Swala la ulaji wa nyama nyekundu ni swala ambalo katika jamii nyingi huwa na maana ya uthamani. Nikisema uthaman namaanisha ni swala linalofurahiwa na watu.
Mfano wa nyama nyekundu ni nyama ya ng’ombe na mbuzi; chakula ambacho mara nyingi hutumika katika sherehe za hapa na pale.
Ulaji wa nyama huashiria furaha, pongezi, ushindi, na kadhalika. Siku za sikukuu bucha za nyama hupata mauzo makubwa kwa sababu watu wengi hupendelea kutumia nyama ili waweze kufurahia na familia zao.
Kuna misemo unaweza kukutana nayo mtaani mfano, “ Leo sikukuu tunakula nyama”. Unaweza kusikia watu wengi wakisema haya mtaani kwako hasa vipindi vya sikukuu hivyo kuashiria nyama ni chakula muhimu sana kwenye siku yoyote maalum katika jamii.
Hivyo sababu kubwa iliyonifanya niandike makala hii ni kukupa mwanga wa ufahamu wa lishe unaohusu chakula cha nyama katika mwili wako ili muda ujao ukila nyama ujue nini kitatokea. Soma hadi mwisho, utajifunza kitu.
Kwanini watu wengi wana hofu kuhusiana na ulaji wa nyama nyekundu?
Tabasamu hili la furaha linalosababishwa na historia ya vipindi vya ulaji wa nyama huingia dosari pale tu mlaji wa nyama anaponiuliza: Je, naruhusiwa kula nyama? Ni salama kula nyama?
Hii ni kutokana na sababu na changamoto za kiafya mbalimbali zinazoendelea katika jamii zetu kama vile magonjwa yasiyoambukiza mfano, ugonjwa wa moyo, shida za joints, na kadhalika.
Maswali haya ya ulaji wa nyama huulizwa sana na watu wenye changamoto mbalimbali za kiafya kama za magonjwa ya moyo zinazopelekea kupata matatizo ya kiafya na kupewa taarifa ya kupunguza au kuacha chakula hichi cha nyama ambacho kinafurahiwa sana na wengi katika jamii zetu.
Shirika la Afya Duniani (WHO, 2023) lilitoa chapisho lililoeleza kwa kina kuhusiana na nyama nyekundu na kutoa faida zake ambapo lilieleza nanma nyama nyekundu inajulikana kwa upatikanaji wake wa virutubishi hasa vya Madini chuma pamoja na Vitamini B12.
Madini Chuma husaidia sana katika ongezeko la damu mwilini na ubebaji wa gesi ya oxygen katika mwili wa binadamu kwa ajili ya matumizi ya kuupa uhai.
Vitamin B12 yenyewe ni kirutubishi muhimu sana katika utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu za binadamu yaani red blood cells pamoja na mchakato wa utengenezwaji wa vinasaba (DNA synthesis) ambazo kazi yake kubwa ni katika ukuaji wa ubongo na mfumo wa neva wa mawasiliano katika mwili.
Hata hivyo chapisho hili la Shirika la Afya duniani liliendelea kuongelea jinsi nyama nyekundu imekua ni nyama yenye kiwango kikubwa cha mafuta yanayoganda na hivyo basi tunapaswa kutumia chakula hichi kwa kiasi.
Je, ni kiasi gani salama kutumia kwa nyama nyekundu?
Kiasi cha nyama nyekundu ambacho kimependekezwa kuliwa, kutokana na tafiti mbalimbali pamoja na wataalamu mbalimbali ni gramu 98 kwa wiki na kisizidi gramu 500 kwa wiki.
Kwa lugha rahisi hupaswi kula nyama nyekundu zaidi ya nusu kilo kwa kipindi cha wiki nzima!
Hivyo basi unapoenda katika sehemu mbalimbali za migahawa na kuagiza nyama, kumbuka kiwango hichi cha wiki ili kuepukana na magonjwa yasioambukiza kama vile magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu, kiharusi, kisukari, na kadhalika.
Mwisho
Kwa kumalizia ningependa kukwambia kwamba kuna vyakula mbalimbali ambavyo pia ni mbadala wa nyama nyekundu kama vile samaki na kuku ambao kwa sasa, baada ya elimu hii ya nyama nyekundu kuongezeka, nyama ya kuku imeonekana kutumika zaidi na kufikia ongezeko la asilimia 81 ya nyama zinazoliwa – kama ilivyotajwa katika chapisho la mwaka 2023 la Shirika la Afya Duniani.

Providing nutrition education and counselling in Tanzanian local communities, currently in Mkuranga – Pwani region. My goal is to raise awareness on how to improve our health through nutrition – in all human life stages.
