Presha au shinikizo la damu (high blood pressure) ni hali ya mwili kuwa na mgandamizo mkubwa katika mzunguko wa damu, hivyo kufanya moyo kusukuma damu kwa shida kutokana na kuwa na ukinzani (force) mkubwa kwenye damu.
Hali hii hufanya mishipa ya damu kubeba damu katika mgandamizo mkubwa hivyo kupelekea uwezekano wa kupasuka na kuvujia ndani, au moyo kutanuka.
Presha inaweza kuwa pia ya kushuka kutokana na kuwa na mgandamizo mdogo kwenye damu.
Presha ya kushuka hutokea mara kwa nadra. Mara nyingi husababishwa hali zinazosababisha mishipa ya damu kutanuka au mwili kupoteza maji na chumvi nyingi (septic, hypovolemic shock nk).
Presha ya kupanda ipo katika aina kuu mbili:
1. Essential (primary) hypertension.
Mara nyingi hii huweza kutokana na mkusanyiko mwingi wa chumvi na maji mwilini hivyo kupelekea mgandamizo mkubwa kwenye mzunguko wa damu. Mgandamizo huu hupelekea kutumika fosi kubwa ili damu iweze kuendelea kuzunguka vizuri na hapa ndio presha ya mwili hupanda.
Presha ya namna hii ndiyo maarufu na inayotokea kwa watu wengi. Huambatana pia na vinasaba vya urithi.
Mfano Baba au Shangazi akiwa na aina hii ya presha, basi na wewe uko kwenye hatari ya kuipata baadae. Ukishalitambua hili ni vizuri kujua nini cha kufanya.
2. Secondary hypertension
Mara nyingi ni presha inayoletwa na mwili au baadhi ya viungo vya mwili kuwa na hitilafu, hivyo kuufanya mwili ufanye kazi katika hali ya mgandamizo wa juu na hupelekea shinikizo la damu kuongezeka.
Mfano ugonjwa wa Figo na Rovu (goiter) husababisha presha kupanda.
Presha ya aina hii pia husababishwa na mifumo ya kimaisha kwa ujumla hasahasa ulaji na namna tunavyojali afya zetu.
Sasa kwanini presha yako inazidi kupanda pamoja na kumeza dawa?
Jambo moja la kufahamu hapa ni kwamba dawa inatumika kusaidia kubalansi presha yako lakini bado haiwezi kutibu tatizo lako.
Kuna visababishi vingi vinavyopelekea kupanda kwa presha yako, hivyo focus yako inapaswa kuwa kwenye kubalansi visababishi hivyo na dawa inakuja kusaport juhudi hizo.
Tatizo lako wewe ni kwamba akili yako yote umeiweka kwenye dawa bila kufanyia kazi visababishi vya ugonjwa. Mfano mzuri ni pale ukiwa unamwaga maji kwenye pipa lenye matundu, lengo ni kujaza pipa, lakini pipa litajaa vipi wakati maji yanaendelea kuvuja? Kwanini usizibe matundu kwanza kabla ya kuweka maji?
Asilimia kubwa ya wagonjwa wa presha wameiweka akili yao kwenye kumeza dawa na kusahau kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya kuwaza dawa ya kushusha presha. Kumeza dawa tu bila kuangalia vigezo vingine ni sawa na kupanda mbegu bila kumwagilia maji, itanyauka na kufa.
Leo nitakupa sababu tano kwanini presha yako haipungui pamoja na kumeza dawa kila siku:
1. Lishe yako haiyendani na masharti ya shinikizo la damu (high blood pressure)
Kama tulivozitaja aina za presha hapo juu, mojawapo ya visababishi ni mkusanyiko mkubwa wa chumvi na maji mwilini, uzito uliokithiri, na magonjwa mbalimbali.
Chumvi
Moja ya chakula kinachoongoza kuongeza presha yako ni kiungo aina ya chumvi. Ukiwa na presha hasa aina ya ‘essential hypertension’, mwili wako unakuwa na tatizo la kutunza chumvi nyingi mwilini jambo ambalo hupelekea mkusanyiko wa maji mengi na hivyo kupandisha presha yako.
