Dalili Tatu za Hatari Kwenye Kipindi cha Ujauzito

Kubeba mimba na kuzaa mtoto ni tamanio la kila mwanamke japo huwa ni safari yenye changamoto mbalimbali. Maombi yangu kwako ewe mama mjamzito Mungu akutangulie ujifungue salama. Unapojifungua salama, safari isiiishie hapo bali endelea kuwaombea na wamama wengine nao wajifungue salama.

 

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za afya, imejitahidi sana kupunguza vifo vya wajawazito kwa kuongeza miundombinu thabiti na kuongeza utoaji elimu kwa jamii.

 

Katika yake ya tarehe 10 July 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dk. Jessica Leba alielezea kupungua kwa vifo vya kina mama wajawazito kutoka 112 mwaka 2020 mpaka 26 mwaka 2024. Hii ni kutokana na miundombinu kuboreshwa na vitendea kazi kuongezwa na serikali pamoja na WHO.

 

Pamoja na hayo, bado haiondoi ukweli kwamba elimu ya afya ya ujauzito bado inapaswa kuongezwa zaidi kwani itakuwa mkombozi wa jamii.

 

Wewe ni mjamzito au unatarajia kubeba mimba siku za usoni?
Mimba ina dalili nyingi ambazo nyingi ni za kawaida kutokana na mabadiliko ya vichocheo vya mwili mfano kichefuchefu, kizunguzungu, kukojoa mara kwa mara, kuwa na hasira, kukosa hamu ya vyakula fulani na kadhalika.

 


Dalili hizo ni za kawaida na huwa mama anashauriwa kutulia nyumbani, kujitazamia pamoja na kuhudhuria kliniki kila mwezi. Lakini kuna baadhi ya dalili ukiziona kwenye mimba basi tambua ni za hatari na zinapaswa kupewa nafasi ya kuonwa na watu wa afya.

 

Muhimu: Kabla sijakupa dalili za hatari za mimba basi nikutaadharishe tu kwamba mimba haina mazoea! Inawezekana mimba iliyopita uliumwa tumbo au kutokwa na damu na bado ulijifungua salama, lakini mimba hii mpya dalili hizo hizo zinaweza kuashiria kitu cha tofauti kabisa. Hivyo kukariri kunaweza kukuingiza kwenye mtego mkubwa.

 

Mwandishi maarufu wa vitabu nchini Marekani (Robert Greene) katika kitabu chake cha 48 Laws of Power anasisitiza kwamba “Never fight the last battle”; kwakuwa mimba iliyopita haikuwa na shida haimaanishi na mimba mpya njia ile ile itafanikiwa! Kila ujauzito uangaliwe kwa umakini zaidi.

 

Hizi ni dalili 3 ambazo ukiziona basi sio za kuchukulia kawaida:

 

1. Kutokwa na damu wakati wa ujauzito

Hali hii bahati nzuri huwa inatisha hivyo wengi hukimbilia mapema hospitali kujua nini kinaendelea. Lakini bado kuna wale wamama ambao hukaa nyumbani na kusubiri mpaka kesho waone kama hali itabadilika.

 

Kutokwa na damu wakati una mimba sio jambo la kawaida na linahitji kuangaliwa ili kuhakikisha halina madhara. Hali hii hutegemea muda wa mimba na huwa ni dalili ya mambo mbalimbali kwenye mimba.

 

Zinazofuata ni baadhi ya sababu kwanini damu hutoka katika kipindi fulani cha mimba:

 

I. Kuanzia wiki 2 mpaka miezi mitatu
Hii mara nyingi huashiria sababu mbalimbali ambazo huweza kuwa dalili ya mimba kutishia kutoka (threatened miscarriage) au kutoka kabisa (miscarriage). Utokaji wa damu katika muda huu unaweza kuwa damu za matone (spotting), damu ya wastani au damu nyingi yenye mabonge.

