Kukuza misuli na kuwa na muonekano wa kuvutia ni lengo la vijana wengi. Ndio maana ukienda gym utaona vijana wanavyopambana kukuza misuli.
Kwa bahati mbaya au nzuri, huwa sio rahisi kama wengi wanavyodhani na utafiti unaonyesha asilimia 75% ya vijana wanaojaribu kukuza misuli huishia njiani au kufeli kabisa kwa kushindwa kuendelea na kukaa tamaa moja kwa moja.
Misuli sio rahisi kukua, uhitaji uvumilivu kuweza kukubali, mpango mkakati na sio kutamani tu kuipata. Misuli ili ikue inahitaji kuumizwa kwanza na kupata majeraha kadhaa kwa ndani na wakati inapona ndipo hukua.
Hatua hii uhitaji juhudi kweli kweli. Na sio juhudi tu, bali inakuwa na principles ambazo usipozifuata, unaweza kwenda gym muda mrefu bila kufanikiwa kabisa.
Mfano mzuri ni mimi hapa. Nilipoenda gym kwa mara ya kwanza, focus ilikuwa kunyanyua vyuma na kukuza misuli. Nilifanya hivyo kwa mwezi mzima bila mafanikio, nikakata tamaa na kuamua kuviacha maana nilikuwa natumia pesa bila mafanikio.
Baadae nilikuja kugundua sababu kadhaa za kiafya, nitakazokwambia, ndipo misuli yangu ikaanza kukua.
Kila jambo linalouhusisha mwili wako lina kanuni za kiafya ambazo lazima uzifahamu. Baada ya muda mrefu wa kujaribu na kufanya utafiti mdogo kama daktari, niligundua sababu zifuatazo kwanini misuli yako inaweza isikue pamoja na kufanya mazoezi muda mrefu:
1. Lishe yako haitoshi
Misuli ili iweze kukua inahitaji virutubisho muhimu vya protini, wanga, mafuta na vitamini. Nitaanza kuelezea protini.
Protini ina kazi kubwa ya kujenga mwili na misuli yako, na uhitajika kwa kiasi kikubwa. Maharage na nyama ni moja ya vyakula vyenye protini nyingi.
Kama unafanya mazoezi gym lazima uhakikishe unakula nyama na/au maharage ya kutosha ili mwili uweze kujengeka. Changamoto kubwa hapa Tanzania, chakula kinachopatikana kwa mwingi ni wanga (Wali, ugali, mihogo, na kadhalika). Hapa unakuta uwiano wa vyakula hauko sawa.
Unakula sahani kubwa la wali, nyama vipande vitatu, mchuzi mwingi, pamoja na maharage kiduchu. Hapa mwili wako utapata nguvu ya kutosha lakini protini kidogo hivyo hautakua kama unavyotakiwa. Utaenda gym kila siku lakini misuli itagoma kukua, itakomaa tu.
Kwa upande mwingine misuli uhitaji madini na vitamini za kutosha ambazo inawezekana wewe huvipi kipaumbele. Vyakula kama matunda, mboga za majani, madini ya chuma, zinc na phosphorus. Maana ili misuli ikue lazima ipate damu ya kutosha, hivyo madini ya chuma yakiwa machache, misuli haikui.
Kumbuka: Mwili wako utahitaji zaidi kadiri unavyofanya kazi. Kama umeanza program ya mazoezi halafu msosi wako bado ni ule ule – wali, nyama mbili, kabichi kidogo, maharage kidogo na maji – hapo sahau kuhusu kukuza misuli.
Tambua jambo moja, gramu moja ya wali inatoa kalori 4, sawa na gramu moja ya nyama ambayo hutoa kalori 4. Jitahidi kubalansi vyakula hivi ili upate kiwango sahihi cha nguvu kwa ajili ya misuli na mwili wako.
Utahitajika pia kunywa maji ya kutosha kuwezesha misuli yako kuvimba. Kumbuka asilimia 60 ya uzito wa mwili ni maji. Hivyo kwakuwa unafanya mazoezi mazito mwili wako utahitaji maji zaidi – kabla na baada ya mazoezi.
