“Naitwa Jamila, nina miaka 32, uzito wangu ni kilo 102. Nafanya mazoezi sana lakini sipungui, tatizo ni nini?”
Habari yako Jamila, pole sana na hongera kwa kuwa muwazi na kuelezea tatizo lako. Kupungua uzito ni moja ya kitu kigumu kutokea na mara nyingi hatua zake huwa ni changamoto kwani uhitaji nidhamu kubwa ambayo itakutaka kujitoa sadaka ili ufikie lengo lako.
Walio wengi hupungua kwa sababu ya shida za kimaisha au magonjwa, wachache hupungua kwa juhudi.
Kupunguza uzito uliopitiliza una faida lukuki. Ningependa nikutajie baadhi:
- Kiasi cha mafuta (cholesterol) mwilini kupungua hivyo kushusha uwezekano wa magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, kisukari, presha na kadhalika.
- Kuwa mwepesi na kuongeza uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuchoka haraka.
- Husaidia kuongeza uwezo wa kufanya tendo la ndoa kwa muda mrefu.
- Na zaidi ya yote huongeza kujiamini.
Nirudi kwenye swali lako, kwanini uzito wako haupungui licha ya kufanya mazoezi?
Tambua kufanya mazoezi peke yake sio sababu ya kupunguza uzito. Unaweza kuwa unakimbia kilomita 10 kwa siku na bado usiweze kupungua.
Kitu kinachofanya upungue ni balance ya nguvu (calories) unazopoteza na unazoingiza mwilini. Hapa naongelea nidhamu ya kile unachokula.
Mfano umekimbia kilometa 20 na ukapoteza kalori 1000, halafu ukarudi nyumbani ukala chakula chenye kalori 1500. Hapa umekimbia, umechoka na umetoka jasho jingi lakini hakutakuwa na mabadiliko kwenye uzito wako maana ulichopoteza ni kidogo kuliko ulichoingiza.
Tambua unapofanya mazoezi mwili wako unapoteza ile nguvu katika fomu ya kalori. Baada ya hapo mwili huwa na uhitaji mkubwa wa chakula ili kuweza kurudishia kilichopotea kwenye mazoezi.
Mwili utaongeza hamu na haja ya kula na hivyo utajihisi una njaa sana na kuhitaji kula chakula kingi. Hapa ndio kuna mtego. Ukiweza kutambua mtego huu, utakua umeshinda mtihani na uzito wako utapungua.
Unachopaswa kufanya katika hali hii ni kuunyima mwili kwa kiasi – kula kwa wastani. Mwili hautapata kile kiasi unachokitaka na utarespond kwa kugeukia njia zingine za kupata nguvu. Hii itapelekea mafuta (fats) yako kutumika kama njia ya kurudishia ile nguvu inayohitajika na mwili. Ukifanya hivi muda mrefu, mwili utakuwa unalazimika kuchoma mafuta kila siku.
Usisahau: Mafuta huwa ni chaguo la pili la mwili kupata nguvu, chaguo la kwanza ni vyakula vya wanga. Mkusanyiko wa mafuta ndio huongeza uzito.
Nimesikia kuna mahesabu ya kupunguza uzito, ni kweli daktari?
Ndio Jamila, mahesabu yapo. Ni ngumu sana kupoteza uzito uliopitiliza bila ya kutokua na elimu ya kalori.
Mfano ukikimbia kilometa 1, unaweza kuchoma kalori mpaka 100. Wakati huo ndizi-sukari moja inaweza kukupa kalori 100 vile vile. Sasa jiulize unahitaji nidhamu ya aina gani kupoteza uzito.
Mwili ili upungue lazma uunyime ili uweze kutumia akiba iliyopo. Hili halikwepeki!
Umeshawahi kujiuliza kwa nini mtu anayekosa chakula au mwenye maradhi baada ya muda hukonda?