Chumvi ni kiungo muhimu katika ulaji na kuleta ladha ya chakula hivyo ni vigumu kutoitumia lakini kwa bahati mbaya chumvi huchangia kupandisha presha yako (hii ni kwa wale ambao miili yao kiasili inashindwa kuchakata vizuri kiasi cha chumvi mwilini).
Walio wengi hujaribu kuruka kipengele hiki, hawataki kupunguza kiasi cha chumvi kwenye chakula chao na hivyo kufanya juhudi za kupunguza presha kuwa finyu.
Tatizo hili hutokana na kutokuwa na elimu sahihi au kutotaka kula chakula kisicho na ladha.
Unapaswa kujua kwamba mpaka pressure yako inapanda maana yake tayari mwili wako una hitilafu na kazi yako wewe ni kusaidia mwili kupambana na tatizo hili na sio kuongeza mzigo juu.
Chumvi mbaya zaidi ni ile mbichi ya mezani, au tuseme chumvi ya kuongeza. Mfano umekuta chakula hakina chumvi, halafu ukaamua kuongeza chumvi mbichi.
Au vyakula vinavyohusisha chumvi ya moja kwa moja mfano chips, mihogo, nyama choma na kadhalka. Au kachumbari inayoongezwa kwenye nyama pia huwa na chumvi mbichi.
Elewa kwamba mwili bado unahitaji chumvi kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, unachopaswa kufanya ni kuweka chumvi kidogo sana na muhimu ipikwe kwenye chakula.
Ulaji wa vyakula kupitiliza
Katika mambo yanayoweza kuongeza presha yako ni uzito uliopitiliza. Sawa unapenda kula lakini tayari mwili wako una hitilafu, hivyo unapaswa kuanza kuangalia aina ya vyakula unavyokula.
Matumizi ya vyakula vya wanga na mafuta, kupita kiasi, huongeza uzito wa mwili na kukuweka katika hali ya presha yako kupanda na kuwa na ugumu wa kushuka, kukulazimu kutumia dozi kubwa ya dawa kushusha.
Nidhamu ya chakula na kupunguza uzito ni jambo gumu sana kwa watu wengi. Wagonjwa wengi wanalalamika presha kutoshuka lakini hawataki kujinyima kwenye chakula, hivyo uzito wao huzidi kuongezeka. Mkusanyiko mkubwa wa cholesterol mwilini huweza kuongeza mgandamizo zaidi kwenye mzunguko wa damu kwa kufanya mishipa ya damu kuwa myembamba.
Sasa kazi yako iwe kwenye kuangalia namna unavyoweza kubalance hivi vitu. Lishe yako ihusishe mlo kamili katika kiasi cha wastani. Vyakula vya wanga na mafuta uvile katika kiwango cha kawaida sana; unaweza ukafidia na mboga za majani nyingi.
Mwili wako una tabia ya kuzoea mabadiliko. Kula chakula kisicho na chumvi kwa mwanzoni inaweza kuwa ngumu ila baadaye mwili ukizoea hautaona ugumu wowote.
Jaribu pia kupunguza matumizi ya viungo na kachumbari nyingi kwenye chakula, nazo huwa na chumvi mbichi. Kwa walaji wa kuku, epuka kula ngozi ya kuku, huwa na mafuta mengi sana, hivyo huongeza cholesterol nyingi mwilini.
Kumbuka kunywa maji ya kutosha. Ukikojoa mara kwa mara husaidia kupunguza chumvi chumvi kutoka mwilini hivyo kusaidia presha kushuka; kunywa maji mpaka mkojo wako uwe mweupe.
Pima uzito walau kila mwisho wa wiki. Weka target ya kushusha uzito wako taratibu walau kwa miezi 6. Kumbuka palipo na uzito mwingi, presha iko pembeni, kama haijapanda basi ujue inakuja, hivyo unaweza kuwa hatua moja mbele kwa kuanza kuifanyia kazi lishe yako.
2. Haufanyi mazoezi ya kutosha
“Nipo busy sana doc. Sipati muda wa mazoezi!”
Hii sababu haina maana kama presha yako itaendelea kupanda. Hauna muda wa mazoezi kwasababu haujaweka kipaumbele chake au huoni umuhimu wake.