Nikuibie siri: Watu wa kusini na magharibi mwa Africa (Namibia, Botswana, South Africa, Cameroon, na Nigeria) wana miili mikubwa sana, na siri yao kubwa sio mazoezi, ni kula nyama za kutosha, kila siku.
2. Kunyanyua uzito mwingi mwanzoni
Wakati unaanza kufanya mazoezi ya kukuza misuli, jitahidi kuondoa tabia ya kufakamia vyuma ilimradi tu unyanyue. Hii tabia itakuchosha mapema sana bila kusukuma misuli katika kiwango kinachotakiwa.
Katika kubeba chuma, ili msuli uweze kusukumwa katika kiwango sahihi, kuna kitu kinaitwa training volume. Training volume inapatikana kwa kuchukua idadi ya misukumo (reps), kuzidisha kiasi cha seti utakazofanya, kuzidisha uzito wa chuma unachobeba.
Mfano: Uzito 50kg, seti 4 (unarudia zoezi mara nne) na reps 20 (unasukuma au kuvuta mara 20) huwa “50 x 20 x 4 = 4,000”. Hivyo training volume yako ni 4,000.
Punguza uzito kwenda 40kg, fanya reps 25 mara 4 utapata training 4,000 hiyo hiyo.
Hapa utagundua ukianza na uzito mdogo, utasukuma mara nyingi na misuli itafaidi zaidi bila kuchoka haraka. Lakini ukianza na uzito mkubwa utasukuma misuli mara chache na utachoka haraka; na uwezekano wa kuumiza misuli yako ni mkubwa.
Ukifika gym anza na uzito mdogo ambao unauweza, kwa ajili ya kufanya warm ups na kuandaa misuli. Kabla hujanyanyua uzito zaidi inabidi kufanya warm up kwa ajili ya kuruhusu damu kwenda kwenye misuli unayoisukuma na baada ya hapo unaweza kuamua kwenda kwenye uzito mkubwa taratibu.
Kuepuka makosa hayo, ni vyema ukapata gym coach ili ufanye mazoezi kwa maelekezo ya viwango sahihi.
3. Kufanya ngono ‘mara nyingi’ na kupiga nyeto (masturbation)
Usishangae, maneno unayoyasoma ni sahihi! Stori ya ngono na misuli huanzia kwenye sayansi ya shahawa (sperms).
Shahawa hutengenezwa na mwili kuanzia kwenye amri ya ubongo (hypothalamus) ambapo huamuru kutolewa kwa homoni ya testosterone, ambayo ndiyo huusika na kutengeneza shahawa.
Sasa sifa ya shahawa ni kubeba nguvu ya kiume. Mtu unapokuwa na hamasa ya ngono (tendo la ndoa), ubongo huamuru kuzalishwa kwa homoni hii ambayo huja kusaidia utengenezwaji wa shahawa. Shahawa zikishatengenezwa huifadhiwa kwenye korodani mpaka zitakapohitajika.
Sasa kisayansi mshindo mmoja wa kumwaga shahawa wakati wa tendp la ndoa unaweza kufanya mwili upoteze nguvu kuanzia kalori 60 mpaka kalori 100, na kwa punyeto huweza kupoteza mpaka kalori 200 hadi 300.
Piga hesabu mtu anayepiga punyeto mara 5 kwa wiki. Anapoteza kalori karibia 1,500 kwa wiki, 6,000 kwa mwezi!
Wakati mwili unahitaji nguvu zaidi kwa ajili ya kukua, wewe unazitoa kwa njia ya puli! Mwisho wake misuli haiwezi kukua.
Moja ya mbinu kubwa ambayo wakuza misuli huitumia ni kupunguza upotevu wa shahawa zao kwa kupunguza idadi ya tendo la ndoa au kuacha kabisa kwa muda fulani.
Nguvu ambayo mwili utabaki nayo ni nyingi sana, na inaweza kutumika katika shughuli mbalimbali za mwili, moja wapo ni kukuza misuli.
