inaweza kutokea katika umri wowote.

 

Wanawake wanaonekana kuathirika zaidi kuliko wanaume.

 

Nini kinasababisha changamoto hii?

Trigeminal neuralgia husababishwa na shinikizo kwenye mshipa wa fahamu wa usoni, ambao ni moja kati ya mshipa mkuu kwenye uso.

 

Shinikizo hili linaweza kutokana na sababu mbalimbali kama vile msongamano wa mishipa ya damu karibu na hii trigeminal nerve au uvimbe unaoshinikiza mshipa huo wa fahamu.

 

Nitajuaje nina ugonjwa huu?

Dalili kuu ya ugonjwa huu ni maumivu makali kwenye sehemu za uso zinazosimamiwa na mshipa wa trigeminal.

 

Maumivu haya yanaweza kutokea kama mshtuko wa ghafla na mara nyingi, kama nilivyokwisha kusema awali, mtu huhisi maumivu haya upande mmoja tu wa uso.

 

Baadhi ya watu huielezea kama mshtuko wa shoti ya umeme au kuchomwa kwa moto katika eneo au upande wa uso na baadaye huwa maumivu makali mno.

 

 

Mara nyingi maumivu haya yanapotokea hukaa kwa sekunde zisizozidi 20. Baada ya maumivu haya kupita, mgonjwa hubaki na kutetemeka kwa uso (facial twitching).

 

Wagonjwa hutofautiana juu ya mara ngapi maumivu haya huja kwao. Mtu mwingine hupata maumivu haya chini ya mara mbili kwa siku lakini mwingine anaweza kuyapata kila baada ya lisaa ndani ya siku moja.

 

Mgonjwa wa “trigeminal neuralgia” hupata maumivu haya wakati anafanya kazi za kawaida tu za kila siku kama vile kunyoa ndevu, kupigwa na upepo upande huo wa uso, kupenga makamasi, kunywa kinywaji cha baridi au cha moto, kupiga muhayo, kuongea, kucheka, kushika upande huo wa uso – hata kama ni kidogo sana, akilalia upande huo, akipiga mswaki, kunawa uso, au hata pale mdada anapotaka kujipaka poda usoni.

 

Ugonjwa huu una tiba?

Maumivu haya hutokea kwa vipindi vya mzunguko. Mgonjwa anaweza akapata nyakati za kuumwa maumivu haya kwa muda mrefu halafu akakaa wiki, miezi au hata miaka bila kuingia katika kipindi kingine cha maumivu.

 

Ugonjwa huu hufanana kwa karibu sana na magonjwa mengine ya mishipa ya uso, hivyo hakuna njia kamili ya uchunguzi wa kuhakikisha kuwa mgonjwa anaumwa ugonjwa huu.

 

Zaidi sana daktari wako wa kinywa na meno huchukua historia yako na kusikiliza kwa makini dalili za maumivu haya. Mbali na hapo kipimo cha MRI husaidia kuchunguza zaidi kama ni shinikizo la mishipa ya damu ndiyo inasababisha au la.

 

Matibabu ya trigeminal neuralgia yanaweza kuwa utumiaji wa dawa au kwa wale wagonjwa ambao dawa hazisaidii kupunguza au kuondoa maumivu, upasuaji unaweza kufanyika, kama tatizo limeletwa na shinikizo la mishipa ya damu au uvimbe karibu na mshipa wako wa trigeminal.

#!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=11#!trpen#Leave a Comment#!trpst#/trp-gettext#!trpen#

#!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=723#!trpen#Your email address will not be published.#!trpst#/trp-gettext#!trpen# #!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=715#!trpen#Required fields are marked *#!trpst#/trp-gettext#!trpen#

en_USEN