Changamoto 5 Zinazoweza Kupelekea Kushindwa Kupata Mtoto

Naitwa Jackson, nina miaka 35, nimejaribu sana kupata mimba na mchumba wangu kwa miaka miwili sasa bila mafanikio. Mimi na mchumba wangu tulikutana mwaka 2020 na mwaka uliofuata tukaanza kutafuta mtoto lakini ni miaka miwili sasa bila mafanikio, nifanyeje daktari?

 

Majibu na Dr. Ansbert Mutashobya

Pole sana bwana Jackson kwa tatizo hilo. Ni jambo linaloleta mawazo sana katika mahusiano na likiendelea kwa muda mrefu huwa chanzo cha mgogoro katika mahusiano. Linaweza kutokea kabla hamjapata mtoto au mkiwa tayari na mtoto mmoja au wawili. Sababu mbalimbali huweza kupelekea hali hii, usipozijua na kutatua mapema inaweza kuleta shida baadaye.

 

Sababu inaweza kuwa ni nini?

Kwanza nikwambie tu kwamba hili tatizo sio lenu peke yenu, ni tatizo ambalo lipo katika jamii nyingi na swala la mwanamke kupata mimba sio jambo rahisi kama inavyodhaniwa. Huwa kuna mambo mengi yanaendelea aidha katika mwili wako au wa mwanamke, hivyo ni vyema kutambua kwamba kila mtu ana muda wake na wakati mwingine unahitaji subira zaidi – baada ya kuhakikisha kwamba hakuna shida zingine za kiafya.

 

Utafiti unaonyesha, ni moja kati ya couples 5 ambayo mwanamke hupata mimba katika mzunguko wa kawaida, wengine mimba hutokea tu katika muda wowote na wakati mwingine huchukua muda mrefu.

Kwa maana hiyo kati ya wapenzi watano, wanne wanahangaika kupata aidha mimba ya kwanza au mtoto wa pili. Usiwaone watu wanapata mimba ukadhani ni rahisi, jua kwamba kama kuna wanaopata mimba, wapo wengi pia wanapata shida kupata mimba. Kiufupi kumpa mwanamke mimba huwa ni matokeo ya kuotea zaidi kuliko uhakika.

 

Kushindwa kumpa mimba mwenza wako huweza kusababishwa na mambo mbalimbali ambayo unapaswa uyajue. Hivyo kabla hujakata tamaa unapaswa ujiulize maswali yafuatayo:

 

1. Mbegu zako za uzazi ziko vizuri?

Afya nzuri ya uzazi ni hali ya mwili wako au wa mwanamke wako kuwa na uwezo utakaoruhusu kutungisha au kubeba mimba. Mbegu zako ziko vizuri kwa maana ya kiasi (volume) na hazina matatizo yanayoweza kushindwa kuingiliana (Morphology) na yai la kike? Au uwezo wa mbegu zako kuogelea kuelekea mirija ya uzazi (motility) kuwa mdogo.

 

 

Unahitaji kiasi cha mbegu walau Milioni 15 kuweza kuwa na kiasi cha kutosha kufanya mbegu zako kufika kwenye mirija. Walau wingi wa millilitre 5 au wingi wa kijiko kimoja kikubwa. Japo wingi au volume sio hoja sana lakini bado kiasi cha mbegu katika wingi huo kina maana kubwa.

 

Mbegu zinapokuwa nyingi huwa zinasaidiana kusukumana kuelekea mirija ya uzazi na nyingi huishia njiani na kupotea; na kati ya milioni 15 mbegu 200 tu ndio huweza kufika salama ambazo huanza kulainisha ukuta wa yai la kike na baada ya hapo mbegu moja tu ndio hupenyeza kutengeneza mimba. Hivyo ukiwa na kiasi kidogo cha mbegu uwezo wako wa kutungisha mimba hupungua.

 

Mbegu zako pia lazima ziwe na uwezo wa kuogelea kufika katika mirija ya kike kwa ajili ya kukutana na yai. Kushindwa kutungisha mimba kunaweza kusababishwa na mbegu zako kutokuwa na uwezo wa kuogelea kufika kwenye mirija. Pia muundo wa mbegu zako kuwa mbaya au na umbo bovu ambalo haliwezi kuingiliana na yai.