Mfano mzuri ni mpiganaji Mike Tyson. Wakati wa ujana wake alipofungwa gerezani kwa makosa ya uhalifu aligundua kutopiga punyeto na kutofanya ngono ni faida kwake. Hivyo kwa kipindi chote (zaidi ya miaka mitano) alichokuwa gerezani na alipokuwa akifanya training kuwa bondia, hakumgusa mwanamke au kupiga punyeto.
Baada ya hapo alikuwa na nguvu kubwa sana ya misuli. Akiwa na miaka 20 tu alivunja rekodi ya dunia.
Njia hii pia hutumiwa na wafugaji wanapowahasi mifugo yao. Umeshawahi kujiuliza kwa nini mnyama akihasiwa huwa ananenepa na kuwa na nyama nyingi? Sababu ni hiyo ya kutunza shahawa bila kuzitoa.
Kama unapiga punyeto na kufanya ngono zaidi ya mara tatu kwa wiki, sahau kuhusu misuli yako kukua vizuri.
Mada ya ngono na nguvu za kiume utaisoma zaidi kwenye chapisho langu la “faida ya kutofanya ngono – mara kwa mara – kwa mwanaume”.
4. Kutokua na siku ya mapumziko
Kukuza misuli ni hatua kwa hatua, unapaswa kuweka progress chart ili kufanya mwili wako kukubaliana na hali taratibu, na misuli kupata nafasi ya kupona na kuvimba.
Tambua jambo moja, misuli inaposukumwa kwa uzito huwa inakuwa kama inaumia. Baada ya kuumizwa misuli uhitaji mpaka masaa 48 ya kutosumbuliwa tena ili iweze kufanya recovery, hivyo ni muhimu kuweka siku ya mapumziko walau mara 2 kwa wiki ili kuupa muda misuli kujitengeneza upya na kutuna.
Bila kufanya hivo misuli yako inaweza isikue. Kama wewe ni muscle builder utagundua unaweza kufanya zoezi la misuli ya mikono leo na usione mabadiliko, lakini kesho yake muda kama huo utagundua misuli yako inaanza kukua na jioni yake utaona mabadiliko kidogo kwenye misuli. Hii huwa ni baada ya misuli kurecover na kuvimba.
Kwenda gym kila siku ya Mungu hupelekea misuli yako kudumaa na kutokua kwa muda unaotarajia.
Usiwaze kupata misuli kwa haraka haraka, nenda taratibu. Inachukua walau mwezi mmoja wa juhudi kuanza walau kuona misuli kwa mbaali. Hivyo usiwe na papara, panga walau siku 4 za mazoezi kwa wiki, pumzika siku mbili, na utaona matokeo mazuri.
Mwisho
- Usisahau kunywa maji ya kutosha kabla na baada ya mazoezi.
- Usisahau kuongeza sukari mwilini kabla ya kuanza mazoezi ili mwili upate nguvu ya mazoezi. Mfano kula kipande cha Apple au kunywa juisi kidogo.
- Jitahidi kuwa kwenye timu ya kufanya nao mazoezi ili wakupe msukumo, maana safari ya kujenga misuli sio ya kitoto.
- Jitahidi kuwa na mwalimu wa kukuelekeza mazoezi ya kufanya. Kufanya peke yako ni upotezaji wa muda maana unahitaji elimu ya mazoezi kujua aina ya mazoezi kwa ajili ya misuli flani.
Asante kwa kuendelea kusoma mada zetu, usisite kutoa maoni au kuuliza swali kwa changamoto yoyote utakayopata.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
“faida ya kutofanya ngono – mara kwa mara – kwa mwanaume” chapishp lenye hio mada apo kaka limetoka? Nimejaribu kutafuta kwenye izi ambazo ziko apa ila sijafanikiwa kuona.
Asante Wilson, lipo jaribu kusearch kwenye makala zetu..
Ila Kuna Kitabu chake ambacho kimesheheni taarifa nyingi..
Jaribu kucheki kwenye shop…