 

Mimba kutaka kutoka au kutoka kabisa katika miezi mitatu ya mimba huweza kusababishwa na mambo mbalimbali kama mimba kutokuwa na viini viwili vya yai la baba na mama (blighted ovum), mimba kuumbika vibaya (yaani vinasaba vya mayai mawili kutengeneza kiumbe ambacho hakiko kamili), vinasaba vya wazazi wawili kutorandana au kuelewana vizuri (ABO incompatibility) mfano Baba ni blood group negative wakati mama ni positive (nitaelezea zaidi kwenye makala zijazo), pamoja na mimba kutunga nje ya kizazi.

 

Sababu zingine zaweza kuwa mlango wa uzazi wa mama kutokuwa imara kushikilia mimba hivyo mimba ikianza kuwa kubwa mlango hufunguka na kufanya itoke, matumizi ya dawa zisizofaa kwa mimba, utoaji wa makusudi wa mimba, kupigwa na kitu kizito au ajali, kupata maumivu ya kihisia mfano kufiwa na mpendwa au taarifa za kushtua sana.

 

Sababu zote hizi huweza kusababisha damu kutoka wakati wa mimba na unapoona damu inatoka haijalishi ni ndogo au nyingi kiasi gani, we nenda kliniki au hospitali ili wataalam wakabainishe sababu na kukusaidia.

 

Shida kubwa huwa ni kuchelewa hospitali na hivyo kama ni mimba ambayo ingesaidiwa kubaki unafika imeshatoka au umepoteza damu nyingi.

 

Usichukulie poa damu inapotoka wakati una mimba, wahi hospitali mapema kwa ajili ya kujua sababu na kupata msaada wa kuzuia changamoto kubwa zaidi.

 

II. Kuanzia miezi 3 na kuendelea
Miezi mitatu na kuendelea damu huweza kutoka kwa sababu maalum pia ikiwemo mimba kutunga sehemu ya chini ya kizazi (placenta previa) hivyo kadiri mimba inavyokuwa, kuna namna mishipa ya damu eneo hili itapasuka na kusababisha kuvuja damu.

 

Mjamzito anaweza kuamka usiku akajikuta yuko kwenye dimbwi la damu nyingi. Bahati nzuri huwa haina matokeo mabaya ukiwahi hospitali. Hali hii hujitokeza hasa katika wiki ya 30 mpaka 34 ya mimba.

 

Hii ni dalili ya hatari na inapaswa kuonwa hospitali mara moja. Hali hii huja bila maumivu yoyote, jambo ambalo linaweza kukupumbaza na kuhisi ni hali ya kawaida kumbe ni majanga.

 

Sababu nyingine zinaweza kuwa kubeba mimba katika umri mkubwa, ajali (kuanguka au kupigwa), mfuko wa mtoto (kondo) kuachia kutoka kwenye mfuko wa uzazi, abruptio placenta, na hii hupelekea kutoka damu na maumivu makali ya tumbo hasa kuanzia wiki ya 36 na kuendelea na matokeo yake kwa mtoto huwa sio mazuri. Dalili kama hii huweza kuwa na damu kidogo tu lakini maumivu makali yakupe uharaka wa kuwahi hospitali.

 

2. Maumivu ya tumbo

Wakati wa ujauzito maumivu ya tumbo huja na kuondoka. Mengi huwa ni kawaida kutokana na mimba inapokuwa inakua na kila hatua ya mimba yaweza kuwa na maumivu ya aina yake.

 

Mfano, mimba ikiwa inatoka wiki ya 12 kwenda juu mama anaweza kusikia maumivu ya tumbo. Inapofika wiki ya 24 kwenda 30 mtoto anapokuwa anajigeuza, mama atasikia maumivu kutokana na position ya kichwa au miguu ya mtoto.

 

Lakini, kuna maumivu ya tumbo ambayo yanaambatana na hatari kwenye mimba na hayo hayapaswi kuchukuliwa poa. Yafuatayo ni baadhi:

 

I. Maumivu yanayoambatana na kutoka damu
Maumivu hayo yanaweza kuwa kwasababu ya mimba kutaka kutoka (miscarriage), mimba kutunga nje ya uzazi (ectopic pregnancy), mimba kutunga sehemu ya chini ya kizazi (placenta previa), sehemu ya mfuko wa mtoto (placenta) kujiondia kutoka kwenye kizazi (abruptio).

