Kipindi nikiwa mtoto nakumbuka kusistizwa kunywa kijiko cha mafuta ya Samaki, Mama yangu alisisitiza kuwa ni mazuri sana kwa afya.
Leo nimekumbuka kipindi hicho na baada ya kusoma masomo yangu ya shahada ya lishe nikagundua faida zilizomo katika mafuta ya samaki.
Mafuta ya samaki yana tofauti gani na mafuta ya kawaida?
Wengi wetu tukisikia mafuta ya samaki lazma swali hili liingie akilini.
Utofauti wa mafuta ya samaki na mafuta mengine ya kupikia upo katika uwepo wa asidi ya mafuta ya omega 3 ambapo katika samaki omega 3 iko kwa wingi na wakati katika mafuta mengine ya kawaida, tuliozoea kupikia, huwa na kiwango kikubwa cha mafuta yanayoganda yanayofahamika kama saturated fats.
Mafuta haya yanayoganda, kupitia tafiti mbalimbali, yameendelea kuhusishwa na athari mbaya katika mfumo wa usukumwaji wa damu pamoja na moyo wa mwanadamu.
Binafsi huwa napenda kuwaambia wateja wangu kama mafuta yako yakiwa katika hali ya kawaida huwa na uzito na hali ya kuganda basi hata katika mwili hali inakua vivyo hivyo.
Je! mafuta ya samaki yana tofauti gani na mafuta ya wanyama wengine kama Nguruwe, Mbuzi, au Ng’ombe?
Jibu ni kwamba pamoja na kwamba vyote hivi ni vyakula katika kundi moja na kutupa kirutubishi cha utomwili, protein, lakini kwa upande wa aina ya mafuta kuna utofauti.
Mafuta ya samaki hayana asili ya kuganda kama mengine, huyeyuka kwa urahisi katika mwili na huwa na asidi ya mafuta muhimu ya Omega 3 ambayo hayapatikani katika mafuta ya wanyama wengine kama nguruwe, mbuzi na ng’ombe.
Mafuta ya Samaki yanatoka wapi?
Mafuta ya Samaki yanatoka katika Samaki wenye mafuta maarufu kwa jina la Fatty fish. Mifano ya Samaki hawa ni Sato, Sangara, Vibua, Dagaa pamoja na Samaki Jodari.
Mafuta ya samaki yanaweza kupatikana na kulika katika “njia” gani?
Mafuta ya samaki hupatikana katika samaki wanaovuliwa baharini na ziwani na huliwa pale ambapo utakua umemuandaa samaki wako kwa kutumia njia ambazo husaidia asipoteze virutubishi.
Njia zinazopendekezwa kusaidia samaki wako asipoteze virutubishi ni kutumia mvuke, kuoka, au kuchemsha.
Ukikaanga samaki katika mafuta makali husababisha upungufu wa virutubishi na upotevu wa asidi hii ya mafuta ya omega 3 ambayo wengi wetu huita kwa jina la mafuta ya samaki.
Kuna Faida Zozote za Kutumia Mafuta ya Samaki
Mafuta ya Samaki yana faida zifuatazo:
1. Kuimarisha hali ya kumbukumbu ya binadamu
Asidi ya mafuta ya Samaki husaidia katika kuimarisha na kusaidia uwepo wa kumbukumbu nzuri na kuepusha hali ya kusahau.
2. Kuimarisha afya ya mfumo wa damu na moyo
Matumizi ya mafuta ya samaki au samaki wenye mafuta husaidia katika kuzuia ugandaji wa damu na hivyo kuhakikisha hali ya damu kutembea bila vikwazo katika mfumo wake wa kawaida.
Hii ni muhimu kwasababu damu inapoganda na kutengeneza “clots” huweza kupelekea matatizo mengi ya kiafya ikiwemo kupooza.
3. Husaidia katika ukuaji wa ubongo kwa watoto
Watoto hukua kila siku kimwili na kiakili hivyo basi mafuta haya ya samaki husaidia katika ukuaji wa ubongo.
Tafiti moja ilifanyika nchini Ureno na kuangalia mabadiliko mbalimbali ya ukuaji wa watoto; watoto wenye miaka minne walipewa mafuta ya samaki kwa muda wa miezi minne na walionekana kuongeza hali ya kusikiliza kwa makini na ufikiri wao uliongezeka.
Waliweza kudadavua maswali vizuri katika mitihani midogo waliopewa.
4. Husaidia katika uoni
Faida nyingine ambayo imeonekana katika tafiti ya nchini Poland ni kwamba mafuta ya samaki husaidia katika kuimarisha uonaji, na hii ni kwa sababu husaidia kutengeneza eneo la retina ambalo ni muhimu katika kuona.
Ukosefu wa mafuta haya huweza kupelekea upungufu wa uimara katika uoni (kufifia kwa macho) kwani yanafanya kazi kubwa katika kuimarisha afya ya macho.
ZINGATIA:
Njia ya rahisi ya kupata mafuta haya ya samaki ni kutoka kwa samaki wenyewe ambapo sokoni hupatikana kwa bei nzuri kuliko kununua dawa za nyongeza.
Kumbuka kwamba samaki wanaweza kupikwa kwa njia ya kuchemsha, mvuke au kuoka ili kuhakikisha wewe pamoja na familia yako mnapata virutubishi vyote.

Providing nutrition education and counselling in Tanzanian local communities, currently in Mkuranga – Pwani region. My goal is to raise awareness on how to improve our health through nutrition – in all human life stages.