 

Kuna tafiti moja ilifanywa mwaka 2014 mpaka 2016 kuangalia mambo yanayoweza kuathiri hayo mambo matatu ya mbegu zako. Waligundua mambo yafuatayo:

 

Lishe binafsi

Upungufu wa virutubisho mwilini kama zinc, vitamin c, selenium na vitamin E kutokana na kutopata mlo sahihi ilionekana kuwa sababu ya mwanaume kuwa na mbegu chache. Umewahi kusikia mtaani unaambiwa ule karanga mbichi, mara matikiti, mara mihogo mibichi, mara nazi au pweza na kadhalika?

 

Basi hadithi hizo huwa zinalenga kuongeza virutubisho ambavyo vinaongeza utengenezaji wa mbegu, lakini pia kuwezesha mbegu zako kuwa na uwezo wa kuogelea kufika kwenye via vya uzazi.

 

Baadhi ya vyakula unavyoshauriwa ule ni karanga na mbegu (mfano mbegu za maboga, walnuts & almond seeds, na mbegu za alizeti).

 

Iwe kawaida yako kula matunda yenye Vitamini C mfano mapapai na machungwa, pamoja na maboga ya majani mfano spinach na broccoli.

 

Vyakula vya wanga ambavyo havijakobolewa, wali wa brown, nyama ya kuku, samaki na kadhalika. Kwa ufupi sio kula tu, bali kula mlo kamili mara kwa mara, sio wikiendi pekee au mwisho wa mwezi.

 

Uvutaji wa sigara na uteja wa pombe

Kwa mujibu wa jarida la mwaka 2016, ilionyesha uvutaji wa sigara kama sababu kubwa ya kupunguza uwezo na kiasi cha mbegu zako.

 

Katika utafiti uliofanyika mwaka 2023, pia ilionyesha matumizi makubwa ya pombe kuwa chanzo cha mbegu zilizoharibika, upungufu wa mbegu na uwezo mdogo wa kuogelea kwa mbegu zako mpaka asilimia 30.

Vingine ni matumizi ya kahawa.

 

Nifanye nini ili kujua kiwango na muundo wa mbegu zangu?

Nenda hospitali shauriana na daktari akufanye kipimo cha kupima mbegu zako (sperms analysis). Kupitia kipimo hiki utaweza kujua kiasi na uwezo wa mbegu zako. Kama ziko sawa, basi ni kuangalia sababu zingine, na kama zina shida daktari wako atakushauri cha kufanya.

 

Muhimu: Ni upotevu wa muda kukaa bila kufanya uchunguzi wa mbegu zako kwa muda mrefu wakati haujawahi kutungisha mimba hata ya kusingiziwa. Lakini pia kuwa na mtoto kwa mwanamke mwingine sio sababu ya kuwa na uwezo wa kumpa mimba mwanamke mpya. Inawezekana hapa katikati mbegu zako zimeharibika kutokana na sababu mbalimbali au huyo mtoto mwingine sio wako.

 

Hakikisha unapima kama hili jambo limekuwa tatizo. Pia pamoja na kuwa na mbegu chache bado unaweza kutungisha mimba. Endelea kusoma makala hii hadi mwisho.

 

2. Afya ya uzazi ya mwenza wako ikoje?

Afya ya uzazi ya mwanamke ina mambo mengi lakini machache unayoweza kuangalia ni kama:

Anapata mzunguko wake wa hedhi kama kawaida? Mzunguko wa kawaida wa mwanamke ni kiashiria kizuri kwamba anaweza kupata mimba kwa maana ana homoni za kutosha na kizazi.

 

Baada ya hilo ni vema kujua kama mirija na mayai yake yana na afya nzuri. Hii inaweza kujulikana kwa kwenda hospitali na kufanya vipimo vya homoni pamoja na ultrasound kuangalia via vya uzazi na kuhakikisha hana hali yoyote inayoweza kusababisha kutobeba mimba.

Wakati mwingine kuingia katika hedhi sio sababu ya kuweza kupata Mimba. Anaweza kuwa anaingia kama kawaida lakini mfumo wake wa uzazi kwenye ovaries hautoi mayai kwa ajili ya kukutana na mbegu za kiume (an ovulatory cycle). Bila mayai huwezi kutungisha mimba!

Sababu kubwa huwa ni, kukaa muda mrefu bila kubeba mimba Lakini Pia matumizi ya uzazi wa mpango kama sindano au kijiti au hata kitanzi vinaweza kuchelewesha mtu kupata mimba mpaka mwaka au zaidi. Ni vizuri kuzungumza na daktari ili kumpatia dawa ya kusaidia yai kutoka mfano clomiphene.

 

3. Unazijua siku za hatari za mwenza wako?

Unajua mwenza wako anaingia muda gani kwenye siku zake za hatari?