Ila usijali ndio maana Abite Afya ikaanzishwa.
Nikuulize swali? Hivi leo hii ukiambiwa,”fanya mazoezi kila siku ndani ya mwezi, tutakupatia gari!”, utakosa muda wa mazoezi kweli? Hakuna muda mdogo bali kuna kipaumbele kidogo. Siku nzima ina masaa 24, kwenye hayo masaa yote umekosa dakika 30 za mazoezi kweli?
Sasa kumeza dawa tu bila kusaidia mwili wako kuweka mambo sawa ndio sababu unameza dawa bila matokeo chanya.
Faida ya mazoezi na kazi yake kwenye presha yako.
Utafiti uliofanywa na American College of Sports ulionyesha kufanya mazoezi ya kukimbia (aerobic) au kubeba vitu vizito (resistance exercises) walau kwa dakika 30 mpaka saa moja huweza kupunguza presha yako ya juu systolic mpaka kwa digit 5mmhg.
Presha hii huweza kubaki katika upungufu huu kwa muda wa masaa 24.
Kupungua huku kwa presha huwa na faida zifuatazo:
- Vifo vinavyoweza kusababishwa na Magonjwa ya mishipa ya moyo hupungua kwa asilimia tisa (9%)
- Vifo vinavyoweza kusababishwa na ugonjwa wa kiharusi huweza kupungua kwa asilimia kumi na nne (14%)
- Vifo vinavyosababishwa na matatizo mengine huweza kupungua kwa asilimia saba (7%),
Utafiti huu unasisitiza kwamba watu wote wasio na presha, wenye presha ya mwanzoni (prehypertensive) na wenye presha (hypertensive) wanapaswa kufanya mazoezi mara kwa mara.
Kupitia utafiti huu unaweza kuona kwamba ukiwachukua watu wawili wenye presha, mmoja anafanya mazoezi na kumeza dawa, mwingine hafanyi mazoezi ila anameza dawa tu; anayefanya mazoezi ana nafasi kubwa ya kuhitaji dozi ndogo ya dawa na kuwa na presha ya kawaida kinyume na aisyefanya mazoezi.
Lakini pia hata urefu wa maisha utakuwa tofauti. Anayefanya mazoezi ana uwezekano mkubwa wa kuishi muda mrefu kuliko asiyefanya mazoezi.
Mfano halisi wa faida za mazoezi ni Baba yangu, Mr Phillbert Bitegera. Huwa anafanya mazoezi kila siku asubuhi kwa kutumia mazoezi ya television (ITV). Hana presha lakini mazoezi haya yamemfanya kuwa fiti sana na kutozeeka haraka. Amefikisha miaka 61 lakini ni kijana kabisa.
Kumbuka ukiwa na shinikizo la damu la juu kwa muda mrefu, kitu cha kwanza kupata madhara ni moyo wako kwa sababu ndio pump ya damu, ikifuatiwa na Figo. Mazoezi yanasaidia kupunguza kazi kwa viungo hivi na kufanya uwe na uwezekano mkubwa wa kuishi muda mrefu.
Kazi yangu inanifanyisha mazoezi kila siku, hii nayo si husaidia?
Kufanya kazi nyingi kazini na kuchoka sio mazoezi ninayoyaongelea. Unaweza ukashinda umesimama lakini hayo sio mazoezi ya kutosha kuufanya moyo wako ukimbie kwa mwendo unaotakiwa na mazoezi ya aina hiyo hayasaidii mwili kuseti mzunguko wake vizuri.
Hapa naongelea mazoezi ya mwili (aerobic). Mazoezi yanayokutoa jasho mfano kukimbia, kuendesha baiskeli, kucheza mpira, kikapu na kadhalika. Mwili unapopoteza jasho hupoteza na chumvi pia hivyo kusaidia mwili kushusha presha.
Kufanya kazi nyingi ni mazoezi ila yanaweza yasitoshe kuufanya ubongo uzalishe homoni ya endophine ambayo hukufanya ujiskie furaha na kupunguza stress.
Hii utapata pale utakapokimbia walau kuanzia kilometers 3 kuendelea.
