Naitwa Jamila, nina miaka 22. Juzi nilishauriwa na rafiki yangu kuanza kutumia dawa za majira lakini sina elimu ya dawa hizi kabisa. Sina Uhakika kama ni sahihi kwangu au la. Naomba daktari unieleweshe ili nipate elimu na niweze kuwaelimisha wengine.
Majibu na Dr. Ansbert Mutashobya
Asante Jamila kwa kuliweka wazi ili na kutamani kujifunza. Vidonge vya majira ni mojawapo ya njia za uzazi wa mpango amabayo hufanywa kwa kumeza kidonge kila siku kwa muda wa siku 28 bila kukoma. Ningependa nianze kwa kukupa kahistoria kidogo kuhusu dawa hizi.
Vidonge vya majira (combined oral contraceptive pills) viliruhusiwa kuanza kutumiwa kwa ajili ya uzazi wa mpango na Shirika la dawa duniani, FDA, mnamo tarehe 23 Juni, 1960. Mwaka huu unajulikana kama mwaka wa ukombozi kwa wanawake duniani na ndio kipindi ambacho wanawake wengi walianza kufurahia tendo la ndoa bila hofu ya kupata mimba. Dawa hizi zilikuja kuleta uhuru kwa walio wengi.
Inakadiriwa kwamba mpaka mwaka 2019 kiasi cha wanawake Milion 150 duniani walikuwa wanatumia dawa za majira (Coc) kwa ajili ya kuzuia mimba zisizotarajiwa.
Dawa hizi zina faida gani mwilini?
Faida kubwa ni kukukinga na mimba zisizotarajiwa au kupangwa. Hakuna kitu kinachoweza kuleta msongo wa mawazo kwa mwanamke au wapenzi kama mimba ya bahati mbaya.
Huwa ni chanzo cha kupoteza amani, kuongeza majuto, na kwa wengine huwa ni chanzo cha kufanya abortion (utoaji mimba). Kitendo ambacho hakikubaliki katika afya na jamii nzima kama hakifuati maagizo maalum ya daktari.
Faida nyingine ni kama kupunguza maumivu ya tumbo wakati wa hedhi, kupunguza upotevu mkubwa wa damu hasa kipindi cha hedhi, kusawazisha homoni zako za uzazi kuwa sawa, kupunguza uwezekano wa kupata vivimbe maji vya ovari (ovarian cyst), kupunguza uwezekano wa magonjwa ya kansa ya kizazi na ovari zako, na pia kupunguza uwezekano wa chunusi (Acne).
Madhara yanayoweza kuambatana na matumizi ya dawa hizi ni kama kuogezeka uzito, kichefuchefu, msongo wa mawazo (sonona), kuvuruga mzunguko wako wa hedhi (irregular menstruation), kuwa na moods tofauti tofauti, na matiti kuvimba na kuuma . Madhara yaliyo mengi huweza kuisha baada ya miezi miwili mpaka mitatu, yakiendelea hapo unapaswa kumuona daktari kwa ajili ya ushauri zaidi.
Kumbuka…
Matumizi ya vidonge vya majira hayakukingi na magonjwa ya zinaa kama Ukimwi na kaswende. Matumizi ya dawa hizi hayaondoi ulazima wa kutumia kondomu; kondomu hasa kwa wapenzi wasiofahamiana vyema ni lazima.
Kumekuwa na tafiti nyingi zilizoonyesha kuongezeka kwa magonjwa ya zinaa kwa wanawake wanaotumia uzazi wa mpango na sababu kubwa ni wao kudhani vidonge vya majira vinazuia magonjwa ya zinaa.
Njia ya uzazi wa mpango pekee inayoweza kuzuia mimba na magonjwa ya zinaa ni kondomu.
Dawa hizi hufanyaje kazi?
Dawa za majira hufanya kazi kwa kuingiza homoni mwilini kwako ambazo hufanya mayai yasitolewe (huzuia ovulation) hivyo kuondoa uwezekano wa mbegu ya kiume kukutana na yai la kike kutengeneza mtoto. Pia hufanya mlango wa shingo ya uzazi kutengeneza ute mzito ambao huzuia mbegu za kiume kwenda kusababisha mimba.
Njia hii ya uzazi wa mpango ina mapungufu gani?
Mtumiaji wa dawa hizi hupaswa kuzitumia kila siku ya Mungu bila kusahau. Kusahau hupunguza ufanisi wa dawa na kukuweka kwenye hatari ya kubeba mimba. Ikimezwa kila siku, dawa hizi huwa na ufanisi mkubwa sana.
Nikisahau kumeza dawa nifanyeje?
Ukisahau kumeza dawa siku moja au mbili huwa unajiweka kwenye hatari ya kupata mimba. Ikitokea siku umesahau kumeza kidonge, inashauriwa siku inayofata umeze viwili halafu endelea siku inayofata na kimoja kama kawaida.
Ukisahau siku mbili basi meza viwili siku mbili zinazofuata na baada ya hapo endelea na kimoja. Njia hii haikupi ulinzi kwa asilimia 100 bali hupunguza uwezekano wa kupata mimba.
Nikitaka kuacha kutumia dawa nafanyaje?
Kuacha matumizi ya dawa za majira ni rahisi tu, unaacha kuzinywa. Japo unaweza kupata changamoto kiasi kama mvurugiko wa hedhi yako ambayo baada ya muda hukaa sawa.
Angalizo: Kuacha matumizi ya dawa hizi hata kwa siku mbili kunaweza kupelekea kupata mimba, hivyo unapoacha tu, endelea na matumizi ya kondomu wakati unajaribu kuamua utumie njia gani nyingine. Usipofanya hivyo utapata ujauzito!
Vitu gani vya kuzingatia kabla ya kuanza matumizi?
Kwanza kabla hujaanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango unapaswa kupata ushauri wa daktari na sio kuanza tu kiholela mtaani.
Daktari atakushauri mambo mbalimbali yahusuyo dawa za majira na afya yako. Baadhi ya mambo ambayo nitakushauri kama daktari ni:
- Kama una ugonjwa wa presha ya kupanda ambayo inasumbua kukaa sawa hata kwa dawa basi njia hii ya uzazi wa mpango sio nzuri kwako, inaweza kufanya presha yako kupanda zaidi, tumia njia nyingine.
- Kama una tatizo la sukari na cholesterol ya juu sikushauri utumie dawa za majira kwasababu zinaweza kuongeza madhara zaidi hasa uwezekano wa kupata magonjwa ya kiharusi (stroke).
- Bahati mbaya hospitali nyingi haziwezi kupima cholesterol lakini unaweza kujua cholesterol yako iko juu kwa kuangalia uzito wako. Kama una uzito mkubwa, BMI kuanzia 25 kwenda juu, usitumie hizi dawa za majira kama uzazi wa mpango, kumbuka zinaongeza uzito pia.
- Kama ulishawahi kupata ugonjwa wa stroke (kiharusi) haushauriwi kutumia dawa za majira.
- Una Magonjwa ya moyo hasa mishipa ya moyo? Sikushauri utumie njia hii. Kuna njia inayokufaa kama kitanzi, kondomu au kalenda.
- Unavuta sigara au ugoro? Jua ni marufuku kutumia dawa hizi wakati unavuta sigara. Ukifanya hivyo muunganiko wa dawa za majira na nicotine iliyopo kwenye sigara huongeza zaidi madhara ya sigara na kukuweka kwenye hatari ya madhara makubwa ya sigara kama kansa ya kizazi, mapafu, matiti, presha kuwa juu na kadhalika.
Kuna njia nyingine za uzazi wa mpango tofauti na vidonge? Zipo na tutazizungumza katika toleo lijalo la njia za uzazi wa mpango.
Kuna tofauti gani kati ya vidonge vya majira na sindano?
Zote hufanya kazi sawa japo sindano huchomwa mara moja kila baada ya miezi mitatu hivyo kuondoa adha ya kumeza dawa kila siku.
Sindano huweza kukaa zaidi mwilini na wakati mwingine inaweza kukuchukua mpaka mwaka kupata ujauzito baada ya kuacha matumizi ukilinganisha na vidonge ambapo ukiacha tu unapata mimba.
Ulishawahi kusikia kuhusu morning after pill? (Vidonge vya dharura vya kuzuia mimba)
Tambua hauna haja ya kubeba mimba kama hujaamua hasa pale unapokuwa umefanya ngono nzembe au kondomu imepasuka na shahawa zikaingia kwa uke au umeingiliwa kinyume na utashi wako (kubakwa). Unaweza kutumia hiki kidonge cha morning after pill au emergency pill ambacho ni majira lakini kina muunganiko unaoweza kuzuia mimba walau ndani ya masaa 72 tangu ulipofanya sex.
Vidonge hivi huzuia yai lako na mbegu ya kiume kukutana kwa kufanya mbegu za kiume kwenda taratibu na hivyo kufa kabla hazijakutana na yai. Pia dawa hii huweza kuzuia mimba kujishikiza kwenye ukuta wa kizazi (implantation).
Dawa hizi huuzwa pharmacy kwa bei ya kawaida. Huna haja ya kupata mimba isiyotarajiwa labda kwa kukosa elimu tu. Nenda pharmacy mapema na utaelekezwa matumizi.
Madhara yanayoweza kuambatana na kumeza dawa hii ni kama kizungu zungu, kichefuchefu, uchovu wa mwili, maziwa kuuma, na kupata period kwa muda kadhaa. Dawa hizi zikitumika mara kwa mara huwa na madhara katika mzunguko wako wa hedhi. Inaweza kuvuruga kabisa mzunguko wako na kukupa matatizo ya hedhi.
Angalizo…
Dawa hii sio kigezo cha wewe kufanya ngono nzembe maana haitazuia kupata magonjwa ya zinaa, hivyo usiweke ulinzi wako chini kwa kutegemea morning after pill.
Tambau dawa hii hukinga mimba kwa asilimia 85 pekee, asilimia 25 iliyobaki unaweza kupata ujauzito. Pia kwa watu wanene dawa hii huwa na ufanisi mdogo ukilinganisha na wembaba.
Kabla hujatumia dawa hii hakikisha huna mimba, dawa hizi zinaweza kuwa na madhara kwa kiumbe chako tumboni au kusababisha mimba kutoka.
Pia matumizi ya dawa hii kipindi ukiwa katika dawa nyingine kama dawa za msongo wa mawazo na magonjwa ya akili inaweza kufanya ufanisi wake kuwa mdogo hivyo kutokukukinga na mimba.
Ushauri: Weka kipaumbele kwenye matumizi ya kondomu. Acha matumizi ya emergency pill au zitumie kwa emergency tu kutokana na sababu tulizozitaja hapo juu.
Kuna madhara yoyote ya matumizi njia za uzazi wa mpango katika umri mdogo?
Kiafya kuanzia miaka 16 sio mbaya na haina madhara tofauti na mtu mzima; tatizo kubwa lipo kijamii. Matumizi ya uzazi wa mpango huwasukuma mabinti kuanza ngono nzembe mapema. Kumbuka, unaweza ukawa unatumia vidonge hivi na bado ukapata mimba kulingana na ukosefu wa umakini na kusahau kumeza, hivyo kuongeza uwezekano wa kupata mimba katika umri mdogo.
Lakini pia kuna maambukizi ya virus vya Human Papilloma Virus (HPV) ambayo kuanza ngono nzembe katika umri mdogo huweza kuwasababisha kuvipata na baadaye kupelekea kansa ya shingo ya kizazi.
Kama wewe ni mzazi, pambana sana kumuelimisha binti yako madhara ya ngono nzembe na matumizi sahihi ya kondomu na sio kuwa mzembe kutaka mwanao atumie uzazi wa mpango, atalala na wanaume wengi bila kujali.
Nikuibie siri..
Mabinti wadogo hawaogopi magonjwa ya zinaa, wanogopa mimba kwa sababu ndiyo inayoonekna hivyo wakiwa na uhakika wa kutopata mimba wanakuwa warahisi kutoa sex na wanakuwa hatarini kulala na wanaume bila kondomu kwasababu wanajua mimba hakuna.
Baada ya muda mwanao atakuwa cha wote. Mjengee uoga wa kufanya ngono katika umri mdogo. Muelimishe; ataogopa na kuepuka.
Bila shaka umepata mwanga wa dawa za majira, naamini utakuwa chanzo cha elimu kwa wengine na familia yako. Siwezi kuelezea kila kitu hapa lakini nina imani utauliza maswali na nitakujibu. Katika mada ijayo nitaongelea njia zingine za uzazi wa mpango.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.