Ni muhimu kuzijua hasa kama wewe sio mkaaji sana wa nyumbani. Maana utapaswa kujua ni muda gani uvizie kwa ajili ya kuja kutupia vitu la sivyo inaweza kuwa ngumu.

 

Mara nyingi njia inayotumiwa ni kuhesabu mzunguko wa hedhi kwa mwezi na kujua siku zake za hatari ni zipi, jambo ambalo limekuwa linachanganya sana na mara nyingi kutokuwa na matokeo mazuri kutokana na tabia ya mzunguko kubadirika mara kwa mara.

 

Maana yake sio lazima kama mwezi huu yai limetolewa tarehe 15, basi na mwezi ujao itakuwa tarehe hiyo; siku za mwanamke zina tabia ya kubadirika kutokana na sababu mbalimbali kama vyakula, dawa na msongo wa mawazo.

 

Lakini pia sio wanawake wote wana mzunguko wa siku 28. Wengine wana mzunguko wa siku 21 wengine 35 hivyo huleta ugumu kujua siku ya hatari ni lini hasa.

 

Njia nzuri ya kutumia ni kujua dalili na tabia za mwanamke aliye kwenye siku za hatari.

Kwanza, mabadiriko katika ute wa shingo ya kizazi (cervix). Ute huongezeka, huwa mwepezi na mwingi zaidi ya kawaida.

 

Pili, joto la mwili huongezeka zaidi. Katika kipindi hiki ukimgusa mwanamke wako kitandani utagundua ana joto zaidi ya kawaida na yeye anaweza kukwambia kabisa.

 

Tatu, kuogezeka kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Muda huu mwanamke huwa na tamaa na wewe sana na hutaka kufanya mapenzi. Takwimu zinaonyesha ni katika kipindi hiki wanawake wengi hupata mimba maana kwa hamu wanayokuwa nayo husaau hata kutumia kinga.

 

Kuwa makini kama ukigundua mwanamke ana hamu sana na wewe, inawezekana yuko kwenye hatari na kama unataka mtoto, huu ndio wakati wenyewe.

 

Nyingine ni chuchu za matiti kuvimba na kuuma kwa mbali, kichefuchefu na tumbo kujaa gesi.

 

Angalizo: Kama mwanamke anapata hedhi kawaida lakini hapati hizi dalili, basi kuna uwezekano mayai yake hayatolewi (An ovulatory cycle) na ndio maana itakuwa ngumu kumpa mimba kwa sababu haingii kwenye hatari. Hapa atahitaji msaada wa dawa kuweza kuongeza uwezo wa mayai kutolewa (ovulation). Wasiliana na mimi kwa kulipia kiasi kidogo ili nikushauri.

 

Kumbuka: Siku ya hatari sio tu ile siku yai linapotolewa bali huanza siku 4 kabla ya hiyo siku na siku moja baada kwa maana ya siku 5 jumla hivyo sio lazima kufanya na mwenza wako siku halisi ya hedhi.

 

Hata mkifanya siku tatu kabla ya hiyo tarehe mimba itatungwa kwa sababu mbegu ya kiume inaweza kukaa kwa zaidi ya siku 3 mpaka 4 ikisubiri yai lije. Ukifanya siku mbili baada ya yai kutolewa unaweza usimpe mimba mwanamke wako kwasababu yai la kike linaishi kwa masaa 24 tu, baada ya hapo hufa.

 

4. Umbali kati yenu ukoje?

Moja kati ya changamoto kubwa ya kumpa mimba mwanamke wako ni umbali. Unaweza kujua siku za mwenza wako A mpaka Z lakini kutofanya sex mara kwa mara kunaweza kuwa kikwazo kwasababu kila siku unazokuja kwake sio za hatari.

 

Mara nyingi kumpa mwanamke ujauzito ni jambo la kuotea kwa sababu mzunguko wa mwanamke una tabia ya kubadilika badilika na hivyo siku za hatari za mwezi huu hazitakuwa za hatari mwezi ujao.

 

Kama mpo karibu na mnafanya mara kwa mara uwezekano wa kuotea na kupata ujauzito ni mkubwa mno. Kwahiyo ni vyema kama uko mbali kikazi, uwe unachukua hata likizo ya mwezi, kaa na mwenza wako, mfanye mara kwa mara na unaweza ukamuotea akapata mimba.

 

 5. Afya zenu za mwili zikoje?

Kabla ya kujilaumu au kumlaumu mwenza wako, hakikisha afya yako na yake ziko sawa. Magonjwa ya zinaa kama gonorrhea yanaweza kukusababishia kushindwa kumpa mwanamke mimba. Ni vyema kupima magonjwa ya zinaa na mwenza wako.