Unaishi mjini na muda mwingi unapotelea kwenye foleni?
Fanya hivi, lipia gym mjini, ukitoka home asubuhi nenda na nguo za mazoezi. Ukitoka kazini saa kumi, badala ya kukimbizana na mafoleni, wewe nenda gym lisaa limoja mpaka mawili.
Faida yake: wakati unafanya mazoezi, jamu barabarani inapungua. Ikifika jioni saa moja mara nyingi jam inakuwa imepungua.
Presha yako haikai sawa? Piga tizi ndugu yangu.
3. Haupati tiba sahihi
Moja ya tatizo kubwa la kufanya presha yako isishuke ni tiba unayopata. Tatizo linaanzia pale unapoambiwa una presha na hauambiwi presha yako inasababishwa na nini. Hili ni tatizo la madaktari sio lako.
Mtu kukutwa presha imepanda halafu anaanzishiwa tu dawa bila kufanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha presha ni kitu gani?
Mfano, presha inayopanda kwa sababu ya msongo wa mawazo kazini haiwezi kutibiwa kwa dawa pekee. Tiba sahihi ni kutatua chanzo cha msongo wa mawazo, baada ya hapo presha inaweza kushuka yenyewe bila kuhitaji dawa ya muda mrefu.
Ni sawa na kumtibu mgonjwa wa malaria kwa kumpa panadol tu kushusha homa wakati hujampima malaria.
Unapogundulika una presha, kinachopaswa kufanywa ni uchunguzi wa mwili mfano kupima Figo, homoni zako, kujua kama una msongo wa mawazo au matatizo ya kifamilia.
Kama presha yako inaletwa na tatizo la homoni fulani mfano magonjwa ya rovu (goita), tiba sahihi ni kutoa dawa ya kushusha presha na kutibu kisababishi ambacho ni goita.
Kwa bahati mbaya kumekuwa na huduma duni za afya kutokana na kila mtu kuwa na uwezo wa kufungua hospitali au famasi.
Ili kuepukana na changamoto kama hizi, hakikisha unaweka appointment na daktari bingwa walau kila baada ya miezi sita ili aweze kukusaidia kuangalia dozi zako na kukupa ushauri wa kila mara. Lakini hakikisha kila mwezi unahudhuria klinic ya presha Ili walau daktari aweze kuangalia presha yako na kukushauri.
Kuna madhara yoyote ya presha isiyoshuka?
Unaweza kudharau hii lakini madhara ya presha isiyoshuka ni makubwa sana; mojawapo ya madhara ni kiharusi.
Ukishapata kiharusi kinachosababishwa na presha kubwa maana yake mishipa yako ya ubongo inaweza kupasuka, na ikipasuka hiyo ni sawa na nusu mfu. Uwezekano wa kuendelea na maisha ya kawaida ni mdogo.
Matibabu ya presha yanapaswa yahusishe dawa sahihi + dozi sawa ya dawa + mchanganyiko sawa wa dawa + ushauri wa mara kwa mara kupitia clinic.
Epuka kununua dawa za presha famasi bila kumuona daktari – kisa unakwepa gharama. Weka afya yako kipaumbele namba moja.
4. Hauna nidhamu ya afya
Nidhamu ya afya ni muhimu sana katika kuhakikisha presha yako inakaa sawa.
Nidhamu ni pale unapojua kitu fulani nikila au kunywa presha yangu itapanda na ukaamua kukiacha. Utafiti unaonyesha presha nyingi hazishuki kwa sababu ya nidhamu mbovu ya afya.
Ni rahisi sana mgonjwa kuja hospitali hajameza dawa kwa wiki nzima kwa sababu alikosa muda wa kuja hospitali. Hii ni moja kati ya ukosefu wa nidhamu.
Hospitali na pharmacies zimejaa kila mahali, kama ukikosa muda wa hospitali basi kwa siku hizo ni vyema ukanunua dawa kidogo zikusukume mpaka pale utakapoweza kwenda hospitali.
Nidhamu pia inakosekana kwenye maisha ya kila siku. Hakuna asiyejua kwamba kuvuta sigara kunafanya presha iwe juu. Unakuta mtu anakazana kumeza dawa lakini sigara hataki kuacha.
Kwanza mpaka umeamua kunywa dawa maana yake unaelewa kwamba kuna tatizo mwilini. Sasa kwanini unazidi kuupa mwili kazi kubwa ya kufanya?
Hivi leo hii ukiambiwa, “ukiacha sigara tunakununulia BMW mpya!”, hautaacha? Swala hapa ni wewe kukosa nidhamu. Sigara ni kiburudisho lakini ni bora kuliko afya yako?
Kama unataka presha yako ishuke basi kuwa na nidhamu. Nidhamu ya vyakula, nidhamu ya vinywaji, nidhamu ya mazoezi, nidhamu ya uzito wako na kadhalika.
5. Maisha yako yana stress nyingi
Unapokuwa na msongo wa mawazo mwili hutoa homoni kadhaa mfano cortisol, adrenaline, growth hormone n.k. Homoni hizi huenda kuongeza mgandamizo kwenye mishipa ya damu na hivyo kuongeza shinikizo la damu. Kila mara unapopata stress hicho ndicho kinatokea.
Kwahiyo ukiwa na stress mwaka mzima, uwezekano wa presha yako kupanda unakuwa mkubwa. Stress inaweza kutokana na kazi, shule, mahusiano, familia n.k.
Siri mojawapo ya kufanya presha yako iwe sawa ni kudhibiti msongo wako wa mawazo uwe katika hali ya kawaida. Muda mwingine ni ngumu sana kuondoa stress lakini sio jambo la kuendekeza.
Wanasaikoloji wanasema stress ya muda mrefu ni matokeo ya kushindwa kutatua matatizo yako. Kila mmoja wetu anapata stress kwa muda kadhaa lakini ni wale tu wanaopambana kutafuta suluhisho ndio humaliza stress zao. Wale ambao hufanya stress kama sifa na kushindwa kupata ufumbuzi basi baada ya muda hujikuta presha yao inapanda.
Kuna stress nyingine ni za kujitakia, mfano kufanya kazi na bosi mnyanyasaji wa kijinsia. Sawa inakupa hela lakini kama kazi inalenga kukuua mapema then ina faida gani? Hapa lazima uwe na ujasiri wa kuacha kazi na kutafuta nyingine, baada ya muda utagundua furaha yako imerudi.
Au kukaa na mwenza mnyanyasaji kwa muda mrefu bila kufanya maamuzi magumu kwa kuogopa kubaki peke yako, baada ya muda stress itakuwa juu, utapata msongo wa mawazo na presha itakuwa juu. Kwanini usiondoke kwanza ukapumzika?
Unavyozidi kubaki ndivyo mwili unapata stress nyingi na baada ya muda presha inakuwa juu, ndio maana utagundua ukikaa naye mbali kidogo furaha yako inarudi.
Umenunua gari bovu kila siku linakupa hasara, kwanini uling’ang’anie? Kwa faida gani? Tafuta mteja lipige bei, fanya mambo mengine.
Una kijana nyumbani hajishughulishi na hana nidhamu pamoja na kumsomesha, Lakini bado tunakaa naye Karibu, anakutukana na kurudi usiku, bado tunakaa naye kwa kuogopa kwamba ukimfukuza ataenda kuishi vipi? Kwani watoto wa wengine wanaishi vipi?
Kama Mungu asingemfukuza Adam kutoka bustani yake, angeweza kutengeneza maisha yake na kujivunia kazi ya mikono yake? Fukuza, wala hatokufa kama unavyodhani, atajifunza maisha na kurudi akiwa na akili njema.
Pressure yako inapanda kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi kwa wakati na kusubiri mpaka uanze kuugua moyo.
Mwaka 2020 nilileta gari bovu kutoka kwa mzee wangu Biharamulo lije dar tutengeneze pesa, likataka kuniua na presha, kila nikiona namba ya dereva natukana, nikapata stress sana hadi tukaamua kuliuza.
Hili gari lilikuwa linamfirisi mzee wangu na lilikuwa limenimaliza hata mimi. Mzee alikuwa amekonda sana, mimi pia nilipoteza kilo nyingi na ilibaki kidogo nifirisike. Tulipoliuza, japo kwa bei hafifu sana, stress yote kwisha.
Nilivorudi kijijini kumtembelea mzee wangu, nilikuta amenenepa, amependeza sana. Je ingekuwaje kama tungeling’ang’ania kwa kuogopa aibu?
Kwa ufupi njia pekee ya kupunguza stress za maisha ni kuchukua hatua mapema kabla hujachelewa.
Baadhi ya majanga kama wizi, vifo na magonjwa – kama kansa na HIV/Ukimwi n.k. – yanaweza kuleta stress sana lakini bado unatakiwa kukubali matokeo na kuendelea na maisha.
Mwisho
Pata muda wa kufurahi na rafiki zako, pata muda wa kuskiliza muziki unaoupenda, jitengenezee mazingira ya furaha. Oa au olewa na mtu anayekupenda, using’ang’anie watu wasio na habari na wewe, huko ni kujipendekeza.
Tafuta marafiki wanaokutia moyo, achana na marafiki wahuni watakupa hasara. Mwisho kabisa uwe mtu wa kujiamini na kuchukua hatua katika maisha.
Yote hayo ni kuhakikisha stress yako inakuwa chini; presha yako haitakuwa na namna bali kushuka tu.
Chukua hatua katika maisha yako, epuka stress zisizo na msingi. Utashangaa presha uliyokua unaambiwa unayo imepotea ghafla.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Kuna mtu anapima pressure yake lakini haitulii ametumia dawa za hosp zaidi ya wiki, lakini akipima inaweza kusomeka 210, baada ya masaa ikaja 190 baadae 170 baadae 160 ikaja tena 170 halafu 150 ikarudi tena 160 kwa nini inashuka na kupanda, wakati anatumia dawa pamoja na tiba lishe kama vile maji ya ndimu, vitunguu swaumu na maji ya madafu mara kwa mara?
Karibu bwana fahrat,
Dawa ya Presha ikititolewa huwa inahitaji muda walau wiki kuonesha majibu,
Sababu Kwanini haishuki inaweza kuwa
1. Dozi aliyopewa haitoshi, inapaswa kupandishwa.
2. Anapaswa kuongezewa dawa nyingine ya kusaidiana na aliyonayo Sasa.
3. Kuna tatizo lingine kama stress Nyingi, au matumizi ya chumvi nyingi nk.
Ushauri wangu ni kwamba arudishwe kwa daktari Aloyemuandikia dawa kwa ajili ya kufanyiwa review na kuangalia kati ya hayo matatu lipi ni sababu.
Kwa ushauri zaidi wasiliana na Mimi kupitia mawasiliano yetu hapo chini
Nilipatwa na tatizo la presha baada ya kujifungua 2019 nilitumia dozi ya mwezi hospital ya rufaa mloganzila nikapona baada ya miaka minne nikabeba ujauzito cku ya kuumwa uchungu presha ikawa juu tangu nijifungue haijawahi kukaa sawa natumia Dawa mwezi was nane Sasa nakosa Amani
Pole sana fatuma. Asilimia 40% ya Presha za Mimba hubaki Jumla bila kuondoka, kulingana na takwimu na uzoefu. Sio vizuri kupambana na Uhalisia, inapelekea kuwa na msongo wa mawazo. Swala la kufanya ni kupata msaada wa kimbinu wa kuhakikisha presha yako inakaa sawa na unatumia walau dawa kidogo sana.
Unaweza kufanya booking kupitia huduma yetu ya daktari binafsi wa nyumbani tuanze sessions za kila mwezi.
Naomba kufahamu wapi mlipo.ai hospitali gani mnapatikana.
Habari yako samwel,
Unaweza kutupata kwa kupiga simu au shuka mpaka chini kabisa utakuta sehemu imeandikwa Duka letu, bonyeza hapo, utapelekwa moja kwa moja kwenye office yetu na kuona huduma zetu.
Tuna huduma ya Daktari kiganjani. Huduma hii itakusaidia kuwa na daktari wako binafsi atakayekuwa anafatilia mwenendo wa afya yako au ya mgonjwa wako kwa ukaribu.
Karibu kwa huduma.