 

Mama mjamzito hapaswi kufikiria mara mbili anapokuwa na maumivu yoyote ya tumbo yanayoambatana na damu kutoka. Kinachopaswa kufata ni kutafuta huduma ya afya mara moja. Kama ni kitu cha kawaida basi utaelezwa huko huko hospitali. Au kama una daktari wako binafsi ni wakati sahihi wa kumpigia na kupata maoni yake.

 

Unahitaji daktari binafsi? Tupigie kwenye simu namba +255-767-226-702 au tembelea tovuti yetu kuona huduma za daktari binafsi ambaye atakusaidia kukupa mwongozo kutoka mwanzo mpaka mwisho wa ujauzito wako.

 

II. Maumivu yanayoambatana na kutoka uchafu ukeni
Maumivu ya namna hii sio ya kudharau. Mimba huwa katika hatari ya kupata maambukizi ambayo yanaweza kupelekea mimba kutoka au kupata uchungu wa mapema.

 

Ukipata maumivu ambayo yanaambatana na uchafu, basi usiende tu kununua dawa pharmacy na kumeza, hakikisha umeonwa na daktari kwanza ili upewe dawa sahihi maana mimba ni kitu cha kuheshimu sana.

 

Maumivu mengine yanaweza kuja wakati unakojoa. Hii inaweza kuwa dalili ya UTI kwenye mimba. Ni vizuri pia kutembelea kituo cha afya cha karibu ili kupata vipimo na matibabu.

 

Muhimu: Kuna muda mama mjamzito hutokwa na uchafu mweupe unaowasha tu bila maumivu wala harufu. Hii yaweza kuwa fangus; inapaswa kutibiwa la sivyo ikiwa nyingi inaweza kuathiri mfuko wa uzazi na kupelekea maambukizi ya mfuko na kusababisha ya chupa ya maji kupasuka kabla ya muda.

 

3. Kutokwa na maji meupe ukeni

Hali hii huitwa chupa kupasuka (ruptured membranes). Hapa mama huona maji meupe ambayo hutiririka mpaka mapajani na miguuni hasa akijikamua au kukohoa. Hali hii ni ya hatari!

 

Ikitokea kuanzia wiki ya 12 mpaka 24 yaweza kuashiria mimba kutoka na kuanzia wiki ya 34 na kuendelea yaweza kupelekea mama kupata uchungu wa mapema. Hivyo ikijitokeza mama huitaji kupata uangalizi akiwa hospitali amelazwa.

 

Kupasuka chupa huweza kusababishwa na mambo mbalimbali yanayotokana na kondo la uzazi kuwa dhaifu. Hii husababishwa na hali tofauti tofauti hasa maambukizi ya bakteria.

 

Bahati nzuri hali hii hutibika vizuri hospitali na mimba ya mama huendelea mpaka kufikia umri halisi. Ingawa kwa baadhi ya wajawazito hali hii yaweza kufika pabaya mpaka kulazimika kujifungua kabla ya wakati.

 

Dalili za ziada

1. Kuvimba miguu

Hali hii kwa mama mjamzito, kwa asilimia 90%, huwa ni kawaida. Lakini haupaswi kukaa nayo bila kwenda hospitali na kuhakikisha ni kuvimba tu na sio shida nyingine kwasababu mara nyingine kuvimba miguu huambatana na presha ya mimba na changamoto nyingine ijulikanayo kama Pre-eclampsia.

 

Pre-eclampsia ni presha ya mimba inayoambatana na changamoto zingine kama kuathiri ubongo, figo, ini na kadhalika. Dalili zake huwa ni kuvimba miguu, kuumwa kichwa, kizunguzungu, maumivu
ya tumbo na kama haijatibiwa huweza kupelekea kifafa cha mimba.

 

Hivyo miguu ikivimba onana na wataalam wa afya kwanza wahakikishe vipimo vingine viko kawaida.

 

2. Kutapika kupita kiasi (Hyperemesis Gravidarum)
Hali ya kutapika kwa mama mjamzito huwa ni kawaida lakini kuna wakati mama anatapika kupitiliza kiasi kwamba hakuna kinachokaa. Mara nyingi watu husubiri mpaka mama alegee sana, kutokana na kupoteza maji na madini mengi mwilini, ndio wampeleke hospitali.

 

Kama anatapika sana ni vyema kutembela kituo cha afya na kupata vipimo, inawezekana kuna sababu zaidi ya mimba; pia ili kupata huduma ya kwanza kama drip. Hepuka kusikilizia nyumbani labda kama una daktari binafsi anayekuona home.

 

3. Michezo ya mtoto kupungua
Mama mjamzito amezoea mtoto kucheza mara kwa mara labda mara nne au tano kwa siku. Mtoto akianza kupata changamoto yoyote ndani michezo inaweza kuanza kupungua mpaka 3 au 2 kwa siku. Basi ni vizuri kuja kliniki mara moja ili uangaliwe pamoja na vipimo kadhaa vifanyike, mfano
Ultrasound, kuona hali ya mtoto ndani.

 


Hii inamuhitaji mama kuwa makini kwenye mimba yake na kujua pale tu changamoto inapotokea. Wajawazito wengi huja hospital pale wanapokuwa hawasikii kabisa michezo ya mtoto na mara nyingi utakuta mtoto alishakufa tumboni. Kuwa makini kuongea na kumsikiliza mwanao ili anapokuwa
hachezi ujue mapema.

 

Ufanye nini kupunguza hatari hizi kwenye mimba?

1. Epuka matumizi ya sigara wakati una mimba

Hii ni hatari sana na moja ya hatari yake ni kusababisha mama kupata uchungu mapema au mimba kutoka kabla ya wakati.

 

Katika muda niliofanya kazi, nimeshuhudia wanawake wajawazito 7 kati ya 10 mimba zao zikitoka mapema au walijifungua kabla ya muda na kuwasababisha kubaki hospitali muda mrefu ili motto afikie kilo sahihi.

 

Sigara huambatana na kupata mtoto mwenye kilo ndogo na pia uwezekano wa mtoto kupata utindio wa ubongo. Sigara pia ni moja ya kisababishi cha mama kupata presha ya mimba na kifafa cha mimba. Sasa wewe hapo chagua nini unakitaka zaidi!

 

Vipi kuhusu pombe?
Kuna utafiti ulionyesha matumizi ya pombe wakati wa ujauzito pia kuwa sio salama kwa mtoto. Pombe hupita moja kwa moja mpaka kwenye mfuko wa mtoto (placenta) na huathiri ubongo wa mtoto. Usishangae kupata mtoto kichwa ngumu, au mwenye matatizo ya akili baadaye.

 

2. Epuka matumizi ya dawa kiholela

Ukigundua una ujauzito anza kumeza zile dawa tu ulizoandikiwa na daktari na sio kukimbilia pharmacy kila ukipatwa na shida.

 

 

Kuna dawa zinazoweza kupelekea mimba yako kutoka, kuwa makini.

3. Mahudhurio ya kliniki, sio tu ni muhimu, ni lazima!

Kliniki ndipo matatizo mengi ya mimba hugundulika na kuchukuliwa hatua mapema. Acha kujifanya mzoefu wa mimba kwakuwa umeshajifungua sana, kila mimba ina utofauti wake.

 

4. Epuka kuzalia nyumbani

Kuzalia nyumbani ni jambo lisilofaa hasa pale utakapokutana na changamoto za uzazi. Hii hufanywa zaidi na wale wamama waliojifungua mara nyingi, wao huisi wana uzoefu sana na mimba na matokeo yake hujikuta wakipoteza mtoto na uhai pia.

 

Mimba inapokaribia uchungu sogea karibu na kituo cha afya. Bahati nzuri sikuhizi hospitali nyingi zinatoa hifadhi ya wamama kusubiri uchungu. Kuzalia nyumbani kwa kwa lugha nyepesi ni kama unabeti.