 

Magonjwa kama sukari kwa mwanamke na mwanaume pia yanaweza kuleta ugumba na kufanya ngumu kupata mtoto. Ni vizuri mkafanyiwa vipimo mbali mbali vya afya kabla ya kuanza kutafuta mtoto au kudhani ni wagumba.

 

Hakikisha pia mchumba wako ana kizazi, mirija yake iko sawa na hatumii uzazi wa mpango bila wewe kujua.

 

Nimeshapokea kesi nyingi sana ambapo mwanamke anafahamu kabisa hana kizazi au alishafunga mirija ya uzazi na hawezi kupata mimba lakini hamwambii mwenza wake na hivyo kuamuacha mwanaume ahangaike huku na kule wakati tatizo ni yeye.

 

 

Hakikisha mnafanya vipimo vya ultrasound na homoni kuhakikisha hamna hiyo changamoto. Mwanaume, ukiona kila ukimwambia mwenza wako mkapime na hataki au anakwambia mwende kwa daktari wake, shtuka, hakikisha daktari anawapa majibu wote kwa pamoja na anaandika majibu kwenye karatasi ili kama ni muongo baadaye unaweza kumfungulia kesi ya ulaghai.

 

Ulishawahi kupata mtoto kwingine?

Hili ni jambo la msingi sana kuliongelea. Kuwa na mtoto sehemu nyingine inaweza kuwa dalili nzuri kwamba una uwezo wa kuzalisha, hilo nakubali. Lakini sio sababu ya kukufanya uendelee kuwa na uwezo wa kutungisha mimba.

 

Kwanza inawezekana mtoto akawa sio wako kwani katika utafiti uliofanywa iligundulika kwamba mmoja kati ya wanaume watano ana mtoto asiye wake hivyo inawezekana akawa sio wako pia.

 

Sababu nyingine kubwa ni kwamba mwili wako hubadirika kutokana na mazingira na style za maisha kwa ujumla. Utafiti uliofanywa katika hospitali ya muhimbili mwaka 2012 ulionyesha kuwa kuna asilimia 47 ya ugumba kwa wanaume. Kati ya hao asilimia 30.3 walikuwa na mbegu dhaifu zisizoweza kutungisha mimba na asilimia 17.03 walikuwa hawana mbegu kabisa. Hii ni baada ya kupima wanaume zaidi ya 250 waliojitokeza kufanyiwa vipimo.

 

Kupata mtoto mmoja na kushindwa kupata mwingine baada ya hapo nayo iliwekwa katika kundi la ugumba. Sababu zinazoweza kusababisha kutotungisha mimba hata baada ya kuwa na mtoto ni kama magonjwa mbalimbali ya tezi, ajali, matumizi makubwa ya pombe, sigara, shisha na ajali mbalimbali. Pia kuna baadhi ya kazi kama udereva wa masafa marefu na uendeshaji bodaboda vilitajwa.

 

Point hapa ni ipi?

Usitumie kigezo cha kuwa na mtoto mwingine kujiaminisha kwamba uko vizuri. Ugumba waweza kutokea muda wowote ule. Hivyo kubali kufanya vipimo mbalimbali na sio kumnyanyasa mwenza wako kwamba ana tatizo na wewe uko vizuri.

 

Mwisho

Katika ziara ya Waziri wa Afya mheshimiwa Umu Mwalimu akitembelea hospitali ya Kairuki mwaka huu alitoa takwimu ya ugumba kuwa asilimia 30 ya watu nchini wana tatizo hili na katika rekodi za kidunia walau kati ya kundi la wapenzi wanne, moja wana tatizo la kutopeana mimba.

 

Ugumba huweza kufafanuliwa kama kushindwa kumpa au kupata mimba mwaka mmoja baada ya kufanya mapenzi, mara kwa mara, na mwenza wako bila matumizi ya kondomu na sababu kubwa ni hizo nilizozitaja.

 

Kama kuna moja ambayo unahisi hujaifatilia basi chukua hatua stahiki mambo yatakuwa sawa tu, usijifiche kwenye kivuli cha kulaumu mwenza wako, shirikianeni mubaini chanzo.

 

Endelea kufuatilia makala zetu zinazofata na zilizopo katika blogu yetu. Pia unaweza kuingia dukani kwetu kununua vitabu vizuri vya kukupa elimu ya afya ya kutosha, amini elimu ni ufunguo wa maisha.

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW