Fahamu vyakula bora kwa afya njema ya uzazi

Afya ya uzazi ni swala ambalo limekua likigusa watanzania wengi na katika kufanya kazi kwenye  maeneo ya hospitali ni swala ambalo nimekutana nalo mara kwa mara.

 

 

Katika jamii zetu, changamoto za uzazi zimekua zikiongezeka kila siku na kwa kasi kubwa; watu wengi wanahangaika kutafuta suluhisho za aina mbalimbali bila mafanikio. Hii ndio sababu kubwa iliyonifanya niandikie Makala hii.

 

Afya ya uzazi ina maana gani?

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea maana ya Afya ya Uzazi kama….

Hali ya ustawi kamili wa kimwili, kiakili na kijamii na si tu kutokuwepo kwa ugonjwa au udhaifu, katika masuala yote yanayohusiana na mfumo wa uzazi na kazi na taratibu zake. Afya ya uzazi ina maana kwamba watu wanaweza kuwa na maisha ya ngono ya kuridhisha na salama na kwamba wana uwezo wa kuzaliana na uhuru wa kuamua kama, lini na mara ngapi watafanya hivyo.”

Katika makala hii nitaongelea zaidi maswala ya ustawi wa Afya ya uzazi yanayohusiana na lishe bora.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya maswala ya afya bora ya uzazi na lishe na hii inahusisha jinsia zote mbili, nikimaanisha maswala ya lishe hayahusiani tu na kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume lakini pia yanahusiana na kuimarisha afya ya uzazi kwa wanawake pia.

 

Kwanza kabisa swala la muhimu  linalopaswa kuzingatiwa  kuhusiana na lishe kwa afya bora ya uzazi ni  kwamba inabidi tutumie vyakula kutoka makundi yote ya vyakula ili tuweze kuwa na afya nzuri ya uzazi.

 

Kutumia vyakula katika makundi yote ya vyakula itatusaidia kuupatia mwili virutubisho vyote kwa ajili ya kuleta uimara katika afya ya uzazi hasa kwa kuzalisha mayai yaliyo na ubora na mbegu za kiume zilizo bora.

 

Kupitia makala hii utajifunza namna ambavyo vyakula mbalimbali na virutubishi vinaweza kukusaidia katika kuimarisha afya yako ya uzazi.

 

Uhusiano wa lishe bora na afya bora ya uzazi

Lishe bora inachukua nafasi kubwa katika ukuaji na uimarishaji wa mifumo ya uzazi kwa binadamu. Virutubishi ambavyo vinapelekea ukuaji na uimarishwaji wa mifumo ya uzazi ni kama vile madini chuma, foliki asidi, kalsium, selenium, protini pamoja na zinki.

 

Virutubishi hivi ni muhimu na vyenye kipaumbele kikubwa katika kusaidia ukuaji na uimarishwaji wa via vya uzazi kwa mwanamke na mwanaume.

 

Swali linalokuja ni kwamba:

Ni vyakula gani hasa vinakua na virutubishi tajwa hapo juu?

 

1. Vyakula vyenye kirutubishi cha PROTINI kama vile samaki, dagaa, nyama, mayai, maziwa; na vyakula vya protini vyenye jamii ya mikunde kunde kama vile maharage, njugu , choroko na njegere.

 

2. Vyakula vyenye kirutubishi cha madini aina ya ZINC ambavyo husaidia katika kupevusha mayai na kusaidia katika kuleta usawa katika vichocheo mbalimbali vya uzazi mwilini ambavyo hujulikana kama balance hormone kwa kugha ya kiingereza.

 

Mfano wa vyakula hivi ni nyama ya ngombe, nyama ya mwana-kondoo (lamb), mbegu za ufuta, mbegu za boga, dengu, pweza, samaki gamba ambao hujulikana kama shellfish, kuku, pamoja na chaza ambao makala na tafiti nyingi huonyesha kuwa na kiwango kikubwa zaidi cha madini ya zinc.

 

3. Vyakula vyenye kirutubishi cha SELINIAMU (selenium) ambacho husaidia sana katika uumbwaji wa mbegu za kiume.

 

Mifano ya vyakula vyenye kirutubishi hiki ni samaki, nyama ya bata mzinga, nyama ya kuku, pamoja na mayai.

 

4. Vyakula vyenye kirutubishi cha OMEGA-3 ambacho husaidia katika kuimarisha afya ya kizazi kwa wanawake. Vyakula hivi ni kama vile mbegu za chia, jozi (walnuts), dagaa, samaki wenye mafuta – mfano, sangara au sato.

 

5. Vyakula vyenye VITAMIN E.

Vyakula hivi husaidia katika kuimarisha afya ya mbegu za kium. Mifano yake ni parachichi, mbegu za alizeti, broccoli, kale, spinachi, pamoja na lozi.

 

6. Vyakula vyenye VITAMIN C.

Hasa kwa wanaume husaidia katika kuongeza ubora wa mbegu za kiume pamoja na wingi katika ujazo wa mbegu.

 

Vyakula hivi ni kama vile papai, pilipili hoho, broccoli, strawberry, nanasi, koliflower, kabichi, mboga ya majani aina ya chainizi.

 

7. Vyakula vyenye virutubisho aina ya L-argenine ambavyo ni virutubisho muhimu vya amino acid ambazo ni aina ya protini muhimu kwa kujenga mwili. Katika afya ya uzazi husaidia katika kuongeza mzunguko wa damu.

 

Kirutubishi hichi humsaidia mwanaume kuwa na nguvu za kutosha wakati wa kujamiiana. Vyakula vinavyosaidia kupata kirutubishi hichi ni nyama ya ngombe, samaki, soya, maharage, maziwa, mbaazi pamoja na nyama ya kuku.

 

8. Vyakula vingine ni vyenye kirutubishi cha carnitine ambacho ni aina ya amino acid. Amino acid ni matokeo ya mwisho ambayo hutokea baada ya protini kumeng’enywa katika tumbo la binaadamu.

 

Kupitia mchakato huu mzima wa umeng’enywaji wa chakula hichi, ndipo tunapata kirutubishi aina ya carnitine ambacho husaidia katika kuongeza vichocheo vya kiume vinavyojulikana kama testosterone pamoja na kuimarisha spidi ya mbegu za kiume zinapokua zinakimbia kukutana na yai la mwanamke kwa ajili ya kupevushwa pamoja na afya ya mbegu ya kiume kwa ujumla.

 

Vyakula vyenye kirutubishi hichi cha cartinine ni nyama ya ngombe, samaki aina ya chewa, nyama ya kuku, parachichi, n.k.

 

Muhimu

  • Virutubishi hivi hufyonzwa vizuri vinapokutana na tumbo lisilo na vyakula.
  • Huweza kufyonzwa vizuri wakati wa kulala ambapo ukuaji hutokea kwa asilimia kubwa kwani virutubishi hivi huwekezwa katika ukuaji.

 

#!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=11#!trpen#Leave a Comment#!trpst#/trp-gettext#!trpen#

#!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=723#!trpen#Your email address will not be published.#!trpst#/trp-gettext#!trpen# #!trpst#trp-gettext data-trpgettextoriginal=715#!trpen#Required fields are marked *#!trpst#/trp-gettext#!trpen#

en_USEN