Mtu akiumwa hamu ya kula inapungua na muda mwingine akila anatapika, hivyo hupunguza kiasi cha kula na baada ya muda ataanza kupungua uzito kwa kasi sana.
Kwa haraka utaona siri ipo kwenye chakula. Kama ukiweza kuunyima mwili ipasavyo, basi kilo zako huweza kupungua hata bila mazoezi.
Hayo yote nafanya daktari lakini bado sipungui! Shida iko wapi?
Kama unafanya hayo yote na hupungui, basi inawezekana una vinasaba vya uzito-mwingi. Lakini bado unaweza kupungua. Fanya mambo yafuatayo:
- Kuwa na subira: kama ilivyochukua muda mrefu kuongeza uzito wako, itachukua muda mrefu pia kupoteza. Unatakiwa kujiwekea malengo ya muda mrefu na kuwa na mfululizo mzuri wa mazoezi na chakula chako.
- Mtiririko mzuri wa mazoezi: Asilimia 70 ya watu hufanya mazoezi kwa kwenda mbele na nyuma, Hawana mtiririko mzuri. Atafanya kwa wiki mbili alafu atatingwa na kazi au majukumu na ataacha mazoezi kwa mwezi mzima na badaye atarudi, hivyo kila siku unajikuta tunaanza upya. Ukiwa na mtiririko mzuri wa mazoezi na chakula walau kwa miezi 6, unaweza kuanza kukaribia malengo yako.
Nikibeba mimba itakuaje daktari?
Wanawake wengi hupata ugumu wa kupunguza uzito kutokana na uhalisia wa maisha mfano kuzaa. Mwanamke anapobeba mimba, kama alikuwa anafanya mazoezi ya kupungua, mara nyingi huacha na mwili uhitaji chakula kingi, hivyo kupelekea unene.
Baada ya hapo hufata kipindi cha kunyonyesha ambapo itahitajika kula chakula cha kutosha na mwisho wa siku uzito wako huongezeka.
Hili huwa ni pigo sana kwa mwanamke anayehitaji kupunguza uzito. Lakini sio mwisho wa safari. Kuna mazoezi ya kufanya kwa kina mama waliotoka kujifungua. Tutayajadili katika mada zetu zinazoendelea.
Fomula
Kupoteza uzito (weight loss) = Mazoezi zaidi + Chakula kiasi (moderate diet) + Nidhamu ya mwendelezo (consistency) + Imani (trust the process).
Mwisho
Mwili wako unahitaji kalori 2,500 mpka 3,000 kwa siku katika hali ya kawaida. Ukifanya mazoezi mwili utahitaji kalories zaidi ya 4000+. Focus yako wewe iwe kwenye kubalance hizi kalori.
Mfano ukifanya mazoezi, mwili unaweza kupoteza kalori 800, wewe jitahidi usirudishe kalori zote 800 kupitia msosi. Kula chakula cha kawaida urudishie walau kalori 450.
Ukifanya hivyo hata mara tano kwa wiki utakuwa umepoteza kalori 2,250 kwa wiki. Ukiendelea hivi baada ya mwezi utakuwa umepoteza kalori 9,000. Kwa miezi 6 utakuwa umepoteza kalori 54,000.
Kupoteza kalori hizi kutakua na mchango mkubwa kwenye kupunguza uzito wako na baada ya muda nidhamu hii itakubeba.
Tukutane katika mada zinazoendelea za afya, huko utapata kujua vyakula gani vya kupunguza uzito, na mazoezi muhimu wakati wa mimba na kunyonyesha. Kama utakua na maoni yoyote, usisite kutuandikia hapo chini.

Chief Content Officer (CCO) at Abite Afya
I’m responsible for overseeing the entire content strategy, ensuring that all published materials align with the blog’s mission, audience needs, and business goals.
Asante sana daktari, hakika nimepata elimu ya kutosha kuhusu uzito. Ni kama unanizungumzia Mimi, nitajitahidi kubalance chakula ili nipunguze uzito. Asante sana.🙏