 

Stori Binafsi
Wakati nikiwa mdogo, Baba yangu (Mr. Phillbert Bitegera) aliniadithia kuhusu mama yao; Bibi alizalia nyumbani watoto 6 kwa kutumia wakunga. Alipobeba mimba ya saba nayo alilazimisha kujifungulia nyumbani kwakuwa tayari ana uzoefu na huwa anajifungua vizuri.

 

Bahati mbaya mtoto huyu wa 7 hakuwa katika nafasi nzuri ya kuzaliwa nyumbani. Mtoto alishindwa kutoka nje na mwisho wa siku, wote – mama na mototo – walifariki nyumbani.

 

Inawezekana angekuwa hospitali angehitaji operation ya haraka ila hakupata fursa hiyo kwakuwa hakuwa hospitali.

 

Jambo la kujifunza hapa ni kwamba, mimba hazifanani. Kwakuwa ulijifungua vizuri katika mimba iliyopita haimaanishi mimba hii utajifungua kawaida, labda mimba hii utahitaji operation na sio kuzaa kawaida.

 

5. Fanya ngono salama

Epuka kufanya ngono hovyo na watu wasioaminika ili kuepuka maradhi mbalimbali ya zinaa yanayoweza kuathiri ujauzito wako. Ikiwezekana tumia condom kama mwanaume ni mpya au hujaonana naye muda mrefu.

 

6. Pata matibabu mapema

Epuka kuchelewa matibabu kwa sababu ya uzembe. Pia unapopewa dawa hakikisha unamaliza dozi ili kuepusha maradhi ya mara kwa mara.

 

7. Fanya kazi kwa kiasi

Hasa mimba yako ikiwa bado kwenye miezi mitatu ya mwanzo na mwisho. Punguza kusafiri umbali mrefu ukiwa na ujauzito mchanga, inaweza kuleta changamoto ya mimba kutoka – japo hii sio kwa kila mwanamke.

 

8. “Gentle sex”

Kufanya mapenzi wakati wa mimba haina shida kuanzia mwanzo mpaka mwisho, ila ifanywe kwa ustaarabu bila kutumia nguvu kubwa sana na pia ni muhimu kuchagua style ambayo haileti kubanwa kwa tumbo.

 

Mwisho…

Kama wewe ni mwanaume basi jitahidi sana kumpa sapoti mwenza wako wakati wa ujauzito. Mambo hayo yote yatafanikiwa iwapo mume yupo karibu na mwenza wake. Hii inahusisha pia kuwa karibu na watoa huduma ili wakupe maendeleo ya mama na mtoto.

 

Mwaka 2018 wakati mke wangu anajifungua mtoto wa kwanza, kulikuwa na changamoto ya uchungu kuchukua muda mrefu bila kujifungua. Basi nilipata wasaa wa kuongea na manesi na daktari, wakashauri afanyiwe operation. Akafanyiwa tukapata mtoto wetu wa kwanza.

 

Naamini kuwepo karibu kulirahisisha maamuzi bila kupoteza muda. Wenza wetu wakiwa wajawazito wanatuhitaji zaidi ya kawaida. Tuwajibike kwa ajili ya watoto wetu. Tabia ya kupenda kuitwa baba halafu mimba hauna habari nayo, sio sawa!

 

Wamama wajawazito nanyi muwe wawajibikaji. Unakuta mama mjamzito lakini anavuta shisha, sigara na bangi. Anakunywa pombe kama kawaida utadhani hamna kitu tumboni. Matokeo yake unaleta mtoto mlemavu wa akili anakuja kuwa janga kwa familia kiuchumi na kijamii. Tuwe wawajibikaji kama tumeamua kuwa wazazi.

 

Kumbuka, hata kama umebakwa ndio ukapata mimba, haifanyi mtoto asiwe wako. Mwisho wa siku akizaliwa ni wako hivyo usinyanyapae mimba wakati unajua ni mtoto atakuja.

 

Kama wewe ni mjamzito, bila shaka unahitaji kuwa na daktari binafsi atakayekuwa anajibu maswali ya dukuduku zako zote, basi ingia hapa upate huduma ya daktari kiganjani, itakusaidia sana. Asante!

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW