Ni Dawa Gani Sahihi Kwa Ajili ya Meno Yangu?

Hili swali nimeulizwa mara nyingi sana na watu wangu wa karibu. Kupitia makala hii, ningependa kujibu swali  hili ili kuwasaidia nyote wenye utata katika kuchagua dawa sahihi ya kutumia kwa ajili ya usafi na uimara wa meno yanu.

 

Ningependa nianze na historia fupi ya jinsi gani sisi kama binadamu tumekuwa na namna mbalimbali za kusafisha meno yetu, ili japo kwa leo tu uweze kuona na kuthamini kwa jinsi gani sisi kama viumbe wenye utashi na akili tumesonga katika swala hili.

 

Historia…

Hapo awali binadamu waliishi kwa kutembea sehemu moja kwenda nyingine, wakiwinda na kukusanya ili kupata chakula chao cha kila siku. Binadamu huyu alikuwa na meno imara sana. Tafiti mbalimbali zinaonyesha sababu kuu ya uimara wa meno yake ilikuwa aina ya vyakula alivyokuwa anatumia. Vyakula  hivi havikusapoti bakteria waharibuo meno.

 

Baada ya muda na  maendeleo mbalimbali kutokea, binadamu huyu alianza kutengeneza na kuishi katika jamii mbalimbali na kulima kukawa sehemu kubwa ya maisha.

 

Binadamu huyu alilima vyakula mbalimbali ikiwemo wanga (carbohydrates). Mabadiliko haya yalipelekea hata hali na aina ya bakteria walioishi mdomoni mwa binadamu huyu kubadilika. Ugunduzi wa sukari ulipoingia ndipo balaa nalo lilipozidi, idadi ya watu walioharibika meno iliongezeka zaidi. Bakteria wa mdomoni walitumia aina hii ya chakula kuharibu meno kwa kasi zaidi.

 

Dawa ya meno ya kwanza ilikuwako miaka 5000 nyuma, ndani ya mji wa Egypt, ambayo haikuwa kama hii tunayoijua leo bali unga ambao ulikuwa aidha na mifupa ya samaki ya kuponda, gamba la yai, ganda la konokono au ganda la samaki wa aina ya oyster; haya yalisaidia kutengeneza hali ya ugumu ambao ulitumika kusugua meno ili yawe masafi.

 

 

Pia waliongezea majani ya mint ili kutoa harufu mbaya mdomoni.  Waliweka unga huu wenye mchanganyiko wa vitu mbalimbali kwenye meno yao kwa kutumia aidha vijiti vya kutafunwa, nguo au hata kwa kutumia kidole.

 

Miaka ya 1800, aina mbalimbali za dawa ya meno ziliendelea kutengenezwa kutumia vitu mbalimbali kama vile chaki, chumvi, glycerine na hata unga wa risasi.

 

Dawa hii ilianza kuwekwa katika tubes zenye muundo ambao unatumika hadi leo. Baadae sabuni pia iliongezwa katika dawa ya meno lakini katika karne ya 20, sabuni za sintetiki ziligundulika na zikaondoa matumizi ya sabuni katika dawa ya meno.

 

Miaka ya 1950, baada ya tafiti nyingi, umuhimu wa madini ya florini ulionekana katika kuimarisha meno na ndipo madini hayo yalipoongezwa katika dawa ya meno.

 

Kwanini kuna aina nyingi za dawa ya meno?

Katika historia unaweza kuona ni kwa jinsi gani uhitaji wa tiba ya magonjwa ya meno ulivyopelekea mabadiliko mengi katika vitu vinavyotumika katika kutengeneza dawa ya meno. Hadi sasa tafiti zaidi zimepelekea maendeleo na madiliko mengi yanaonekana kupelekea kuwa na  dawa za meno za aina nyingi.

 

Dawa za meno kwa sasa hazitengenezwi tu kwa lengo la kukinga fizi na meno dhidi ya magonjwa au kuondoa harufu mbaya mdomoni, bali hutengenezwa kwa kuzingatia matakwa au matamanio kadha wa kadha ya watu wengi katika mambo kama vile rangi, harufu, ladha, au muundo. Kwani ingawa binadamu ni viumbe sawa, kila mmoja wao hupendelea vitu tofauti.

 

Vitu muhimu vya kuzingatia kabla hujanunua dawa ya meno

Ikiwa ni kweli kwamba dawa za meno zipo za aina nyingi lakini lengo kuu la dawa hizi linabaki kuwa lile lile – kukukinga na magonjwa ya fizi na meno. Hivyo basi, wanasayansi wamebaini vitu muhimu ili dawa yako unayotumia ifanye hivi mbali na kuangalia ladha, rangi, muundo au harufu ya dawa ambayo ungependezwa nayo zaidi.

 

Ni vyema kuvifahamu vitu hivi ili hata kabla hujaangalia vionjo vingine basi hivi ndivyo viwe vya kwanza kuzingatia wakati wa kununua dawa yako ya meno.

 

1. Madini ya Florini

Hapo awali madini haya hayakuwepo katika dawa za meno zilizotumika kama tulivyoona; ni mpaka miaka ya 1950 ambapo madini haya yaliongezwa katika dawa hiyo. Si hapo tu, bali hata katika maji yaliotumika katika jamii zetu ili madini haya yafikie na kusaidia jamii kwa uwigo mpana zaidi.

 

Madini ya florini hukinga meno na magonjwa kwa kufanya meno kuwa magumu zaidi na kuzuia kuharibiwa na bakteria. Madini haya huunganika na sehemu ya nje ya jino (enamel) na kutengeneza muundo uitwao fluoroapatite ambao huongeza uimara zaidi wa jino.

 

Katika dawa yako ya meno, kabla hujanunua ni vyema kuangalia kama madini haya yapo. Unaweza kuchunguza dawa yako kwa kuangalia boksi lake au kwenye tubu ya dawa yako mahali palipoandikwa active ingredients yaani viungo hai katika dawa yako ya meno. Hapo huandikwa aina na kiwango cha madini ya florini yaliyomo.

 

Kuna aina tatu kuu za madini haya ambayo utakuta katika dawa yako ya meno. Kufahamu hizi itakusaidia ujue ni aina gani ya dawa ya meno utahitaji kulingana na mahitaji yako kwa wakati huo.

Aina ya kwanza ni Sodium fluoride, ya pili ni Sodium monofluorophosphate

Hizi hufanya kazi sawa kwa kuongeza tu uimara wa meno na kukinga kutoboka kwa meno yako. Kwa kawaida kabisa, madini ya florini ya aina hizi mbili huunda dawa ya kukubalika kwa matumizi ya kila siku na yenye kukidhi vigezo vya kuimarisha meno (standard toothpaste) ili kuzuia uharibifu wa meno yako.

 

Unaweza kutumia dawa ya meno yenye aina hizi ya florini ikiwa huna tatizo lingine lolote katika kinywa chako.

 

Aina ya mwisho ni stannous fluoride

Aina hii ya madini ya florini, mbali na kwamba huzuia kutoboka kwa meno na kuimarisha meno yako, yenyewe ina faida za ziada kama vile kutibu magonjwa ya fizi kama kutokwa na damu au fizi kuvimba (gingivitis), unyeti wa meno (tooth sensitivity), huzuia mmomonyoko wa meno kwa asidi kupitia bakteria na huuwa bakteria wanaoharibu meno.

Hivyo unaweza kutafuta dawa ya meno yenye madini haya ya florini kulingana na hali yako ya kinywa.

 

Kiwango cha florini katika dawa yako ya meno hutegemeana na umri wa mtu. Kuanzia umri wa miaka 6 na zaidi hutumia dawa ya meno yenye kiwango cha madini ya florini 1450ppm, lakini watoto chini ya miaka 6 hutumia kiwango cha 500ppm mpaka 1000ppm.

 

Kumbuka taarifa zote hizi unazipata kwenye boksi la dawa ya meno kabla ya kununua.

 

2. Madini ya Potassium nitrate

Haya madini husaidia kuondoa unyeti (sensitivity) katika meno yako. Unyeti wa meno yaani tooth sensitivity ni ile hali ya kuhisi maumivu kwenye meno ambayo hukaa kwa muda mfupi baada ya aidha kupiga mswaki, kunywa, kula, au hata pale upepo unapopita katika kinywa chako.

 

 

Hali hii hutokana na ile sehemu ngumu ya nje ya jino kulika sana (enamel erosion) hivyo jino kuwa wazi au mzizi wa jino unapokuwa nje kutokana na fizi kushuka chini zaidi ya eneo lake la kwanza ambapo hufunika jino.

 

Hivyo basi, kwa mtu mwenye tatizo hili, ni vyema kununua dawa yenye madini haya ili kusaidia tatizo hilo. Taarifa za madini haya hupatikana pia katika sehemu ya active ingredients, yaani viungo hai, katika boksi lako la dawa ya meno.

 

3. Mkwaruzo unaopatikana katika dawa yako ya meno (Abrasiveness of a toothpaste)

Jambo hili huwezi kuliangalia kwenye boksi au tubu ya dawa yako ya meno kama ilivyo kwa madini ya florini au madini ya potassium nitrate. Hii unaweza kuipima kwa kuangalia kama dawa yako ya meno ni ya kung’arisha meno kuwa meupe zaidi au la (whitening or non-whitening toothpaste).

 

Kwa kawaida dawa hizi huwa hazina kemikali ya kuongeza uweupe bali kama tulivyoona kwenye historia kuwa unga ule wa zamani uliotumika kama dawa ya meno uliongezewa mambo kama mifupa ya samaki iliyopondwa kuwezesha jino kusuguliwa au kukwaruzwa ili kuongeza weupe, ndivyo basi hata sasa dawa za meno huongezewa vitu vya kusugua au kukwaruza meno ili yawe meupe zaidi, ila sio kwamba hubadili rangi ya ndani ya jino bali huondoa madoa ya nje (stains) pekee.

 

Njia sahihi kwa mtu ambae angependa rangi ya meno yake kuwa meupe zaidi basi ni vyema kumtembelea daktari wa kinywa ili akusafishe kitaalamu zaidi na si kwa kutegemea dawa ya meno yenye lebo ya “whitening toothpaste”.

 

Kupitia mambo hayo makuu matatu unaweza sasa kufanya uchaguzi sahihi wa dawa yako ya meno kulingana na mahitaji yako lakini pia ukitazama vitu upendavyo kama vile rangi, ladha, harufu au muundo wa dawa yako ya meno.

 

Zile rangi (color codes) tofauti chini ya tubu ya dawa ya meno zina maana gani?

Dawa za meno huwa na rangi mbali mbali ambazo hupatikana chini ya tubu ya dawa yako ya meno na huwa katika muundo wa mstatili (rectangle) au wakati mwingine katika pembe moja ya tubu ya dawa ya meno.

 

Watu wengi wamekuwa na maoni mbalimbali juu ya maana za rangi hizi. Rangi hizi huwa katika kijani, bluu, nyekundu, nyeusi au kuna wakati rangi hizi hazionekani kabisa (nyeupe).

 

Rangi hizi ni muhimu wakati wa kuchakata tubu ya dawa hizi za meno na hazina uhusiano wowote na vilivyomo ndani ya dawa hiyo. Rangi hizi (color codes) huwekwa kwa lengo la kuijulisha mashine wakati wa uchakataji wa dawa hizi ili zifahamu wapi pa kukata au kukunja zile tumbu za kubebea dawa hizo.

 

Wakati mwingine ukisikia mtu anayaongelea haya, basi na wewe muelimishe!

2 thoughts on “Ni Dawa Gani Sahihi Kwa Ajili ya Meno Yangu?”

  1. Ansbert mutashobya

    Asante Sana daktari, baada ya kuisoma hii ndio nimeanza kukagua dawa yangu ya meno leo….😃😃

Leave a Comment

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *

swSW